March 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Viti Maalum vya Ubunge, mtihani mwingine Chadema

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa

Spread the love

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, kinakabiliwa na mtihani mwingine mzito juu ya hatma ya nafazi zake za wabunge wake wa Viti Maalum. Anaripoti Hamisi Mguta, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini humo zinasema, wapo baadhi ya viongozi wandamizi wa Chadema wanaounga mkono na kushinikiza chama kikubali kufanya uteuzi wa nafasi, huku kuna wengine wakipinga uteuzi huo.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wetu, wanaopinga hoja hiyo, wanajiekeleza kuwa kufanya uteuzi wa wabunge wa viti maalum ni sawa na kuhalalisha mchakato mzima wa uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano ya tarehe 28 Oktoba 2020.

           Soma zaidi:-

“Kuteuwa wabunge wa viti maalum, katika mazingira ya sasa na ukizingatia kilichotokea katika uchaguzi mkuu uliyopita, ni sawa na kuhalalisha matendo yaliyofanyika,” ameeleza mmoja wa viongozi wa juu wa chama hicho kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Amesema, “tayari chama chetu kimetangaza bayana kuyakataa na kutotambua uchaguzi huo na matokeo ya uchaguzi. Kupeleka majina ya wabunge kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ni kwenda kinyume kabisa na msimamo wetu.”

Amesema, msimamo wake binafsi, ni kwamba wasipeleke mbunge hata mmoja, ili kuwaonyesha wananchi wao na ulimwengu kwa ujumla wake, kuwa “Chadema haikubaliani na kilichofanyika.”

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Katika uchaguzi mkuu wa 28 Oktoba, Chadema kilitangazwa kushinda jimbo moja la Nkasi Kaskazini, kutoka majimbo zaidi ya 35 iliyoshinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

MwanaHALISI Online limeelezwa, mtego mkubwa katika hili, ni kwamba chama hicho kinaweza kujikuta kinapasuka, kufuatia makamu mwenyekiti wake (Bara), Tundu Lissu, kueleza bayana  hakubaliani na hoja za wanaotaka chama kuteuwa wabunge hao.

Lissu ambaye alikuwa mgombea urais wa Tanzania, amenukuliwa mara kadhaa akipinga ushiriki wa wabunge wake, katika Bunge lijalo, akiwamo aliyetangazwa msindi katika jimbo la Nkasi Kaskazini, Aida Khenani ambaye alimshinda Ally Keissy wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika moja ya andishi lake kupinga wabunge wake kushiriki Bunge lijalo, Lissu anasema, “hatukufanya kampeni na kushiriki uchaguzi, ili kutoa fursa kwa watu fulani kuwa wabunge au madiwani tu. Tulikuwa na agenda ya uchaguzi: Uhuru, Haki na Maendeleo ya Watu.”

Anahoji: “Je, kushiriki kwetu katika matunda haramu ya Jumatano iliyopita, kunatusaidia nini, katika kutekeleza agenda yetu hiyo?”

Halima Mdee, Mwenyekiti Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha)

Aidha, wanaopinga chama kupeleka wabunge wa viti maalum, wanakwenda mbele zaidi kwa kueleza Bunge lijalo, halitakuwa na fursa ya kuwapo kwa kiongozi wa kambi rasmi ya waliowachache bungeni; kambi yenyewe na mawaziri vivuli.

“Hili la kutokuwapo kwa kambi, ni jambo kubwa sana. Wabunge wa upinzani watakuwa bungeni wakielea, kwa kuwa mambo mengi, yatategemea huruma ya Spika, ambayo haikuonekana katika Bunge lililopita,” ameeleza kiongozi mmoja wa Chadema ambaye alikuwa mbunge katika bunge lililopita.

Anasema, “hakutakuwa na hotuba zetu. Hakutakuwa na Mnadhimu wa Upinzani. Hakutakuwa na wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, kutoka upinzani. Katika mazingira hayo ya Bunge la chama kimoja, hawa watasikilizwa na nani?”

Anasema, “wanataka twende bungeni tukasikilizwe na watu tunaowatuhumu kushiriki kuvuruga uchaguzi. Wanataka tukashirikiane na wanaochekelea kilichotokea. Kwa maoni yangu, hapana. Ni bora kufa na tai shingoni. Hatuwezi kubariki haya.”

Lakini wanaotaka chama kipeleke wabunge, wanajielekeza katika hoja kuwa kufanya hivyo, kutakisaidia chama kuimarika kifedha na kuweza kujiendesha, na kuongeza kuwa “kutokwenda bungeni, kunaweza kusababisha serikali, kuwanyima ruzuku.”

Hata hivyo, haijafahamika rasmi, msimamo wa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ambaye anatajwa na wachambuzi wa kisiasa kuwa ni mmoja wa viongozi anayeendesha chama kwa kuzingatia maoni ya kila mmoja na kuchukua kila tahadhari.

Kamati Kuu (CC) ya Chadema, inatarajiwa kukutana leo Jumamosi, tarehe 7 Novemba, 2020 jijini Dar es Salaam, ambako pamoja na mambo mengine, inaangaliwa na wachambuzi, kuwa yaweza kukiangamiza chama au kukiimarisha.”

Mbali na mjadala wa uteuzi wa Viti Maalum, Kamati Kuu ya chama hicho, inatarajiwa kutoa msimamo wake rasmi, kuhusiana na kilichotokea katika uchaguzi mkuu uliyopita na hatua ambazo itazichukua.

Kabla ya kufanyika kwa vikao hivyo vya kikatiba, viongozi wakuu wa Chadema na chama rafiki cha ACT- Wazalendo, Jumamosi iliyopita tarehe 31 Oktoba 2020, walitoa tamko la kutotambua matokeo ya uchaguzi na kutangaza kufanyika kwa maandamano ya amani yasiyo na kikomo, kuanzia Jumatatu ya tarehe 2 Novemba  2020.

Vyama hivyo, vilisema matokeo ya uchaguzi uliosimamiwa na Tume mbili ile ya Zanzibar (ZEC) na Tanzania Bara (NEC) hawayatambui kwani uligubikwa ukiukwaji wa sheria, kanuni na miongozi hivyo kutaka uitishwe upya chini ya uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya.

error: Content is protected !!