March 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Corona yamuua Rais wa zamani Burundi

RAIS wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya

Spread the love

RAIS wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya (71) amefariki dunia akiwa jijini Paris nchini Ufaransa kwa ugonjwa wa COVID-19. Inaripoti mitandao ya Kimataifa …(endelea).

Buyoya ambaye ni Jenerali mstaafu wa Jeshi nchini Burundi amefikwa na mauti jana Alhamisi tarehe 17 Desemba 2020.

Oktoba 2020, Mahakama ya Burundi, ilimhukumu Buyonga kifungo cha maisha gerezani baada ya kubainika kuhusika katika mauaji ya aliyekuwa rais wa taifa hilo, Melchior Ndadaye mwaka 1993.

Hata hivyo, Buyoya alikuwa akikana kuhusika na tuhuma hizo, akieleza zina lengo la kumchafua kisiasa.

Mauaji hayo, yalisababisha vurugu za kikabila na kusababisha mauaji ya watu zaidi ya 300,000 yaliyokoma mwaka 2006.

Buyoya aliingia madarakani kwa mara ya kwanza baada mapundizi ya kijeshi dhidi ya utawala wa rais Jean-Baptiste Bagaza mwaka 1987 ambaye naye aliingia madarakani kwa mapinduzi dhidi ya mtangulizi wake, Michel Micombero mwaka 1976.

           Soma zaidi:-

Buyonga alidumu madarakani kwa miaka sita huku ukikithiri na mambo mbalimbali ambayo yalibadili sura ya nchi kama vile mauaji ya kinyama yaliyofanyika kitongoji cha Ntega-Marangara mwaka 1988, makubaliano ya umoja wa Warundi yaliyoidhinishwa mwaka 1991, kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1993, na mengine mengi.

Aliondoka madrakani mwaka 1993 baada ya kushindwa katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi kuwahi kufanyika tangu mwaka 1960.

Wakati huo, mtangulizi wake, Prezida Melchior Ndadaye kutoka chama cha Frodebu ndiye aliyemshinda kwa asilimia zaidi ya 65 ya kura na Pierre Buyoya aliyekuwa wakati huo amegombea kwa tiketi ya chama cha Uprona aliibuka na asilimia 33 za kura.

Buyoya alirejea tema madarakani Julai 1996, baada ya kumpindua tena madarakani rais wa mpito Sylvestre Ntibantunganya, ambaye wakati huo alichukua madaraka kufuatia kifo cha Cyprien Ntaryamira ambaye alifariki katika ajali ya ndege pamoja aliyekuwa rais wa Rwanda wakati huo Juvenal Habyarimana.

Rais Ntaryamira alikuwa ameshikilia kiti cha urais kwa miezi miwili pekee, baada ya kifo cha Rais Ndadaye.

Kuuawa kinyama kwa Rais Ndadaye kulilitumbikiza taifa katika vita vya kikabila, kati ya Watusi na Wahutu nchini humo.

Hali hiyo ilimlazimu Rais Buyoya kufanya mazungumzo na wapinzani wa serikali waliokuwa wameanzisha vita, mazungumzo yaliyodumu kwa muda wa miaka miwili kuanzia mwaka 1998 hadi pande hizo mbili zilipoweza kusaini makubaliano ya amani Agosti 2000.

Tangu wakati huo, Rais Buyoya alikubaliwa kuhudumu kwa kipindi cha mpito cha kilichokubaliwa katika makubaliano ya kwanza kwa mujibu wa makubaliano ya amani yaliyoidhinishwa Arusha nchini Tanzania na baadaye akaondoka madarakani mwaka 2003 na utawala wa nchi kuchukuliwa na Rais Domitien Ndayizeye.

Mwaka 2008, aliteuliwa kuwa mjumbe maalumu wa amani Umoja wa Mataifa katika nchi ya Mali na Sahel kufuatia mzozo wa kivita uliokuwa ukitokota kati ya Mali na nchi jirani ya Sudan.

Januari 2013, ndipo aliteuliwa tena na Umoja wa Afrika kama mjumbe maalumu katika nchi ya Mali na eneo la Sahel.

Mwaka 2014, alijaribu kugombea nafasi ya uongozi wa nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa na wakati huo serikali ya Burundi ilimuunga mkono kwani uhusiano baina yao ulikuwa bado ni mzuri.

Hata hivyo, mambo yalibadilika kuanzia mwaka 2015,wakati ulipoibuka mzozo wa kisiasa kuhusiana na aliyekuwa rais wa Burundi hayati Pierre Nkurunziza, kugombea muhula wa tatu wa urais.

Wakati huo, wapinzani wa serikali walisema, hatua ya Nkurunziza ni kinyume cha sheria, lakini chama chake cha CNDD-FDD, walisisitiza kuwa hatua hiyo ni kwa mujibu wa sheria.

Buyoya hakukubaliana na hatua ya Nkurunziza kugomea urais kwa muhula wa tatu akinukuu kuwa “makubaliano ya amani ya Arusha” yanabainisha wazi rais anapaswa kuongoza kwa mihula miwili pekee.

Kutokana na kauli hiyo, uhusiano wake na utawala wa Nkurunziza uliharibika na hakuweza tena kukanyaga katika ardhi ya Burundi.

Mwishoni mwaka 2018, Buyoya aliwekwa katika orodha ya watu 17 wanaoshukiwa kuhusika na mauaji ya Rais Melchior Ndadaye.

Buyoya hakutarajia hilo kwani alitarajia makubaliano ya Arusha yatamlinda, ambayo alisema kuwa suala la mauaji ya Ndadaye litachunguzwa na mahakama kubaini ukweli kuhusu mauaji hayo.

Buyoya alisema kesi hiyo ina misingi ya kisiasa.

Alisema uchunguzi wa kifo hicho unaweza kuibua ghasia za ubaguzi wa kikabila.

Hilo halikuizuia mahakama kumhukumu kifungo cha maisha jela pamoja watu na wengine 16 waliopatikana na hatia ya mauaji ya Melchior Ndadaye, hukumu iliyotolewa Oktoba 2020.

Buyoya na wenzake walisema watakata rufaa dhidi uamuzi huo wa mahakama.

error: Content is protected !!