Babu Duni, Selasini watofautiana NCCR-Mageuzi kushirikiana na Chadema, ACT-Wazalendo

Spread the love

MAKAMU Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo-Zanzibar, Juma Duni Haji maarufu ‘Babu Duni’ amekitaka Chama cha NCCR-Mageuzi kukubali kushirikiana na vyama vingine vya upinzani nchini Tanzaia kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea)

Babu Duni amesema, ili kukishinda chama tawala cha mapinduzi (CCM) ni lazima vyama hivyo vishirikiane licha ya magumu ambayo NCCR-Mageuzi iliyapata katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa tarehe 25 Oktoba 2015.

Hata hivyo, Mbunge anayemaliza muda wake wa Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, Joseph Selasini amesema, NCCR-Mageuzi haipingi ushirikiano lakini baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wanarudisha nyuma mapambano ya mageuzi nchini humo.

Selasini amemtuma Babu Duni kwa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania cha Chadema kwamba wao NCCR-Mageuzi, wako tayari kushirikiana na endapo wakishindwa kuelewana viongozi wa juu, watarudi kwa wananchi kuwaeleza nini cha kufanya.

Hayo yamejili leo Ijumaa tarehe 7 Agosti 2020 katika Mkutano Mkuu wa NCCR-Mageuzi unaofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubile jijini Dar es Salaam ambapo wawili hao wamepewa fursa ya kuzungumza na Babu Duni amekuwa wa kwanza kisha akafuatia Selasini.

Katika mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa siasa, dini, asasi za kiraia na taasisi binafasi akiwemo Joseph Butiku, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Akizungumza katika mkutano huo, Babu Duni amesema, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amekuwa akisema “Mama Tanzania, lakini wengine wanatutenga, sasa hii mama Tanzania isigeuke wengine mama wa kambo.”

Amesema, amefurahi kumwona katika mkutano huo, Mzee Butiku akisema, “wakati Mzee Butiku wanaongoza nchi hii na Mwalimu Nyerere, walidai uhuru kwa sababu, kulikuwa na utawala unaowaonea babu zetu.”

Babu Duni amesema, babu hao walipigania uhuru ambao umegawanyika katika hatua tatu.

Mosi, ni kuondoa utawala wa kigeni, “Zanzibar tulikuwa tunatawaliwa na waarabu na bara tunatawaliwa na Waingereze sasa hawapo. Mwaka 1961 ukapatikana uhuru wa Tanganyika na mwaka 1964 Zanzibar yakapatikana Mapinduzi.

 

“Babu zetu walipambana ili kizazi cha leo, sisi tuishi maisha ya uhuru, salama, kupendana, maisha ya kujua sisi sote tuna haki, hiyo ilikuwa lengo la babu zetu.”

Babu Duni amesema, “sasa baada ya kupata uhuru wetu, ilifuata uhuru wa kukusanyika na kufanya uamuzi wa kile tunachokitaka, kutoa maoni, kukosoa, kushauri, hiyo ilikuwa hatua ya pili.”

Ametaja hatua ya tatu, “ni kuwa na uwezo wa kauli, unasimamiwa na uchaguzi wa demokrasia, uchaguzi wa kwenda katika kisanduku cha kura na kusema huyu tunakubali na huyu tunamkataa, aliye na wengi anaambiwa tangulia kwenye serikali utuongoze na baada ya miaka mitano tunarudi tena kwenye kisanduku cha kura.”

“Tuko kwenye vyama vingi, lakini kwa kipindi furani, mambo hayajaenda vizuri, lakini pamoja na mambo mengi tunayofanyiwa na Serikali, hatuwezi kukataa mengine kuna shida,” amesema mwanasiasa huyo mkongwe nchini

“Sasa NCCR, Chadema, ACT tunakwenda kuchagua viongozi, tunaomba waliopo kwenye utawala, watuache tuchague viongozi tunaowataka, kwa hiari yetu na yule tunayemkubali aendeshe nchi hii. Baada ya miaka mitano, turudi tena tukampime je anafaa au hafai.”

Babu Duni akagusia ushirikiano wa vyama vinne vya Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 akisema, “tulifanya vizuri kama vyama vya upinzani na ninajua katika wahanga walioumia vibaya sana ni chama cha NCCR-Mageuzi.”

“Si vizuri kusema machungu uliyokuwa ukiyapata (Mbatia), mengine tulikuwa tunanong’ona lakini mimi nasema no Pain no gain, (hakuna kufanikiwa bila kuumia). Sasa sisi ACT Wazalendo, tunaamini katika ushirikiano, pamoja na machungu mliyonayo, ili kushindana na chama tawala, tunahitaji ushirikiano na katika hilo mlizingatie katika mazungumzo yenu.,” amesema

Katika uchaguzi huo wa mwaka 2015, Babu Duni alikuwa mgombea mwenza wa urais wa Tanzania amesema “mimi nina miaka 20 nikiwa upinzani, kilichoendelea kubaki, babu zetu walitupigania tubaki na uhuru wetu. Tunahitaji mabadiliko na mabadiliko makubwa ni kulinda utu wetu.”

Tayari vyama vya ACT-Wazalendo na Chadema viko katika majadiliano ya kushirikiana kuelekea uchaguzi huo mkuu.

Selasini: Tuko tayari kushirikiana lakini…

Baada ya kumaliza kuzungumza Baba Duni, alifuatia Selasini kuzungumza kwa niaba ya wabunge wanaomaliza muda wake.

Selasini amerejea NCCR-Mageuzi akitokea Chadema miezi ya hivi karibuni akianza kuzungumza kwa kurejea jinsi chama chake kipya kilivyoanza harakati za mageuzi tangu miaka ya tisini.

“Tarehe 11 Juni 1991, wanamageuzi tulikutaka katika ukumbi huu (Diamond Jubilee), tukiidai Serikali mageuzi na baada ya mkutano ule, ulizaliwa vyombo viwili NCCR -baraza la kitaifa kwa ajili ya kutafuta marekebisho ya katiba.”

Selasini amesema “wanaosema ajenda ya katiba ni yao wanakosea, imeanza siku nyingi na katika ule mkutano kilizaliwa chombo kinaitwa Kama Huru. Nacho kilikuwa chombo cha kupigania katiba ya Zanzibar. Nafurahi tunafanyia mkutano huu hapa kama kufufua mageuzi na tupo na tunafufua mageuzi upya.”

Huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo, Selasini amesema “upinzani siyo uadui na kwa sababu hiyo hatuna sababu ya msingi ya kugombana wenyewe kwa wenyewe badala ya chama tawala. Anayetumia hoja kugombana anakuwa hana hoja, wanyama ndiyo wanafanya hivyo. Vyama hivi ni taasisi za umma, vyama vya Watanzania na kutoka katika vyama hivi ndiyo tunapata viongozi.”

“Kwa hiyo ni lazima lile linalosemwa vizuri kwa manufaa ya Watanzania liungwe mkono kama hutaki unataka Watanzania wasilipate,” amesema

Kuhusu ushirikiano, Selasini amesema “mwaka huu ni wa 28 tangu tumeanza mageuzi na tunakwenda katika uchaguzi huu mara ya sita (uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi ulianza mwaka 1995). Ni vizuri vyama vyote tufanye tathimini tuko wapi, tunatoka wapi na tunakwenda wapi. Mbona kama ni mtoto amekuwa mkubwa.”

“Kuna mambo yanatoka kwa wenzetu ambao hatuna mamlaka nayo, hili alilosema Duni kwa nini hatushirikiani, ubinafsi, uroho wa madaraka, sasa tusiilaumu serikali kwamba inatugawa itutawale vizuri.”

Selasini amesema “Duni yale mambo yaliyotokea na vifo kule Zanzibar, lakini ilitengenezwa serikali ya umoja wa kitaifa, Maalim Seif (Sharif Hamad) ambaye ni kiongozi wa kisiasa mvumilivu nafikiri kuliko wote, wakaunmda serikali ya umoja wa kitaifa, sisi huku upinzani tukasema ni CCM B.”

Amesema, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, walikwenda kumpigia magoti Maalim Seif ili washirikiane nay eye alikubali huku akikumbushia kile kilichomtokea Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo alipofukuzwa ndani ya chama chake mwaka 2013 kwa tuhuma za kutumika na Serikali “lakini leo hii Zitto ameanzisha chama (ACT-Wazalendo) na leo hii Zitto anaombwa ushirikiano (na Chadema).”

“Mapema mwaka huu, Rais aliwaalika Ikulu Mbatia, Profesa (Ibrahim) Lipumba na Maalim Seif wakasema Mbatia ni CCM B, sasa katika upinzani kuna watu wanaturudisha nyuma kwa maslahi yao wenyewe. Sasa mimi nasema hakuna mahali popote nimesoma katika NCCR hakuna panapokataa ushirikaino.”

Selasini amesema “Duni nakutuma, Mbowe akiwa jimboni kwake Hai, alisema Chadema hakipo tayari kushirikiana na chama kilichosalimu kwa Serikali ikiwemo NCCR, sasa mwambie hivi sisi tupo tayari kushirikiana kwani tunaijua agenda ya ushirikiano.”

“Ushirikaino ni utu, katiba, mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora, kwa hiyo, mwambie (Mbowe) sisi tupo tayari kushirikiana na yoyote na sisi hatuko chama tawala na sisi ni wapinzani na niwaanzilishi wa mageuzi na tulianza mageuzi wengine wakiwa katika biashara zao,” amesema huku akishangiliwa.

“Pamoja na tabu tunazozipata kutoka Chama Cha Mapinduzi, lakini sisi wenyewe tunarudishana nyuma kwa propaganda za kijinga na kitoto. Chama kitafanya uamuzi kwa hoja iliyoletwa na Duni, lakini ikishindikana, Watanzania wanatufahamu sisi,” amesema

Selasini amesema kama hawatafikia maelekewano ya ushirikiano, wakirudi katika majimbo na kata, wataanzisha ushirikiano ambao “ukifika katika jimbo ambalo mgombea wako ni dhaifu na wa Chadema ananguvu mpigie kampeni huyo, ukienda katika jimbo ACT na kukuta mgombea ana nguvu na Chadema ni dhaifu, mpigie kampeni huyo.”

“Wakikataa ushirikiano huku juu, sisi tunauhamishiwa kwa wananchi. Ushirikiano usiishie hapo.”

Mwanamageuzi huyo, ametoa rai kwa vyama vya siasa, kukubali kurejesha moyo konde na kuwapokea vijana waliokuwa ndani ya vyama hivyo kisha kuhamia vyama vingine kuwapokea na kuwalea ili waje kuwa viongozi wa kesho.

“Ninaviomba vyama vyote, NCCR, CCM, Chadema tusiwatupe vijana hata vijana walihama wakaenda CCM wakaenda kushindwa kura za maoni, walitoka NCCR na wakashindwa, tunajua kama vijana wanavyotafuta wachumba, tunawaomba NCCR, Chadema na CCM fungueni milango tuwachukue, tuwalee, tuwarekebishe,” amesema

Mkutano huu mkuu utateua mgobea urais wa Tanzania na Zanzibar. Waliojitokea kuwania nafasi ya urais wa Tanzania wako watatu, Yeremia Maganja, Peterson Mushenyera, Abubakari Juma huku Haji Hamisi.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online, MwanaHALISI TV na mitandao yetu ya kijamii kwa taarifa na habari mbalimnali

MAKAMU Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo-Zanzibar, Juma Duni Haji maarufu ‘Babu Duni’ amekitaka Chama cha NCCR-Mageuzi kukubali kushirikiana na vyama vingine vya upinzani nchini Tanzaia kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea) Babu Duni amesema, ili kukishinda chama tawala cha mapinduzi (CCM) ni lazima vyama hivyo vishirikiane licha ya magumu ambayo NCCR-Mageuzi iliyapata katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa tarehe 25 Oktoba 2015. Hata hivyo, Mbunge anayemaliza muda wake wa Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, Joseph Selasini amesema, NCCR-Mageuzi haipingi ushirikiano lakini baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wanarudisha nyuma mapambano ya mageuzi…

Review Overview

User Rating: Be the first one !

About Mwandishi Wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!