BARAZA Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinafanyika leo Jumatatu tarehe 3 Agosti 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kikao hicho, kinafanyika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam kikiwa na kazi ya kupendekeza majina ya wagombea urais wa Tanzania, mgombea mwenza na wa Zanzibar.
Pia, baraza hilo litapendekeza, Ilani ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.
Tayari wajumbe wameanza kuingia ukumbini kuhudhuria mkutano huo huku majina ya Tundu Lissu na Lazaro Nyalandu yakisikika zaidi kati ya wagombea saba wanaowania kupitishwa na chama hicho kugombea urais wa Tanzania.
MwanaHalisi Online lipo ukumbini kufuatilia kinachoendelea na litakuletea taarifa na habari mbalimbali.
Baadhi ya wajumbe waliozungumza na MwanaHALISI Online wakiomba hifadhi ya majina yao wamesema, kuna mchuano mkali kati ya Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara na Nyalandu, mwenyekiti wa chama hicho kanda ya kati.
“Aise, sijajua nani ataibuka kati ya Lissu au Nyalandu. Ila dalili ukiona kama Lissu anapenya lakini Nyalandu hayuko nyuma sana. Amejipanga vizuri na lolote linaweza kutokea,” amesema mjumbe huyo wa baraza kuu kutoka kanda ya Serengeti
Mjumbe wa kanda ya Pwani amesema,”hakuna ubishi katika hili, Lissu ndiye tunayemta. Anayeweza mikiki mikiki.”
Hadi saa 6:45 mchana, kikao hakijaanza.
Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online, MwanaHALISI TV, kwa habari, taarifa mbalimbali
Safari njema ya uchaguzi