Wizara ya Afya kufanya udahili wa wanafunzi

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, inatarajia kufanya udahili wa wanafunzi kwa asilimia 100 kutoka wanafunzi 150 hadi 180 wa kada za Afya nchini. Anaripoti Khalifa Abdallah … (endelea).

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) wakati wa hafla ya makabidhiano ya majengo ya chuo cha Uuguzi Tanga, yaliyojengwa kupitia ufadhili wa mfuko wa Dunia wa kupambana na UKIMWI, KIFUA KIKUU (TB) na MALARIA (Global fund).

Waziri ummy aliendelea kusema kuwa majengo yaliyokabidhiwa ni juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha wanazalisha wataalamu wa kada za Afya, hususani wauguzi na wakunga jambo litalowawezesha kuwa wataalamu bora.

“Udahili wa wanafunzi umeongezeka kutoka 190 hadi 260, Huwa tunapata shida sana, wanafunzi wengi wanafaulu na tunakuwa hatuna nafasi ya wapi pakuwapeleka, kwahiyo tunawashukuru Global fund, tunaweza kudahili hadi wanafunzi 368,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Aidha, amemwagiza Mkurugenzi wa Mafunzo na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Afya kushirikiana na NACTE kuwachukua wanafunzi wote waliosoma na kufaulu vizuri masomo nya Sayansi na wenye vigezo na wenye vigezo katika kada ya Afya.

Waziri Ummy aliongeza kuwa kutokana na jitihada hizo kumekuwepo na ongezeko la wahitimu ngazi ya astashahada na Stashahada kwa mafunzo kutoka wahitimu 4473 mwaka 2012/2013 hadi 7561 kwa mwaka 2016/2017, ongezeko hili ni sawa na Asilimia 69.

Wakati huo huo, Kaimu katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Otilia Gowelle amesema kwa mwaka huu wa fedha , Wizara imetenga shilingi Bilion 8 kwaajili ya ukarabati wa majengo chakavu katika chuo hicho.

Aliendelea kuwa Wakufunzi 143 wamepangiwa kufanya kazi katika vyuo vya Afya nchini, vikiwemo vyuo vya Wauguzi na Wakunga ambao ndio msingi wa kupunguza athari ya uzazi pamoja na vifo vya wakina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Nae Mwakilishi wa Global Fund Dk. Eltrudis Temba amesema kuwa, Global fund imeboresha miundombinu yakufundishia katika vyuo 14 na kuwezesha kufadhili zaidi ya wanafunzi 1500 wa kada za Uuguzi na Ukunga wa Technolojia dawa, Technolojia maabara na Tabibu katika kipindi cha Mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018, pamoja na kutenga shilingi Billion 1.1 kwaajili yakuboresha mifumo ya Afya.

Kampuni ya Ulinzi wamwita Waziri Mhagama

WAFANYAKAZI wa kampuni ya ulinzi ya Tele Security Campan Ltd wamemuomba Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama kuingila kati mgogoro uliopo kati ya wafanyakazi hao na kampuni kutokana na fedha zao kutoingizwa katika mfuko wa jamii NSSF. Anaripoti Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Wafanyakazi hao wakizungumza na vyombo vya ulinzi walisema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiwakata fedha zao kwa madai kuwa wanaingiza katika mfuko wa jamii lakini fedha hizo hazipelekwe kama inavyotakiwa.

Hata hivyo walisema kuwa viongozi wa kampuni hiyo wamekuwa wakiwafukuza kazi wafanyakazi ambao wamekuwa wakionesha nguvu ya ushawishi wa kudai pesa zao kwa ajili ya mafao.

Mmoja wa wafanyakazi ambaye alijitambulisha kwa jina la Mlugu Chilewa alisema kuwa tangu mwaka 2011 hadi sasa.

Chilewa alisema kuwa katika mwaka 2011 kampuni ilikuwa ikiwakata sh.11500 kwa ajili ya NSSF na ilipofika mwaka 2016 mwezi wa pili walikanza kukatwa kiasi cha sh 11700 ambazo nazo haziingizwi NSSF.

Naye Ruzoya Julius alisema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiwatishia kuwafukuza kazi au pale wanapokuwa wakidai mafao yao.

Aidha alisema kuwa wafanyakazi wa kampui hiyo wanapoendelea kudai makato yao yapelekwe kwenye mifuko ya jamii wanaambiwa waandike barua ya kuacha kazi ndipo waweze mafao yao yawee kupelekwa kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii.

Kutokana na hali hiyo wamekuomba Waziri mwenye dhamana Jenistara Mhagama kuingilia kati ili kuweza kutatua hali hiyo kwani inawafanya wafanyakazi wa kampuni hiyo kuishi Maisha magumu na yenye wasiwasi.

Mbali nahilo walisema pamoja na kukatwa hela hizo bado kampuni haipeleki makato NSSF na kampuni haichangii fedha kama inavyotakiwa kisheria.

Alipoulizwa Meneja wa Kampuni hiyo kanda ya Dodoma Fidelisi Luhunga kuhusu malalamiko hayo alisema kuwa yeye siyo msemaji wa kampuni ila msemaji mkuu ni meneja wa Kampuni ambaye yupo Jijini Dae es Salaam.

Hata hivyo alisema yupo mtu mmoja ambaye anakusanya fedha zote kwa ajili ya kuziingiza katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii.

Alipotafutwa Mkurugenzi mkuu ambaye alijitambuliwa kwa jina moja la Mkeni kwa ajili ya kutoa ufafanuzi juu ya malalamiko hayo alisema kuwa yeye awezi kusema lolote wenye majibu ni NSSF.

Hata hivyo NSSF walithibitisha kuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo hawana fedha yoyote na majina yao hayapo.

Kangi Lugola azivaa kampuni za ulinzi

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ametoa mwezi mmoja kwa Kampuni binafsi za Ulinzi kuhakikisha yanarekebisha mfumo wao wa kuajiri pamoja na utoaji wa mishahara kabla ya Wizara yake haijaanza kuyahakiki makampuni hayo. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Akizungumza na mamia ya wananchi mjini Bunda, mkoani Mara katika mkutano wa hadhara uliofanyika Stendi ya zamani mjini hapo, Waziri Lugola alisema, Serikali ya awamu ya tano kamwe haitataka uzembe, hivyo makampuni hayo yanayovunja utaratibu huo siku zao zinahesabika.

“La kwanza kabisa makampuni haya yanafanya mambo ya hovyo kwa kuajiri vikongwe kufanya kazi za ulinzi, utamkuta kikongwe kavaa sare ukimuuliza anasema mimi ni mfanyakazi wa kampuni fulani, hii haikubaliki hata kidogo, kwasababu kwa umri ule hawawezi kupambana na wahaarifu, na kwa umri ule muda wote usinzia na baadhi yao unyang’anywa silaha,” amesema Lugola.

Pia lugola amesema kitendo cha baadhi ya makampuni hayo kulipa mishahara midogo, au kutowalipa kabisa wafanyakazi hao, hiyo hali inasababisha uhalifu kwasababu wafanyakazi hao hawataridhika na kipato duni hivyo uweza wakashirikiana na wahalifu au wenyewe kushiriki matukio hayo.

“Nataka makampuni haya yajirekebishe na yasipojirekebisha ndani ya mwezi mmoja ambapo tunataka kuyaakiki makampuni haya, wasije wakamlaumu waziri wa mambo ya ndani ya nchi ambapo yapo baadhi ya makampuni tutaondoa tulichoridhia ili wasifanye kazi katika nchi hii,” amesema Lugola.