Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa ACT- Wazalendo, CUF waingia tena vitani
Habari za SiasaTangulizi

ACT- Wazalendo, CUF waingia tena vitani

Spread the love
CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimejigamba kuwa kinawasubiri wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), waliopanga kuchukua kwa nguvu, mali na majengo, wanayodai ni mali yao. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 6 Desemba 2019 na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Joran Bashange. Kwa sasa, Bashange ni mwenyekiti wa kamati ya kampeni na uchaguzi wa chama cha ACT-Wazalendo.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI ONLINE, Bashange ambaye amewahi kuwa Katibu wa Bodi ya Wadhamini ya CUF amesema, “ACT-Wazalendo, haijachukua mali za CUF, bali inatumia mali na majengo ya waliokuwa wanachama wa chama hicho na ambao sasa, wamejiunga na ACT -Wazalendo.”

Kutokana na hali hiyo, Bashange amesema, wanachama wa ACT- Wazalendo, wameamua kulinda kwa gharama yoyote ile, mali zao na chama chao.

“Kama wakitufuata mitaani kutaka kupora mali zetu; na au zile za wanachama wetu, hatutakuwa na njia nyingine, zaidi ya kujibu mapigo,” amesisitiza Bashange na kuongeza, “yeyote atayetusogelea tutapambana naye. Hii ni kwa sababu, wao ndio watakaokuwa wametufuata na siyo sisi.”

Kuibuka kwa Bashange, kumefutia kauli ya Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CUF, Mussa Haji Kombo, kudai kuwa chama chake, kiko mbioni kuvamia ofisi za ACT- Wazalendo, kwa lengo la kurejesha mali zake.

Kombo aliwaambia waandishi wa habari, juzi Jumatano, tarehe 4 Desemba 2019, kwamba chama chake kiko katika taratibu za kuzirejesha mali hizo, yakiwamo majengo na samani.

Alisema, hatua yake hiyo, inatokana na maelekezo ya Baraza Kuu la uongozi la taifa la CUF (BKUT), kuelekeza kurejeshwa kwa inazoita, “mali zake,” mara moja.

Akijibu madai hayo, Bashange anasema, hakuna mali yeyote ya CUF, ikiwamo magari na majengo ambayo yameporwa na ACT- Wazalendo, na kwamba kama kuna mtu mwenye ushahidi wa jambo hilo, anaruhusiwa kwenda mahakamani kuthibitisha madai yake.

“CUF ina miliki majengo matatu tu, mawili yako Zanzibar na moja liko Buguruni, jijini Dar es Salaam. Hata taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaeleza kuwa chama hicho kinamiliki majengo hayo.

“Hayo mengine yanayotajwa, ni mali za watu binafsi. Wenyewe wameamua kubadilisha matumizi na hivyo, huwezi kuzidai na kusema ni zako,” ameeleza.

Akionekana kuchukizwa na kauli ya viongozi hao wa CUF, Bashange amekishauri chama hicho, kusubiri maamuzi ya Mahakama katika kesi ya msingi Na. 16 ya mwaka 2019, pamoja na shauri dogo Na. 19/2019, iliyoifungua katika Mahakama Kuu ya Vuga, Unguja.

“Hawa watu wamefungua shauri mahakamani kuhusu suala hilo. Miongoni mwa watuhumiwa, ni mimi Bashange, Maalim Seif na Mazrui. Tunatutuhumiwa  kuiba mali za chama chao,” anasimulia.

Anasema, “Mahakama ikawaambia walete ushahidi, ikiwemo nyaraka zinazothibitisha kwamba majengo hayo ni ya kwao. Mpaka sasa, hawajaweza kufanya hivyo.”

Katika kesi hiyo, CUF inataka irejeshewe mali zake ikiwemo majengo, ambapo inamtuhumu Maalim Seif Sharrif Hamad, ambaye alikuwa katibu mkuu wa chama hicho na Nassoro Mazrui, aliyekuwa naibu katibu mkuu Zanzibar. Wote wawili wamejiengua CUF na kujiunga na ACT- Wazalendo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!