SIKU moja baada ya Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, kumtoa kwa nguvu Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika, Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), limeaalani kitendo hicho cha udhalilishaji kilichofanywa na Spika, anaandika Hamisi Mguta.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Kibamba aliamuliwa jana kutoka nje ya Bunge na kutohudhuria vikao saba vya bunge vinavyoendelea kutokana na kilichoitwa na spika kuwa ni utovu wa nidhamu uliofanywa na Mnyika kwa kubishana na kiti baada ya kutokea malumbano kati yake na spika.
Patrobas Katabi, Mwenyekiti wa Bavicha, akizungumza na wanahabari leo katika makao makuu ya chama hicho Kinondoni ameeleza kuwa Ndugai hakutumia busara kumtoa Mnyika bali alikuwa na jazba katika kutoa uamuzi huo.
“Tunasikitika na kitendo kilichofanywa na Ndugai, nadhani busara alizisahau nyumbani basi angejaribu hata kuzikumbuka kuliko kutoa uamuzi kama ule.
“Adhabu ya Mnyika kutoka nje ya Bunge ilitosha kabisa. Lakini si kumwambia asihudhurie vikao kwa siku kadhaa, ni wakati muafaka wa Ndugai kufanya upya marejeo ya uamuzi aliyoutoa ambao anadai ulikuwa wa jazba kuliko busara,” amesema Katambi.
Katambi amesema vita ya madini haiwezi kufanikiwa kwa kuwatoa wapinzani nje ya Bunge ambao wana mawazo mbadala ambayo yanaweza kuwasaidia kwa namna moja au nyingine.
Leave a comment