Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Askofu Munga amvaa Musiba, adai anavuruga nchi
Habari za SiasaTangulizi

Askofu Munga amvaa Musiba, adai anavuruga nchi

Askofu Stephen Munga
Spread the love

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Stephen Munga, ameonya kuwa kitendo cha Cyprian Musiba, kukashifu na kutuhumu viongozi wakuu wa wastaafu, kinamega taifa na kwamba yeye amejitolea kumkabidili kwa gharama yeyote ile, ili kulinda umoja na mshikamano nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Katika andishi lake alilolisambaza kwa umma kupitia mitandao ya kijamii, Baba Askofu Munga anasema, kama kuna makosa yaliyofanywa na viongozi hao, basi washughulikiwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

“Kama wapo baadhi ya viongozi wetu walioihujumu nchi, basi wachukuliwe hatua. Siyo kumuacha Musiba kuwa kama mahakama ya kutuhumu na kuhukumu. Hilo haliwezekani,” ameeleza Askofu Munga. 

Kuibuka kwa Askofu Munga kumekuja siku nne tangu Musiba anayejipambanua kama mwanaharakati huru na mtetezi wa Rais Magufuli, kuibuka na kutuhumu Rais Jakaya Kikwete; Benjamin Mkapa na Ali Hassani Mwinyi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Alhamisi iliyopita jijini Dar es Salaam, Musiba amesema, “ukimuondoa Mwalimu Julius Nyerere, wengine wote walioshika nafasi hiyo,  walikuwa wezi watupu.”

Kwa mujibu wa Musiba, viongozi hao watatu – Mkapa, Mwinyi na Kikwete – pamoja na wenza wao, walitumia ofisi za umma (Ikulu), kujitajirisha binafsi; na waligeuza ofisi hiyo, kuwa kama pango la kujipatia utajiri.

Alisema, “Watanzania wamepata rais bora na ambaye hana harufu ya wizi, amekuja anataka kufumua mifumo ya wizi, watu wanalalamika.”

Musiba anasema, “siwashambulii binafsi. Sina ugomvi nao, bali huo ndio ukweli. Viongozi hawa waliitumia Ikulu kujitajirisha. Hata wake zao, walianzisha taasisi kwa lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya matumizi yao.”

Kufuatia tuhuma hizo zinazovurumushwa na Musiba, dhidi ya marais hao wastaafu, Askofu Muga anasema, “miaka ya 2010s, nilikuwa nchini Ghana. Aliyekuwa rais wa nchi hiyo wakati huo, Prof. John Atta Miller, alianzisha mahakama maalum ya kushughulikia wahujumu uchumi.

“Wote waliotuhumiwa walitokea mbele ya jopo la majaji kujibu tuhuma zao. Ulikuwa mchakato na mfumo rasmi wa kushughulika na masuala hayo. Nilifuatilia sana kesi zile na niliona kuwa utaratibu uliofuatwa ulikuwa wa wazi (transparent) na ulikuwa rasmi. Sheria zilifuatwa na kila mtuhumiwa alipewa haki ya kusikilizwa.” 

Askofu Munga anasema, “iwapo utaratibu wa aina hiyo ungefuatwa nchini, nisingekuwa neno. Lakini hili la kumuacha Musiba kama mahakama huku nchi mzima ikimtazama, hapana.  Hatua ya Musiba, kutuhumu viongozi wakuu wa nchi na watu wengine, inaliweka taifa zima katika mawimbi ya uharibifu.” 

Anaongeza: “Mimi sijui ni nani anampa kinga Musiba, lakini niseme tu kwamba kwa muelekeo huu hakuna aliye salama. Musiba ni kiumbe hatari kwa umoja, usalama, na mshikamano wa taifa. Musiba anafifisha uwezekano wa uzalendo kwa nchi na taifa letu. Iwapo anachokifanya ni mkakati uliopangwa kwa malengo yeyote, basi malengo hayo yatafeli. 

“Hatuwezi kuona viongozi wa taifa hili waliotumika hadi kukabidhi madaraka kwa utawala huu wakinyanyaswa na mtu asiye na heshima. Tumevumiliana mengi kwa ajili ya ustawi na amani ya nchi hii, lakini Musiba anavuruga nchi. HAPANA! HAPANA! HAPANA!”

Soma hapa chini andishi kamili na Baba Askofu Munga: 

Je, Musiba amekuwa Mflame wa Wafalme na Bwana wa mabwana?

Ikiwa ni kweli. Narudia tena: Ikiwa ni kweli, kwamba Cyprian Musiba, ameanza kuwashambulia marais waliotangulia basi tumeingia katika tatizo kubwa. Nasema haya kwa sababu kuu zilizo dhahiri. 

Kwanza, niseme kwamba mimi binafsi sijawahi kumsema rais yeyote wa taifa langu hadharani! Nimefanya kazi wakati wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete. Nilikuwa na desturi ya kuwaona kila nilipokuwa na neno la kuongea nao na walinisikiliza kwa uvumililivu wote. 

Mazungumzo yetu hayakuwa mepesi wakati mwingine, lakini tulifikia mwisho mwema. Hawajawahi kunitishia uhai wangu na zaidi sana waliweka ulinzi ili niwe salama.  Sijawahi kumvunjia heshima rais yeyote wa taifa langu na kwa hakika hata Rais wangu wa sasa, John Pombe Magufuli, sitamvunjia heshima. 

Nimefanya hivyo kwa kuzingatia hatari na athari zinazoweza kutokea iwapo rais wa nchi atavunjiwa heshima. Taasisi ya Uraisi lazima iheshimiwe na lazima ilindwe kwa ajili ya umoja na ustawi wa nchi na taifa. Kwa hali hiyo, nimekuwa mtumishi na mwanaharakati wa uzalendo wa nchi na taifa langu kwa miaka mingi kuliko Musiba.

Rais Magufuli hakuingia madarakani kwa Mapinduzi, bali kwa kukabidhiwa ofisi na watangulizi wake kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM). Niweke wazi jambo moja. 

Kwamba, wakati Rais Kikwete anakwenda Dodoma kwenye mkutano mkuu wa kuchagua mgombea wa chama chake, alitokea mkoani Tanga na alifanya mazungumzo nami. Sikilizeni hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM ambapo alitaja kwa kifupi maoni yangu na kunitaja kwa jina. Acheni mambo yenu yanayochanganya wananchi! 

Nchi hii haikuzaliwa baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 na naweka mambo haya wazi ili anayetaka kunikamata afanye hivyo. Tena nchi hii haiongozwi na kuwa salama kutoka Ikulu na Usalama wa Taifa (TISS). Nchi na taifa hili ni moja kwa sababu, wananchi wake walishirikishwa katika ulinzi na maendeleo ya taifa lao. 

Mimi nikiwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Lund, nchini Sweden, nilipanga kuonana na Baba wa taifa Mwalimu Nyerere. Kwa mapenzi ya Mungu alimuita mbinguni kabla hatujaonana na alizikwa wakati ningali nje ya nchi; kwa hiyo sikushiriki hata mazishi yake.

Nilitaka kuonana naye kwa lengo la kuzungumzia hatma ya nchi yetu kwa wakati ule. Tunaipenda nchi yetu na sisi ni wazalendo waliokubuhu juu ya taifa hili kuliko huyo Musiba anayejifanya ni mwana harakati wa Rais. 

Wala Rais wa awamu ya tano, hakuingia madarakani kwa mapinduzi, bali kwa utaratibu wa vikao rasmi vya CCM vya kuchagua wagombea wake. Katika mshikamano na umoja wake, CCM wakampigania mgombea wao kushinda nafasi ya urais na akashinda. 

Nijuavyo mimi, hapajawahi kuwa na msuguano juu ya urais wa Mhe. Magufuli isipokuwa matatizo yalijitokeza baada ya urais wake akiwa ofisini. 

Tena niseme wazi kwamba watu walikuwa na matumaini makubwa kwamba Rais Magufuli angeliunganisha na kuliletea maendeleo taifa letu na kujenga ustawi na demokrasia zaidi kuliko tawala zilizopita. 

Lakini katika kufanya hayo ni pamoja na kutambua kwamba amekalia kiti alichokabidhiwa kwa urithishaji wa madaraka na sio kwa mapinduzi ya nchi.

Nimelitetea taifa langu kwenye makongamano mengi ya kitaifa na kimataifa, japo kuwa si mtumishi wa umma. Jubilee 2000 kudai Afrika ifutiwe madeni nilikuwa mstari wa mbele nikiwa bado nje ya nchi. Asante sana Mhe. Mkapa kwa kutambua mchango wangu na wa makanisa katika kampeni hii kubwa ya kimataifa.

Mimi sasa ni mzee na siogopi kifo. Miaka aliyonipa Mungu kumtumikia na kutumikia taifa langu inatosha; na kamwe sina cha kulalamika. Nchi na taifa hili halikustawi toka Ikulu na TISS bali ni matokeo ya mshikamano wa wadau mbalimbali zikiwemo NGO na wananchi wote kwa jumla. Uzalendo wa taifa unajengwa katika mshikamano wa jinsi hiyo na si vinginevyo. 

Lakini naona uchungu kuona viongozi wa taifa hili wanadhalilishwa na kunyanyaswa na mtu mmoja anayejiita mwanaharakati wa rais; na eti sisi sote tunatakiwa tuogope na kukaa kimya. HAPANA. 

Taifa hili limefika tulipo kwa sababu tumekuwa na viongozi waliolifikisha 2015 wakati Rais Magufuli anachaguliwa. Tanzania  ni taifa kubwa kuliko marais wake sembuse kidudu mtu Musiba! 

Inakuwaje leo Musiba anachafua viongozi waliolibeba na kulivusha taifa hili kwenye mawimbi na misukosuko na tunatakiwa eti tukae kimya! Tanzania isingekuwepo kama sio Mwl. Nyerere, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na Mzee Kikwete. 

Hawa wanayo heshima ya kipekee katika Tanzania ya leo na kama hatuoni, hivyo basi kuna tatizo kubwa. Musiba anachokifanya analiweka taifa letu mahali pagumu sana na hatuko tayari kwenda safari hiyo.

Mimi sikatai kwamba kama wapo walioihujumu nchi wasichukuliwe hatua. Miaka ya 2010s nilikuwa Ghana na kule aliyekuwa rais wakati huo, ni marehemu Rais Prof. John Atta Miller.

Huyu alianzisha Mahakama Maalum ya Wahujumu wa Uchumi, ambapo wote waliotuhumiwa walitokea kwenye jopo la majaji kujibu tuhuma zao. Huu ulikuwa mchakato na mfumo rasmi wa kushughulika na mambo. 

Nilifuatilia sana kesi zile na niliona kuwa utaratibu uliofuatwa ulikuwa wa wazi (transparent) na ulikuwa rasmi, kwa maana ya kwamba ulizingatia taratibu za kisheria katika kutoa haki kwa watuhumiwa. 

Iwapo hapa kwetu tungefuata taratibu za jinsi hiyo, nisingekuwa na neno. Tatizo nilionalo ni kwamba taifa zima tunamtazama Musiba kama mahakama ya kutuhumu na kuhukumu viongozi na watu wengine na kuona kwamba ni sahihi. HAPANA! HAPANA! HAPANA! 

Musiba, kwa kuwatuhumu viongozi wakuu wa nchi na wengine, analiweka taifa zima katika mawimbi ya uharibifu. Mimi sijui ni nani anampa kinga Musiba lakini niseme tu kwamba kwa muelekeo huu hakuna aliye salama. 

Musiba ni kiumbe hatari kwa umoja, usalama, na mshikamano wa taifa. Musiba anafifisha uwezekano wa uzalendo kwa nchi na taifa letu. Iwapo anachokifanya Musiba ni mkakati uliopangwa kwa malengo yeyote, basi malengo hayo yatafeli. 

Hatuwezi kuona viongozi wa taifa hili waliotumika hadi kukabidhi madaraka kwa utawala huu wakinyanyaswa na mtu asiye na heshima. Tumevumiliana mengi kwa ajili ya ustawi na amani ya nchi hii lakini Musiba anavuruga nchi. HAPANA! HAPANA! HAPANA! 

Hatuna shida ya kuwepo mfumo rasmi wa kushughulikia tuhuma anazosema Musiba, lakini Musiba hana cheo na sifa za kuwa hakimu kwa mambo ya viongozi wa taifa letu na CCM waliotangulia. 

Siye Musiba peke yake aliyetakiwa kuwa mwana harakati wa Rais bali Watanzania wote walitakiwa wawe wana harakati wa Rais, lakini Musiba amewanyima nafasi hiyo. 

Nimeyasema haya kwa dhamiri yangu safi. Ikiwa itanigharimu kifo niko tayari. Nasema kama Mchungaji Dkt. Martin Luther: Hapa nasimama, Mungu nisaidie. (Here I stand, God help me).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!