Serikali yatangaza tahadhari ya uwepo wa ugonjwa wa Ebola

UMMY Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amewataka watanzania kuchukua tahadhari ya hali ya juu ili kujikinga na kudhibiti na ugonjwa wa Ebola nchini. Anaripoti Khalifa Abdallah … (endelea).

Mwalimu amesema Wizara inatoa tahadhari ya ugonjwa huo wa Ebola kwa wananchi wote katika Mikoa yote ya Tanzania, lakini hasa ile inayopakana na nchi jirani za DRC, Uganda na Rwanda.

Mikoa hiyo ni pamoja na Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe. Aidha tahadhari na hatua stahiki zichukuliwe katika maeneo yote ya mipakani ambapo abiria wanaingia nchini kutoka nchi jirani.

Amesema hatua hiyo ni baada ya kugunduliwa kwa ugonjwa huu kwenye jimbo la Kivu Kaskazini linalopakana na nchi za Uganda na Rwanda jambo ambalo linaiweka Tanzania kwenye wasi wasi kwani eneo hili liko karibu sana na nchi yetu kuliko eneo lingine lolote ambako ugonjwa huu umeshawahi kutokea kwenye nchi ya DRC.

Nchi hiyo ya DRC imetangaza tena kuwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mnamo tarehe 1 mwezi Agosti, 2018, ambapo jumla ya wagonjwa 26 na vifo 10

Wanawake wanaotumia uzazi wa mpango waongezeka

SERIKALI kupitia Wizara ya Áfya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa idadi ya wanawake wanaotumia huduma za Afya za Kisasa za uzazi wa mpango zimeongezeka nchini mpaka kufikia Asilimia 32. Anaripoti Khalifa Abdallah … (endelea).

Hayo yamesemwa na Waziri wa Áfya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati alipoupokea ugeni wa Waziri wa Maendeleo kutoka nchini Uingereza katika Zahanati ya Tabata jijini Dar es salaam ukiwa na lengo la kutatua changamoto za Sekta ya Áfya hususani katika huduma za Afya ya mama na mtoto.

“Kupitia Msaada wao tumeweza kuongeza idadi ya wanawake wanaotumia huduma za Kisasa za uzazi wa mpango, hatupo vizuri, tupo Asilimia 32, tumeweka lengo itapofika 2020 tufikie Asilimia 45 ya wanawake walioolewa wanatumia njia hizi” Alisema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa, bado kuna changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi nchini, takribani wanawake 556,000 katika kila vizazi hai laki moja wanafariki na kwa mujibu wa Wataalam uzazi wa mpango utaweza kuchangia Mpaka Asilimia 30 katika Kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Pia Waziri Ummy alisema kuwa Serikali ya Tanzania imechukua hatua kwa kutenga fedha za ndani katika kupambana na changamoto za sekta ya Áfya ikiwemo kuajiri watumishi wa sekta ya Áfya jambo linalosaidia Kupunguza changamoto hizo za vifo vya akina mama wajawazito na mtoto wachanga.

“Sisi kama Serikali tumejiongeza, tumechukua hatua na kutenga rasilimali fedha za ndani ikiwemo kuajili watoa huduma za afya, kuhakikisha Kwamba tunatatua changoamoto hiyo ” alisema Waziri Ummy.

Hata hivyo Waziri Ummy aliishukuru Serikali ya Uingereza kupitia kwa Waziri wa Maendeleo Mhe. Penny Mordaunt kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za afya hasa katika huduma za mama na mtoto.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo kutoka Uingereza Mhe. Penny Mordaunt ameshukuru Serikali ya Tanzania.

Chuo cha Mati Ilonga kusaidia vijana kujikwamua kiuchumi

VIJANA nchini wametakiwa kukitumia vyema Chuo cha Kilimo – Mati Ilonga ili kupata elimu mbalimbali ikiwemo ya usindikaji wa mazao itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi sambamba na kufikia uchumi wa viwanda. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Dk. Mdangi Mashaka amesema hayo kwenye maonesho ya wakulima 88 kanda ya Mashariki wakati akiongea na waandishi wa Habari ndani ya viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere eneo la Tungi nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro.

Dk. Mashaka alisema, chuo hicho kilichopo wilayani Kilosa mkoani hapa kina uwezo wa kutoa elimu za usindikaji na uzalishaji wa mazao mbalimbali kama vile mazao ya mikunde, mbegu, mbogamboga na mizizi kinauwezo wa kupokea wanafunzi 180 kwa mwaka lakini kinapokea wanafunzi wasiofika 100 na kufanya elimu inayotolewa kutofika vyema kwa jamii.

Alisema, kufuatia elimu hiyo vijana wanaweza kufikia hatua ya kujiajiri katika kukuza uchumi wa viwanda na hivyo kufikia uchumi wa kati mwaka 2025 kama ulivyo mpango wa Serikali.

Naye Mkuu wa Idara ya Elimu ya Ushauri kwa wakulima kutoka Mati-Ilonga, John Ngairo alisema, elimu inayotolewa katika chuo hicho huweza kuwasaidia wakulima kuongeza mnyororo wa thamani na kuweza kuuza kwa bei kubwa na yenye faida.

Hivyo aliwashauri vijana na wakulima kwa ujumla kwenda kwenye chuo hicho kujifunza namna ya kuongeza mnyororo wa thamani na hivyo kuondokana na umaskini wa kipato kufuatia kuwa na ujuzi wa kuweza hata kuanzisha viwanda vidogovidogo.

“usindikaji wa mazao hauhitaji vitu vingi na haugharimu fedha nyingi bali ni elimu tu ambayo mkulima akiamua kuielewa naweza anzisha na kujikwamua kiuchumi” alisema.

Naye Mkufunzi kutoka Chuo hicho, Hamisi Ramadhani alisema, usindikaji una faida mbalimbali kwa mkulima na hata kwa mtumiaji wa bidhaa za usindikaji kwani bidhaa hizo huongezewa thamani na hivyo kuwa na vitamin, protin na madini yanayoweza kulinda afya ya mlaji.

Polisi wajichunguza tuhuma za kumpiga mwandishi

JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limesema linalaani vikali tukio linalosambaa mtandaoni la kupigwa kwa mwandiishi wa habari wa Wapo Radio aitwaye Sillas Mbise lililotokea August 08, 2018. Anaripoti Khalifa Abdallah … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema Polisi Kanda Maalum imeanza uchunguzi wa tukio hilo kwa kufungua jalada la uchunguzi wa picha ya video hiyo inayosambaa inayoonesha askari wa Polisi na mwandishi huyo wa habari ili kubaini ukweli.

Mambosasa amesema hilo linaenda sambamba na kumtaka mtendewa wa kosa hilo la kupigwa kutoa taarifa kituo cha Polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwakuwa mtu yeyote anatakiwa kutoa malalamiko yake pale anapoona ametendewa vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria.

Sambamba na hayo Mambosasa amesema kuwa jukumu la Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao na si kuwapiga raia wakitenda kosa ambao hawajakataa kutii sheria ya kukamatwa.

Hans Poppe kuondolewa kwenye kesi ya Aveva, Kaburu

HAKIMU mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba ametoa siku saba kwa upande wa Jamhuri kubadilisha hati ya mashtaka ili kuwaondoa kwenye kesi aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe na Frank Lauwo kwenye kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili Evans Aveva na Godfrey Nyange (Kaburu). Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Hakimu huyo amesema kuwa washtakiwa hao wanatakiwa kuondolewa kwenye kesi hiyo kutokana na kutohudhulia mahakamani hapo hata siku moja hivyo kufanya shauri hilo kuchelewa kusikilizwa na itafika mahali uvumilivu utawashinda na kama Jamhuri wameshindwa bora waifute.

Kwa upande wa wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai ameieleza mahakama hiyo kuwa, kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na tayari wameshaifanyia marekebisho hati ya mashtaka na kwamba wanasubiri kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kesi hiyo iendelee na kesi hiyo imeahilishwa hadi 17 agosti mwaka huu.

Chadema, NCCR-Mageuzi wapigwa ‘stop’ Tarime

MSIMAMIZI Msaidizi wa Uchaguzi wa Kata ya Turwa wilayani Tarime, Mara amesitisha mikutano yote ya kampeni ya vyama vya upinzani kwenye kata hiyo. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Taarifa hizo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii kupitia barua inayodaiwa kutolewa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Turwa, Peter Julius yenye kichwa cha habari; KUSITISHWA KWA KAMPENI ZA UCHAGUZI KWA CHAMA CHA NCCR-MAGEUZI KUANZIA TAREHE 10/08/2018 HADI 11/08/2018’.

Sehemu ya barua hiyo inaeleza kuwa, hatua hiyo imekuja baada ya NCCR-Mageuzi kudaiwa kukiuka sheria ya taifa ya uchaguzi.

“Nakujulisha kwa kufuatia chama tajwa hapo juu kukiuka kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, Maadili ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2015, Kamati ya Maadili ya Uchaguzi Kata ya Turwa kupitia kikao kilichoketi tarehe 10/08/2018 kimesitisha kampeni za chama hicho kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 10/08/2018 hadi 11/08/2018,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Kabla ya NCCR-Mageuzi kusitishwa kufanya kampeni kata ya Turwa, Chadema pia ilisitishwa kufanya kampeni za udiwani kwenye kata hiyo.

Barua hiyo imeeleza kwamba, kuanzia leo kampeni zitaendelea kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) pekee.

Mbunge wa Chadema awamwaga Polisi

MBUNGE wa jimbo la Mbozi mkoani Songwe kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Pascal Haonga na wenzake wameshinda kesi iliyokuwa inawakabili katika Mahakama ya Wilaya ya Mbozi, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha makosa dhidi ya watuhumiwa. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Haonga na wengine Katibu wake Wilfred Mwalusamba na Mashaka Mwampashi walikuwa wakikabiliwa na makosa ya kuvuruga mkutano wa uchaguzi wa baraza la mji mdogo wa Mlowo kosa la pili na la tatu kuwazuia askari kutekeleza majukumu yao makosa hayo wanadaiwa kuyatenda tarehe 28 Agosti, mwaka huu.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi Nemes Chami alisema katika mashtaka yote matatu yalikuwa yanawakabili, hakuna hata sehemu moja upande wa mashtaka uliothibitisha.

“Hakuna mahali walipoonesha kwamba washtakiwa hawa waliwazuia askari kutekeleza majukumu yao na hakuna mahali walipo thibitisha kwamba washtakiwa walilazimisha kurudi ukumbini baada ya kutolewa nje” Alisema Chami.

Baada ya kusoma hukumu hiyo hakimu huyo alisema kuwa kama kuna upande ambao haujarizika na hukumu hiyo una haki ya kukata rufaa ndani ya muda.

Lugola awageukia Polisi wanaobambikia watu kesi

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amehidi kufanya ziara za kushtukiza kwenye vituo vya polisi nchini ili kupambana na baadhi ya polisi wenye tabia ya kubambikizia kesi wananchi. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Waziri Lugola aliyasema hayo jana Agosti 9, 2018 wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Kenkombyo wilayani Bunda.

Waziri Lugola alisema kitendo hicho kinaichafua wizara yake pamoja na serikali kwa ujumla, ambapo amesema polisi watakaobainika kufanya makosa hayo hata waonea huruma.

 “Nilishawaambia polisi na leo nawaaambia tena, nitakuwa nafanya ziara ya kushtukiza mara kwa mara katika vituo vya polisi, na hamjui saa wala siku lini nitakuja, hili nilisemalo sitanii kabisa, lazima nitapambana nanyi, hii ni serikali ya Awamu ya Tano inataka wananchi waishi kwa amani zaidi bila kua na hofu ya aina yoyote,” alisema Lugola.

Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi waache tabia ya kufungua kesi polisi ili kuwakomoa watu wenye chuki nao.

TEF, TFF wapinga wanahabari kushambuliwa

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limelaani kitendo cha Jeshi la Polisi kumfungulia Mwanahabari wa gazeti la Tanzania Daima, Sitta Tuma mashitaka ya kuandamana bila kibali. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Tamko la TEF lilitolewa hapo jana Agosti 9, 2018 na Kaimu Mwenyekiti wake, Deodatus Balile ambapo alisema mwanahabari huyo alikuwa kazini akitekeleza wajibu wake wa kukusanya habari.

Tuma alikamatwa Agosti 8 mwaka huu pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na wafuasi  18 wa chama cha Chadema wakiwa kwenye mkutano wa kampeni ya mgombea udiwani wa chama hicho Kata ya Turwa.

Wakati TEF likipinga kukamatwa kwa mwanahabari Tuma, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania  (TFF) jana lilitoa tamko la kulaani tukio la shambulio lililodaiwa kufanywa na polisi kwa mwandishi wa habari za Michezo, Sillas Mbise lililotokea katika mchezo wa kirafiki kati ya Simba na Asante Kotoko kutoka Ghana uliofanyika  uwanja wa Taifa juzi Agosti 8, 2018.

Kufuatia kadhia hiyo, TFF imesema imekutana na viongozi wa Chama cha waandishi wa habari za michezo nchini TASWA na kujadiliana kuhusu tukio hilo na hatua stahiki zitachukuliwa.