Nelson Teich, Waziri wa Afya wa Brazil

Brazil: Saa 24 wagonjwa 15,305 wa corona, mawaziri wajiuzulu

Spread the love

TAIFA la Brazil linazama, virusi vya corona vinatesa wakazi wake. Katika saa 24 zilizopita wagonjwa 15,305 wameripotiwa, vifo 824 na kufanya jumla ya waliofariki kuwa 14,817. Inaripoti mitandao ya kimataifa … (endelea).  

Jumamosi wiki iliyopita, Brazil imeipiku Hispania na Italia na kushika namba nne katika mataifa yaliyo na maambukizi makubwa duniani.

Marekani inaongoza kwa kuwa na maambukizi 1,467,820, Urusi 281,752 na Uingereza ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na maambukizi 243,695. Kwa mujibu wa BBC, Wizara ya Afya ya Brazili imetangaza kuwa na jumla ya maambukizi 241,000.

Nelson Teich, Waziri wa Afya wa Brazil, amejiuzulu kutokana na maambukizi kuongezeka kwa kasi huku akisema, haoni juhudi za wizara yake kupambana na kuwasaidia wananchi wake.

Teich aliyedumu kwenye wizara hiyo chini ya mwezi mmoja, amekuwa waziri wa pili wa wizara hiyo kujiuzulu.

Aliteuliwe Aprili 2020 baada ya Luiz Henrique Mandetta kujiuzulu kutokana na kutoelewana na Rais Jair Bolsonaro kuhusu mapambano yake dhidi ya virusi vya corona.

Akijivua madaraka hao, Teich amemshukuru Rais Bolsonaro kwa kumwamini na kumpa madaraka hayo akisisitiza, haoni sababu ya kuendelea kuwa waziri wa afya wakati wananchi wanaendelee kuangamia kwa kasi.

Teich ni miongoni mwa viongozi wa taifa hilo waliojitokeza wazi kupinga shinikizo la Rais Bolsonaro la kufuta kujifungia, kwa madai ya kuathiri uchumi wa taifa hilo.

Wataalamu wa afya nchini humo wametahadharisha kuwa, watu walioathirika na virusi hivyo wanaweza kuwa wengi zaidi ya namba inayotangazwa na serikali, kutokana na wengi wao kutopata vipimo.

Rais Bolsonaro amekuwa akipingwa ndani na nje taifa hilo kutokana na misimamo yake ya kuuchukulia ugonjwa huo kama ‘kitu kidogo’ hivyo kusababisha raia wake wengi kuangamia.

Msimamo wa Rais Bolsonaro licha ya maambukizi makubwa na vifo vingi, ni kwamba kufungia watu ndani kutaharibu uchumi wa taifa hilo.

Machi, 2020, alipokuwa pamoja na waandamanaji aliwataka mameya kulegeza masharti ya watu kujifungia ndani akisisitiza “maisha lazima yaendelee. Kazi lazima ziendelee. Lazima turejee kwenye maisha yetu ya kawaida.”

Jair Bolsonaro, Rais wa Brazil

Alisema, kufunga biashara, shule pamoja na kuweka vikwazo ni sera zinazohitaji kuchomwa moto.

Pamoja na maambukizi kuwa makubwa na vifo, Rais Bolsonaro amesema, wananchi akiwemo yeye hawana cha kuhofia na wanaendelea ‘kupiga kazi.’

“Kama ilivyo historia yangu ya uanariadha, kama nitaambukizwa virusi vya corona, sina cha kuhofia. Siwezi kujisikia tofauti yoyote, na itakuwa ni mafua tu,” amesema.

Bruno Covas, Meya wa Jiji la São Paulo amesema, mji huo unaelekea ‘kuinua mikono’ kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa wanaopelekwa katika hospitali zakez.

Mpaka sasa, zaidi ya asilimia 90 ya matumizi ya vifaa na nguvu kazi kwenye mji huo tayari vinatumika, na kwamba wiki mbili zijazo jiji hilo halitakuwa na uwezo tena kwenye hospitali zake.

São Paulo ni moja ya miji mikubwa nchini Brazil ambapo mpaka sasa limeripoti vifo zaidi ya 3,000.

About Masalu Erasto

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!