Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mwaka 2020 mchungu kwa Mangula
Habari za SiasaTangulizi

Mwaka 2020 mchungu kwa Mangula

Philiph Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
Spread the love

 

PHILIP Japhet Mangula, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alichungulia kaburi katika mwaka huu wa 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Vyombo vya habari vya ndani na vile vya kimataifa, vimeripoti katika mwaka huu, kuwa Mangula, alinyweshwa sumu na wanaoitwa, “watu wasiojulikana.”

Hata hivyo, mpaka wakati huu, tunakoelekea kumaliza mwaka 2020, wananchi bado hawajajua lolote kuhusu yaliyomsibu kiongozi huyo.

Taarifa za Mangula kulishwa sumu, zilithibitishwa na Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, tarehe 9 Machi 2020.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya polisi, Mangula alidondoka ghafla akiwa ofisini kwake, Lumumba jijini Dar es Salaam. Alianguka mara baada ya kumaliza kuhudhuria kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho.

Mkutano wa NEC ambao Mangula alianguka, ulifanyika tarehe 28 Februari mwaka huu. Ulikuwa mahususi kupitia taarifa ya Kamati ya Maadili, iliyoshughulikia suala la madai ya utovu wa nidhamu, yaliyokuwa yakiwakabili makatibu wakuu wawili wastaafu wa chama hicho na kada mmoja.

https://www.youtube.com/watch?v=U7tDuwOJ8c0

Viongozi hao watatu wakongwe ndani ya chama hicho – Abdulrahman Kinana, Yusuph Makamba na Benard Membe – walikuwa wametuhumiwa kwa ukiukwaji wa maadili, utovu wa nidhamu na kumhujumu mwenyekiti wao, Rais John Pombe Magufuli.

NEC iliyomuangusha Mangula, ilifikia maamuzi ya kumfukuza kutoka ndani ya chama hicho Membe; kumuweka chini ya uangalizi wa muda wa miezi 18 Kinana na “kumsamehe Makamba.”

Hata hivyo, miezi kadhaa baadae, Kinana alisamehewa kufuatia hatua yake ya kumuomba radhi hadharani Rais Magufuli na chama chake.

Kinana na Makamba, walihojiwa na Kamati ya Maadili ya Usalama na Maadili, chini ya mwenyekiti iliyoongozwa na Mangula, tarehe 10 Februari 2020. Mahojiano yalifanyika, ofisi ndogo ya chama hicho, Lumumba.

 

SACP Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam

Kwa mara ya kwanza Taarifa ya Mangula kuugua ilitolewa tarehe 29 Februari 2020 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa, siku moja baada ya mwanasiasa huyo kuanguka ghafla.

Kwa mujibu wa taarifa ya Msigwa, baada ya Mangula kuanguka ghafla, alikimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kisha kulazwa katika Chumba cha Uangalizi  Maalumu (ICU).

Rais John Magufuli alikwenda kumjulia hali mwanasiasa huyo tarehe 29 Februari 2020.

Msigwa kupitia taarifa hiyo, alisema Mangula kabla ya kukumbwa na tukio hilo, alishiriki katika kikao Kamati Kuu ya NEC, ambacho kiliongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Magufuli katika ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilifanyika kwa ajili ya kumjadili aliyekuwa kada wa CCM, Benard Membe, Makatibu Wakuu wastaafu wa chama hicho, Mzee Yusuph Makamba na Abdulrahman Kinana waliokuwa wakituhumiwa kwa kukiuka maadili ya chama hicho.

Bernard Membe (kulia) akisalimiana na Rais John Magufuli walipokutana katika mkutano Mkuu wa CCM 2015

Membe, Kinana na Mzee Makamba walituhumiwa kukiuka maadili ya CCM, baada ya sauti zao kusambaa katika mitandao ya kijamii wakielalamikia uongozi wa chama hicho kwa kushindwa kuwalinda dhidi ya watu waliokuwa wanatoa shutuhuma dhidi yao.

Makada hao watatu, “walikabiliwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili,” kufuatia sauti zao, wakati wakifanya nawasiliano kwa njia ya simu, kuvujishwa kwenye mitandao nchini Tanzania, wakizungumzia masuala mbalimbali kukihusu chama na mwenyekiti wake.

Sehemu ya mazungumzo yaliyovuja ya Makamba na Kinana, ni pamoja na kuandaa taarifa ya malalamiko dhidi ya anayejiita, “mwanaharakati huru,” Cyprian Musiba, ambaye walimtuhumu kwa “kuwadhalilisha,” bila kuchukuliwa hatua yoyote na kisha wakahoji, “analindwa na nani?”

Lakini nani aliyeanza kujulisha umma kuhusiana na kilichompta Mangula? Alikuwa ni Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, ambaye alinukuliwa siku moja baada ya mwanasiasa huyo kuanguka ghafla, kwamba Mangula ni mgonjwa.

Msigwa aliviambia vyombo vya habari, tarehe 29 Februari 2020, kwamba “Mangula ameanguka ghafla na amekimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kwa ajili ya matibabu.”

Alisema, “mara baada ya kufikishwa Muhimbili, Mzee Mangula amechukuliwa vipimo na sasa amelazwa katika Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU).”

Rais Magufuli alikwenda Muhimbili kumjulia hali mwanasiasa huyo, tarehe 29 Februari 2020.

Msigwa kupitia taarifa hiyo, alieleza kuwa kabla ya kukumbwa na tukio hilo, Mangula alishiriki katika kikao Kamati Kuu ya NEC, ambacho kiliongozwa na mwenyekiti wake, Rais Magufuli.

Mahitaji ya taarifa za Mangula kulishwa sumu na chanzo chake ulikuwa mkubwa sana, kiasi kwamba jeshi la polisi lilikumbana na maswali juu ya jambo hilo mara kwa mara.

Kwa mfano, tarehe 16 Machi 2020, baadhi ya waandishi wa habari walimuuliza Mambosasa, kuhusiana na uchunguzi wa tukio hilo na kusema, “bado uchunguzi unaendelea” na akaahidi kuwa mara baada ya kukamilika, atatoa taarifa kwa umma.

Alisema, jeshi la polisi, limeamua kufanya uchunguzi wa suala hilo kwa umakini mkubwa, ili kubaini namna sumu hiyo ilivyoingia katika mwili wa Mangula; mhusika wa tukio hilo la jinai ili aweze kuchukuliwa hatua na sababu za kufanya hivyo.

Alisema, bado wanaendelea kukusanya ushahidi kwa ajili kufungua kesi mahakamani. Lakini mpaka sasa, siyo jeshi la polisi wala Ikulu ya Magogoni, iliyozungumzia suala la Mangula kulishwa sumu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

Habari za SiasaTangulizi

CAG aibua madudu halmashauri 10, TANESCO na MSD

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

error: Content is protected !!