Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Alichokisema Rais Mwinyi miaka 57 ya Mapinduzi
Habari za SiasaTangulizi

Alichokisema Rais Mwinyi miaka 57 ya Mapinduzi

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar
Spread the love

RAIS wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, amewaomba Wazanzibar kushirikiana na Serikali yake kufanya mageuzi ya kiuchumi, ili kuyaenzi mapinduzi matukufu ya tarehe 12 Januari 1964. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Rais Mwinyi ametoa maombi hayo leo Jumanne tarehe 12 Januari 2021, katika sherehe za maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilizofanyika viwanja wa Mnazi Mmoja visiwani humo.

Viongozi mbalimbali wamehudhulia sherehe hizo, miongoni ni Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mapinduzi ya Zanzibar yalifanyika tarehe 12 Januari 1964 chini ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, amesema dhamira ya mwasisi wa mapinduzi hayo, ilikuwa ni kutoa fursa kwa Wazanzibar kuwa huru katika kuijenga nchi yao.

“Maoni yangu, sasa wakati umefika tuhangaike na uchumi wa mapinduzi. Maana kama nilivyosema awali, shabaha ya mapinduzi ilikuwa ni kustawisha maisha ya Wazanzibar, ndio maana baada ya mapinduzi Karume alisema mapinduzi tumeshinda, sasa tujenge nchi,” amesema Rais Mwinyi.

Aidha, Rais Mwinyi amesema, dhamira ya Serikali yake ni kuyatumia mapinduzi hayo, kuipa Zanzibar msukumo mpya wa kiuchumi.

“Katika hotuba yangu ya kufungua Baraza la Wawakilishi niliahidi kulinda mapinduzi matukufu ya Zanzibar, katika hotuba yangu nilianisha dhamira yangu katika Serikali ninayoiongoza ya kuyapa mapinduzi hayo msukumo mpya wa kiuchumi,” amesema Rais Mwinyi.

Amesema ili kufanikisha azma yake hiyo, aliamua kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ili kujenga maridhiano na umoja wa kitaifa.

“Umoja wa kitaifa ni nguzo muhimu ya ujenzi wa Zanzibar mpya, kwa kutambua haja hiyo, miongoni mwa hatua za mwanzo nilizochukua ni kujenga maridhiano na umoja wa kitaifa. Nimetekeleza takwa la kikatiba ya Zanzibar, lililonitaka kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi amesema, Serikali yake itafanya mapinduzi katika sekta ya uvuvi na kilimo.

“Mapinduzi ya kiuchumi ndio mapinduzi yatakayojibu changamoto zetu za leo na za vizazi vijavyo, tunapaswa kuleta mapinduzi katika sekta ya uvuvi ili wavuvi wetu wavue kwa dhana za kisasa na tuweze kufaidika na rasilimali za bahari kuu,” amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi amesema “Tunapaswa kuleta mapinduzi kwenye kilimo ili wakulima wetu waongeze tija na kutuondolea utegemezi wa chakula kutoka nje ya Zanzibar pamoja na kuendeleza zao la karafuu na mwani.”

Pia, itafanya mapinduzi katika sheria na taasisi za Serikali ili kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara. Sambamba na kuimarisha uwajibikaji wa watumishi katika utoaji huduma kwa wananchi.

“Tunahitaji mapinduzi katika sheria na taasisi ili kumuwezesha Mzanzibar anayefanya biashara afanye bila bughuza wala vikwazo, tuna hitaji mapinduzi kwenye sanaa na michezo ili Mzanzibar atumie vyema kipaji chake kujiendeleza kimapato,”amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi amesisitiza “Ni azma ya Serikali kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje kwa ajili ya kuendeleza nchi yetu. Lengo ni kufungamanisha sekta za uvuvi, utalii na uchukuzi kwa kupanua shughuli za utalii, ikiwemo uwekezaji wa utalii Pemba.”

“Kujenga bandari mpya na kuwezesha wavuvi wetu kuvua kisasa zaidi ikiwemo uwekezaji katika uvuvi wa bahari kuu.”

Sambamba na hayo, Rais Mwinyi amesema, Serikali itapambana kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

“Kilio hiki nilikisikia wakati wa kampeni zangu, malalamiko ya wananchi ni kwamba vyombo husika kutochukua hatua pale zinapotolewa taarifa. Aidha liko lile la baadhi ya wazazi na ndugu kutaka masuala haya yamalizwe kifamilia kwa kile kinachodaiwa kuficha aibu au kunusuru udugu,” amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi amesema “Natoa wito kwa vitendo hivi kukomeshwa mara moja, pale anapopatikana mtu aliyetenda kitendo hiki cha kinyama, basi sheria ichukue mkondo wake. Yeye ni mharifu tu, awe ndugu au jirani.”

Pia, Rais Mwinyi amesema, Serikali yake itahifadhi mali kali kwa ajili ya kuenzi historia na umaarufu wa Zanzibar duniani.

Awali, akizungumza katika sherehe hizo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah amesema mwaka 2021 matukio 18 yamefanyika kwa ajili ya kuadhimisha kumbukumbu ya Mapinduzi.

Amesema miongoni mwa matukio hayo ni uwekaji jiwe la msingi katika miradi mitatu ya maendeleo inayogharimu zaidi ya Sh.46 bilioni na usafi wa mazingira uliofanyika tarehe 31 Desemba 2020.

“Miradi yote iliyofunguliwa, itaijengea uwezo Serikali ya Zanzibar kutoa huduma bora za kijamii kwa wananchi ambao ni wadau wakuu wa kuvuna matunda ya mapinduzi,” amesema Abdallah.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!