January 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yawapa rungu Watanzania kuwamaliza Mdee na wenzake

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefungua milango kwa wanachama wake na Watanzania kwa ujumla kupendekeza adhabu kwa wanachama wake 19 waliokiuka maagizo ya chama hicho ya kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumatano tarehe 25 Novemba 2020 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Mnyika ametoa wito huo, ikiwa ni siku moja imepoita tangu wanachama wake 19 wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) kwenda bungeni kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum.

Wabunge hao, waliapishwa jana Jumanne viwanja vya Bunge jijini Dodoma na Spika Job Ndugai ambaye baada ya kumaliza, aliahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha katika safari yao ya miaka mitano bungeni.

Mnyika amewaomba wanachama wa Chadema na Watanzania kutoa mapendekezo yao juu ya adhabu inayotakiwa kutolewa kwa wabunge hao viti maalumu.

Amesema mapendekezo hayo yatafanyiwa kazi katika kikao maalum cha kamati kuu ya Chadema kitakachofanyika Ijumaa terehe 27 Novemba 2020 chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

“Tunakwenda kufanya kikao cha kamati kuu tarehe 27 Novemba, natoa wito kwa wanachama na wadau wa demokrasia, milango iko wazi kutoa maoni kwa chama ni hatua gani zichukuliwe dhidi yao,” amesema Mnyika.

Amesema, wanachama hao 19, wataitwa mbele ya kamati hiyo
kujieleza kwa nini walikiuka maagizo ya chama na kwenda kuapishwa huku wakijua hakuna majina yaliyopendekezwa na kamati kuu.

Kwa mujibu wa Mnyika, wanachama hao wamekiuka msimamo wa Chadema kwa kushiriki kuubariki mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, ambao chama hicho kimepinga kukukubali matokeo yake kwa madai hayakuwa halali.

“Walioapa walijiteua na kushiriki katika kuhalalisha ubatili kwa kushiriki hiko kiapo,” amesema Mnyika.

Aidha, Mnyika amewaomba wanachama wa Chadema wenye taarifa juu ya watu waliohusika katika sakata hilo kuzitoa, ili wachukuliwe hatua.

“Na hakika walioshiriki na walihusika nao huu uhalifu. Kama kuna mtu ana taarifa zozote juu ya kiongozi yoyote katika Ofisi ya Katibu Mkuu aliehusika nao, tupewe taarifa hizo ili tutoe hukumu,” amesema Mnyika.

Mbali na Mdee, wengine walioapishwa ni wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Halima Mdee, Ester Bulaya na Esther Matiko.

Wengine ni, Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Nusrat Hanje. Katibu Mkuu Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Grace Tendega.

Makamu Mwenyekiti Bawacha-Bara, Hawa Mwaifunga, Naibu Katibu Mkuu Bawacha-Bara, Jesca Kishoa na Katibu Mwenezi Bawacha, Agnesta Lambat.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Mtwara, Tunza Malapo, Ceciia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.

error: Content is protected !!