Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CUF Tanga ‘yamla’ Mbaruku
Habari za Siasa

CUF Tanga ‘yamla’ Mbaruku

Mbunge wa jimbo la Tanga mjini (CUF), Mussa Bakari Mbaruku
Spread the love

MBUNGE wa jimbo la Tanga mjini na kiongozi mwandamizi katika Chama cha Wananchi (CUF), Mussa Bakari Mbaruku huenda akaingia matatizoni baada ya msimamo alioutoa kuhusu kinachoendelea ndani ya chama hicho, kupingwa na wenzake wilayani, anaandika Mwandishi wetu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Utendaji ya CUF Wilaya ya Tanga, msimamo wa Mbaruku kuwa haungi mkono upande wowote katika mvutano wa uongozi unaokikabili chama haukubaliki na umesabisha kamati hiyo kukutana.

Taarifa iliyotolewa juzi na Kurugenzi ya Habari na Uenezi Wilaya, imesema Mbaruku ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, ametangaza anaouita msimamo wa CUF Wilaya ya Tanga mjini akisema haiungi mkono upande wowote katika mvutano wa uongozi unaokikabili chama hicho.

Ana maana kwamba hayuko upande wa Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa mwenyekiti na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, wala upande wa chama unaoongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad.

Mbaruku, imeelezwa katika taarifa hiyo, alieleza msimamo huo katika mahojiano na kituo cha radio cha Clouds FM, kupitia kipindi cha Amplify kinachoendeshwa na mtangazaji Millard Ayo.

Kamati ya Utendaji ilimkumbusha Mbaruku msimamo wa chama wilaya ya Tanga ilipokutana Septemba mosi 2016; ikiazimia kukubaliana na azimio la Baraza Kuu la Uongozi Taifa (BKUT) la kutomtambuwa Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali.

Taarifa ya Kamati hiyo imesema msimamo huo ulitolewa wakati Mbaruku akiwemo katika kikao kwa kuwa ni mjumbe. Mwenyekiti wa kikao alikuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Tanga mjini, Rashid Jumbe Hamza.

Iliamuliwa kwamba chama kinaheshimu uamuzi wa ngazi ya juu wa kwamba Profesa Lipumba alijiuzulu mwenyewe uongozi kwa tamko alilolitoa hadharani Agosti 5, 2015, na akafukuzwa uanachama baada ya kubainika alisababisha matukio ya kukihujumu chama.

Miongoni mwa matukio yaliyotumika kumchukulia hatua katika kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika Septemba 2016, mjini Zanzibar, ni kuvamia mkutano mkuu maalum wa Agosti 21, 2016, uliofanyika Ubungo Plaza, na kuvamia ofisi kuu za Buguruni, akisindikizwa na maofisa wa Jeshi la Polisi na kusababisha kujeruhiwa kwa mlinzi aliyekuwa na silaha na kuvunja milango ya ofisi na kuingia ndani kwa nguvu.

« Chama cha Wananchi CUF Wilaya Tanga mjini hakimuungi mkono Profesa Lipumba katika harakati zake za kuibomoa CUF. Kauli ya Mbunge Mussa Bakar Mbaruku ni ya kwake mwenyewe binafsi na haina mafungamano na Chama Cha Wananchi CUF Wilaya ya Tanga, » imesema taarifa hiyo.

« Msimamo wetu CUF Tanga, Lipumba sio mwanachama wetu, hatumuungi mkono kabisa ; kurudi kwake ndani ya chama sio kwa nia njema bali kuja kuivunja CUF na UKAWA kwa ujumla. Nia yake ni kuhakikisha CUF inakosa utulivu na kudhoofika kabisa. Tupo pamoja na Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad na bado tunamtambua kama katibu mkuu wetu halali.”

Taarifa ya Kamati ya Utendaji Wilaya ya Tanga imesema kwamba inashangaa kwamba Mbaruku amesahau kuwa ushindi wake wa ubunge ulichangiwa na nguvu za UKAWA, umoja ulioasisiwa na viongozi wakuu wa CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).

Imesema chini ya ushirikiano huo, CUF imepata mafanikio makubwa katika historia yake. “tulipata viti vingi vya udiwani, 15 vya jukwaa, na vitano viti maalum. Jumla 20, dhidi ya CCM madiwani 12 wa jukwaa na vitatu viti maalum. Jumla 15. Haikuwa rahisi kufikia mafanikio haya bila ya UKAWA.”

“Kauli ya Mbunge Mussa Mbaruku kusema CUF Wilaya ya Tanga hatuna upande katika mgogoro, tunaipinga na kuilani kwa nguvu zote. Tunamsihi mheshimiwa aache kuwa na sura mbili, asimame upande mmoja, tena asimame pamoja na chama. Kusema huna upande ni kauli ya kinafki… itakuwa anawahandaa wananchi na kujihadaa mwenyewe pia.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

Habari za Siasa

CCM yakemea ufisadi, yaipa kibarua TAKUKURU

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekemea vitendo vya ubadhirifu wa...

Habari za Siasa

Bajeti ya Ikulu 2024/25 kuongezeka, bunge laombwa kurudhia Sh. 1.1 trilioni

Spread the love  WIZARA ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa...

error: Content is protected !!