Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Bodi ya Lipumba kimbembe leo
Habari za SiasaTangulizi

Bodi ya Lipumba kimbembe leo

Prof. Ibrahim Lipumba, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF (kulia) akiwa na Katibu Mkuu CUF Bara, Magdalena Sakaya
Spread the love

SIKU ya leo Jumatatu yaweza kuwa chungu mfano wa shubiri kwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi – Civic United Front (CUF) – iliyoidhinishwa na serikali baada ya kupendekezwa na kaimu katibu mkuu anayetambuliwa na kundi linalomtii Profesa Ibrahim Lipumba, anaandika Jabir Idrissa.

Wajumbe wa bodi hiyo wameitwa mbele ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Dyansobera kwa nia ya kujieleza kuhusu uhalali wao kisheria. Ni wito uliotolewa kwa ajili ya maendeleo ya usikilizaji wa kesi iliyoko mahakamani ambayo ilipangwa kuendelea leo tarehe 13 Novemba 2017.

Ni hatua itakayoshuhudiwa wakati huu chama hicho kikiwa katika mwaka wa pili wa kuzama kwenye mgogoro wa uongozi uliochimbwa na hatua ya Prof. Lipumba kulazimisha kurudi uongozini baada ya kuwa aliyejiuzulu kwa hiari yake Agosti 5 mwaka 2015.

Jaji Dyansobera anasikiliza kesi iliyofunguliwa na CUF kupinga uhalali wa bodi hiyo na hatua yake ya kusimamia shughuli za chama hicho chenye nguvu kubwa na mtandao wa matawi ulioenea nchini kote – Bara na Zanzibar.

Katika kesi hiyo, mawakili Juma Nassoro na Hashim Mziray, wanaosimamia kesi zilizofunguliwa na uongozi unaoshikwa na kamati ya uongozi iliyo chini ya mwenyekiti Julius Mtatiro na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Shariff Hamad, watakuwa wamepiga hatua muhimu ya kusikilizwa mashauri yanayohoji uhalali wa Prof. Lipumba ambaye ameshikilia kiti baada ya kutambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania.

Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini inayomtambua Prof. Lipumba ni pamoja na Peter Malebo ambaye ndiye Mwenyekiti na Thomas Malima ambaye ni Katibu wa Bodi. Wengine ni Hajira Siria, Aziz Iss Nagesha, Abdul Magomba, Amina Msham, Asha Said, Mussa Haji Kombo, Saria Hilal Mohamed na Suleiman Makame.

Wajumbe hawa wametakiwa kufika mahakamani huku ikitarajiwa kila mmoja atatakiwa kujieleza.

Bodi ya Wadhamini ya kundi linalomtii Prof. Lipumba, likiongozwa na Magdalena Sakaya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama, na Abdul Kambaya, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano na Umma, iliidhinishwa na Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi wa Serikali (RITA) kwa tamko lililotolewa Juni 12 mwaka huu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Emma Hudson, mnamo katikati ya Juni mwaka huu, alikiri mbele ya wahariri wanachama wa Jukwa la Wahariri Tanzania (TEF) waliokuwa katika mkutano wa ushirikiano na taasisi hiyo kwamba Bodi hiyo imekidhi vigezo vya kisheria.

Uamuzi wa RITA ulipingwa haraka. Na hatimaye uongozi wa CUF ulifungua kesi mahsusi ya kumshitaki Emma kwa nafasi binafsi, na kujumuishwa RITA kuwa taasisi nyingine ya kidola inayochukuliwa kama adui wa chama hicho. Awali chama hicho kilianza na Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania.

Kutambuliwa kwa bodi hiyo kulikuwa na maana ya kuiengua bodi inayotambuliwa na uongozi, ambayo inaongozwa na Abdallah Said Khatau (mwenyekiti) na Joram Bashange (Katibu). Khatau aliongoza bodi hiyo Septemba mwaka jana kutangaza kutomtambua Prof. Lipumba kama ni mwenyekiti kwa kuwa alijiuzulu mwenyewe hadharani.

Prof. Lipumba alijiuzulu wakati chama kikikabiliwa na jukumu la kushiriki uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, hatua aloichukua ndani ya kupuuza nasaha za viongozi wenzake, wanachama na wapenzi wa chama hicho waliomtaka aahirishe uamuzi huo mpaka uchaguzi utakapomalizika.

Bodi ya Wadhamini ya CUF ina wajumbe tisa – watano wakitoka upande wa Tanzania Bara na wanne kutoka Zanzibar. Kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, bodi hiyo huteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi Taifa (BKUT).

Uongozi unapinga uhalali wa Bodi ya Wadhamini ya kundi linalomtii Prof. Lipumba kwa maelezo kuwa haikutokana na utaratibu wa kikatiba wa chama hicho ambao unaelekezwa kufanywa na Katibu Mkuu wa chama anayetambuliwa na kufanya kazi za chama kwa mujibu wa katiba ya chama hicho. Katibu Mkuu wa CUF ni Maalim Seif Shariff Hamad ambaye nafasi yake haijabishaniwa kwa vyovyote vile.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!