Wednesday , 17 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Bashe amchokonoa Rais Magufuli
Habari za SiasaTangulizi

Bashe amchokonoa Rais Magufuli

Hussein Bashe, Mbunge wa Nzega Mjini
Spread the love

SERIKALI ya Rais John Magufuli imeguswa kisawasawa, anaandika Jabir Idrissa.

Ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linaloendelea na mkutano wa bajeti mjini Dodoma, kumetolewa tuhuma kwamba idara yake ya usalama wa taifa, inatajwa katika matukio ya kutekwa na kupotea wananchi mbalimbali.

Kwa mujibu wa yaliyotokea bungeni asubuhi leo, ndani ya idara hiyo, inayotambuliwa kwa jina rasmi kama Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), kipo kikundi “kinaendesha matukio ya kutekwa na kupotea kwa watu.”

Hayo ni maelezo yaliyotolewa bungeni leo hii na Hussein Bashe, mwanachama maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na ambaye ni mbunge wa kuchagauliwa, anayewakilisha wananchi wa jimbo la Nzega Mjini.

Bashe, ambaye pia ni Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa kampuni ya New Habari Corporation (NHC) inayomiliki magazeti kadhaa likiwemo Mtanzania, pamoja na mtambo wa kuchapia, ameliambia bunge ni muhimu lichukuwe hatua kukabiliana na matukio hayo.

“Bunge na Serikali haiwezi kulifumbia macho jambo hili la haramu wakati Watanzania wanatekwa na watu wasiojulikana,” amesema akiashiria kumwelekea Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ambaye ndiye kiongozi mkuu wa taasisi hiyo mhimili wa dola.

Muda mfupi baada ya mbunge huyo kueleza hayo ukumbini, kwenye akaunti yake ya Twitter, kulikutwa ujumbe usemao,“Kuna watu wamenitumia ujumbe kwamba mimi ni kati ya watu 11 waliopo hatarini kufanyiwa vitu vibaya popote pale tulipo.”

“… kuna kikundi kilicho chini ya idara ya Usalama wa Taifa kinachoendesha matukio hayo na kinaharibu Serikali,” amesomeka.

Maelezo ya Bashe na kule kuamua kwake kutumia haki yake ya kikatiba na kikanuni kuyatoa ndani ya bunge, ni hali inayoongeza msukumo wa umma kufahamu tatizo kubwa hilo liliopo nchini na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kulikomesha.

Bashe anatoa maelezo hayo siku moja tu tangu itangazwe kuwa msanii Roma Mkatoliki, kwa jina halisi Ibrahim Mussa, pamoja na wasanii wengine watatu, wameonekana kituo cha polisi cha Oysterbay, wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, baada ya kuripotiwa kuwa walitoweka.

Roma alichukuliwa usiku wa Jumanne, tarehe 4 Aprili, akiwa kwenye studi za kurikodia muziki. Vifaa vyake vya kazi pia vilichukuliwa na watu waliosadikiwa kuwa watekaji wake.

Kutwa nzima juzi Jumamosi, Roma na wenzake walikuwa wakihojiwa na wapelelezi wa Jeshi la Polisi kituoni Oysterbay, lakini mpaka mchana huu, hakujatolewa taarifa yoyote ya kile kilichowasibu wasanii hao.

Polisi haijaeleza kama wasanii hao walikamatwa popote pale, na ni nani aliyewakamata na kama walikamatwa wakiwa gurupu; au walifikishwa na nani mikononi mwa jeshi hilo. Haijaelezwa pia walifikaje kituo hicho.

Hata ile ahadi aliyoitoa mwenyewe Roma kuwa leo Jumatatu, atakutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kueleza kinagaubaga kadhia hiyo, haijatekelezwa.

Wakati kungali na ukungu mzito wa taarifa za kilichotokea usiku huo Jumanne waliporipotiwa kutoweka, kinachoeleweka ni kwamba walionekana ndani ya muda ambao Paul Makonda, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, aliahidi.

Makonda ambaye anakabiliwa na tuhuma nzito ikiwemo ya kutumia madaraka vibaya kufanya matukio yenye sura ya jinai, alinukuliwa akisema katikati ya wiki iliyopita, kwamba “watapatikana kabla ya Jumapili.”

Alitoa kauli hiyo mbele ya wasanii waliokwenda kumuomba msaada wa kumtafuta Roma na wenzake.

Yeye akisema hivyo, Jeshi la Polisi, kupitia kwa Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, akizungumzia kutoweka kwa wasanii hao, alisema uchunguzi wa tukio hiolo unaweza kuchukua miezi miwili kukamilika.

Kamishna Sirro alisema kauli yake hiyo inatokana na uzoefu wa kufanya uchunguzi wa matukio yenye sura hiyo ya kijinai.

Lakini alipoulizwa anachukuliaje kauli ya Makonda, alisema “aulizwe huyo aliyesema.”

Akihutubia mkutano wa hadhara wa kwanza tangu afukuzwe uwaziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, Nape Nnauye, alisema mwishoni mwa wiki kuwa kuna umuhimu wa kuundwa tume maalum ya kuchunguza matukio hayo.

Alipofanya mahojiano maalum na gazeti la MwanaHALISI, Nape, mbunge wa Mtama mkoani Lindi, alimtaja Makonda kuwa mtu anayepaswa kuchunguzwa kwa kuwa kauli yake inajenga taswira pana kuwa anajua kilichotokea.

“Jambo hili linachafua Serikali, linachafua Chama cha Mapinduzi (CCM) na linachafua sura ya Tanzania ulimwenguni. Sikiliza kaka hii michezo yote imechezwa na Mkuu wa Mkoa (Paul Makonda),” alisema Nape.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Samia arejesha mikopo ya 10%, bilioni 227.96 zatengwa

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amerejesha utaratibu wa utoaji mikopo...

Habari za Siasa

Rais Samia amfariji mjane wa Musa Abdulrahman

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan leo Jumanne amempa pole Mwanakheri Mussa...

Habari za Siasa

Nape: Wanasiasa, wanahabari, wafanyabiashara mteteeni Samia

Spread the loveWaziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,...

Habari za Siasa

CAG: TAWA imegawa vibali vya uwindaji bila idhini ya waziri

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

error: Content is protected !!