July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Asasi za kiraia 272 Tanzania kushiriki uchaguzi mkuu 2020 

Dk. Wilson Mahera, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC

Spread the love

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania, imetoa vibali vya kushiriki shughuli za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, kwa Asasi za Kiraia 272. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo amesema Dk. Wilson Mahera, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, leo Jumanne tarehe 30 Juni 2020 wakati akizungumza kwa simu na MwanaHALISI ONLINE.

Dk. Mahera amesema, vibali hivyo vimetolewa jana Jumatatu tarehe 29 Juni 2020 na kwamba kuanzia leo, AZAKI zilizokidhi vigezo vya kupata kibali cha kushiriki uchaguzi huo, vitapewa barua rasmi.

Dk. Mahera amesema, AZAKI 245 zimepewa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura na 27 zimepewa vibali vya kuwa waangalizi wa ndani wa uchaguzi.

“Tulitoa vibali jana kwa hiyo barua zao wanaanza kupokea kuanzia leo.  Azaki 245 ni zile zilizopatiwa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura na asasi 27 zimepewa vibali  vya kuwa waangalizi wa ndani wa uchaguzi,” amesema Dk. Mahera.

Kuhusu waangalizi wa nje, Dk. Mahera amesema, NEC itatoa tangazo la maombi ya vibali vya uangalizi wa uchaguzi, kwa waangalizi wa uchaguzi wa nje, mwanzoni mwa Julai 2020.

Sanduku la kura

“Waangalizi wa nje hao tangazo lao bado halijatoka, tutatoa tangazo hivi karibuni ili waweze kuomba. Mwezi ujao tutatoa tangazo,” amesema Dk. Mahera.

Dk. Mahera amesema, NEC itatoa ratiba rasmi ya uchaguzi huo, pindi itakapopata tangazo la kuvunjwa kwa Bunge.

“Bado tangazo la kuvunjwa Bunge hatujalipata, lakini tunaamini tutapata hivi karibuni na tukishapata, tutatoa ratiba ya uchaguzi,” amesema Dk. Mahera.

Tarehe 16 Juni 2020, Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli alilihutibia kwa mara ya mwisho Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kisha kinachosubiriwa ni tangazo la kuvunjwa kwa Bunge kutangazwa katika Gazeti la Serikali.

error: Content is protected !!