Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Ahadi ya CCM 2020 – 2025
Habari za SiasaTangulizi

Ahadi ya CCM 2020 – 2025

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kupunguza pengo la wenye nacho na wasiokuwa nacho, endapo kitafanikiwa kushinda Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Kauli hiyo imetolewa na Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM wakati akieleza muhtasari wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2020 ya chama hicho, katika uzinduzi wa Kampeni za Urais wa Tanzania.

Katibu Mkuu huyo wa CCM amesema, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali ya chama hicho itakuwa na jukumu la kuhakikisha wanyonge wanapata fursa ya kustawisha maisha yao.

“Aidha CCM, itaendelea kutambua kwamba Serikali  ina jukumu kuhakikisha kuwa wanyonge katika jamii wanapata fursa ya kustawisha maisha yao na kuondokana na unyonge wao ili nchi ipunguze pengo la wenye nacho na wasiokuwa nacho,” amesema Dk. Bashiru.

Akielezea sehemu ya ilani hiyo, Dk. Bashiru amesema Serikali ya CCM itatumia rasilimali zilizokuwepo Tanzania kuleta mafanikio ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

“CCM inatambua nchi yetu ina watu na raslimali za kutosha pamoja na fursa nzuri za kijiografia, rasilimali hizi tutazitumia vizuri ili iwe chache ya mafanikio yetu. Hayo niliyoeleza ni msingi wa ahadi tuliyotoa katika sekta ya maji, barabara miundombinu,” amesema Dk. Bashiru.

Aidha, Dk. Bashiru amesema “Katika miaka 5 ijayo CCM itahakikisha Tanzania inaendelea kulinda uhuru wake, kudumisha mapinduzi matukufu ya Zanzibar na muungano ili kujenga taifa imara lenye ustawi wa watu wake lenye kuenzi na kudumisha desturi yetu.”

Dk. Bashiru amesema  Serikali ya CCM itaendelea kudumisha umoja wa nchi pamoja na kuhimiza Watanzania kufanya kazi.

“CCM itaendelea kuamini kwamba uzalendo wa nchi ndio msingi wa maendeleo ya Tanzania ambayo yanaleta kwa Watanzania wenyewe, CCM itaendelea kuhimiza wananchi kufanya kazi. Ndani ya miaka 5 CCM itaendelea kusisitiza kwamba kila mtu ana jukumu la kufanya kazi ili kutoa maendeleo binafsi na Taifa,” amesema Dk. Bashiru.

CHAMA CHA MAPINDUZI

MUHTASARI WA ILANI YA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2020

Imetolewa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Agosti, 2020

Muhtasari wa Ilani ya uchaguzi Mkuu mwaka 2020

Muhtasari wa Ilani ya uchaguzi Mkuu mwaka 2020

CHAMA CHA MAPINDUZI

MUHTASARI WA ILANI YA UCHAGUZI WA MWAKA 2020-2025

UTANGULIZI

1. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa vyama vya TANU na ASP na baadae CCM, imejengwa katika misingi ya ujamaa na kujitegemea inayozingatia utu, usawa na haki. Misingi hii imeimarishwa na siasa safi na uongozi bora wa CCM na imekuwa ndio nguzo ya kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. CCM itaendelea kuzisimamia serikali zake kuhakikisha kuwa zinazingatia, kulinda na kudumisha misingi hii adhimu.

2. CCM itahakikisha kuwa Tanzania inaendelea kulinda Uhuru wake, kudumisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, na kuimarisha Muungano wetu wenye mfumo wa serikali mbili ili kuendelea kujenga Taifa imara linalojitegemea kiuchumi na kisiasa, lenye ustawi wa watu wake na linaloenzi na kuthamini mila nzuri, desturi na utamaduni wetu.

3. CCM inaamini kwamba uzalendo kwa nchi ndio msingi wa maendeleo ya kweli ya Tanzania ambayo yataletwa na Watanzania wenyewe. Hivyo basi, CCM itaendelea kuhimiza wananchi kuwa wazalendo kwa nchi yetu kwa kufanya kazi kwa uadilifu, bidii na maarifa kama msingi imara wa maendeleo.

4. CCM inaamini pia kuwa kila mtu ana jukumu la kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kujiletea maendeleo yake na Taifa kwa ujumla. Imani hii ndiyo chimbuko la kauli mbiu za Hapa Kazi Tu! na Kuacha Kufanya Kazi kwa Mazoea! Aidha, CCM inatambua kuwa serikali inazoziongoza zina jukumu la msingi la kuhakikisha kuwa walio wanyonge katika jamii wanapata fursa ya kipekee ya kustawisha maisha yao na kuondokana na unyonge wao ili kupunguza tofauti za matabaka.

5. CCM inatambua kuwa nchi yetu ina watu wenye uwezo na rasilimali za kutosha kama vile ardhi, madini, gesi asilia, misitu, wanyama, malikale/mambo ya kale, bahari, maziwa na mito, pamoja na nafasi na fursa nzuri za kijiografia. Rasilimali na fursa hizi zikitumiwa vizuri zitakuwa chachu kubwa kwa maendeleo ya Taifa, kama ambavyo imethibitika katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 na kwamba tukiamua tunaweza. Ni katika muktadha huu CCM inaamini kuwa Tanzania ni nchi tajiri.

6. Katika miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 -2020 chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, mafanikio makubwa yamepatikana katika nyanja na sekta zote za maendeleo kwa ustawi wa wananchi. Mafanikio haya ni pamoja na:-

(a) Kuendelea kulinda na kuimarisha umoja, mshikamano, amani, utulivu, ulinzi na usalama;

(b) Kuendelea kulinda, kuimarisha na kudumisha Uhuru, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Muungano wa Tanzania;

(c) Kuendelea kulinda na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi, haki za binadamu, nchi isiyofungamana na dini yoyote, na kupambana na unyanyasaji na udhalilishaji wa aina zote;

(d) Kuendelea kuwa nchi isiyofungamana na upande wowote ili kuweza kutetea na kulinda masilahi ya nchi yetu kwa kuzingatia misingi tunayoiamini;

(e) Kuimarisha utumishi wa umma unaozingatia weledi, nidhamu, uadilifu, bidii na maarifa katika kazi;

(f) Kuimarisha mifumo ya kisera, kitaasisi na kisheria ikiwemo kutungwa kwa sheria inayotaka Serikali za mitaa kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake (4%), vijana (4%) na watu wenye ulemavu (2%);

(g) Kuimarishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kulikowezesha kusimamia na kuboresha utendaji wa mashirika ya umma yaliyoweza kuchangia jumla ya shilingi trilioni 1.052 kama gawio na michango kwa Serikali.

(h) Kuhamishia Serikali Makao Makuu ya Nchi Dodoma;

(i) Kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, uhujumu wa uchumi na ufisadi na hivyo kuokoa fedha na rasilimali nyingine na kuzielekeza kwenye mipango ya maendeleo ya nchi;

(j) Kuimarisha mapambano dhidi ya uzalishaji, uagizaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya, utakatishaji wa fedha haramu na biashara ya kusafirisha binadamu;

(k) Kujitosheleza kwa chakula na kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya nje;

(l) Kuimarisha uchumi wa viwanda ambapo idadi ya viwanda imeongezeka kutoka viwanda 52,633 mwaka 2015 hadi kufikia viwanda 61,110 mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la asilimia 16.1. Kutokana na hatua hii, uzalishaji wa bidhaa na ajira umeendelea kuongezeka;

(m) Kutekeleza miradi ya kimkakati yenye tija kubwa katika uchumi na ustawi wa jamii ikiwemo miradi ifuatayo: Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere; ujenzi wa reli ya kisasa (SGR); kufufuliwa kwa Shirika la Ndege la Taifa kwa kununua ndege mpya 11; kununua meli mbili mpya Zanzibar; na ujenzi wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume;

(n) Kuimarisha mfumo wa udhibiti, usimamizi na umiliki wa madini na hivyo kuongeza mapato yatokanayo na mazao ya madini kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 346 mwaka 2019;

(o) Kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.3 mwaka 2019. Kwa upande wa Zanzibar mapato ya Serikali yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 428.5 mwaka 2015/2016 hadi kufikia shilingi bilioni 748.9 mwaka 2018/19. Mafanikio hayo yameongeza uwezo wa Serikali wa kutekeleza miradi ya maendeleo na kutoa huduma za jamii kwa wananchi;

(p) Kuchukua hatua thabiti za kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari za uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuondoa matumizi ya mifuko ya plastiki; na

(q) Kuendelea kupiga hatua za maendeleo katika maeneo mbalimbali kama vile ujenzi wa miundombinu ya kisasa, kukua kwa kasi kwa uchumi na kuimarika kwa ustawi wa jamii. Tanzania ni miongoni mwa nchi kumi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi barani Afrika na hivyo kuwezesha kufikia nchi ya uchumi wa kati.

(r) Matokeo ya mafanikio haya kwa maendeleo na ustawi wa wananchi ni pamoja na:-

(i) Kwa upande wa Tanzania Bara:

Wastani wa Pato la Mwananchi limekua kutoka shilingi 1,968,965 mwaka 2015 hadi shilingi 2,458,496 mwaka 2018, na Pato la Taifa limeongezeka kwa wastani wa asilimia 6.7 kwa mwaka;

Wastani wa umri wa kuishi umeongezeka kutoka miaka 61 mwaka 2015 hadi miaka 65 mwaka 2020;

Kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme kutoka megawati (MW) 1,308 mwaka 2015 hadi megawati (MW) 1,602.32 mwaka 2020. Vilevile, usambazaji wa umeme vijijini umeongezeka kutoka asilimia 16.4 mwaka 2015 hadi asilimia 67.1 mwaka 2020;

Kuimarika kwa huduma ya umeme nchini na hivyo kuondoa mgao wa umeme uliokuwa kero na kikwazo kikubwa kwa shughuli za kiuchumi na kijamii;

Kutoa elimu bila malipo katika ngazi ya shule za msingi na sekondari na hivyo kuongeza udahili wa wanafunzi katika ngazi zote za elimu. Kwa mfano, idadi ya wanafunzi wa sekondari imeongezeka kutoka wanafunzi 1,648,359 mwaka 2015 hadi 2,185,037 mwaka 2019;

Kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu nchini kutoka 65,064 mwaka 2015 hadi 87,813 mwaka 2019;

Kuongezeka kwa idadi ya wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 70.1 mwaka 2020. Kwa upande wa mijini, idadi ya wananchi wanaopata maji safi na salama imeongezeka kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 85 mwaka 2020. Kwa ujumla, idadi ya kaya zinazopata maji safi nchini kutoka vyanzo salama imeongezeka hadi kufikia asilimia 77 mwaka 2020;

Kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za afya (zahanati, vituo vya afya na hospitali) kutoka 7,014 mwaka 2015 hadi 8,446 mwaka 2020;

▪ Kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa

dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoka asilimia 42 ya mahitaji mwaka 2015 hadi asilimia 94.5 mwaka 2020;

▪ Kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kimepungua kufikia asilimia 26.4; na

▪ Kuboresha makazi na nyumba za wananchi, ambapo asilimia ya kaya zinazoishi katika nyumba zenye mapaa ya kisasa imeongezeka kutoka asilimia 68.0 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 84.1 kwa mwaka 2018/19.

(ii) Kwa upande wa Zanzibar

Wastani wa Pato la Mwananchi limekua kutoka shilingi 1,666,000 mwaka 2015 hadi shilingi 2,549,000 mwaka 2019, na Pato la Taifa limeongezeka kwa wastani wa asilimia 6.8 kwa mwaka;

Wastani wa umri wa kuishi umeongezeka kutoka miaka 66.6 mwaka 2015 hadi miaka 68.4 mwaka 2020;

Usambazaji wa huduma za umeme umeongezeka kutoka asilimia 70 mwaka 2015 hadi asilimia 90 mwaka 2020;

Kuendelea kutoa elimu bure hadi ngazi ya sekondari ikiwa ni utekelezaji wa sera ya msingi ya Mapinduzi ya 1964;

Kuongezeka kwa idadi ya wananchi wanaopata maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 60 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 72 mwaka 2020. Kwa upande wa mijini, idadi ya wananchi wanaopata maji safi na salama imeongezeka kutoka asilimia 80 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 87 mwaka 2020. Kwa ujumla, idadi ya kaya zinazopata maji kutoka vyanzo salama imeongezeka hadi kufikia wastani wa asilimia 83 mwaka 2020;

Kuendelea kutoa huduma ya matibabu bure na kuongeza bajeti ya ndani ya ununuzi wa dawa muhimu kutoka shilingi bilioni 0.5 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 12.7 mwaka 2020 na hivyo kuongeza ugharamiaji huo kutoka asilimia 7 ya mahitaji hadi asilimia 97 ya mahitaji yote; na

▪ Kuimarisha na kupanua matumizi ya utafiti katika kufanya maamuzi sahihi ya sekta mbalimbali.

MALENGO YA UCHAGUZI YA MWAKA 2020 – 2025

7. Ilani hii inalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. Vilevile, maudhui ya Ilani hii yamezingatia Mwelekeo wa Sera za Chama Cha Mapinduzi wa 2020-2030, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020-2050. Aidha, Ilani hii imezingatia fursa na changamoto zinazotokana na mabadiliko mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiteknolojia yanayotokea nchini na duniani, pamoja na madhara ya janga la ugonjwa wa Corona.

8. CCM inatambua kwamba utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo utafikia kikomo chake katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani hii. Hivyo Chama kitazisimamia serikali zake kuandaa Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2050, na kuanza utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2020 – 2050. Katika miaka mitano ijayo, lengo la CCM ni kuendelea kustawisha maisha ya kila Mtanzania. Katika kufikia lengo hili vipaumbele vikuu vya serikali za CCM katika miaka mitano ijayo vitakuwa vifuatavyo:-

(a) Kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa, haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa letu;

(b) Kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi;

(c) Kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi;

(d) Kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini;

(e) Kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi; na

(f) Kutengeneza ajira zisizopungua 8,000,000 (milioni nane) katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana.

Mambo muhimu yatakayozingatiwa katika kutekeleza vipaumbele vikuu vya Ilani hii ni kama ifuatavyo:-

A. Kulinda na kuimarisha utu, usawa, haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa letu:-

(i) Kuendelea kudumisha na kuimarisha umoja, udugu, mshikamano, amani, utulivu, ulinzi na usalama;

  (ii) Kuendelea kuimarisha Muungano wa serikali mbili, kuenzi Uhuru wa nchi yetu na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na kutumia tunu nyingine za kitaifa ikiwemo falsafa ya Mwenge wa Uhuru katika kujenga moyo wa uzalendo wa kitaifa na uwajibikaji;

(iii) Kuendelea kuimarisha demokrasia, utawala bora na haki za binadamu na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, pamoja na udhalilishaji wa aina zote;

(iv) Kuendelea kuimarisha Serikali za Mitaa ili ziweze kutimiza wajibu wao kwa wananchi katika maeneo husika;

(v) Kuendelea kujenga mazingira wezeshi kwa asasi za kiraia, kidini na vyombo vya habari kustawi ili kuchangia katika maendeleo ya Taifa; na

  (vi) Kuendelea kuimarisha huduma na kulinda haki kwa makundi maalum wakiwemo wanawake, vijana, wazee, watoto na watu wenye ulemavu.

B. Kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi:-

(i) Kuendelea kujenga na kukuza uchumi shindani hususan kupitia sekta za viwanda na huduma za kiuchumi utakaowezesha ustawi wa wananchi wote;

(ii) Kuendelea kuimarisha miundombinu ya kimkakati ili kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya shughuli zao kwa ufanisi na tija;

(iii) Kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kukua na kustawi pamoja na kuvutia wawekezaji ili watoe mchango stahiki katika maendeleo ya nchi yetu;

  (iv) Kuendelea kuboresha masilahi na mazingira ya kazi kwa wafanyakazi katika sekta zote;

  (v) Kuongeza faida ambazo nchi yetu inapata kutokana na maliasili zetu na utajiri wa nchi kwa kuimarisha usimamizi wa mikataba ya uzalishaji na kujenga uwezo wa ndani wa kuvuna na kuchakata/kusarifu rasilimali hizo;

  (vi) Kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa mazingira na uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi;

  (vii) Kutenga maeneo maalum ya akiba ya ardhi na uwekezaji;

(viii) Kuendelea kuimarisha mawasiliano ya simu za mkononi nchini ili yaweze kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa maendeleo ya wananchi; na

  (ix) Kuendeleza diplomasia ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni ikiwa ni pamoja na kufanya lugha ya Kiswahili kutumika kikamilifu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN).

C. Kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi:-

(i) Kuhakikisha uzalishaji unaongezeka katika mazao ya chakula, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula na lishe bora;

  (ii) Kuongeza tija katika kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya uchumi hasa katika sekta za viwanda na huduma;

  (iii) Kuimarisha ushirika ili kuunganisha nguvu za wazalishaji hasa katika kupata pembejeo na kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi;

  (iv) Kuimarisha miundombinu na kuongeza maeneo ya umwagiliaji katika kilimo ili kupata mazao mengi zaidi kwa wakati wote wa mwaka; na

  (v) Kukamilisha na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya shughuli za kijamii, uwekezaji na uzalishaji.

D. Kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za Afya, Elimu, Maji, Umeme na Makazi vijijini na mijini:-

(i) Kuongeza kasi ya usambazaji majisafi na salama ili kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya asilimia 85 vijijini na zaidi ya asilimia 95 kwa mijini kwa upande wa Tanzania Bara ifikapo mwaka 2025, na zaidi ya asilimia 95 kwa upande wa Zanzibar;

  (ii) Kuendelea kuimarisha mfumo wa elimu ili uweze kuzalisha wataalam mahiri zaidi wenye uwezo katika sayansi, teknolojia, ufundi na nyanja nyingine ambao wanaweza kujiajiri na kuajirika ndani ya nchi na mahali popote duniani;

  (iii) Kusambaza umeme kwenye mitaa na vijiji vyote ifikapo mwaka 2025;

  (iv) Kutoa huduma za afya kwa wote;

  (v) Kuhamasisha na kuweka mazingira wezeshi ili wananchi katika maeneo yote nchini wawe na makazi bora (“Nyumba bora kwa wananchi wote inawezekana”).

E. Kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi:-

(i) Kuimarisha na kuhuisha taasisi za utafiti, sayansi, teknolojia na ufundi ili ziweze kubuni nyenzo za kuongeza tija katika sekta za uzalishaji na huduma;

(ii) Kuhakikisha kila shule ya sekondari nchini inakuwa na kompyuta na huduma za intaneti;

(iii) Kusomesha Watanzania nje ya nchi katika vyuo bora na maalum duniani kwenye masuala ya sayansi, tiba,

teknolojia na maeneo mengine yenye umuhimu ili kupata maarifa bora na ya kisasa na ujuzi ili kuchochea maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini; na

  (iv) Kuchochea na kuendeleza ubunifu, uvumbuzi na ugunduzi nchini kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

F. Kutengeneza ajira zisizopungua 8,000,000 (milioni nane) katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana:-

(i) Kuchochea ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, maliasili na sekta ya huduma za kiuchumi ikiwa ni pamoja na utalii;

(ii) Kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za ujasiriamali, ikiwemo kuwapatia mafunzo na kuwaunganisha na taasisi na asasi za utoaji mikopo yenye riba na masharti nafuu;

(iii) Kuwahamasisha na kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika utamaduni, michezo na sanaa kwa ajili ya afya bora na burudani na pia kuongeza fursa za ajira na kipato; na

   (iv) Kuhakikisha kuwa miradi mikubwa ya kimkakati inaajiri vijana wengi zaidi wa Kitanzania.

AHADI YETU

9. CCM itahakikisha serikali zake zinatekeleza mambo yote yaliyoahidiwa katika Ilani hii kwa manufaa na ustawi wa Taifa letu. Utekelezaji wa Ilani hii utaongozwa na kauli mbiu ifuatayo: “Tumetekeleza kwa Kishindo, Tunasonga Mbele Pamoja”

10. Ilani hii ni tamko na ahadi maalum ya nia na uwezo wa CCM kuendelea kuongoza nchi, kuleta ustawi wa Watanzania wote na kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hususan wanawake, vijana, watoto, wazee, pamoja na watu wenye ulemavu. Katika miaka mitano ijayo, CCM itahakikisha matarajio ya wananchi katika nyanja zote yanafikiwa. Chama Cha Mapinduzi kinawaomba Watanzania wote waendelee kukiamini na kukichagua ili kiendelee kuongoza nchi na kuleta maendeleo makubwa na ya haraka kwa faida ya wananchi wote.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!