Kisa cha Panya, Kuku, Mbuzi na Ng’ombe

NYUMBANI kwa mwanadamu uliwekwa mtego wa panya, lengo likiwa kumnasa panya. Anaandika Babu Jongo … (endelea).

Panya alipoona mtego akamuambia kuku amsaidie kuutegua, kuku akakataa, akasema hakutegwa yeye kwa hiyo haumuhusu.

Panya akamfuata mbuzi, akamwambia amsaidie kuutegua, mbuzi akasema haumuhusu kwa kuwa hakutegwa yeye.

Panya hakukata tamaa, akamfuata ng’ombe akamuomba amsaidie kuutegua mtego, akiamini nguvu za ng’ombe hata kama akiukanyaga tu mtego utavunjika.

Ng’ombe akacheka kwa dharau akasema haumuhusu, akamjibu panya apambane na hali yake.

Siku moja usiku kwenye mtego aliotegwa panya akanasa nyoka, baba mwenye nyukba aliposikia kishindo kwenye mtego akajua panya tayari ameshanasa.

Baba akamtuma kijana wake akamuue panya aliyenasa kwenye mtego, kijana alipokwenda kichwakichwa akagongwa na nyoka, sababu mtegoni alinasa nyoka na sio panya.

Kijana akafariki baada ya kugongwa na nyoka. Asubuhi kulipokucha watu wakaanza kujaa msibani.

Kwa kuwa watu walikuwa wengi kiasi, usiku akachinjwa kuku ili kuwapa watu kitoweo.

Siku ya pili ya mazishi akachinjwa ng’ombe ili kukidhi haja ya kitoweo na siku ya tatu ya kuondoa tanga akachinjwa mbuzi.

Kumbuka mtego alitegwa panya, alipowaambia kuku, mbuzi na ng’ombe wamsaidie kuutegua kutokana na uwezo wao wakakataa sababu hawakutegwa wao.

Lakini sasa wote hao waliojiona hawahusiki wamechinjwa na panya bado yuko hai.

Wakati raia wa kawaida wanatekwa na kupotezwa kuna watu walisema “shauri yao sisi hayatuhusu.”

Wakati Ben Saanane alipotekwa wengine wakapaza sauti za kutaka haki za raia zizingatiwe, lakini wengine wakasema watajuana wenyewe na Chadema wenzao.

Aliposhambuliwa Tundu Lissu, wapo waliosema amezidi kusema hovyo, wacha yamkute.

Akapotezwa mwandishi Azory Gwanda, wengine wakasema watajuana na waandishi wenzao waliozidi kufukunyua yasiyowahusu.

Akatekwa Roma Mkatoliki, upande mmoja wakapiga kelele aachiwe akiwa hai wengine wakasema afe kabisa, eti nani alimtuma aimbe siasa za kukosoa.

Watu wakaendelea kutekwa hasa upande wasiounga mkono chama kilichopanga Ikulu, na wale wanaojiona wenye chama na nchi wakafurahia.

Akakamatwa Manji, mwenyekiti wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, akatupwa mahabusi, huyu ni mwanaccm kindakindaki, lakini baadhi ya mashabiki wa upande wa pili wakafurahia, wakatamani hata afilisiwe au afe kabisa, wengine bila kujali kuwa ni mwanaccm mwenzao.

Leo ametekwa Mohammed Dewj (MO), mwanaccm mwengine, mshirika wa karibu wa viongozi wengi serikalini na chamani.

Huyu ni mwanahisa kiongozi kwenye klabu ya Simba ya Dar es Salaam, ameshawahi kuwa mfadhili wa miaka mingi kwenye klabu hiyo.

Nuru inayowaka Simba kwa sasa inatokana na mkono wa MO, bahati mbaya tena yanatokea yaleyale.

Kuna mashabiki wa upande wa pili wanaomba MO asipatikane mpaka Ligi iishe au asipatikane kabisa akiwa hai.

Kutekwa kwa MO wao hakuwahusu, bado wanaamini wao wako salama.

Ni akili zilezile zilizotumiwa na kuku, mbuzi na ng’ombe, kuona mtego hawakutegewa wao.

Nani aliamini kama iko siku MO atatekwa kwenye ardhi ya Tanzania, tena asubuhi kweupe?

Nakuomba Mungu umsaidie MO apatikane akiwa hai na afya yake.

Lakini kipindi hiki ni muhimu kupata somo kwa wale waliokuwa wanajiona matukio haya hayatawagusa.

Ukiwa raia wa kawaida, mfuasi wa chama fulani, kiongozi wa chama, taasisi, serikali au hata dola – pinga, zuia upuuzi huu, jua nawe hauko salama hata kama unahusika na vitendo hivi vya utekaji.

BringBack MO Dewj & Others!

Mafia inasubiri ya MV Nyerere?

NAWAKUMBUSHA tu wale mahodari wa kutuma salaam za rambirambi, na wakukataza majanga ya ajali yasigeuzwe mtaji wa kisiasa,  wakumbuke na Kisiwa cha Mafia kabla ya janga jingine kutokea. Anaandika Babu Jongo…(endelea).

Kwa miaka zaidi ya 50 tangu tupate uhuru, bado wakazi wa kisiwa cha Mafia kilichopo mkoani Pwani wanatumia usafiri huu wa boti za mbao, zisizokuwa na usalama wowote kutoka na kuingia kisiwani humo.

Boti hizi zenye kuhatarisha maisha ya wananchi wa Mafia na wageni wengine, ndio kiunganishi kikubwa kati ya kisiwa cha Mafia na maeneo mengine kama Dar es Salaam na hata wilaya nyingine za mkoa wa Pwani.

Kila siku boti hizi husafiri umbali wa km 30, kutoka Kisiwani Mafia mpaka Nyamisati wilayani Kibiti, huku zikiwa na uwezo wa kubeba wastani wa watu 45 – 70.

Wabunge wote waliopata kuongoza jimbo la Mafia walihaha kupata kivuko cha uhakika bila mafanikio.

Hata mbunge wa sasa ameshafanya juhudi kubwa kuiomba serikali kuitazama Mafia kwa jicho la huruma bila mafanikio.

Ameshawahi kuiomba serikali ya chama chake impe hata lile boti lililokuwa linachukua saa tatu kusafisha abiria kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, lakini akaambulia matupu.

Naikumbusha tu serikali, kwamba rambirambi zao wasichange mapema wanunue boti ya uhakika kusafirisha wananchi wa Mafia, ambao kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, kisiwa hicho kilikuwa na wakazi wapatao 52,000.

Naamini kwa jitihada za mheshimiwa rais kutoa elimu bila malipo, watu watakuwa wameongezeka sana hasa baada ya rais kusema wazaane tu kwa kuwa elimu ni bure.

Toeni rambirambi mapema mnunue kivuko kuwavusha wakazi wa Mafia, msisubiri kuchanga rambirambi baada ya kufa kwa uzembe!

Maalim Seif kumkwamisha Dk. Magufuli

SERIKALI ya Rais John Magufuli ndani ya mwaka mmoja kutoka sasa itaingia kwenye wakati mgumu wa kujiendesha kutokana na masharti magumu waliyoweka wahisani ili kurejesha misaada, anaandika Yusuf Aboud.
Mtoa taarifa ndani ya serikali na Benki Kuu (BoT) ameeleza kwamba, tayari wataalamu  wameonya juu ya kuibuka kwa mfumuko wa bei pia ….
Kwa habari zaidi soma gazeti la MwanaHALISI la leo

Kubenea ‘kumvua nguo’ Masaburi

MWANDISHI wa habari mahiri nchini, Saed Kubenea, ameteuliwa na Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwa mgombea ubunge wa jimbo la Ubungo, jijini Dar es Salaam. Anaandika Yusuf Aboud … (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya Chadema zinasema, Kubenea ameteuliwa kupeperusha bendera ya Chadema kwa mwavuli wa UKAWA baada ya kushinda kura za maoni, wiki mbili zilizopita.

Kubenea ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited, wachapishaji wa magazeti ya MwanaHALISI, MSETO na gazeti linatoka kwa njia ya mtandao – MwanaHALISI Online pamoja na mtandao wa MwanaHALISI Forum, anatarajiwa kupambana na Dk. Didas Masaburi, anayewania jimbo hilo kupitia CCM.

Akizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti hili, Kubenea amesema, amejitosa katika kinyang’anyiro hicho siyo kushiriki, ila kushinda.

“Sikuja hapa kushiriki uchaguzi. Nimekuja hapa kushinda,” ameeleza Kubenea, akiwa katika ofisi za Chadema, jimbo la Ubungo.

Amesema, “Ninamfahamu mshindani wangu (Masaburi). Ninajua udhaifu wake, makandokando yake na zaidi tuhuma zinazomkabili. Muda ukifika, nitamvua nguo.”

Kubenea, mwandishi wa habari anayeheshimika nchini, anapewa nafasi kubwa ya kushinda jimbo hilo.

Familia ya Kikwete yaumbuka

FAMILIA ya Rais Jakaya Kikwete, imepata pigo baada ya Bernard Membe kupigwa mweleka katika kinyang’anyiro cha kusaka urais. Anaandika Yusuf Aboud … (endelea).

“Kwa zaidi ya miaka minane, familia ya Rais Kikwete ikiongozwa na mwanawe, Ridhiwani Kikwete na mkewe, Salma Kikwete, ilikuwa inahaha kutaka kumfanya Membe kuwa rais,” anaeleza mmoja wa viongozi wa juu ndani ya CCM.

Anasema, “…waligombana na kila aliyewapinga. Kwa kweli, familia hii ya Rais ililenga maslahi binafsi yanayotokana na kutaka kulinda wizi na uhalifu walioufanya nchini.”

Membe mwanasiasa aliyetokea katika ukachero, alipigwa mweleka katika Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Aliagushwa na John Magufuli, Balozi Amina Salum Ali na Dk. Asha-Rose Migiro.

Kabla ya mchuano huo, Membe alifanikiwa kupenya kwenye tundu ya sindano baada ya kambi ya Edward Lowassa, mwanasiasa anayeaminika kuwa nguvu ndani ya chama hicho, “kuamua kufa naye.”

Taarifa zinasema, nguvu ya Lowassa ndiyo iliyosababisha Membe kushindwa.

Mkutano mkuu wa CCM unaoendelea mjini Dodoma, unatarajiwa kumtangaza John Pombe Magufuli kuwa mgombea wake wa urais.