Wafugaji washauriwa kutumia dawa za mifugo

WAFUGAJI hapa nchini wameshauriwa kuzingatia matumizi ya dawa za mifugo wanayopewa na wataalamu ili kuongeza kipato na kuboresha uchumi wao na Taifa kwa ujumla. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Kiwanda cha usambazaji Dawa za Mifugo na Kilimo nchini Farmbase Ltd, Suleiman Msellem wakati akimuelewesha Mkuu wa Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Sauda Mtondoo alipotembelea banda hilo lililopo kwenye maonesho ya wakulima ya Mwalimu Nyerere 88 Kanda ya Mashariki.

Msellem amesema, kwa kufuata ushauri wa kitaalam na kutumia dawa ya kuogeshea mifugo inayotengenezwa na kampuni hiyo ijulikanayo kama Paranex inayodhibiti magonjwa ya mifugo kwa asilimia 80 kutasaidia wafugaji kumudu na kutotetereka na ufugaji.

Amesema, dawa hiyo inayopatikana Tanzania pekee kati ya nchi za Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza awali ilikuwa ikipatikana nchini Uswis Pekee ambapo kufuatia Kiwanda hicho kuanza kuizalisha hapa nchini inapatikana kwa bei nafuu kwa ajili ya wafugaji wa hapa nchini na nchi za jirani.

Hivyo amesema kuwa dawa hiyo inayouzwa kwa bei ya sh 35,000 hapa nchini kunawezesha wafugaji kutoka nchi zingine kuinunua kutoka Tanzania na hivyo kuiingizia nchi mapato tofauti na zamani walikuwa wakinunua nje ya nchi na kupeleka fedha huko.

Pia amesema, dawa hiyo husaidia hata kwa kuzuia magonjwa kwa mazao shambani kama ikitumiwa wakati wa kuandaa shamba na kwamba Farmbase ilishawahi kwenda kutoa elimu kwa msimu wa kilimo wa mwaka jana katika mikoa ya Pwani na Morogoro pindi walipokumbwa na changamoto ya wadudu waharibifu wa mazao shambani.

Hata hivyo Msellem amesema, Farmbase inampango wa kuhakikisha dawa nyingi zaidi zinazalishwa katika Kampuni hiyo ambayo tayari imeshaanza kufanya kazi kwa kasi ili kusaidia wafugaji kupata dawa na utaalam kwa wepesi na pia kuboresha mapato ya nchi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga Sauda Mtondoo aliwashauri wasambazaji hao kuona umuhimu wa kufungua matawi yao maeneo mbalimbali hasa walipo wakulima na wafugaji ili kuweza kuwarahisishi upatikanaji wa huduma hizo muhimu.

Mtondoo amesema, kutomsogeze huduma mkulima au mfugaji kumesababisha watu kuzikosa na pengine kutumia wanazopata mbali kidogo na bila kuzingatia kiasi kamili wakizilinda zisiishe na hivyo kutoleta ufanisi unaokusudiwa.

Akizungumza katika Maonesho hayo mfugaji mmoja Richard Rwegerela ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuiunga mkono Farmbase kufuatia kujikita katika kuzalisha dawa za mifugo na kilimo na kuweza kuwakomboa wakulima na Taifa kwa ujumla.

Serikali yaendelea kulisakama TWAWEZA

SHIRIKA linaloshughulika na masuala ya utafiti nchini, linalofahamika kwa jina la TWAWEZA, lidai kutishwa na vyombo vya serikali. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Kutishwa kwa watendaji wa Twaweza, kumethibitishwa leo tarehe 3 Agosti 2018 na Mkurugenzi Mtendaji wake, Aidan Eyakuze.

Hata hivyo, Eyakuze amesema, “pamoja na kupokea vitisho hivyo, shirika langu litaendelea kufanya kazi zake za kitafiti na halitakubali kurudishwa nyuma.”

Eyakuze aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuwa kwa sasa shirika lake, linapita katika kipindi kigumu chenye changamoto nyingi.

Amesema, “…hatutatikisika. Hatutarudi nyuma. Twaweza litaendelea kufanya kazi zake kwa mujibu wa misingi na sharia za nchi.”

Amesema, tangu shirika hilo litoe taarifa zake za kitafiti mbili kupitia wanachoita, “Sauti za Wananchi,” mahusiano yake na taasisi za serikali yamekuwa mabaya.

Amesema, “tangu Twaweza izindue ripoti zake, imepokea barua mbili kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), zilizohoji uhalali wa program (mpango) ya Sauti za Wananchi na kutaka litoe ufafanuzi kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yetu.”

Tarehe 5 Julai mwaka huu, Twaweza ilizindua ripoti mbili zenye vichwa vya habari, “Kuwapasha viongozi na Nahodha wa Meli yetu wenyewe,” ripoti ambazo zinaonekana kuwaudhi baadhi ya viongozi serikalini.

Katika moja ya ripoti hizo, Twaweza walidai kuwa umaarufu wa Rais John Pombe Magufuli, umeshuka kutoka asimilia 96 mwaka 2016 hadi asilimia 71 mwaka 2017.

Akiongea kwa kujiamini, Eyakuze amesema, uhuru wa shirika lake katika kutekeleza majukumu yake, wanaupa kipaumbele kikubwa, hasa wakati wa kufanya kazi za kitafiti, ikiwamo kuhoji na hata kutoa majibu ya utafiti.

“Tumekubaliana kuwa tutaendelea kufanya kazi zetu pasipo kujibana na kujidhibiti. Tutafanya kama kawaida na kwa kushirikiana na serikali,” ameeleza.

Kwa mujibu wa Twaweza, kati ya Watanzania 10, saba wanaunga mkono utendakazi kazi wa Rais Magufuli.

Hii ina maana kuwa umaarufu wa Rais Magufuli umeshuka kwa asilimia 25, jambo ambalo linaonekana kuikera serikali.

TRA yapewa ushauri kuokoa makusanyo ya kodi

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeshauriwa kuweka mikakati thabiti itakayowezesha kudhibiti upotevu wa makusanyo ya kodi yatokanayo na sekta madini kuanzia kwa wachimbaji wadogo na kuiingizia Serikali mapato. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Sauda Mtondoo amesema hayo wakati alipotembelea banda la TRA lililopo kwenye maonesho ya wakulima ya Mwalimu Nyerere 88 Kanda ya Mashariki yaliyopo kwenye eneo la Tungi mkoani hapa.

Mtondoo amesema kuwa bila ya kuweka mikakati ya makusanyo kwa sekta hiyo ya madini wanaweza kujenga nafasi kubwa ya upotevu wa mapato kufuatia kwa sasa kushughulika na wachimbaji wenye leseni pekee na kuwaacha wasio na leseni na hivyo kupoteza mapato ya Serikali.

Akizungumzia hilo, Ofisa Huduma na Elimu kutoka Makao Makuu TRA, Patrick Ezekiel amesema, TRA tayari imeshaandaa mipango ya kutathmini shughuli za wachimbaji wadogo wa madini na kisha kuangalia namna ya mapato wanayostahili kuyatoa na kuweza kuingiza serikalini.

Ezekiel amesema, kwa kushirikiana na Wizara ya Madini watahakikisha wanazitambua Sekta husika na kuzirasimisha kwa kuanzia na vikundi vidogo vidogo ambapo tayari wameshaanza na wamachinga.

Amesema, katika sekta ya madini kuna wachimbaji, wachenjuaji, madalali na wasafirishaji ambao wote kwa pamoja wanahitajika kulipa kodi kwa manufaa ya Umma.

Aidha amesema, mpango mkakati wa jinsi ya kufanya makusanyo ya kodi na kuongeza mapato ya Serikali kupitia sekta hiyo mtambuka unaweza kutolewa baada ya miezi 2-3 ijayo.

Simba watangaza viingilio vya ‘Simba Day’

MABINGWA wa Tanzania Bara Simba kupitia mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wao Haji Manara wametangaza vingilio katika tamasha lao kubwa la kila mwaka ‘Simba Day’ ambalo litafanyika tarehe 8 Agosti, 2018 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Vingilio hivyo katika tamasha hilo vitakuwa Sh. 5,000 kwa mzunguko, Sh. 20,000 kwa VIP A na Sh 15,000 kwa upande wa VIP B.

Manara amesema wameweka vingilio vya bei ya chini kwa lengo la kutoa nafasi kwa mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo waweze kupata fursa ya kuja kwa wingi kuisapoti timu yao.

Simba ambao kwa sasa wameweka kambi nchini Uturuki wanatarajia kucheza na klabu ya Asante Kotoko ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu nchini Ghana.

Watekaji waliotumia gari ya UN, wanaswa

JESHI la Polisi Kanda Maluum ya Dar es salaam linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuteka watu na kudai fedha kwa  kutumia gari yenye namba za Umoja wa Mataifa (UN) ambazo ni T 452 CD 639 Toyota Land Cruiser huku ndani ya gari hilo wakiwa na watu watano waliowateka. Anaripoti Khalifa Abdallah … (endelea).

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema watuhumiwa hao ni Hussein Shilingi (30) mkazi wa Kimara Mwisho na Martin Pumba (35) makazi wa Tabata.

Mambosasa amesema baada ya upekuzi ndani ya gari hilo walifanikiwa kukamata vifaa vilivyokuwa vikitumiwa na wahalifu ambavyo ni, redio call moja, pingu jozi tatu, plate namba za magari za mashirika ya serikali, namba za umoja wa mataifa na namba za watu binafsi, kitambulisho cha kughushi chenye nembo ya polisi chenye jina la Martin Pumba.

Vitu vingine walivyokutwa navyo ni pamoja na simu za mikononi za aina mbalimbali, kadi za simu, panga moja, sime mbili, nondo moja, marungu matatu, visu vikuba vinne, maganda matatu ya risasi yanayodhaniwa kuwa ni ya bunduki aina ya SMG, mkasi mkubwa mmoja na karatasi za maelezo ya watu mbalimbali waliokuwa wanawateka pamoja na hirizi mbili.

Mambosasa amesema watuhumiwa  hao walikamatwa tarehe 26 Julai, 2018 maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) wakiwa na gari yenye namba za umoja wa mataifa (UN) ambazo ni T 452 CD 639 Toyota Land Cruiser huku ndani ya gari hilo wakiwa na watu watano waliowateka.

Jeshi la Polisi lilifanya mahojiano na watu waliotekwa na walieleza kuwa walitekwa katika kipindi cha kuanzia tarehe 23 hadi 25 Julai, 2018 na walikuwa wanatakiwa kutoa Sh. 60 milioni, ambapo watekaji hao walikuwa wanatumia mbinu ya kupiga simu kwa ndugu au jamaa wa waliowateka na kudai fedha hizo ili waweze kuwaachia huru mateka hao.

Inaelezwa kuwa  watuhumiwa hao wamekuwa  wakibadili namba za magari pindi wanaapomaliza kuteka watu ili wasigundulike kwa haraka.

Aidha amesema wanaendelea na mahojiano na watuhumiwa ili kubaini watu wanaoshirikiana nao na watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao.

Mkurugenzi Twaweza anyang’anywa ‘Passport’

MAOFISA wa Uhamiaji wamemnyang’anya Hati ya Kusafiria (passport) Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti isiyo ya kiserikali Twaweza Aidan Eyekuze. Anaandika Regina Kelvin … (endelea).

Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo katika ukurasa wake wa twitter ameandika kuwa ‘baada ya wiki kadhaa taasisi hiyo kuchapisha utafiti wake na matokeo kuonesha umaarufu wa rais kushuka. Hati ya kusafiria ya Eyekuze imekuckuliwa na uhamiaji.’

Julai 6, Twaweza ilieleza utafiti wake kwamba, Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli umeshuka kutoka asilimia 96 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 55 mwaka huu.

Na kwamba, asilimia 55 ya wananchi wanaukubali utendaji wa Rais Magufuli tangu alipoingia madarakani mwaka 2015. Kukubalika huko kulipungua kutoka asilimia 96 mwaka 2016, na 71 mwaka 2017.

Kiwango cha kukubalika kwa Rais kimeshuka kutoka kwenye rekodi ya juu kuwahi kuwekwa na Rais wa Tanzania mpaka rekodi ya chini tangu takwimu hizi zianze kukusanywa mwaka 2001.

CAF yawatoa kifungoni waamuzi wa Tanzania

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Africa (CAF) limetoa majibu ya uchunguzi wa waamuzi wanne wa Tanzania waliofikishwa kwenye Shirikisho hilo kufuatia kuripotiwa kwa vurugu kwenye hoteli waliyofikia nchini Burundi walipokwenda kuchezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Africa Kati ya Rayon ya Rwanda na Lydia Ludica kutoka nchini Burundi. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Waamuzi hao ambao ni Soud Idd Lila, Frank John Komba, Mfaume Ali Nasoro na Israel Mujuni walikuwa katika hali ya sintofahamu baada ya kuibuka kwa vurugu kubwa katika hoteli waliofikia kutokana ya madai ya kuwa moja ya timu hizo mbili ilitaka kupanga matokeo kupitia waamuzi hao.

Taarifa iliyotolewa na shirikisho la mpira wa miguu nchni TFF, ilisema CAF, kupitia Katibu wake Mkuu Amr Fahmy ilijilidhisha kuwa hakuna jambo lolote baya lililowazunguka waamuzi hao kuhusiana na mchezo huo uliochezwa tarehe 21 Februari, 2018 katika dimba la Prince Louis Rwagasore, Burundi. Na hivyo wapo safi kuendelea na majukumu yao.

Kikwete: Asante serikali, asante wadau

RIDHIWANI Kikwete, Mbunge wa Chalinze mkoani Pwani ameeleza kufurahishwa na namna serikali na wadau wa maendeleo wanavyoshiriki kulivusha Jimbo la Chalinze katika vikwazo mbalimbali ikiwempo sekta ya afya. Anaripoti Yusuph Katimba … (endelea).

Ameeleza hivyo baada ya serikali kuipatia Halmashauri ya Chalinze Sh. 1.3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya katika maeneo ya Kibindu, Mkange na Lugoba kwa lengo la kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi.

Ridhiwani ametoa pongezi hizo wakati akipokea msaada wa vifaa vya ofisi kutoka Taasisi ya Tanzania Health Promotioni Support (THPS).

“Fedha hizi zimetolewa katika kutekeleza mpango wa kujenga vituo vya afya kwenye Halmashauri ya Chalinze,” amesema mbunge huyo na kuongeza;

“Kituo cha Afya Kibindu kimepatiwa shilingi milioni 420 na kituo cha afya Mkange kimepata katika hatua za mwisho kukamilika, milioni 700 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Lugoba.”

Ridhiwani amesema kuwa, pamoja na mchango wa wadau katika juhudi za kukabiliana na afya kwa wananchi wake, serikali imetoa madaktari 47 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze.

Amesema kuwa, lengo la serikali kutoa madaktari hao ni kupunguza tatizo la watoa huduma ya afya ambapo Hospitali ya Wilaya Msoga watapatiwa madaktari 10.

Ridhwani ambaye ni mtoto wa Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete amesema kuwa, msaada huo unaeleza ni kwa namna gani serikali imekuwa bega kwa bega na wananchi katika kuhakikisha hawatembei umbali mrefu kupata huduma hiyo muhimu.

Mwakilishi wa THPS, Sisty Moshi amesema, taasisi yao kupitia usaidizi wa Serikali ya Marekani imekuwa ikisaidiana na serikali kutoa huduma ya afya.

Na kwamba, kwa sasa imekuwa ikijihusisha katika utoaji wa huduma kwenye Mikoa ya Kigoma, Pwani na Zanzibar na ikijielekeza zaidi katika utoaji wa huduma ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI katika utoaji wa huduma na tiba.

Mzee Majuto alazwa tena Muhimbili

MFALME wa maigizo ya uchekeshaji nchini, Amri Athuman anayefahamika kama ‘Mzee Majuto’ amelazwa chumba cha wagonjwa mahtuti (ICU) kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Taarifa hizo zimethibitishwa na Afisa Habari wa Chama cha Waigizaji, Masoud Kaftany ambaye amesema kuwa, Mzee Majuto kwa sasa anafanyiwa vipimo ili kubaini ugonjwa unaomsumbua.

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano Hospitali ya Taifa ya Muhimbilli, Aminiel Aligaesha amethibitisha uwepo wa Mzee majuto hospitalini hapo.

Aligaesha amesema Mzee Majuto yuko kwenye chumba cha wagonjwa mahututi hospitalini hapo, baada ya kuletwa siku ya Jumanne majira ya saa kumi na mbili jioni.

Mnangagwa ashinda uchaguzi Zimbabwe

RAIS wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ameshinda uchaguzi wa urais nchini Zimbabwe kwa kwa asilimia 50.8 ya kura dhidi ya mpinzani wake wa karibu kutoka chama cha MDC, Nelson Chamisa aliyepata kura 44.3%.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC), kura hizo zimetoka katika majimbo 10.

Polisi waliwaondoa upinzani wakati wa kutangazwa matokeo baada ya kukataa kuyakubali matokeo hayo.

Mwenyekiti wa chama cha MDC Alliance, Nelson Chamisa amesema kuhesabiwa kwa kura hakukufanyiwa uhakiki.

Kwa ushindi wa asilimia 50 wa Mnangagwa umesababisha aepuke kwenda duru ya pili ya uchaguzi dhidi ya Chamisa.

Rais Mnangagwa amesema katika ukurasa wake wa Twitter kuwa huu ni mwamzo mpya.