Tuesday , 19 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema yawakana Mdee na wenzake
Habari za Siasa

Chadema yawakana Mdee na wenzake

John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema
Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, kimekana kutambua wabunge wake 19 wa viti maalum walioapishwa jijini Dodoma. Anaripoti Kelvin Mwaipungu…(endelea).

Wabunge hao 19 wakiongozwa na Halima Mdee, wameapishwa leo mchana Jumanne tarehe 24 Novemba 2020 viwanja vya Bunge jijini Dodoma na Spika Job Ndugai.

Mara baada ya kuapishwa, Mdee ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), alizungumza kwa niaba ya wenzake na kuishukuru Chadema chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kwa kuwateua.

Katika salamu hizo fupi, Mdee aliwahakikishai wana Chadema, watakiwakilisha vyema chama hicho licha ya uchache wao bungeni.

Hata hivyo, kauli ya Mdee ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema inakwenda tofauti na ile iliyotolewa na Katibu Mkuu wake, John Mnyika ya kutokutambua orodha hiyo ya wabunge.

Mnyika kupitia akaunti yake ya Twitter, alieleza, chama hicho hakijateua wala kupeleka majina ya wabunge wa viti maalum Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Soma Zaidi: Walichosema Mdee, Matiko baada ya kuapishwa 

“Niliandika barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) kuwajulisha. Tunafuatilia yanayojiri Ofisi ya Spika wa Bunge na tukithibitisha hujuma au usaliti hatutasita kuchukua hatua,” aliandika Mnyika.

Mara baada ya kuapishwa kwa wabunge hao, MwanaHALISI Online limezungumza na mtendaji mkuu huyo wa chama, Mnyika kupata msimamo wa Chadema katika jambo hilo;

Mnyika amejibu kwa kifupi, “Tutakaa katika kamati kuu na fahamuni kwamba mimi katibu mkuu sikupeleka majina tume na wala kamati kuu ya chama haikufanya uteuzi wowote.”

Alichokisema Mnyika, kinafanana na kile ambacho amekuwa akikieleza mara kadhaa, Tundu Lissu, aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema.

Lissu alisema, kukubali kupeleka wabunge wa viti maalum bungeni, ni kuhalalisha uchafuzi wa uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano ya tarehe 28 Oktoba 2020.

Chadema na ACT-Wazalendo ni miongoni mwa vyama vya siasa vilivyojitokeza hadharani kupinga matokeo hayo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa madai, uligubikwa na ukiukwaji wa kanuni na miongozo.

Lissu alisema, kamati kuu ya chama hicho, iliyokutana baada ya uchaguzi mkuu ilikubaliana kutokupeleka wabunge wa viti maalum bungeni.

Halima Mdee, Mbunge wa Chadema Viti Maalim

Katika uchaguzi huo, Chadema ilijipatia jimbo moja tu la Nkasi Kaskazini aliloshinda Aida Khenani akimwangusha Ally Keissy wa CCM.

Mbali na Mdee aliyeapishwa, wengine ni, Grace Tendeka, ambaye ni Katibu Mkuu wa Bawacha, Hawa Mwaifunga, Makamu Mwenyekiti wa Bawacha na Jesca Kishoa, Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha na Agnesta Lambat, katibu mwenzi wa Bawacha.

Wengine ni; Esther Matiko, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu, Nusrat Hanje, Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha).

Pia, Mjumbe wa Kamati Kuu, Ester Matiko, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mtwara, Tunza Malapo na Cecilia Pareso.

Wabunge wengine ni; Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba na Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza.

Kati ya wabunge hao 19 walioapishwa, wanaoingia kwa mara ya kwanza bungeni ni wanne; Agnesta, Asia, Stella na Felister.

1 Comment

  • Usaliti upo lakini siyo wa kiwango cha kula keki na kuibakiza. Wale yote wamalize sisi mbona njaa na mateso tumezoea.

    Kwanza bado tunaugulia majonzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Zanzibar mbioni kuanza uchimbaji mafuta na gesi baharini

Spread the loveSERIKALI ya Zanzibar, imekamilisha mchakato wa uchimbaji wa mafuta na...

Habari za Siasa

Wizara ya afya yataja mafanikio 10 miaka mitatu Samia madarakani

Spread the loveWIZARA ya Afya imetaja mafanikio 10 iliyoyapata ndani ya miaka...

Habari za Siasa

Mbozi walilia kuwa manispaa, majimbo 3

Spread the loveHALMASHAURI ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imeeleza dhamira yake...

Habari za Siasa

Wabunge waitaka TPDC kuongeza kasi ya kuunganisha wateja gesi asilia

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini...

error: Content is protected !!