Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema, ACT- Wazalendo kushirikiana uchaguzi mkuu 2020?
Habari za SiasaTangulizi

Chadema, ACT- Wazalendo kushirikiana uchaguzi mkuu 2020?

Spread the love

VYAMA viwili vya upinzani nchini Tanzania – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na chama cha ACT-Wazalendo – viko mbioni kushirikiana ili kukabiliana na Rais John Pombe Magufuli, katika uchaguzi mkuu ujao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kuna kila dalili na ushahidi wa mazingira kwamba, Chadema ambacho kwa sasa ndio chama kikuu cha upinzani nchini humo, kitaingia kwenye uchaguzi huo, kikiwa kimejifunga na ushirikiano na ACT- Wazalendo.

Uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani nchini Tanzania, umepangwa kufanyika tarehe 25 Oktoba 2020.

Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameeleza katika ukurasa wake wa twitter, “…tunahitaji umoja madhubuti wa vyama viwili tu.”

Kauli ya Zitto, imetafsriwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa vyama hivyo viwili, havitaki kushirikiana na vyama vingine takribani 16 vilivyosalia.

ACT- Wazalendo, ni moja ya vyama vyenye nguvu nchini, na kwa sasa, ndio chama kiongozi, miongoni mwa vyama vya upinzani vyenye nguvu upande wa Tanzania Zanzibar.

Nguvu ya chama hicho Visiwani Zanzibar, imetokana na kujiunga kwa waliokuwa viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF), wakiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad.

Kwa sasa, Maalim Seif ndiye mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, na kwamba kabla ya kujiunga na chama chake hiki kipya, alikuwa katibu mkuu wa CUF.

Katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, vyama vinne vya upinzani nchini Tanzania vilishirikiana kupitia jumuiko lililopewa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Ushirikiano huo ulianzia kwenye Bunge Maalum la Katiba Oktoba 2014.

UKAWA uliundwa na vyama vya National Convention for Construction and Reform (NCCR- Mageuzi), National League for Democracy (NLD), Chama cha Wananchi (CUF) na  Chadema.

Ushirikiano huo ulihusisha pamoja na kusimamisha mgombea mmoja wa urais wa Jamhuri ya Muungano; mbunge mmoja kwa kila jimbo, diwani kwenye kata au wadi na rais wa Zanzibar.

Katika nafasi ya urais wa Muungano, Chadema ndicho kilichopewa nafasi ya kusimamisha mgombea, ambako waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ndiye aliyepewa jukumu la kupeperusha bendera, huku Maalim Seif akisimama upande wa Zanzibar.

Hata hivyo, katika baadhi ya majimbo, ushirikiano huo ulivurugika, kuafuatia baadhi ya vyama kuweka wagombea, kinyume na makubaliano ya ushirikiano.

Miongoni mwa majimbo ambayo ushirikiano ulivurugika na hivyo kuathirika ushirikiano, ni Segerea, lililopo Manispaa ya Ilala, mkoani Dar es Salaam.

Taarifa zinasema, katika jimbo hilo, Anatropia Theonest, akiwa na baraka za baadhi ya viongozi wake wandamizi wa Chadema, aliendelea kupeperusha bendera ya chama chake, licha ya jimbo hilo kuwa na mgombea wa CUF, Julius Mtatiro.

Muingiliano huo wa wagombe wa UKAWA, ndio ulimuibua mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bonna Kaluwa, kuibuka mshindi.

Katika uchaguzi huo, Anatropia alipata kura 49,000; Mtatiro alipata kura 75,744, huku Bonna akipata kura 94,640. Wagombea hao wawili wa upinzani, Mtatiro na Anatropia, walipata takribani kura 124,744.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa MwanaHALISI umeonyesha, kuna kila dalili kwamba ushirikiano kati ya vyama  vilivyounda UKAWA mwaka 2015, hautakuwapo katika uchaguzi mkuu ujao; badala yake, Chadema chaweza kushirikiana na ACT-Wazalendo.

Kinachotatizo ushirikiano wa sasa, ni hatua ya NCCR- Mageuzi, kuamua kuwachukua baadhi ya viongozi wandamizi wa Chadema, wakiwamo waliokuwa wabunge wake wawili, Anthony Komu na Joseph Selasini.

Komu ambaye alipata kuhudumu kwenye nafasi ya Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema (DF), kwa takribani miaka 13, ametangaza kuondoka chama hicho, mara baada ya kumaliza kuhudu kwenye nafasi yake ya ubunge, tarehe 19 Juni mwaka huu.

Naye Selasini ambaye amekuwa mbunge wa Rombo kwa miaka 10 mfululizo amesema, siku zake ndani ya Chadema, zilimalizika tokea kufanyika kwa uchaguzi wa ndani ya chama hicho, katika Kanda ya Kaskazini.

Selasini alikuwa mmoja wa wagombea katika uchaguzi huo, uliotawaliwa na hila, ghriba na rushwa.

Alishindwa na Godbless Lema, mbunge wa Arusha Mjini, anayedaiwa kuwa alibebwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Wote wawili – Selasini na Komu – wamekuwa wakimtuhumu Mbowe, kuivuruga Chadema kwa kile wanachokiita, “kulinda maslahi yake binafsi.”

“Chadema hakiwezi kushirikiana na CUF, kwani kilichotokea mwaka 2015 kwa Profesa (Ibrahim) Lipumba kuwaacha kwenye mataa, hawawezi kumuamini tena na kushirikiana naye,” kilidokeza chanzo chetu

John Mrema, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema alipoulizwa na MwanaHALISI ONLINE juu ya majadiliano au ushirikiano wa vyama hivyo, kama utakuwapo amesema, “majadiliano yanaendelea na baadhi ya vyama na yatakapokamilika, tutaweka utaratibu wa pamoja wa kutoa taaarifa kwa umma.”

Alipoulizwa majadiliano hayo yanahusisha vyama gani hasa, Mrema aliishia kusema, “muda ukifika tutazungumza.”

Hatua ya Mrema kushindwa kuweka bayana vyama vinavyofanya majadiliano na ujumbe wa Zitto juzi, Jumapili, 31 Mei 2020, unathibitisha kuwa hata muungano wa ACT- Wazalendo na Chadema, nao waweza kushindwa kufikiwa.

Akiandika katka ukurasa wake wa twitter, Zitto alisema, “…namuomba sana Mungu kwanza atupe uhai na pili atuondolee ubinafsi, ili tuweze kuweka Nchi mbele,” badala ya maslahi ya vyama vyao.

Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, ameeleza kuwa pamoja na changamoto zilizopo, bado anaamini kuwa chama chake kinaweza kujenga ushirikiano madhubuti na Chadema.

Mshikamano miongoni mwa vyama vya upinzani unakiamsha chama tawala CCM kukuza demokrasia, kuleta maendeleo, kudumisha utawala bora, na haki za binadamu.

Mwanasheria na mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora, Jovinson Kagirwa amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, “vyama vya upinzani kwa sasa haviwezi kuwa na umoja wa aina yoyote ile katika siasa hizi za kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.”

Anasema, upinzani hauwezi kuwa ushirikiano wa pamoja kwa sababu hakuna tena kitu kinachowaunganisha kama ilivyokuwa mwaka 2014 wakati wanaungana.

UKAWA ulianzishwa mwezi Oktoba 2014 kwa lengo la kupigania uwapo wa Katiba Mpya, kama ilivyokuwa katika rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa chini ya waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!