Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa ACT-Wazalendo: Membe ametupa funzo  
Habari za SiasaTangulizi

ACT-Wazalendo: Membe ametupa funzo  

Spread the love

HATUA ya Bernard Membe, aliyekuwa mshauri mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, kukitelekeza chama hicho, imekera viongozi wake. Anaripoti Brigthness Boaz, Dar es Salaam … (endelea).

Baada ya Membe kubwaga manyanga siku tatu zilizopita katika chama hicho, ACT-Wazalendo kimesema “tumejifunza jambo na sasa hatutakuwa laini laini kupokea wanachama kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).”

Membe alihitimisha safari ya siku 178 za kuwa ACT-Wazalendo tarehe 01 Januari 2021 kwa kutangaza kujiuzulu uanachama na nafasi za uongozi baada ya kujiunga nacho 7 Julai 2020.

Membe aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje (2007 – 2015) chini ya Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Mrisho Kiwkete, alijiunga na ACT-Wazalendo baada ya kufukuzwa CCM akituhumiwa kwenda kinyume na taratibu na miongozo ya chama hicho.

Bernard Membe

Membe aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita alisema, tayari ameandika barua ya kujiuzulu kwa kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kama utaratibu unavyotaka ili abaki kuwa mshauri wa kitaifa na kimataifa wa kushughulikia na kupigia debe masuala ya demokrasia nchini mwake Tanzania.

Leo Jumatatu tarehe 4 Januari 2021, Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo akizungumza na MwanaHALISI Online kuhusu kujiuzulu kwa Membe, amesema “Membe aliwasiliana kwa simu na mimi Katibu Mkuu siku kadhaa nyuma na baadaye akamwandikia barua kiongozi wa chama.”

“Ametueleza kwamba anataka kukaa pembeni, anataka kujiondosha na chama kama mshauri mkuu wa chama,” amesema Ado.

Akijibu swali aliloulizwa chanzo cha uamuzi huo, Ado amesema “hajazungumza lolote kuhusu chimbuko la kufanya hivyo, ila alisema amefanya hivyo, bila kusukumwa na mtu au kushurutishwa bali ameamua kukaa pembeni.”

Bernard Membe (kulia) akiwa na Maalim Seif Sharrif Hamad

“Na sisi kama chama, hatujaona haja ya kuchimbua ili atueleze kwa nini ameamua kukaa pembeni. Sisi ACT-Wazalendo, tunamshukuru Mungu kwani tangu tumeanzishwa, hii ya watu kuondoka na hakuna mgogoro ni kawaida yetu na wala hatutamsakama au kulumbana naye na tunamtakia kila la kheri huko anakokwenda,” amesema.

Kuhusu umuhimu wake ndani ya chama hicho, Ado amesema “Membe ni mwanasiasa mkubwa kwenye nchi kwa maana ya nafasi yake kama mwanadiplomasia na waziri wa mambo ya kigeni, si sifa ndogo, inaweza kuwa na msaada kwenye chama.”

“Ana mazuri yake na mapungufu yake kadhaa na ndiyo maana chama kilimpa nafasi ya heshima ya kuwa mshauri mkuu wa chama. Ameondoka alikuwa na sifa zake na mapungufu yake,” amesema Ado

Katibu mkuu huyo, amezungumzia kutofautiana kwa mitizamo kati ya Membe na viongozi wa chama hicho, Zitto na Mwenyekiti wao, Maalim Seif Sharif Hamad juu ya kumuunga mkono mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Ado Shaibu, Katibu Mkuu ACT-Wazalendo

Wakati Zitto na Maalim Seif wakitangaza chama hicho kumuunga mkono Lissu, Membe alijitokeza hadharani na kuzungumza na waandishi akisema yeye alikuwa bado ni mgombea halali na hatambua msimamo wa viongozi wenzake.

“Chama kikifanya uamuzi kwa ngazi ya vikao na wewe unashiriki, huwezi kusema ni msingi wa kuondoka, yote tuliyoyafanya kamati ya uongozi wajumbe ni pamoja na mshauri mkuu wa chama (Membe), hivyo alijua kinachoendelea,” amesema Ado.

Akijibu walichojifunza kwa kumpokea Membe kutoka CCM amesema “namna alivyokuwa CCM mara baada ya uchaguzi mkuu 2015, alikuwa kama muasi ndani ya chama na tuliona kama ni sahihi kuwa ni mpinzani mwenzetu katika kupigania demokrasia kwa maneno na matendo yake.”

“Tunapaswa kutafakari zaidi, mienendo ya watu kutoka CCM kwa uzoefu wa mwaka 2015 enzi za Edward Lowassa, tulipaswa kufanya uchunguzi wa kina kutafakari kwa kina zaidi na hili litakuwa funzo si kwa ACT-Wazandelo bali vyama vya upinzani vyote,” amesema.

Ado amesema, wao kama ACT-Wazalendo watajifunza zaidi hasa nafasi ya urais “tunapaswa kujiandaa miaka mingi nyuma kuwa na wagombea tuliowaandaa na si kusubiri kutoka CCM.”

Mwaka 2015, Chadema kilimpokea Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani kutoka CCM baada ya kukatwa jina lake kwenye mbio za kuwania kupeperusha bendera ya chama hicho.

Baada ya kujiunga na Chadema, alipitishwa kuwa mgombea urais akiungwa mkono na vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD na kuishia kushika nafasi ya pili nyuma ya Dk. John Magufuli aliyeibuka mshindi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!