Tuesday , 23 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Bunge labainisha mambo nane yanayotafuna halmashauri
Habari Mchanganyiko

Bunge labainisha mambo nane yanayotafuna halmashauri

Spread the love

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) nchini Tanzania, imetaja changamoto nane zinazopelekea matumizi mabaya ya fedha za umma, katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

LAAC imetoa sababu hizo kupitia taarifa yake ya uchambuzi kuhusu ripoti ya ukaguzi wa hesabu za mamlaka za serikali za mitaa, kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2019, uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Taarifa hiyo imewasilishwa  bungeni jijini Dodoma, leo  Jumatano tarehe 27 Mei 2020, na Vedasto Ngombale, Mwenyekiti wa  LAAC.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, changamoto ya kwanza ya matumizi mabaya ya fedha za umma kwenye halmashauri, ni kutowasilishwa ipasavyo,  ruzuku ya fedha za maendeleo katika halamshauri.

LAAC imesema, imebaini, katika mwaka wa fedha wa 2018/2019, Halmashauri 26 zilipokea Sh. 22.8 bilioni, ambazo zilikuwa zaidi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutumika katika miradi ya maendeleo.

“Kiasi hiki ni sawa na 31% ya bajeti nzima ya fedha za maendeleo iliyotengwa kwa ajili ya Halmashauri zote nchini. Hoja ya LAAC ni kwamba halmashauri husika mara nyingi zinakuwa hazikujipanga kutumia kiasi hicho cha fedha, na mara nyingine, zinakuwa hazina rasilimali watu ya kutosha kusimamia matumizi hayo,” amesema Ngombale

Pia, LAAC imesema, katika mwaka huo wa fedha, halmashauri 157 hazikupewa fedha za ruzuku ya maendeleo jumla ya Sh. 556.8 bilioni, wakati mwaka wa fedha wa 2015/16 kiasi cha Sh. 620 bilioni sawa na asilimia 61, ndizo hazikuwepelekwa.

“Katika mwaka 2017/18 kiasi cha Tsh. 480 bilioni sawa na 49% ya bajeti ya maendeleo hakikupelekwa.”

“Katika hali kama hiyo ni vigumu kwa Halmashauri husika kutekeleza kikamilifu mipango yao ya maendeleo. Lakini pia Halmashauri zinaonekana kuwa zimetumia vibaya kiasi kidogo cha fedha zilizopokea,  kwa sababu kinakuwa hakitoshi kukamilisha miradi hiyo,” amesema

Changamoto ya pili, inayotokana na ukiukwaji wa taratibu za Serikali Kuu, ni urasimu katika kukamilisha malipo ya wakandarasi.

“Utaratibu uliopo sasa kwa ajili ya kuhakiki hati za madai yao huanzia kwa mkandarasi kwenda kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri husika kwenda kwa Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), RAS hupeleka OR-TAMISEMI, kisha kwenda hazina,” amesema

“Kamati inaona utaratibu huo una urasimu mkubwa, unaochangia miradi husika kutotekelezwa kwa wakati. Miradi kadha wa kadha katika halmashauri mbalimbali imechelewa kutekelezwa kutokana na urasimu huo,” amesema Ngombale ambaye ni mbunge wa Kilwa Kaskazini kupitia Chama cha Wananchi (CUF)

Changamoto ya tatu, inayotokana na mwenendo wa halmashauri, ambayo  inasababisha matumizi mabaya ya fedha za umma, ni ukiukwaji wa Sheria za Fedha na Manunuzi ya Umma.

Wakati changamoto ya nne ikiwa ni, kutotumika kwa mashine za kielektroniki kwa ajili ya kuimarisha ukusanyaji mapato, kwenye vituo mbalimbali (POS).

“LAAC imebaini kuna udhibiti mdogo wa mashine katika kukusanya mapato. Baadhi ya Halmashauri zinashindwa kufikia matokeo kutokana na uvujaji wa mapato kutokana na kutokuwepo kwa udhibiti wa kutosha katika matumizi ya mashine hizo,” amesema

“Ni vema OR-TAMISEMI ikaimarisha ufuatailiaji katika suala hili,  ili matumizi hayo yaweze kuwa na tija zaidi kwani kwa sasa kuna changamoto zifuatazo,” inaeleza taarifa ya kamati hiyo.

Amesema, baadhi ya halmashauri kutowasilisha makato ya kisheria ya mishahara ya watumishi katika mifuko ya hifadhi ya jamii, ni changamoto ya tano iliyotajwa  katika taarifa ya LAAC.

“Baadhi ya halmashauri kutodai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), katika miradi inayotekelezwa na wafadhili, ni changamoto ya sita iliyotajwa katika taarifa ya kamati hiyo, ambayo inasababisha matumizi mabaya ya fedha,” amesema

Changamoto ya saba, ni upotevu wa mapato ya halmashauri kutokana na kutorejeshwa ipasavyo gharama za matibabu, kwa njia ya bima ya afya kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NHIF).

Wakati changamoto ya mwisho ikiwa ni, kutotumika ipasavyo kwa mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti wa mapato na matumizi ya fedha za umma (EPICOR).

“LAAC imebaini kuwa Mfumo huu haujaunganishwa kikamilifu na mifumo mingine, ikiwa ni pamoja na Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato katika Halmashauri, Mfumo wa Bajeti, Mfumo wa Taarifa za Fedha unaotumiwa katika ngazi za chini za Serikali), na mfumo wa kielectroniki wa malipo ya mishahara ya watumish i(LAWSON), inaeleza taarifa ya LAAC,” amesema

Taarifa ya LAAC imeongeza “Sanjari na hoja hii, LAAC imebaini pia kwamba katika bahadhi ya Halmashauri, makusanyo ya fedha yanafanyika kwa kutumia 11 stakabadhi za kawaida, na malipo ya manunuzi ya vifaa na huduma mbalimbali yanapokelewa kwa kutumia risiti za kawaida zisizo za kielektroniki.”

Kufuatia changamoto hizo, LAAC imependekeza Serikali kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato, pamoja na kupeleka ipasavyo fedha za miradi ya maendeleo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari Mchanganyiko

DC ampongeza Dk. Rose Rwakatare kwa kusaidia waathirika wa mafuriko Mlimba

Spread the loveMWENYEKITI wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk.  Rose Rwakatare...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mbunge ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the loveMBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze kasi...

error: Content is protected !!