Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa ACT-Wazalendo wajifungia kujadili ushirikiano na Rais Mwinyi
Habari za SiasaTangulizi

ACT-Wazalendo wajifungia kujadili ushirikiano na Rais Mwinyi

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo akiwa kaika Harambee ya kuchangia kanisa la EAGT
Spread the love

HATIMA ya Chama cha ACT-Wazalendo kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, kujulikana kesho Jumapili tarehe 6 Novemba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hatma hiyo itatokana na maazimio ya kikao maalum cha Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, kinachofanyika leo Jumamosi tarehe 5 Novemba 2020, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kujadili kama kitashiriki au hakitashiriki katika serikali hiyo.

Kikao hicho cha Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo kinafanyika huku Wazanzibar na wadau wa siasa Tanzania, wakiwa na shauku ya kufahamu hatma ya uundwaji wa serikali hiyo, kama chama hicho kitashiriki au la.

Miongoni mwa wajumbe waliohudhuria kikao hicho cha dharura ni, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Shariff Hamad. Babu Duni Haji (Makamu Mwenyekiti).

Nassor Mazrui (Naibu Katibu Mkuu). Salim Bimani (Katibu wa Kamati ya Itikadi, Uenezi na Mahusiano na Umma) na Omary Said Shaban (Mwanasheria Mkuu).
Akizungumza na MwanaHALISI Online, Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu amesema, baada ya kumalizika kwa kikao hicho, kesho Jumapili watazungumza na waandishi wa habari.

Ado alikuwa akijibu swali aliloulizwa kuhusu agenda za kikao hicho ni pamoja na suala hilo la ushiriki kwenye serikali inayoongozwa na Rais Mwinyi akisema “leo tutajadili masuala mbalimbali na kesho tutazungumza na vyombo vya habari, hivyo tuwe na subira.”

Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo inakutana siku kadhaa baada ya chama hicho kuchukua maoni ya baadhi ya wananchi wa Zanzibar, ili kupata mapendekezo yao kama kishirikiane na Serikali iliyoko madarakani au kisishirikiane nayo.

Chama hicho kilisita kushirikiana na Serikali hiyo, baada ya uwepo wa malalamiko juu ya mchakato na matokeo ya uchaguzi huo, yaliyokipa ushindi Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo awali kilidai , kushirikiana na Serikali ya CCM itakuwa sawa na kuhalalisha malalamiko hayo.

ACT-Wazalendo kilitangaza kususia matokeo hayo sambamba na kutoshiriki katika nafasi za uongozi serikalini kikipinga mchakato wa uchaguzi huo kwa madai haukuwa huru na wa haki.

Miongoni mwa malalamiko yaliyoibuliwa na chama hicho ni, baadhi ya wagombea wake kuenguliwa katika mchakato wa uteuzi kinyume na sheria, udanganyifu wakati wa utangazaji matokeo, kusambaa kwa kura feki.

Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilikanusha madai hayo ikisema iliratibu na kuendesha mchakato wa uchaguzi huo katika misingi ya haki, uhuru na usawa.

Katika matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), CCM kilishinda uchaguzi wa urais, huku kikizoa viti vingi vya ubunge, uwakilishi na udiwani.

Siku kadhaa baada ya aliyekuwa mgombea Urais wa CCM Zanzibar, Rais Hussein Ali Mwinyi kuingia Ikulu na kutangaza baraza lake la mawaziri tarehe 19 Novemba 2020, aliiandikia barua ACT-Wazalendo.

Rais Mwinyi alikiomba chama hicho jina la Makamu wa kwanza wa Rais ili aunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwa kuwa chama hicho kilifikisha zaidi ya asilimia 10 ya kura za uchaguzi wa urais.

Katika matokeo hayo ya urais, Rais Mwinyi alitangazwa na ZEC mshindi kwa kupata kura 380,402 sawa na asilimia 76.27 huku Maalim Seif akipata kura 99,103 sawa na asilimia 19.87.

Baada ya Chama cha ACT-Wazalendo kupokea barua hiyo, kiliueleza umma kwamba kitafanya vikao vyake vya ndani kwa ajili ya kuamua kama kikubali kupeleka wawakilishi wake kwa ajili ya kuunda SUK, au kisishiriki katika serikali hiyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!