JOHN Mnyika, Naibu katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kibamba amesema kuwa rais Magufuli anatumia kivuli cha kuleta maendeleo kuminya demokrasia nchini, anaandika Hellen Sisya.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Kimara Mwisho jimboni humo,mbunge huyo amesisitiza kuwa demokrasia na maendeleo ni lazima viende pamoja.
“Rais Magufuli anataka kwa kivuli cha kuleta maendeleo, serikali isikosolewe pale inapokosea kuhusu maendeleo, kwa kuminya demokrasia, na sisi tunasema demokrasia na maendeleo ni lazima viende pamoja” alisema mbunge huyo.
Aidha, Mnyika aliongeza kuwa chama chake kitatumia mikutano ya kiserikali inayofanywa na wabunge pamoja na madiwani wake kufanya shughuli za chama kama ambavyo Rais Magufuli anatumia mikutano ya kiserikali kushughulika na kazi za chama chake.
“Kwa sababu rais Magufuli ameingia madarakani, amekataza mikutano ya vyama. Na anatumia mikutano ya kiserikali kushughulika na mambo ya CCM. Na sisi pia tumefikia uamuzi kwamba katika mikutano yetu yote ya hadhara, tutashughulika na masuala ya maendeleo, lakini pia tutashughulika na masuala ya demokrasia ” ,alisisitiza Mnyika.
Leave a comment