Rais Kabila akaa pembeni Urais DR Congo

VYAMA vinavyounda Muungano wa Common Front for Congo (FCC) umemteua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo, Emannuel Shadari kuwa mrithi wa Rais Joseph Kabila. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Uamuzi huo umekuja baada ya muungano huo kufanya kikao cha dharula hapo jana mjini Kinshasa ambapo walilipitisha jina la Shadari kugombea kiti cha urais kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Shadari amewasilisha fomu za kuwania urais kwenye Tume ya Uchaguzi Congo leo majira ya mchana.

Shadari anadaiwa kuwa na mahusiano ya karibu na Rais Kabila na aliwahi kuwa Katibu wa Kudumu wa chama tawala cha PPRD. Pia, Shadari anatajwa kwamba, alikuwa mtu wa muhimu kwenye kampeni za Rais Kabila.

Polisi wasambaratisha mkutano wa Zitto Tarime

JESHI la Polisi limezuia mkutano wa pamoja wa wabunge, Zitto Kabwe ( ACT), Upendo Peneza (Chadema) na John Heche (Chadema) wa kumnadi mgombea udiwani Chadema Kata ya Turwa wilayani Tarime. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mkutano huo unadaiwa kuzuiwa kwa sababu ya Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi  wa wilaya hiyo kusimamisha mikutano yote ya Chadema.

Zitto Kabwe ambaye pia ni  Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo amesema Jeshi la Polisi linamshikilia Mbunge Esther Matiko pamoja na Mwandishi wa Habari wa Tanzania Daima, Tuma Sitta.

“Polisi wamenizuia kufika kituoni kumwona Mbunge Esther Matiko. Polisi wamevamia ofisi za Chadema Tarime na kurusha mabomu ya machozi. Udiwani tu unaleta maafa makubwa,” amesema Zitto.

Lissu aruhusiwa hospitalini, kutua nchini muda wowote

TUNDU Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki ameruhusiwa kutoka hospitalini alipokuwa anatibiwa kwa miezi saba, nchini Ubelgiji. Anaripoti Mwandishi Weti … (endelea).

Lissu amesambaza ujumbe wake kupitia mitandao ya kijamii kuwa, ameruhusiwa kutoka hospitalini baada daktari wake kujiridhisha afya yake imetengamaa.

Mbunge huyo ameeleza katika ujumbe wake kuwa pamoja na kurusiwa lakini ataendelea kukaa na chuma pajani kwake kwa miezi saba.

Lissu katika ujumbe wake amemalizia kwa kuwaambia Watanzania, wanachokula wasimale kwani yupo karibu sana kurudi nchini.

Soma kamili ujumbe wa Lissu hapa chini

Hello Friends of Me!!!

Good afternoon to y’all. Kwa mara nyingine nawaleteeni habari njema.

Alfajiri ya tarehe 6 January ya mwaka huu, niliondoka Nairobi Hospital na kusafiri hadi Leuven, Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu zaidi. Jana tarehe 6 Agosti ilikuwa mwezi wa saba kamili tangu niletwe hapa Ubelgiji kwa ajili hiyo.

Leo tarehe 7 Agosti ni miezi 11 to the day niliposhambuliwa na watu wanaojulikana sana kama ‘watu wasiojulikana.’

Tarehe 7 September mwaka jana sikulala nyumbani kwangu. Tarehe 7 Agosti ya leo, miezi 11 kamili baadae, nimeamkia nyumbani kwangu.

Tarehe 7 September iliyopita wote mlikuwa na hofu kubwa kama ningemaliza siku hiyo, au siku chache zilizofuata, nikiwa hai. Miezi 11 kamili baadae, Professor Dr. Wilhelmus Jan Mertsemakers, daktari wangu tangu nilipokuja University Hospital Leuven, amesema sina sababu ya kitabibu ya kuendelea kukaa hospitali.

Prof. Mertsemakers amesema nitaendelea na uponyaji nikiwa nyumbani kwangu. Nitatembelewa na homecare nurses kila siku nyumbani kuniangalia naendeleaje. Na nitarudi hospitali kumwona kila baada ya wiki mbili.

Bado nina lichuma kubwa kwenye paja liko kama antenna ya TV za mwaka ’47. Na Prof. Mertsemakers amesema nitakaa nalo kwa si chini ya miezi sita. Lakini habari ya mujini ndio hiyo: nimetoka hospitalini.

Hongereni sana kwa kazi nzuri ya kuniuguza na kuniponya. Na chochote mtakachokula au kunywa siku ya leo mnibakishie. Siko mbali.

Tundu Lissu,
Brussels, Belgium.

Serikali yaizuia mitambo ya kampuni ya madini

SERIKALI imeiagiza Tume ya Madini Tanzania, kuzuia mali na mitambo yote ya Kampuni ya Canaco inayomiliki leseni ya Uchimbaji Madini ya dhahabu, kutokana na kukiuka masharti ya leseni hiyo. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji madini katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Pia, Waziri Biteko ameagiza kampuni hiyo iliyoko katika Kijiji cha Magambazi Wilayani Handeni Mkoani Tanga, ipewe hati ya makosa kwa sababu ya kwenda kinyume na Sheria ya Madini yam waka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 pamoja na kanuni za mwaka 2018.

Sambamba na hilo, aliumuelekeza Kamishna wa Tume ya Madini Dkt.Athanas Macheyeka kumpa mwekezaji huyo hati ya makosa (default notice) kwa ajili ya kurekebisha makosa waliyonayo kwenye leseni ya uchimbaji wa madini na kama watashindwa kurekebisha makosa kwa muda uliotajwa na sheria, leseni yao ifutwe wapewe wawekezaji wengine.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi katika sakata la utoroshwaji wa Carbon zenye madini ambazo ziliibwa usiku kutoka eneo hilo na kupelekwa mkoani Mwanza kwa ajili ya kuyeyushwa ili kupata dhahabu kinyume cha utaratibu.

Waziri Biteko alisema kuwa mwekezaji huyo awali alifika katika Wizara ya Madini na kuomba kibali cha kusafirisha carbon tani 2.23 kwenda mkoani Mwanza katika kiwanda cha JEMA AFRICA LTD kwa ajili ya kuchenjuliwa lakini wakanyimwa kutokana na matatizo yao ya ndani lakini baadae wakachukua kibali cha kughushi kutoka Dodoma kwa ajili ya kusafirishia carbon kupeleka Mwanza.

Kondoa walia na miundombinu mibovu ya maji

WAKAZI wa kata ya Chemchem wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma wameiomba serikali kuwatatulia kero ya muda mrefu ya uchakavu wa  miundombinu ya mabomba ya maji ambayo toka yawekwe mwaka 1961 hayajafanyiwa ukarabati wowote. Anaripoti Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Wakizungumza na vyombo vya habari kwa nyakati tofauti kuhusiana na kero hiyo, Mariam Said mkazi wa mtaa wa Iboni pamoja na Abuu Mwenda wa mtaa wa Chemchem, walisema kuwa kutokana na uchakavu huo mabomba hayo hivi sasa yanakutu na yaliyo mengi yamepasuka na kusababisha upotevu wa maji.

Mariam ambaye ni mkazi wa mtaa wa Chemchem alisema kuwa uchakavu wa miundombinu hiyo ya mabomba kwa upande wao imewasababishia kukosa hata na huduma ya maji kutokana na yaliyo mabomba yake yametoboka na hata yakitoa maji upotea.

“Hivyo tunaiomba serikali yetu sikivu kulishughulikia jambo hili ya ukarabati wa hii miundombinu ya mabomba ambayo toka yamewekwa mwaka 1961 mpaka leo hii hayajafanyiwa ukarabati na hata maji yake yamekuwa yakitoka kwa shida mno,” alisema Mariam.

Naye Abuu Mwenda alisema kuwa kuwepo kwa uchakavu huo wa mabomba wa muda mrefu kuna kila sababu kuwa tumekuwa tukinywa maji ambayo siyo salama kwa afya kwa kuwa yaliyo mengi yamechokaa na kushikwa na kutu.

Hata hivyo mkazi huyo alisema kuwa kwa hivi sasa huduma hiyo tunaipata kwa wiki mara mbili kwenye kata hiyo,suala ambalo linatulazimisha kutumia maji yanayopatikana kwenye mto wa chemchem ambayo hata hivyo siyo salama pia.

Akizungumza kuhusiana na kero hiyo Diwani wa kata hiyo Kipaya Mdachi alikiri kuwepo kwa shida hiyo ya mabomba ambayo yaliyowekwa katika kipindi cha upatikanaji wa uhuru wan nchi hii.

“Mimi nikiwa Diwani wa kata hii Chemchem ambayo nina mitaa yangu minne ikiwemo mtaa wa Uboni, Ubembeni,  Chemchem na Kwa Pakacha, tatizo hilo la uchakavu wa mabomba ni kweli lipo na wananchi wangu wamekuwa wakikosa maji salama kutokana na miundombinu hiyo uchakavu,” alisema.

Mdachi alisema hata hivyo anaamini serikali kwa kupitia kilio hicho cha wananchi watatengewa fedha kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati huo wa mabomba hayo ambayo hivi sasa hana sifa ya kuweza kahudumia maji yaliyo salama kwa wanadamu.

Diwani huyo alisema kutokana na kero hiyo kwa upande wake anaiomba serikali kuwachimbia visima ambavyo vitakavyowasaidia kwa hivi sasa katika upatikanaji wa maji salama wakati ukidanyiwa mchakato wa kufanyika kwa ukarabati wa mabomba hayo.

Shivyawata waomba walimu maalum mashuleni

SHIRIKISHO la vyama vya watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) mkoa wa Dodoma limeomba Wizara ya Elimu kuwapeleka walimu wenye taaluma ya elimu maalum kwenye shule zote nchini. Anaripoti Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Shirikisho hilo lilisema kuwa shule nyingi hazina walimu wenye ujuzi wa kutoa elimu kwa watu wenye mahitaji maalum jambo ambalo linawafanya watu wenye ulemavu kutofikia mahitaji wanayotarajia kuyapata.

Ombi hilo lilitolewa Wilayani Kondoa mkoani Dodoma, kwenye kongamano la kujadili umuhimu wa kutambua haki kwa watu wenye ulemavu na jinsi ya kupatiwa huduma stahiki.

Akisoma risala kwa Mkuu wa wilaya ya Kondoa, Zezaria Makota kwenye ufunguzi wa kongamano hilo Katibu wa Shirikisho hilo mkoani hapa, Justus Ng’wantalima amesema kuwa kutokuwepo kwa walimu wenye taaluma ya ya utoaji wa elimu mahalumu kwa watu wenye ulemavu kumesababisha elimu ya watoto kushuka kwa kiwango kikubwa kwa upande wao.

“Hali hiyo imekuwa ikiwakosesha wanafunzi hao kutopatiwa elimu stahiki kama ilivyo kwa wengine ambao hawana ulemavu,hivyo haki za msingi za walio wengi uzikosa kwa kuwa walimu wenye sifa hawapangwi kwenye shule hizo.

“Walimu walio wengi hata wale wenye taaluma bado upamgwa kwenye shule za kawaida wakati sifa zao zinatakiwa kufundisha kwenye shule maalumu zenye wanafunzi wenye uhitaji huo wa elimu stahiki ambayo pia ni haki yao ya msing,” amesema.

Katibu huyo amesema kuwa ili kupunguza makali hayo ya kukosa elimu kwa wanafunzi hao kwa upande wa wa halmashauri pia wanatakiwa kutenga bajeti inayokidhi mahitaji katika shule hizo tofauti ilivyo kwa hivi sasa ambapo ni ndogo ukilinganisha na tatizo lililopo.

Amesema kukosa kwa bajeti hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi hao,hata ufaulu kuwa ni mdogo kutokana na walio wengi kutokuwa na vifaa vinavyohitaji kulingana na ulemavu walionao kwa kila mmoja wapo.

Wakizungumza kwa pamoja kwenye ufunguzi wa kongamano hilo Maafisa maendeleo ya jamii wa halmashauri zote mbili ya wilaya na mji, Hadija Abdallah na Latipha Koshuma, walisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wanapata haki stahiki juu ya elimu.

Hivyo kwa upande wao halmashauri itashirikiana na shirikisho hilo la vyama kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali ili kuboresha elimu na hususa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa ajili ya kuwapunguzia makali waliyonayo.

Kwa upande wao kaimu wakurugenzi wa halmashauri hizo za mji na wilaya, Archanus Kilaja na Ally Mwinyikombo, walisema kuwa mbali na chanagamoto walizonazo watu hao wenye mahitaji maalum,pia wanakabiliana na ukosefu wa huduma za kiafya katika vituo mbalimbali.

“Ndugu zetu hao tunafahamu kuwa wana chanagamoto mbalimbali kama vile kwenye miundombinu kutokuwa rafiki,ukosefu wa ajira,kubaguliwa na kunyanyaswa na umasikini,hivyo sisi kama halmashauri tutahakikisha tunashieikiana kwa pamoja kutatua kero hizo,” walisema.

Wakizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo ya Kondoa wakurugenzi hao walisema kuwa kwa kushirikiana na serikali itahakikisha inatatua kero walizokuwanazo watu wenye ulemavu ikiwa na kuwashirikisha katika vikao mbalimbali ili waweze kuleta mchango wao kwa ajili ya maendeleo.

Timu za CECAFA U-17 zawasili, kupimwa umri Muhimbili

IKIWA zimebaki siku tatu kabla ya michuano ya vijana ya kufuzu fainali za Afrika chini ya umri wa miaka 17, katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kuanza, timu zimeanza kuwasili nchini na kufanya vipimo vya afya na umri katika Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI). Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Katika taarifa iliyotolewa na shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF katika tovuti yao imesema utaratibu wa vipimo hivyo utaendelea leo katika taasisi hiyo kwa baadhi ya timu, huku timu ya Taifa ya Tanzania ‘Serengeti Boys’ imeshaanza kufanya vipimo hivyo jana na leo inaendelea na vipimo vingine.

Mashindano hayo yanatarajia kuanza Jumamosi tarehe 11 hadi 26 Agosti, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa na Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam.