July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bunge lapitisha bajeti, wapinzani wapiga kura ya ndio…

Dk. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na MIpango Tanzania

Spread the love

BUNGE la Tanzania, limepitisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/21 ya Sh.34.87 trilioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Bajeti hiyo iliwasilishwa bungeni Alhamisi tarehe 11 Juni 2020 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango na kujadiliwa kwa siku mbili, Ijumaa na Jumamosi.

Upigaji kura wa bajeti hiyo ya tano kwa utawala wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli umefanyika leo Jumatatu asubuhi tarehe 15 Juni 2020 bungeni jijini Dodoma.

Shughuli ya upigaji kura, imefanyika kwa mbunge kuitwa jina lake na kupiga kura hadharani kwa sauti.

Akitangaza matokeo ya kura, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai amesema, wabunge waliopiga kura walikuwa 371 na wabunge 13 hawakuwepo bungeni.

Kagaigai amesema, kura 63 zimepigwa za ‘hapana’ na 304 wamepiga kura ya ‘Ndio.

Sabreena Sungura, Mbunge Viti Maalum Chadema

Baada ya Kagaigai kumaliza kutangaza matokeo, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alisimama na kusema, “ni kura nyingi, rekodi haijapata kutokea. Kura zinaonyesha kwamba yajayo..” kisha wabunge wa chama tawala (CCM) wakaitikia kwa shangwe ‘yanafurahisha.’

Pia, Spika Ndugai ameipongeza wizara ya fedha na mipango chini ya waziri wake, Dk. Philip Mpango jinsi walivyotoa ushirikiano kwa Kamati ya Bunge na Bunge zima wakati wote wa uwasilishaji wa bajeti kwa miaka mitano mfululizo.

Baadhi ya wabunge ambao hawakuwepo bungeni ni; Mwita Waitara, Naibu waziri wa Tamisemi, Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo).

Lathifah Chande, Mbunge Viti Maalum Chadema

Wengine ni; Selemani Bungara maarufu ‘Bwege,’ mbunge wa Kilwa Kusini (CUF) na Willfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema).

Pia, baadhi ya wabunge wa upinzani waliopiga kura ya ndio kwa bajeti hiyo ni; Willy Qambalo (Karatu), Sabreena Sungura, Dk. Immaculate Semesi, Lathifah Chande, Maryam Msabaha, Anna Gidarya na Rose Kamili wote wa viti maalum wote kutoka Chadema.

Wengine ni; Rukia Ahamed Kassim, Riziki Lulinda, Sonia Magogo wa Viti Malum CUF huku James Mbatia, Mbunge wa Vunjo kupitia NCCR-Mageuzi akipiga kura ya ‘Hapana.’

Endelea kufuatilia MwanaHALISI ONLINE & MwanaHALISI TV kwa habari zaidi

error: Content is protected !!