Sheikh Ponda: Nakwenda Hijja kusoma dua nzito

SHEIKH Ponda Issa Ponda, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu anasema, anakwenda Hijja leo Agosti 02, 2018 pamoja na kutekeleza Nguzo ya Tano ya Kiislam pia atasoma dua nzito kwa ajili ya taifa. Anaandika Faki Sosi, … (endelea).

Kupitia taarifa yake aliyoituma kwenye vyombo vya habari leo Sheikh Ponda amesema kuwa, kwanza anakwenda kufanya ibada kama ilivyo kwa mahujaji wote Tanzania na duniani.

“Ninakwenda Hijja kutekeleza ibada ya Hijja kama nguzo ya Tano ya Kiislam. Kwangu na kwa Mwislam yoyote anapaswa kutekeleza hilo anapokuwa na uwezo.

“Kutokana na mwenendo wa taifa leo, kwangu nimeona ni firsa nzuri kuliombea taifa kwani mambo hayaende kama wengi tulivyotarajia. Kuna matukio mengi ya kuogopesha yanatokea na huenda yakaonekana kuwa ya kawaida hapo baadaye,” amesema Sheikh Ponda.

Sheikh Ponda amefafanua kuwa, nchi kwa sasa ipo kwenye wakati mgumu katika masuala ya haki, uchumi na kwamba, sasa ni fursa kumshtakia Allah kwa wale wanaotenda vitendo visivyo vya kibinaadamu.

“Natoa wito kwa mahujaji wengine wa Tanzania kuungana nami kwenye maombi ili Allah afanye wepesi kuinusuru nchi yetu.

“Hili lisiwe la Waislam pekee, kila mmoja na kwa Imani yake ni wakati sasa kumwelekea Mwenyezi Mungu kuhakikisha jambo hili analiondoa kwa namna anavyotaka yeye,” amesema Sheikh Ponda.

Miongoni mwa matukio anayotaja kuogofya ni pamoja na utekaji wa watu kiholela, mauaji ya raia wasio na hatia, vitisho kutoka kwa viongozi pamoja na kuminywa kwa uhuru wa habari na kujieleza.

“Kinachotutokea ama kinachofanywa na watawala kinatuathiri wote hivyo kila mmoja anawajibika kupinga kwa namna inayofaa,” amesema.

Zimbabwe kwatifuka, watatu wauawa

WAFUASI wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe (MDC) wameingia barabarani kwa maandamano baada ya kukishtumu chama tawala Zanu- PF kuingilia uchaguzi huo kwa kuiba kura za ubunge na urais. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Katika ghasia hiyo watu watatu waliripotiwa kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa baada ya vikosi vya Usalama vilipojaribu kutuliza vurugu hizo za wafuasi wa MDC, chini ya kiongozi wao mkuu Nelson Chamisa ambaye yupo kwenye mchuano mkali na Emmerson Mnangawa wa Zanu- PF.

Jeshi la nchi hiyo leo limeonekana likipiga doria katika miji tofauti huku likiwataka wananchi wa nchi hiyo kuwa na nidhamu wakati wakiwa wanasubiri matokeo ya urais huku hali hiyo ikionekana kuzua hofu miongoni mwa wafanya biashara mpaka kufikia hatua ya kufunga maduka.

Baada ya kutokea vurugu hizo umoja wa mataifa (UN) kupitia Katibu Mkuu wake Antonio Guterres amesema serikali nchini humo inatakiwa kuhakikisha kuwa vurugu hizo hazitokei mpaka kusababaisha polisi kufyatua risasi kwa wandamanaji.

Mpaka kufikia siku ya jana Zanu-PF ambayo inaongozwa na Rais wa sasa wa nchi hiyo Emmerson Mnangawa ambaye pia ni mgombea kwenye kinyang’anyiro hicho inaonekana kuongoza kwa wingi wa viti katika nafasi ya Ubunge baada ya matokeo ya awali kutangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi ya nchi hiyo.

Uchaguzi huo unakuwa ni wa kwanza nchini Zimbabwe tangu Rais wa muda mrefu Robert Mugabe kuondolewa madarakani na jeshi.

Posa ya CCM yahamia kwa Mbowe

VUGUVUGU la madiwani wa upinzani kukimbilia Chama Cha Mapinduzi (CCM) halijapoa, jimboni Hai, Kilimanjaro katika Kata ya Kia, diwani wake amehamia chama tawala. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Timoth Laizer, ambaye alikuwa diwani wa kata hiyo kupitia Chadema sasa ni mwanachama wa CCM. Jimbo la Hai ndio linaongozwa na Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa.

Laizer leo tarehe Agosti 2, 2018 amesema kuwa, ameamua kuhama  Chadema kwa sababu alizozitaja kuwa ni kutoridhishwa na maelekezo yanayotolewa na uongozi wa chama hicho yakutoshiriki wala kutotambua kazi ya maendeleo inayofanywa na Serikali ya CCM.

“Nimeamua kujiunga nha CCM chama pekee kilichobaki kuwatetea wanyonge katika nchi hii  kutokana na ukweli kwamba siwezi kuendelea kuwa kwenye chama kinachotupa maelekezo ya kutoshiriki wala kuzitambua kazi zozote zinazofanywa na Serikali wakati kiuhalisia serikali ya Rais John Magufuli ndio iliyoweza kupambana na shida na dhiki za watanzania wanyonge ” amesema Laizer.

Mtoto wa Mbunge Chadema aibua mjadala kesi ya Mbowe, wenzake

MTOTO wa mbunge wa Chadema katika jimbo la Tarime Mjini, Easter Matiko, ameibua mjadala kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kufuatia mama yake huyo mzazi kutotokea mahakamani. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Matiko, ni miongoni mwa viongozi wandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, wanaokabiliwa na kesi ya jinai katika mahakama hiyo.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama ya Kisutu, Wilbard Mashauri, wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, leo tarehe 2 Agosti, ameiambia mahakama kuwa upande wa mashtaka hauna taarifa za kutokuwepo mbele ya mahakama kwa mtuhumiwa namba tano katika kesi hiyo – Easter Matiko.

Awali kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala, ameieleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo amepata dharula ya haraka ya kutakiwa afike shuleni kwa mtoto wake mjini Nairobi nchini Kenya.

Kibatala aliiomba mahakama imruhusu mdhamini wa wake, Patric Assenga, ambaye ni diwani wa kata ya Tabata, eleze dharula aliyopata mdhamana wake.

Asenga alisema, alipewa taarifa na mdhamana wake (Matiko), kuwa jana usiku alipigiwa simu kutoka katika shule anayesoma mtoto wake jijini Nairobi kuwa anatakiwa kufika haraka kuna dharula juu ya mtoto wake.

Baada ya kueleza hayo, wakili Nchimbi ameleza kuwa ana mashaka na kinachoitwa, “dharula ya Matiko,” kwa kuwa hata mawasiliano kati yake na mdhamini wake (Asenga), ambayo yaliyowasilishwa mahakamani, yanaonesha kuwa yaliyafanyika leo saa 3 asubuhi.

“Kama angekuwa ameondoka jana, kama inavyoelezwa, hadi muda huo angeweza kueleza sababu ya kuitwa ghafla shuleni Niarobi,” alieleza Nchimbi.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mashauri alimtaka Asenga kufuatilia kilichosababisha Matiko kuondoka ghafla kuelekea Nairobi.

Aidha, Nchimbi aliomba mahakama kupanga usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo, kufanyika tarehe 6 Agosti.

Hata hivyo, Kibatala alitaka mahakama kupanga siku nyingine kwa madai kuwa tarehe iliyopendekezwa na wakili wa serikali, inakinzana na ratiba yake.

Alisema, siku hiyo atakuwa kwenye Makama Kuu kusikiliza rufaa ya marejeo katika shauri ambalo limefunguliwa na watuhumiwa.

Kibatala akataja pia siku inayofuata, tarehe 7 Agosti kuwa na mashauri mengine Mahakama Kuu; huku tarehe 8 Agosti, akiielezea kuwa mtuhumiwa namba mbili, Peter Msigwa, atakuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi, mkoani Iringa, kusikiliza kesi zinazomkabili.

Baada ya ubishani huo, Hakimu Mashauri, alipanga  tarehe 6 Agosti, kuwa utafanyika usikilizwaji wa awali.

Katika kesi hiyo, mbali na Matiko na Msigwa,  waoshitakiwa wengine, ni pamoja na Freeman Mbowe,  Dk. Vicent Mashinji, Halima Mdee, John Mnyika na Easter Bulaya.

Kushika dola si kazi

VYAMA vingi vya siasa vimejaa ubinafsi, tamaa ya madaraka na kutaka kushinda uchaguzi ili kutawala. Ajenda hiyo ni rahisi mno. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Ni sawa na ule usemi usemao kubeba mimba si kazi kazi ni kulea mtoto. Kushika dola si kazi, kazi ni kutawala na kukidhi maslahi ya wananchi wanyonge.

Viongozi wa vyama hujirudisha wenyewe nyuma, moja ya ufafanuzi wa chama kushika hatamu uliowahi kutolewa na Muasisi wa CCM, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wake alisema kuwa, serikali ni chombo chenye maguvu ambayo yanataka kudhibitiwa.

Ndio maana vyama vya siasa vinashindana ili kinachoshinda vishike hatamu za kuongoza yale maguvu ya kutii maagizo ya viongozi.

Lakini neno hatamu ni ile kamba inayomwongoza farasi kwani mbali na maguvu yote aliyonayo farasi lakini ukishashika ile hatamu basi itamuongoza unavyotaka atatii.

Ukitaka akimbie atakimbia, ukitaka akate kona atakata. Hii ndiyo maana ya chama kushika hatamu za uongozi.

Hivyo viongozi wa vyama vya siasa wana wajibu mkubwa wa kuiambia serikali na kuikosoa ili itende kile kinachotakiwa na wananchi.

Vyama vingi vilivyoogopa kufanya mabadiliko ndani ya chama vimeng’oka kirahisi madarakani hivyo ni funzo kwa vyama vingine vya siasa vinavyotaka kushika dola.

Lazima vyama vyao viwe na muundo na mfumo imara utakaokifanya kuimarisha chama kwani chama legelege huzaa serikali legelege.

Vyama vinapopata misukosuko mikubwa kulingana na tawala na ili kubaki imara, vinapaswa kubadili mbinu na si kupiga yowe.

Jambo kubwa katika maendeleo ya nchi ni kuendeleza demokrasia yenyewe na sio muundo unaoiendesha demokrasia.

Baadhi ya vyama vya siasa vinashindwa kutumia demokrasia katika kuchuana kugombea uongozi hata vijana au wanawake ndani ya vyama hivyo kutokana na uimla na ubabe.

Ningependa kuungana na mawazo ya Mwalimu Nyerere kwa kusisitiza msingi wa chama cha siasa chochote iwe CCM ama vyama pinzani dhidi yake ni kuendelea kukubalika kwa wananchi ili viaminiwe kuongoza nchi.

Hivyo kinapaswa kuwa na masharti ambayo yatimizwe na wanachama na viongozi wa ngazi mbalimbali na kila mara vijichunguze vyenyewe kwa umakini kama vinafuata.

Vyama vya siasa vinapopata matokeo mabaya au mazuri, viketi chini na kujichunguza na uchunguzi wenyewe lazima uanze kwenye shabaha zake.

Uchunguzi huo ufuatiwe na wapi wamefaulu na wapi waliposhindwa na mwisho lazima chama kijiunde upya pale ambapo ni lazima ili kuendelea kutekeleza shabaha zake kwa ufanisi zaidi. Kuhamasisha vurugu au kupuuza wananchi wa kawaida ni hatari.

Baadhi ya vyama vya siasa vina tabia ya kutoa manung’uniko na sababu zenye majibu ya visingizio badala ya kufanya tathmini za kisayansi za kushindwa au kufaulu.

Viongozi hutumia muda mwingi kuwa wapiga debe na kulalamika tu. Lazima vyama vya siasa muda wote vitambue shabaha zao na kuzidi kuzisambaza kwa wanachama wao ili nao wazielewe na hatimaye kuweka mikakati ya utekelezaji.

Vyama vya siasa nchini vinakabiliwa na mgawanyiko mkubwa kutokana na tabaka la kiuchumi na kijamii. Tofauti ya masikini na matajiri kuwepo miongoni mwa wanachama ndani ya vyama vya siasa kunachangia kuwagawa wanachama wa vyama hivi.

Kama watu wachache wanaishi maisha ya kifahari na walio wengi hawapati mahitaji yao ya lazima wataanza kuhaha kutafuta mahema mapya.

Vyama vijifunze taabu iliyowapata CCM kwamba yalikuwa matokeo ya kuwambatia matajiri na kuruhusu wanachama wake wajipatie mali hata nje ya sharia.

Kuruhusu matajiri kutumia fedha zao ovyo ndiyo inayozaa tabia ya kuendelea kupatikana kwa viongozi mbalimbali kwa misingi ya rushwa. Utaratibu huu ni sumbu mbaya ndani ya chama.

Ieleweke tatizo la rushwa linalokabiliwa kwa sasa ni matokeo ya mfumo ndani ya CCM na serikali zake. Hivyo mabadiliko ya mfumo mpya kudhibiti rushwa uwe pia kwa vyama vingine vya siasa.

Chama cha siasa ni chombo kinachowaunganisha watu kwa hiyari zao watu wenye itikadi moja na shabaha moja.

Hivyo kila chama, kinahitaji kila baada ya kipindi kifupi kuchambua shabaha zake. Kwani tuna vyama vingi huku kila chama hudai kinaitakia mema nchi lakini mema yote hayawezi kutekelezwa kwa pamoja na kwa wakati mmoja. Ni wajibu yaliyopangwa kutekelezwa wanachama wote wajue.

Kila chama cha siasa kilichosajiliwa kisiwe kama klabu ya mpira, viongozi wake wakubali hakuna bwana mwingine zaidi ya wanachama wake.

Kuna dhana iliyojengwa na vyama vya siasa umma uamini kuwa unapokifadhili chama fedha na magari unaweza kuwaweka viongozi wa juu wa chama mfukoni.

Vyama vya siasa vyote lazima viwe na mikakati imara ya kujitegemea kifedha ili kisifungwe minyororo na matajiri. Vikao vya juu hadi vya chini vya vyama vitumike kujenga hali bainifu kulingana na mabadiliko mapya.

Mazoea ya kujitathmini kila baada ya kipindi au shughuli kubwa ya kidemokrasia ni utaratibu wa kujiimarisha ili kubaini upungufu. Vyama vyote vya siasa hapa nchini vina watu wengi ambao huingia kwenye vyama kwa matumaini ya kupata vyeo na fedha kwa faida zao.

Kundi hili lina mchango mkubwa wa kudhoofisha demokrasia na kuvidhoofisha vyama kila wanapokosa kutimiza malengo yao. Tayari wapo waliohama kwa kushindwa kufikia malengo ya madaraka.

Ukomavu wa viongozi kutambua kuwa wameshindwa kumshauri kiongozi aliyewateua na kujiuzulu ni utamaduni ambao hajazoeleka, lakini unaufanya umma kutambua kuwa cheo ni dhamana.

Kitendo hiki ni tunu kubwa katika kujenga demokrasia. Wanachama na viongozi wasiotumia uhuru huo kuogopa kuchukiwa au kupoteza nafasi zao ni ubinafsi ambao ni adui wa haki na ukweli.

Meya Ubungo: Magufuli ameingizwa chaka

WALIO MPOTOSHA MH. RAIS KUHUSU MAPATO YA HALMASHAURI ZA MKOA WA DAR ES SALAAM WA WAJIBISHWE

Tangu jana nimepigiwa simu na Waandishi wa habari na wadau wa Maendeleo katika Halmashauri za jiji la Dar es salaam kutaka nitoe ufafanuzi juu ya Mapato ya Jiji la Dar es salaam kupitwa na Jiji jipya la Dodoma.

Ukweli ni kwamba Jiji la Dar es salaam haliwezi kamwe kupitwa Mapato yake na Jiji la Dodoma.

pana utofauti wa Kimuundo wa Jiji la Dar es salaam lenye watu Millioni 5 na Jiji la Dodoma lenye watu Millioni 2

Dar es salaam,Halmashauri ya jiji ni moja wapo katika Halmashauri 6( Kigamboni,Temeke,Ubungo,Kinondoni,Ilala DSM city council lenyewe) kwa Mkoa wa Dar es salaam,wakati Dodoma wao wana Halmashauri moja tuh ya Jiji la Dodoma lenye watu Millioni 2.

Mtu akitaka kulinganisha ulipaji wa mapato kataka Majiji haya ni kama ifuatavyo.

1.Halamashauri ya Manispaa ya Ilala
Budget ya 2017/18 Walipanga makusanyo 46,621 718 036 walichokusanya 44,505,251,223, makusanyo yatakuwa asilimia 95.5

2.Halamshauri ya Manispaa ya Kinondoni
Budget review 2017/2018 Makadirio mapato ya ndani yalikuwa ni Billioni 31,619,825,405.08 na Wamekusanya Billioni 29,754,382,564.86 sawa na Asilimia 94.

3.Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo
Makadirio ya Budget Mapato ya ndani ni 16,505,598,500.00 wakati wamekusanya 13,496,386,027.00 sawa na asilimia 81.8

4. Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam
Makadirio ya Mapato ya ndani kwa Mwaka wa 2017/2018 yalikuwa ni billion 16,413,537 000.00 na wamekusanya 16, 849,660,891.44 sawa na asilimia 102

5. Halmashauri ya Manispaa ya Temeke
Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Mapato ya ndani
walipanga kukusanya Billioni 30,910,528,600 wamepata billioni 29,034,531,092 sawa na asilimia 94.

6. Halamshauri ya manispaa ya Kigamboni
Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Mapato ya ndani ni Bajeti kigamboni ni Billioni 9,218,868,000 makusanyo harisi ni Billioni 5,478,544,722 sawa asilimia 59

SASA UKITAKA KULINGANISHA
chukua mapato ya Halamshauri zote za Dar es salaam ambapo jumla walioanga kukusanya Billioni 151,290,075,441 na wakafanikiwa kukusanya kiasi cha Billioni 139,118,756,519,90 sawa na Asilimia 91.95

kiasi hiki cha fedha ndicho kimechangiwa na watu Millioni 5 wa Dar es salaam sasa ndipo Ulinganishe na Mapato yote ya Jiji la Dodoma waliopata Billioni 24.4 kwa makusanyo ya watu Millioni 2.

Swali Je Billioni 139.118,756,519.90 ni ndogo kuliko Billioni 24.4

Mwisho
Nikubaliane na Mheshimiwa Rais kuwa kuna Upigaji wa Mapato kwenye Halmashauri wa kufa Mtu! hilo halina Ubishi hata kidogo, Waziri Jaffo anajua tunavyopambana kuzuia Mianya hiyo.
Na pili ni utaratibu huu Mzuri wa Mheshimiwa Rais wa kilinganisha na Kushindanisha Mapato ya Halmashauri mbalimbali Nchi nzima,Utaratibu huu Unafanya tupambane kuwa Vinara wa Ukusanyaji Mapato.
Lakini pia Nichukue nafasi kuwapongeza Dodoma na Ubungo halmashauri mpyaa kufanya vizuri kwa mara ya kwanza.

IMETOLEWA Na

Boniface Jacob
MSTAHIKI MEYA
MANISPAA YA UBUNGO

Yanga kumuaga rasmi Canavaro Agosti 12

ALIYEKUWA nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ”Cannavaro” anatarajiwa kuagwa rasmi ndani ya klabu hiyo tarehe 12 Agosti, 2018 kwa mchezo maalumu wa kirafiki baada ya kutangaza kutundika daruga. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Katika taarifa rasmi iliyotolewa na uongozi wa klabu hiyo kupitia kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii, imesema klabu hiyo inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki na timu ambayo bado haijafaamika kwa lengo la kumuaga nahodha huyo.

Cannavaro ambaye alitangaza kustaafu soka 26 Juni, mwaka huu, amefanikiwa kuitumikia klabu ya Yanga kwa miaka 12, toka alipojiunga nayo Mwaka 2006 akitokea Malindi FC, inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar.

Yanga ambayo kwa sasa imeweka kambi mkoani Morogoro kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu pamoja na mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger unaotarajia kuchezwa 19 Agosti, 2018.

Uongozi, Bodi Bank M wapigwa ‘stop’

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesimamiasha shughuli za Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa Bank M. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

BoT imechukua hatua hiyo baada ya Benk M kushindwa kujiendesha kwa kukosa mtaji unaokubalika kisheria ambapo sasa BoT watasimamia uendeshaji wa benki hiyo.

Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, amesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya kubainika kwamba benki M ina upungufu mkubwa wa ukwasi kinyume na matakwa ya sheria ya kibenki.

Prof. Luoga amesema hatua hiyo imechukuliwa ili kulinda maslahi ya wateja na wakopeshaji wote wanaohusika na shughulia ambazo zilikuwa zikiendeshwa na Benki M.

“Kutokana na uamuzi huo, BoT imesimaisha bodi ya wakurugenzi na uongozi wa Banki M kuanzia leo, hivyo kutokana na uamuzi huo imemteua Meneja Msimamzi ambaye atakuwa na shughuli ya kusimamia benki hiyo kwa kipindi ambacho itakuwa chini ya usimamizi wa BoT,” amesema Prof. Luoga.

Katika nyingine, amesema shughuli za utoaji huduma za kibenki katika benki M zitasimama ndani ya siku 90 wakati BoT ikifanya tathimini ya hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa jambo hilo.

Sambamba na hilo, Prof. Luoga amesema wanahisa wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) na benki ya TPB wameamua kuunganisha benki hizo ili kuboresha ufanisi na utendaji wa benki hizo.

Prof. Luoga amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya BoT kuzipa muda wa miezi minne wa kuhakikisha zinafikisha kiwango cha mtaji kinachohitajika na sheria ya benki na taasisi za fedha, kitendo ambacho benki hizo kilishindwa kufikia n akuamua kuungana pamoja.

“Kufuatia muungano huo, kutakuwepo na benki moja ambayo itaendelea kuitwa benki ya “TPB Bank Plc”. Kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 30(1)(a) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ya Tanzania imeridhia ombi la uunganishaji wa benki za TWB na TPB na kuwa benki moja kuanzia tarehe 03 Agosti 2018 itakayoendelea kuitwa benki ya “TPB Bank Plc” ambayo itaendelea kuwa na mtaji wa kutosha kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006,” amesema na kuongeza.

“ Hivyo, wateja, wafanyakazi, mali na madeni yote ya benki ya TWB yataunganishwa na yale ya benki ya TPB. Hivyo, muungano huu utaifanya benki mpya ya TPB Bank Plc kuwa imara zaidi na itakuwa ina mtaji wa kutosha kama inavyotakiwa kisheria chini ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

“Benki Kuu inawaomba wateja wa benki ya TWB kuwa watulivu katika kipindi cha mpito cha uunganishaji wa benki hizi na waendelee kupata huduma za kibenki kwa utaratibu utakaotolewa na menejimenti ya uongozi wa benki ya TPB.”

Waitara kutikisa Ukonga kesho

ALIYEKUWA Mbunge wa Ukonga, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mwita Mwaikabe Waitara, kesho Ijumaa, atapokelewa rasmi jimboni humo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Waitara ambaye aliondoka Chadema Jumamosi iliyopita na kujiunga na Chama Cha Mapimduzi (CCM), anatarajiwa kupokelewa kwenye chama chake hicho kipya, kupitia mkutano maalum wa jimbo la Ukonga.

Kwa mujibu wa Waitara, katika mkutano huo, viongozi kadhaa wa Kata na matawi kutoka jimbo la Ukonga na jimbo jirani la Segerea, wanatajiwa kuondoka na Chadema na kujiunga na CCM.

“Kesho ndio naanza kazi rasmi ya kubomoa Chadema pale Ukonga,” amesema Waitara na kuongeza, “Nataka kuwaonyesha kuwa mimi nina watu na kwamba uamuzi wangu wa kuondoka Chadema ulikuwa sahihi.”

Mbaroni kwa kujiteka jijini Mwanza

Mfanyabiashara Prosper Peniel (26) mkazi wa Kwimba mkoani Mwanza anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kosa la kutoa taarifa ya uongo kuwa ametekwa na watu wasiojulikana kwa lengo la kuishinikiza familia yake imtumie kiasi cha Sh. milioni 53. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 02 Agosti, 2018 na  Kamanda wa Polisi Mwanza, DCP Ahmed Msangi, ambapo amesema mtuhumiwa huyo alisambaza taarifa hizo tarehe 18 Agosti mwaka huu.

Kamanda Msangi amesema Peniel aliwataka ndugu zake kumtumia kiasi hicho cha fedha ili aachiwe kitendo ambacho ni kosa la jinai.

“Mtuhumiwa alimtumia ndugu yake ujumbe mfupi kupitia simu yake ya mkononi kuwa ametekwa na watu wasiojulikana wakati akitembea kwa miguu katika barabara ya Kenyatta karibu na jengo la NSSF plaza hapa jijini mwanza. Baada ya ndugu zake kupokea taarifa hizo walitoa taarifa kituo cha polisi,” amesema Kamanda Msangi na kuongeza.

“Askari kwa kushirikiana na ndugu wa mtuhumiwa walianza kufanya ufuatiliaji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mwanza na maeneo ya mikoa ya jirani ili kuweza kubaini wahusika waliomteka mtuhumiwa na mahala alipopelekwa baada ya kutekwa.

“Ndipo tarehe tajwa hapo juu polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa amelala kwenye nyumba ya  kulala wageni ya majani lodge iliyopo wilayani Kwimba  akiwa na simu ya mkononi aliyokuwa akiitumia kutoa taarifa za uongo kwa ndugu na marafiki kuwa ametekwa.”

Kamanda Msangi amesema Polisi wapo katika upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa, na kwamba pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani. Aidha uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo bado unaendelea.

Serikali yawatangazia vita wanaotorosha madini

SERIKALI imewatangazia vita watu wanaotorosha madini ya Tanzanite pamoja na wanaokwenda kinyume na matakwa ya sheria. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Akizungumza jana tarehe 01 Agosti, 2018 wakati alipofanya ziara ya kutembelea migodi ya madini ya Tanzanite na ukuta wa Mirerani mkoani Manyara, Waziri wa Madini, Angellah Kairuki aliwaonya wezi wa madini hayo kwamba kiama chao kinakuja.

Waziri Kairuki amesema serikali itaendelea kusimamia ulinzi na kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo.

“Utoroshaji madini hausaidii, fedha ni za haraka lakini zinawaadhibu watanzania walio wengi kwa kuwa, fedha hizo hizo zingeweza kutumika katika miradi mingine ya maendeleo. Hivyo, kila mtanzania awe mlizi wa mwenzake,” amesema Kairuki.

Kwa upande wake,  Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mlabwa, amesema  ni lazima Sheria, Kanuni na taratibu zizingatiwe wakati wa utekelezaji shughuli za uchimbaji madini kwa kuwa serikali inatambua mchango wa kila aina ya madini yanayopatikana nchini.

Naye, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Tumaini Magesa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto amesema kuwa, shughuli za uchimbaji katika eneo la Mirerani zinaendelea na hivyo serikali itaendelea kuboresha ulinzi na kuhakikisha kwamba unaimalika.

Spika Ndugai apokea barua ya Kalanga kujiuzulu

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amepokea barua ya kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kujiuzulu nafasi ya ubunge kwa aliyekuwa  Mbunge Jimbo la  Monduli, Julius Kalanga Laizer. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea). 

Taarifa hiyo ilitolewa jana tarehe 01 Agosti, 2018 na Kitengo cha Habari Elimu kwa Umma na Mawasiliano Ofisi ya Bunge. 

“Kufuatia barua hiyo tayari Mheshimiwa Spika amemuandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mheshimiwa Jaji Semistocles Kaijage kumfahamisha kuwa Jimbo la Monduli lililoko Mkoani Arusha liko wazi tangu sasa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Mheshimiwa Spika ameandika barua hiyo kwa mujibu wa kifungu 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Chaguzi (Sura ya 343, ya mwaka 2015)kinachoelekeza kwamba, pale ambapo Mbunge, atajiuzulu, atakufa au sababu nyingine yeyote tofauti na zilizoainishwa katika kifungu cha 113, Spika atamjulisha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kutangaza kwenye Gazeti la Serikali kwamba kiti hicho cha Ubunge kiko wazi.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa, kufuatia barua hiyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi, inaweza kuendelea na mchakato wa kumpata Mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyowazi ya Jimbo la Monduli.