MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ameitaka Tume ya Haki za Binadamu Tanzania kufanya wajibu wake wa kuwaelimisha wananchi kuhusu haki ili kuelewa haki zao pindi wanapokuwa na matatizo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar…(endelea)
Akizungumza ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar alipotembelewa na ujumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Mwanyekiti wake, Jaji mataafu Mathew Pauwa Mhina, Balozi Seif amesema, Zanzibar imekuwa na matukio mengi ya unyanyasaji wa kijinsia jambo ambalo Tume ya Haki za Binadamu inapaswa kuwaelimisha wananchi kuhusu upatikanaji wa haki.
Pia, kuwaeleza madhara ya unyanyasaji wa kijinsia, kwani kufanya hivyo kutaisaidia Serikali kuu kupata nguvu na uwezo wa ziada wa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi hususan wanawake, watoto na hata wananchi wenye mahitaji maalum.
“Tume ya Haki za Binadamu ina kazi kubwa katika kutekeleza majukumu yake kwa upande wa Zanzibar kutokana na migogoro na changamoto nyingi zinazowakabili wananchi hali inayosababisha mitafaruki na mifarakano miongoni mwa jamii yenyewe.”
“Kwa hiyo, nyie kama tume, waelimisheni wananchi wa Zanzibar kufahamu sehemu ya kupata haki zao, lakini pia nyie mna jukumu kubwa la kusaidia kutatua migogoro na mifarakano inayotokea ya wananchi kusumbuliwa katika maeneo tofauti nchini,” amesema Balozi Seif .
Aidha , Balozi Seif ameueleza uongozi wa Tume hiyo yapo matatizo mengi yanayowakabili wananchi hasa wanawake ya kupewa ovyo talaka na matokeo yake kutelekezwa na waume zao sambamba na kuachiwa watoto bila ya huduma hali ambayo inakuwa ni kazi kwao kutimiza majuku ya kulea watoto.
Ametahadharisha tabia hiyo iliyoanza kuota mizizi kwa baadhi ya wanaume wasiojali utu wa binadamu ni ya hatari kwa mtoto kwa vile inawakosesha haki zao za msingi kama vile kupata elimu na huduma za afya kwa sababu ya kutokuwa na ushirikiano wa kimalezi baina ya pande mbili.
Pia, alieleza suala la udhalilishaji wa wanawake na watoto linaloikumba Dunia, hivyo watendaji na viongozi wa Tume wa lazima wajikite zaidi kushirikiana na taasisi za utoaji haki pamoja na wananchi katika vita ya kukabiliana na tatizo hilo linalochangia kupotoshwa kwa maadili ya jamii.
“Kwa sasa, masuala ya wanawake na watoto kudhalilishwa limekuwa ni jambo ambalo duniani kote ni mtihani, kwa hiyo Tume ya Haki za Binadamu jikiteni zaidi katika kufanya upembuzi wa suala hili.”
“Ili taasisi za utoaji haki na Serikali ipate kuwasaidia wananchi kupitia nyinyi, lakini pia msisahau kutoa elimu kuhusu haki zao kwani hiyo itawasaidia kupambana na waharifu na wavunjaji wa haki za binadamu,” alisema Balozi Seif.
Akijibu ombi la Tume ya Haki za Binaadamu la kupewa jengo la Ofisi kwa upande wa Zanzibar, Makamu huyo wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameshauri ujumbe wa Tume kuwa na mpango wa kujenga majengo ya kudumu ya ofisi zake Visiwani Zanzibar kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa maeneo ya ujenzi huo wakati wowote pale itapohitajika kutekelezwa mpango huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Mhina, alisema Taasisi hiyo ni chombo cha umma kilichoundwa kusimamia upatikanaji wa haki za binadamu ili kusimamia utawala bora hapa nchini na kuwawezesha wananchi kupata haki zao za msingi pale inapohitajika
“Tume ya haki za binadamu imeundwa na viongozi wake waliteuliwa na Rais John Pombe Magufuli ili kutetea haki za Watanzania bila kujali imani zao.”
“Kwa hiyo, utekelezaji wa majukumu yake upo kwa ajili ya wananchi wanaopokonywa haki zao, lakini pale ambapo watendaji wa Tume wakienda tofauti ni masuala ya kibinadamu ya kuteleza katika utekelezaji wa majukumu yao,” amesema Jaji Mhina
Aidha, Tume ya Haki za Binadamu Tanzania kupitia Mwenyekiti wake iliipongeza Serikali ya Jamahuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa inayoifanya ya kuhudumia wananchi jambo ambalo uongozi wa Tume hiyo unaliunga mkono.
Makamishina wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania waliteuliwa na Rais Magufuli mnamo tarehe 19 Septemba Mwaka 2019, ili kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji wa haki kwa watanzania katika maeneno yote ya Kijamii.
Leave a comment