Diamond azua kizaazaa msiba wa King Majuto

MWANAMUZIKI wa kizazi kipya Nasibu Abdul maarufu kwa jina la Diamond Platnum leo tarehe 9 Agosti, 2018 amezua kizaazaa kwenye msiba wa Amri Athumani maarufu kwa jina la King Majuto. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Diamond alifika kwenye ukumbi wa Kareem Jee wakati ambao shughuli ya kuaga mwili wa King Majuto ikiendelea na kuzuiwa kutokana na kuchelewa kufika eneo la tukio.

Maofisa wa Usalama wa Rais walimzuia Diamond kutokana na kuchelewa kufika kwenye msiba huo baada ya Rais John Magufuli kuwasili.

Utaratibu wa serikali unaelekeza kwamba rais anapaswa kuwa mtu wa mwisho kuingia eneo la tukio na kuwa wa kwanza kutoka.

Kutokana na kuzuiwa, Diamond alilazimika kubaki nje ya ukumbi akisubiri mwili wa King Majuto utolewe nje tayari kwa safari ya kuelekea Tanga kwa ajili ya mazishi kesho Ijumaa.

Wakati mwili wa King Majuto ulipokuwa ukitolewa nje, Diamond alijiunga sawa na watu wengine katika kuupokea mwili huo lakini ghafla watu waliongezeka kwa mkupuo upande aliokuwepo Diamond.

Hatua hiyo ilisababisha msongamano kuelemea upande wa Diamond jambo lililowasukuma walinzi wake (Diamond) kumwondoa eneo hilo ili kutuliza vurugu zilizokuwa zimeanza kuibuka.

Hata hivyo, baada ya Diamond kundolewa eneo hilo na walinzi wake, idadi kubwa ya watu nayo ilimfuata nyuma na kulipa jeneza mgongo.

Walinzi wake wake walilazimika kuanza kuwasukuma watu waliokuwa nyuma ya Diamond na mbele yake ambao tayari walikuwa wamemzingira. Walinzo hao walimwelekeza moja kwa moja mpaka kwenye gari lake.

Baada ya Diamond kuingia kwenye gari lake, alifunga vioo na kutulia huku walinzi wake wakizungua nje ya gari hilo kwa ajili ya usalama.

Mfumuko wa bei sasa ahueni

MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Julai, 2018 umepungua kutoka asilimia 3.4 mwezi Juni, 2018 hadi kufikia asilimia 3.3. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Takwimu hizo zimetolewa leo tarehe 9 Agosti, 2018 Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim Kwesigabo alipokuwa akitoa taarifa ya mfumuko wa bei kwa mwezi Julai mwaka huu.

Kwesigabo amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kumetokana na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula ikiwemo mihogo, maharagwe na matunda jamii ya machungwa.

“Kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018 kumechangiwa hasa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula, ambapo bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kati ya Julai, 2017 na Julai 2018 ni pamoja na unga wa mahindi kwa asilimia 9.5, mtama kwa asilimia 17.8, unga wa mihogo kwa asilimia 14.1, matunda jamii ya machungwa kwa asilimia 22.2, maharagwe kwa asilimia 5.8 na mihogo mibichi kwa asilimia 12.5,” amefafanua Kwesigabo.

Kwesigabo ameeleza kuwa, ni zaidi ya miaka 15 tangu itokee tarakimu kama hiyo ya mfumuko wa bei ambayo iko vizuri kwa uchumi wa nchi.

Magufuli, Kikwete wamuaga Mzee Majuto Karimjee

RAIS wa Tanzania, John Magufuli na Rais mstaafu Jakaya Kikwete amewaongoza mamia ya watanzania kuaga mwili wa marehemu muigizaji wa vichekesho Amri Athumani ‘Mzee Majuto” kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mwili wa Mzee Majuto uliwasili Ukumbini hapo saa nane na shughuli ya kuaga ikaanza ikiwemo salamu za rambirambi na dua ya kuombea iliongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum.

Viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na vya kijamii na viongozi wa dini wameungana na waigizaji wenzake na marehemu pamoja na wananchi kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa marehemu.

Mwili wa Mzee Majuto ulitolewa kwenye Monchwari ya Muhimbili saa 5 asubuhi na kupelekwa kwenye msikiti wa Maamul Upanga kwa ajili ya kuswaliwa na baadaye saa nane mchana Mwili uliwasilishwa kwenye viwanja vya Kareem Jee kwa ajili ya kuagwa.

Taswira ya Viwanja hivyo ilikuwa imefurika wasanii mbalimbali wa maigizo wakiwamo Jacob Steven JB, Cloud 112, Joti, Dr. Cheni, Haji Manara na wengine wengi.

Pia kulikuwepo watu mbalimbali mashuhuri kama Humphery Polepole, Naibu waziri wa Habari Vijana, Sanaa na michezo Juliana Shoza.

Majira ya saa 9 aliwasili Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakari Bin Zuberi na baadaye aliingia Rais wa Tanzania John Magufuli.

Wakati huo huo vikindi mbalimbali vilitoa salaam za rambirambi pamoja kuuaga Marehemu Mzee Majuto.

Mzee Majuto aliaga dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya taifa Muhimbili jijini dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Wananchi watakiwa kutumia maharage ya SUA

JAMII imeshauriwa kubadilika na kula maharage ya SUA Karanga ambayo yanatengenezwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) huku yakiwa hayana gesi na yenye protini zaidi zinazopatikana katika nyama kwa afya. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Meneja Utafiti wa Maharage hayo Profesa Paulo Kusolwa alisema hayo wakati wa maonesho ya wakulima 88 kanda ya Mashariki yaliyofanyika kwenye uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere ambapo alisema, maharage hayo ni tofauti na maharage mengine kwani yana uwezo wa kuliwa hata na mtu mwenye vidonda vya tumbo na asipate madhara.

Prof. Kusolwa alisema, waliamua kufanya utafiti na kuboresha maharage yanayotumika masokoni kwa kuweka vinasaba au viini vya uvumilivu wa magonjwa na wadudu ili kumsaidia mlaji na mkulima zaidi.

Alisema, jamii ya Maharage ilikuwa na tabia ya kutoa wadudu muda mfupi baada ya kuvunwa na kuzalisha mazao kidogo na kwamba maharage hayo ambayo yanazalisha zaidi hayatoi wadudu wala hayaliwi na wadudu baada ya kuvunwa .

Hivyo aliwashauri wakulima kutumia mbegu za maharage hayo ambazo zinapatikana kwa wingi SUA ili kuweza kuongeza uzalishaji wa mbegu na kumfanya mlaji kupata chakula hicho kwa afya.

Alisema, mpaka sasa wana aina 6 za mbegu za maharage ambazo wanaendelea kuzifanyia tafiti kwa ufadhili wa Shirika la Msaada la Marekani lijulikanalo kama The Mcnight Foundation lengo likiwa ni kupata mbegu bora itakayoendana na hali ya hewa ya aina zote na kumnufaisha mlaji na mkulima.

Hata hivyo Prof. Kusolwa alisema, ni vema ukawepo msukumo wa kisera wa kuboresha lishe kwa watoto mashuleni, wafungwa magerezani na wagonjwa hospitalini ili kuifanya mbegu hiyo yenye lishe kuweza kupata soko na kuingia kwa wingi katika jamii tofauti na ilivyo kwa sasa.

Alisema licha ya mbegu hiyo kuwa bora lakini bado haijapata masoko ya uhakika na kwamba mpaka sasa wana hifadhi ya Tani 30 ndani jambo ambalo huifanya kuendelea kubaki kwenye makabati na hivyo kutoleta maana ya utafiti.

Alisema SUA Karanga ina uwezo wa kuzalisha kg 25-30 kwa kg 1 ya mbegu ambapo pia huweza kupatia mkulima gunia 25 za maharage hayo baada ya kuvuna hekari 1 ya maharage hayo.

Hivyo aliomba wakulima waipokee mbegu hiyo kwa mikono miwili kufuatia kuweza kuongeza chakula kilichoboreshwa sambamba na kuwaongezea kipato.

Naye Mkulima Mzee Flaiton Mlozi wa kijiji cha Nambala – Mbozi mkoani Songwe alisema mbegu hiyo imeweza kuwa na manufaa kwake kufuatia kuwa na mavuno mengi licha ya kukabiliwa na changamoto ya soko.

Alisema awali alikuwa akilima shamba la nusu heka lakini amelazimika kuongeza ukubwa wa shamba na kulima shamba la heka mbili kutokana na kuwa na mavuno mengi na mbegu nyingi kwa sasa.

Hivyo aliiomba Serikali kuingilia kati na kuona umuhimu wa kuwatafutia masoko ili waweze kuuza tofauti na kuwasubiri SUA kwenda kununua maharage hayo kwao huku wao na wakiwa na nia ya kuuza mapema kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao.

Mwijage: Zalisheni mbegu za kunukia kuvutia soko

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Masoko Charles Mwijage amewataka wazalishaji wa mbegu ya Mpunga zinazotoa  harufu ya kunukia aina ya Aroma kuongeza uzalishaji huku wakizingatia ubora wa harufu ya mpunga huo ili kuvutia katika soko. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Waziri Mwijage amesema hayo wakati alipotembelea banda la Maonesho la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI) lililopo kwenye uwanja wa Maonesho ya Kilimo 88 kanda ya mashariki kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo eneo la Tungi nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro.

Mwijage amesema, mbegu hiyo ni nzuri na inanukia lakini upatikanaji wake umekuwa mdogo tofauti na mbegu zingine na hivyo kumfanya mkulima kuendelea kutumia mbegu zingine ambazo hazina harufu nzuri kama ya mpunga aina ya Aroma.

Akizungumzia hilo Mtafiti wa Kilimo ambaye pia ni Ofisa Mfawidhi –TARI- Dakawa Dk. Charles Chuwa alikiri uchache wa uzalishaji wa mbegu hizo na kusema kuwa unatokana na uzalishaji wake kuwa mdogo zikiwa shambani kwa mkulima na kufanya wakulima wengi kuvutiwa na kutumia mbegu aina ya TXD 360-Saro 5 ambayo inauwezo wa kuzalisha tani 6-8 kwa hekta.

Amesema, Mbegu ya Saro 5 ambayo ina harufu kidogo kama Aroma ilitokana na mbegu aina ya Supa inayonukia iliyochanganywa na mbegu inayozaa sana kutoka bara la Asia ambayo hainukii na kupata mbegu hiyo aina ya Saro 5 ili kukidhi mahitaji ya mkulima na kuongeza uzalishaji wa mpunga nchini.

Dk. Chuwa amesema kufuatia mbegu aina ya Saro 5 kuonekana kutumika na wakulima walio wengi wataangalia namna ya kuiboresha harufu yake na kuwa na Aroma zaidi na hivyo kufanya walaji kuendelea kupata chakula kizuri na chenye protini kidogo na stachi huku kikiwa na harufu nzuri.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa TARI, Dk. Furaha Mrosso amesema, TARI imeanzishwa nchini ili kuweza kufanya tafiti za msingi zikiwemo za kutumia matokeo ya awali na kupeleka kwa wakulima na Tafiti za kimkakati ambazo wakulima wanapaswa kuzitumia katika kulima kilimo chenye tija.

Dk. Mrosso amesema, teknolojia zilizopo katika vituo sita vya utafiti vilivyopo kanda ya mashariki zina uwezo wa kukidhi malighafi za viwanda vinavyoanza kuendelezwa hapa nchini na hivyo kuwezesha wakulima kunufaika kufuatia mpango wa serikali wa kufanya bei ngazi ya mkulima kuwa juu na kuondokana na umaskini.

Hivyo alitoa rai kwa wakulima kuhakikisha wanapata teknolojia kutoka TARI na kuitumia ili waweze kuongeza uzalishaji na kuondoka katika umaskini.

Naye Ofisa Kiungo utafiti na ugani kanda ya Mashariki TARI, Magreth Mchovu amewashauri wakulima kuhakikisha wanapata elimu ya kutosha ya mazao ya kimkakati ili waweze kujikita katika kilimo hicho kufuatia mazao hayo kuleta manufaa kwenye kilimo.

Aliyataja mazao ya kimkakati kuwa ni pamoja na Michikichi, Pamba, Korosho, Miwa na mbegu za mafuta kama vile Alizeti ambazo alisema zitasaidia kumfanya mkulima kufikia kwenye uchumi wa viwanda.

Mbunge Chadema aliyekamatwa, atoka ‘sero’

JESHI la Polisi wilayani Tarime limewaachia kwa dhamana, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema) na Mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Sitta Tuma. Anaripoti Regina Kelvin…(endelea).

Matiko na Tuma walikamatwa jana tarehe 8 Agosti, 2018 na Jeshi la Polisi wakiwa kwenye mkutano wa kumnadi mgombea udiwani Chadema Kata ya Turwa.

Polisi waliuzuia mkutano huo kwa sababu ya Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Tarime kuzuia mikutano ya chama hicho.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema Matiko na Tuma wameachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti tena polisi hapo kesho.

Vile vile, Polisi imewaachia kwa dhamana wanachama wa Chadema kumi na nane waliokamatwa jana katika mkutano huo.

Niyonzima azua taharuki Simba

KIUNGO wa Simba Haruna Niyonzima amezua taharuki na hali ya sintofahamu kwa mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo baada ya kutoonekana jana katika tamasha kubwa la ‘Simba Day’ ambalo mara nyingi hutumika kama jukwaa la kutambulisha kikosi kuelekea msimu mpya wa ligi kuu. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Katika tamasha hilo klabu ya Simba iliweka hadharani benchi la ufundi pamoja na wachezaji wake wote watakaotumikia timu hiyo katika michuano ya Ligi Kuu na Klabu Bingwa Afrika, katika msimu wa 2018/19 huku jina la Niyonzima likikosekana.

Huwenda kiungo huyo tayari ameshakuliwa hatua ya kinidhamu baada ya Kaimu Rais wa klabu ya Simba, Salim Abdallah alinukiliwa akisema kuwa kiungo huyo Mnyarwanda atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa kuchelewa kurejea nchini kujiunga na timu baada ya ruhusa maalum aliyopewa kuisha.

Haruna ambaye alipewa ruhusa maalum na klabu yake hadi tarehe 20 Julai 2018, na alitakiwa arejee na kuungana na wenzake kwa safari ya Uturuki, lakini hakufanya hivyo licha ya taratibu zote za safari kukamilika lakini kutokana na kuchelewa alishindwa kwenda.

Prof. Ndalichako aendeleza makali yake

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amelitaka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuvifungia vyuo visivyokidhi vigezo hasa vile vilivyowekwa chini ya uangalizi. Anaripoti Regina Kelvin…(endelea).

Prof. Ndalichako ametoa agizo hilo leo tarehe Agosti 9, 2018 jijini Dar es Salaam wakati akizindua baraza jipya la uongozi la NACTE.

“Mwaka 2017 vyuo 464 vilifanyiwa ukaguzi, 20 kati ya hivyo vilifungiwa baada ya kubainika havijakidhi vigezo, vyengine viliwekwa chini ya uangalizi huku vingine vikapewa muda wa kurekebisha mapungufu yake.

“Hivi vyuo vilivyo chini ya uangalizi mkiona havikidhi vigezo, vifungieni,” amesema na kuongeza;

“Anzieni hapo, msisite kufunga chuo chochote kiwe cha umma au binafsi msione huruma fungeni. Hatutaki kuwa na vyuo utitiri halafu havina ubora, tunataka tuwe na vyuo vinavyokidhi vigezo na kutoa wahitimu wenye elimu bora.”

Vile vile, Prof. Ndalichako amelitaka baraza hilo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vyuo vilivyosajiliwa na vitakavyosajiliwa ili kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wahitimu inakidhi soko la ajira.

Katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako amelitaka baraza jipya la NACTE kuongeza juhudi katika kufanya utafiti wa soko la ajira ili liweze kuwashauri wawekezaji wanaotaka kuanzisha vyuo kutoa mafunzo yanayokidhi soko la ajira.

Sambamba na hilo, ameishauri NACTE kutoa ushauri kwa wanaotaka kuanzisha vyuo, kutoa mafunzo kuhusu sekta zinazotoa ajira kwa sasa, hususani sekta ya kilimo, viwanda, madini na gesi.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi NACTE, Prof. John Kandoro amemhakikishia Prof. Ndalichako kwamba watatekeleza maagizo yake, akisema kuwa, baraza lake litaendelea kufanya tathimini ya ubora wa vyuo pamoja na kuendeleza elimu ya ufundi ili kufanikisha adhma ya serikali ya uchumi wa viwanda.

Mange Kimambi ‘shujaa’ Afrika

TUZO ya mwanamke mwenye ushawishi na mhamasishaji zaidi kisiasa Afrika imechukuliwa na Mange Kimambi, raia wa Tanzania. Anaripoti Regina Kelivin … (endelea).

Waandiaaji wa tuzo hiyo wanaotambulika kwa jina la kingereza Black Entertainment Film Fashion Television and Art (BEFFTA) –Burudani, Filamu, Mitindo, Televisheni ya Watu Aweusi wamemchagua Mange kuwa mshindi wa tuzo hiyo dhidi ya wenzake.

Waliokuwa kwenye kinyang’anyiro hicho ni pamoja ni Elie Johson Sirleaf wa Liberia, Joice Majuru kutoka Zimbabwe, Diane Shima Rwigara raia wa Rwanda, Mbali Ntuli kutoka Afrika Kusini na Alengot Oromait kutoka nchini Uganda.

Lengo la BEFFTA ni kuangaza maslahi ya watu weusi katika nchi za Uingereza, Canada, Marekani, Carribbean na nchi za Bara la Afrika.

Awali taarifa za kuwania tuzo hizo zilitolewa na shirika hilo la BFFTA kupitia ukurasa wao unaopatikana kwenye mtandao wa kijamii wa instagram.

Mange amejipatia umaarufu katika mitandao ya kijamii hasa instagram kutokana jumbe zake za ukosoaji kwa viongozi wa serikali na hata viongozi wa dini nchini Tanzania.

Pia aliongeza ‘presha’ zaidi Tanzania kutokana na kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha maandamano aliyopanga kufanyika Aprili 26 mwaka huu.

Hatua hiyo hiyo iliwalazimu viongozi mbalimbali Tanzania kujitokeza na kupinga maandamano hayo yaliyoonekana kushika kasi kupitia mitandao hiyo.

Mzee Majuto afariki dunia

MUIGIZAJI maarufu Amir Athuman (Mzee Majuto) amefariki dunia usiku huu kwenye Hospital ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akitibiwa. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mzee Majuto ameripotiwa kufariki majira ya saa 2 usiku hospitalini hapo alipokuwa anatibiwa kwa wiki wiki mbili.

Taarifa za kifo cha King Majuto zimethibitishwa na mtoto wake Abuobakari.

King Majuto alizaliwa mwaka 1948 mkoani Tanga na kusoma Shule Msambweni, mkoani humo, alianza kuigiza 1958 akiwa na umri wa miaka 10.