Kubenea, Paresso, wanamtumia Lissu kuomba kura

WaBUNGE wa Chadema – Saed Kubenea (Ubungo) na Cecilia Paresso (Viti Maalum), mkoani Arusha – wamemtumia mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kumuombea kura mgombea udiwani wa kata ya Baray, wilayani Karatu, mkoani Arusha. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Tukio hilo lilitokea leo jioni wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Qangded, kilichopo katika hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo, Kubenea alimuomba Lissu ambaye wakati huo kuongea na wananchi wa kata hiyo ambayo ilikuwa inaongozwa na marehemu Thomas Moshi Darado. Lissu alikubali ombi hilo.

“…hapa nilipo niko na shujaa wa taifa hili, Mheshimiwa Tundu Lissu, ambaye nyote mnajua kilichompata. Yuko kwenye matibabu nje ya nchi. Anaomba kuzungumza na ninyi,” alisema Kubenea huku akishangiliwa na wananchi.

Naye Lissu akihutubia mkutano huo kwa njia ya simu aliwataka wananchi wa Qangded, kumchagua mgombea wa Chadema, Dagharo Hamay Kisimbi kwa maelezo kuwa ndiye mwenye sifa ya kufuata nyayo za diwani aliyekuwapo.

Alisema, “ndugu zangu wa kata ya Baray, mimi naitwa Tundu Lissu. Ninaongea kutoka nchini Ubelgiji ambako nimekuja kutibiwa. Kama ningekuwa na afya nzuri, basi leo ningekuwa nanyi hapo Baray.

“Mnajua kuwa marehemu  Tomas Darabe alikuwa rafiki yangu mkubwa. Hivyo basi, kwa heshima yake na heshima yangu kwenu, nawaomba sana mumchague diwani wa Chadema, ” alieleza.

Alisema, “katu wananchi wa Karatu, msikubali kurudishwa utumwani na CCM. Msikubali. Ninawaomba muendelee kutuunga mkono ili tuweze kuwahudumia.”

Kwa upande wake Kubenea alirejea kauli yake kuwa hana mapngo wa kuondoka Chadema na kuongeza kuwa wanaoeneza habari hiyo, “wanapaswa kupuuzwa.”

Alisema, “ndugu zangu nchi hii imejaa uonevu na njia pekee iliyosalia ya kuondoa uonevu huo na unyanyasaji, ni kukiondoa  Chama Cha Mapinduzi, madarakani.

“Nasikia watu wanasema nataka kujiunga na CCM. mimi siyo mtu wa kutanganga na wala siwezi kujiunga na chama kinachohubiri amani, lakini kikiwa kinatenda uhalifu.”

Aliwataka wananchi kumuenzi marehemu Darabe kwa kumchagua diwani  anayetokana na chama chake na ambaye kweli atakuwa mwakilishi wa wananchi.

Alisema, madai kuwa Chadema itashinda uchaguzi huo, lakini CCM ndio watakaotangazwa mshindi, hayana nafasi katika kata hiyo; yeye binafsi atakuwapo Karatu siku ya uchaguzi kuhakikisha mgombea wao anatangazwa mshindi.

Viongozi Tanga watakiwa kuwa wabunifu

VIONGOZI na watendaji wakuu wa halmashauri ya Jiji la Tanga wametakiwa kuwa wabunifu katika kuhakikisha wanawafikia wanawake wengi wanaoishi mjini ili waweze kujiunga na huduma za uzazi wa mpango. Anaripoti Khalifa Abdallah …. (endelea).

Wito huo umetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akifungua mkutano uliowakutanisha Viongozi na watendaji wakuu wa Halmashauri ya Jiji, Wilaya ya Tanga Mjini pamoja na Wilaya ya korogwe wenye lengo la kuendeleza juhudi za uzazi wa mpango nchini.

Waziri Ummy amesema kwamba Serikali ya awamu ya tano imejipanga kutokomeza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga hivyo imejipanga kuwafikia wananchi wengi ili kuweza kupunguza kwa asilimia 30 vifo vitokanavyo na uzazi.

“Lazima muonyeshe utayari na umakini kama viongozi katika kuwekeza kwenye uzazi wa mpango, mkiwa wabunifu mtawawezesha kuwafikia akina mama wengi wa mjini, hata akina baba kwa kuwapa elimu ya kutosha na kufanya maamuzi ili wapange lini wanataka kuzaa,watoto wangapi na watofautiane kwa miaka mingapi,” amesema Waziri Ummy.

Aidha, aliwataka viongozi kutumia fedha hizo kuziweka kwenye vitu endelevu ili mradi huo uongeze wanawake wengi kutumia njia za uzazi nchini.

“Msiweke mipango ya mardi huu kwenye semina bali mradi huu uwe njia ya kufungua miradi mingine kutoka kwa wadau wa maendeleo,” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa Serikali kupitia Wizara ya afya kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019 umetenga Sh. 14 bilioni kwa ajili ya afya ya uzazi wa mama na mtoto tofauti na miaka ya nyuma ambapo kabla Serikali ya awamu ya tano haijaingia madarakani wizara ilikua ikitenga Sh. 2 bilioni kwa ajili ya matumizi kitengo hicho.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kisa Kasongwe ambaye alimuakilisha Mkuu wa Mkoa wa Jiji la Tanga alisema halmashauri ya Jiji la Tanga ipo tayari kutoa ushirikiano na shirika hilo kwani mradi huo utaleta hali nzuri kwa akina mama pamoja na watoto wachanga.

Wakati huo huo Kaimu Mwakilishi Mkazi wa shirika la jhpiego Dk. Dustan Bishanga alisema kuwa mradi huo unakuja kuongeza rasiliamali ambazo hazitoshi katika kusimamia na kutekeleza katika uwekezaji wa uzazi wa mpango.

“Mradi huu utafanikiwa endapo viongozi wa Jiji la Tanga mtatekeleza na kufanya mpango huu kufanikiwa hivyo mtapelekea tuwaletee mradi mwingine wa afya ya uzazi kwa vijana endapo mradi huu wa kwanza mtaufanikisha ipasavyo,” amesema Dk. Bishanga.

Mradi wa “Tupange pamoja” ulianzishwa mwaka 2016 na kutekelezwa na halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Arusha ambapo kwa jiji la Dar es Salaam walipatiwa shilingi milioni 250 kwa ajili ya kutekeleza uzazi wa mpango kwa halmashauri zote na hivi sasa unaanza kwa Jiji la Tanga.

Idadi ya akina mama wanaotumia uzazi wa mpango kwa Jiji la Tanga ni asilimia 31 ambapo kitaifa inatakiwa kufikia asilimia 45 hadi mwaka 2020 na vifo vya akina mama kwa halmashauri hii imepungua kutoka vifo 69 mwaka 2014 hadi vifo 45 kwa mwaka 2017.

Utumiaji maji safi na salama, kinga kubwa ya kipindupindu

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesisitiza jamii ya Tanzania juu ya utumiaji wa maji safi na salama ili kuweza kupambana na ugonjwa wa kipindupindu kwa urahisi. Anaripoti Khalifa Abdallah … (endelea).

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara ya Afya) Dk. Mpoki Ulisubisya wakati wa ufunguzi wa kikao cha siku tatu cha kujadili mikakati ya kukabiliana na ugonjwa kipindupindu nchini kinachoendelea jijini Dodoma.

“Ili kupambana na ugonjwa huu Watanzania wanatakiwa kutunza mazingira hasa kutumia vyoo bora pamoja na kutumia maji safi na salama katika jamii inayotuzunguka,” amesema Dk. Ulisubisya.

Aidha Dk. Ulisubisya amesema kuwa hadi sasa kwa takwimu iliyopo inaonesha kuwa watu elfu 32 wameugua na watu 600 wamepoteza maisha.

Dk. Ulisubisya amesema kuwa ili kuweza kutokomeza ugonjwa huo mpaka kufikia 2030 wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya maji, TAMISEMI, na wadau wengine wa afya wanatakiwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kuweka mikakati ya kupambana na ugonjwa wa kipindupindu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Prof. Faustine Kamuzora amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaweka pamoja wataalam mbalimbali kwa ajili ya kuzuia ugonjwa wa kipindupindu nchini Tanzania.

Aidha Prof. Kamuzora amesema kuwa tayari wameshaandaa madawati mbalimbali ya wataalamu katika ofisi yake ili kuwexa kuweka mifumo ya kushughulikia kwa uharaka magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu.

Naye Afisa wa kudhibiti na kukinga Magonjwa kutoka Shirika la Afya Duniani hapa nchini Dk. Grace Saguti amesema kuwa kutokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali Serikali ya Tanzania imeweza kufanikiwa kutokomeza ugonjwa wa Kipindupindu kwa sehemu kubwa ya Tanzania.

“Mpaka hivi sasa mikoa inayokabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo yake ni Rukwa, Songwe na Arusha lakini maeneo yote yaliyobaki tumefanikiwa kutokomeza ugonjwa huo,” amesema Dkt. Saguti.

MWISHO.

Watu 13 wafikishwa mahakamani kwa uhujumu uchumi

WATU 13 wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwemo utakatishaji fedha wa Sh. 154 milioni. Anaripoti Khalifa Abdallah … (endelea).

Akiwasomea mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kelvin Mhina wakili wa serikali mkuu, Nassoro Katuga amedai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 5 ambayo wameyatenda katika mikoa tofauti.

Katika kosa la kwanza la kula njama ya kutenda kosa linawakabili washtakiwa wote ambapo wanadaiwa wamelitenda kati ya March 2018 na June 2018 katika jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Rukwa na katika maeneo mengine ya jamhuri ya Tanzania.

Pia kosa jingine ni kusambaza taarifa za uongo kupitia mfumo wa kompyuta ambapo wanadaiwa wamelitenda March na June 2018 wakiwa Dar es Salaam na Rukwa ambapo walichapisha taarifa za ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) ili kujipatia kipato.

Wakili Katuga amedai kosa jingine ni kusambaza jumbe (message) kwa njia ya Elektroniki kati ya March na June, 2018 kwa nia ya kudanganya na kushawishi kati ya Dar es Salaam na Rukwa walisambaza kwenda kwa watu tofauti tofauti ili kuonyesha wana mamlaka hayo.

Pia katika kosa jingine la kusambaza jumbe fupi za Kielektroniki, wanadaiwa walilitenda March na June, 2018 kati ya Dar es Salaam na Rukwa walisambaza jumbe zisizotakiwa kwa njia ya Kielektroniki.

Katika kosa la mwisho wanadaiwa ni utakatishaji fedha ambapo wanadaiwa wamelitenda kati ya March na June 2018 katika maeneo ya Dar es Salaam na Rukwa.

Inadaiwa kwa pamoja walijihusisha katika ufanyaji wa muamala wa Sh.Mil 154,032,830 ikiwa ni zao la kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, wakili Katuga amedai upelelezi haujakamilika ambapo Hakimu Mhina amesema kesi hiyo haina dhamana kwa sababu ni ya uhujumu uchumi, hivyo wataenda lumande ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi August 21,2018.

Katika kesi hiyo washtakiwa Boniface Maombe, David Luvanda, Moshi Sungura, Amos Bosco, Lule Kadenge, Jofrey Kapangamwaka, William Nturo, Regius Mauka, Collins Basham, Francis Kapalata, Kasonde Kapela, Enock Mwandaji na Pascal Kiatu.

Serikali Z’bar yafuta kongamano la maridhiano

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imefuta kongamano la kimataifa la kujadili mustakbali wa maridhiano Zanzibar lililokuwa lifanyike kesho. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Kongamano hilo ambalo lingeshirikisha watu kadhaa mashuhuri na wasomi wa Tanzania na nje ya nchi, limeandaliwa na Kituo cha Katiba cha Afrika Mashariki, asasi ya kitafiti inayojumuisha wanasheria mabingwa katika kanda ya Afrika Mashariki.

Ilikuwa ni matarajio ya wananchi hapa kwamba kupitia kongamano hilo wangepata taarifa za namna gani Zanzibar inaweza kuondokana na migogoro ya kisiasa na hasa huu unaoidhoofisha nchi kwa kuwa imegawanyika kutokana na kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015 uliokuwa umeonesha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilishindwa na Chama cha Wananchi (CUF).

Tangazo la kufutwa kwa kongamano lilitolewa ghafla jioni na halikuwa na ufafanuzi zaidi ya kusema, “tunaomba radhi kwa usumbufu uliosababishwa na taarifa yetu.”

Waandaaji wake wameiambia MwanahalisiOnline kuwa tangazo limetoka baada ya kikao kilichosimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib, Ayoub Mohamed Mfaume ambaye amenukuliwa akisema hali ya usalama inaweza kuharibika iwapo kongamano litaruhusiwa kufanyika.

Ayoub ambaye kwa nafasi yake ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, ametoa msimamo huo mbele ya waandaaji wa kongamano kwenye Hoteli ya DoubleTree by Hilton ya mjini hapa.

Kongamano lenyewe lilikusudia kuzungumzia mapendekezo ya kituo baada ya kufanya utafiti wa hali mbaya ya kisiasa iliyopo Zanzibar kutokana na kuvunjwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyokuwa imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2010.

Baada ya uchaguzi kufutwa kinyemela kwa tangazo la Jecha Salim Jecha aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kulifanywa kilichoitwa “uchaguzi wa marudio” ambao matokeo yake ni Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM, kutangazwa mshindi wa zaidi ya asilimia 90.

Aliunda serikali isiyokuwa na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na mpaka sasa ndiyo inayoendelea kuongoza huku CUF ikiipinga kwa kutoitambua.

Wadau wa kilimo washauriwa kuzalisha mbegu

WADAU wa kilimo na wakulima wakubwa kwa ujumla wameshauriwa kuanzisha makampuni ya mbegu ili kuifanya Sekta ya Mbegu kuwa na uzalishaji wa kutosha kwa mahitaji ya kilimo chenye tija hapa nchini. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Afisa Udhibiti Ubora wa Mbegu kutoka Taasisi ya Kudhibiti ubora wa mbegu Tanzania (TOSCI), Zera Mwankemwa alitoa rai hiyo jana wakati akiongea na mwandishi wa Habari hizi kwenye viwanja vya maonesho ya wakulima vya Mwalimu Nyerere 88 kanda ya Mashariki.

Mwankemwa amesema licha ya kuwepo kwa makampuni zaidi ya 50 yanayozalisha mbegu hapa nchini lakini bado kumekuwa na upungufu mkubwa wa mbegu na kuwafanya wakulima licha ya elimu wanayoipata kujikuta wakitumia mbegu zisizo bora na kupata uzalishaji usio na tija.

“Wakulima hasa wamaeneo ya vijijini baadhi wanajua nini maana ya mbegu bora lakini upatikanaji wake katika maeneo yao unawafanya kushindwa kutumia, na kutumia mfumo wa zamani na kupata uzalishaji kidogo,” amesema.

Amesema, licha ya changamoto za kuanzisha kampuni ya kuzalisha mbegu kuwa ni gharama kubwa lakini, isiwe sababu ya wadau wenye uwezo wa kuanzisha kuacha kujitoa kuanzisha kampuni kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kurudisha nyuma maendeleo ya kilimo nchini.

Mwankemwa amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora kwa maslahi ya kilimo bora na chenye tija ambapo alisisitiza wadau hao kufika TOSCI kupata maelekezo ya sheria za uanzashaji makampuni ambazo zipo wazi.

Aidha Mwankemwa alisema,TOSCI huwajibika kukagua mashamba ya mbegu ya kila Taasisi au kampuni na kuhakikisha mbegu zinazolimwa zinamwezesha mkulima kupata mbegu bora anayokusudia.

Amesema, sheria ya mbegu ya mwaka 2003 iliyofanyiwa marekebisho yaliyofanyika mwaka 2017 inamuongoza muanzishaji kampuni kusajiliwa na TOSCI huku pia akikaguliwa na TOSCI tofauti na zamani.

Hivyo aliwaomba wakulima kupita kwenye banda la hilo lililopo kwenye maonesho ya wakulima kupata elimu zaidi ya kutambua maana ya mbegu bora na jinsi ya kutofautisha mbegu bora na mbegu feki.

Naye Mkulima mdogo Lucas Simon amesema kuwa kupitia TOSCI ameweza kujifunza namna ya kuandaa mbegu bora sambamba na matumizi ya mbegu bora.

Amesema awali alikuwa na wasiwasi wa matumizi ya mbegu kwani hakuweza kujua mbegu bora ni ipi na feki ni ipi ambapo baada ya kupita kwenye banda hilo amepata uelewa ambao atakwenda kuwafundisha na wakulima.

Waganga wa kienyeji mbaroni Mwanza

JESHI la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu watatu kwa kosa la kufanya shughuli za uganga wa kienyeji bila kibali. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Akizungumza na wanahabari leo tarehe 8 Agosti 2018, Kamanda wa Polisi Mwanza, DCP Ahmed Msangi watuhumiwa hao, John Luzaria, Masanja Majige na Mariamu Ramadhani, wote wakazi wa Kijiji cha Mahando walikamatwa jana.

DCP Msangi amesema watuhumiwa hao pia walipatikana na vifaa vya kupigia ramli chonganishi .

“Watuhumiwa hao wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa kosa la kupatikana na vifaa vya kupigia ramli chonganishi na kufanya shughuli za uganga wa kienyeji bila kibali, kitendo ambacho ni kosa kisheria,” amesema DCP Msangi.

DCP Msangi amesema Polisi wapo katika upelelezi na mahojiano na watuhumiwa wote watatu, na kwamba pindi uchunguzi ukikamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamni.

“Aidha upelelezi na msako wa kuwatafuta watu wengine wanaojihusisha kwa namna moja au nyingine kufanya shughuli za uganga wa kienyeji bila kibali pamoja na upigaji wa ramli chonganishi katika maeneo hayo bado unaendelea,” amesema.

Museveni kufanya ziara nchini

YOWERI Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku moja hapa nchini ifikapo tarehe 9 Agosti 2018. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo 07 Agosti 2018 na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

“Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Rais Museveni atapokelewa na mwenyeji wake Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano na ujirani mwema uliopo kati ya Tanzania na Uganda, ambapo Rais Museveni atakutana kwa mazungumzo ya faragha na Rais Magufuli yatakayofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Rais Museveni na Ujumbe wake wataondoka nchini siku hiyo hiyo kurejea Uganda.

Serikali kuinadi Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima

PROFESA Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, amesema Serikali imejipanga kuandaa na kutoa mafunzo ya uwezeshaji wa programu za kisomo na kufanya kampeni kwa kanda za kitaaluma ili watu waelewe kazi za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima. Anaripoti Khalifa Abdallah … (endelea).

Ndalichako amesema hayo wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi hiyo ambayo baadhi ya watu wakiwemo wabunge bungeni walikuwa wakishinikiza ifutwe kufuatia kutokuwa na ufahamu wa majukumu ambayo taasisi hiyo inafanya.

“Watu wamekuwa wanauliza kuwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima inafanya nini lazima tufanye kampeni ya kisomo ili muonekane, watu wajue mnafanya nini na waweze kuja kujiunga,” amesema.

Profesa Ndalichako amesema kuwa imani yake ni kuwa Bodi hiyo mpya kwa kushirikina na Menejimenti ya Taasisi hiyo itaweza kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika.

Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 idadi ya wasiojua kusoma na kuandika imekuwa ni asilimia 22 ambayo Waziri Ndalichako amesema idadi hiyo ilikuwa kubwa hivyo ipungue.

Naye Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Naomi Katunzi amesema anamshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini kumpa nafasi hiyo na kuwa pamoja na nafasi mbalimbali alizowahi kushika katika serikali ya Tanzania lakini amebobea kwenye masuala ya mitaala hivyo kitendo cha Rais kumteua kuwa Mkurugenzi wa Bodi hiyo ambayo mitaala imezungumzwa kwa kiasi kikubwa ni kama amerudishwa nyumbani.

Amesema atahakikisha anaisimamia taasisi hiyo ipasavyo kama matakwa ya serikali ilivyotaka ili kuhakikisha idadi hiyo ya wasiojua kusoma na kuandika inapungua.

Tanesco, REA wapigwa marufuku kuagiza vifaa nje

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) limetakiwa kusitisha uagizaji wa viunganishi vya miundombinu ya umeme (Accessories) kutoka nje ya nchi ifikapo mwezi Novemba mwaka huu. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea)

Agizo hilo lilitolewa jana tarehe 6 Agosti, 2018 na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani wakati alipotembelea Kiwanda cha uzalishaji viunganishi cha Auto Mech Ltd kilichopo Tabata jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo baada ya kujiridhisha kwamba kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha viunganishi vya kutosha, ambapo aliitaka Tanesco kununua viunganishi vinavyotengenezwa hapa nchini.

 “Nimekuja hapa ili kujiridhisha kama Kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha viunganishi vya kutosha, nimejiridhisha kuwa, kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha viunganishi hivyo, kwa hiyo nimetoa miezi mitatu ili TANESCO, REA na Wakandarasi wote kwa pamoja wajiandae sasa kunua vifaa hivi nchini.” Alisema Waziri Kalemani.