Rais Mnangawa achekelea Uchaguzi Zimbabwe

WAKATI kura zikiendelea kuhesabiwa katika uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe baada ya zoezi la kupiga kura kukamilika, Rais wa nchi hiyo Emmerson Mnangawa ambaye ni mmoja wa wagombea ameonesha kuwa, ana matumaini makubwa ya kushinda baada ya kuonesha hisia zake kwenye ukurasa wake wa twitter.

Ujumbe huo unaelezea furaha yake baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wawakilishi wake waliopo kwenye vituo vya kupigia kura.

Hata hivyo amesema, yeye na wafuasi wake watasubiri mpaka matokeo rasmi yatangazwe kama ilivyo taratibu za sheria za nchi hiyo.

” Good morning Zimbabwe. I am delighted by the high turnout and citizen engagement so far. The information from our reps on the ground is extremely positive! Waiting patiently for official results as per the constitution”

Rais Mnangagwa alichukua mamlaka baada ya urais baada ya jeshi kuingilia kati mnamo Novemba 15 mwaka jana kufuatia mgogoro wa kumrithi mhasisi wa nchi hiyo Robert Mugabe.

Huku matokeo ya awali yakitarajiwa kutangazwa muda wote kuanzia sasa.

Serikali kutaifisha mashamba ya MO Dewji

SERIKALI imekusudia kuchukua baadhi ya mashamba yanayomilikiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises na kuwapa wananchi kwa kuwa kampuni hiyo imeshindwa kutimiza masharti ya uendelezaji wake. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hatua hiyo ya serikali imekuja baada ya Naibu Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabulla kufanya ziara ya ukaguzi wa mashamba 14 yanayomilikiwa na kampuni hiyo katika wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Katika ziara hiyo, Waziri Mabulla alibaini kwamba Mohammed Enterprises inamiliki maeneo yenye ukubwa wa hekta 9, 418 yaliyo sawa na hekari 20,779 ambayo kampuni hiyo imechukulia mkopo kwa ajili ya kupanda mkongwe.

“Wizara yangu imejiridhisha kuwa ipo haja ya kugawa maeneo yanayomilikiwa na Mohammed Enterprises ambayo hayajaendelezwa kwa kupandwa mkonge ili wapewe wananchi ambao wana uhaba wa ardhi muda mrefu kwa sababu ya maeneo makubwa kumilikiwa na watu wachache,” amesema Waziri Mabulla.

Kwa upande wake Meneja anayesimamia mashamba hayo kutoka Mohammed Enterprises, Newalo Nyari amejitetea kwa kusema kuwa mashamba hayo waliyaendeleza na kwamba maeneo yaliyo baki waliyaacha kwa ajili ya uhifadhi wa misitu na kuwapa wananchi kwa ajili ya kupanda mazao yao.

Upepo wa CCM wamtesa Lowassa

EDWARD Lowassa, Wziri Mkuu Mstaafu ameonesha kuteswa na hama hama ya wapinzani kuelekea Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Faki Sosi…(endelea).

Lowassa ambaye ni Mjumbe Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ameeleza kusikitishwa na kuhama kwa aliyekuwa Mbunge wa Monduli, Monduli Julias Kalanga (Chadema). Kalaga amehamia CCM usiku wa kuamkia Julai 31, 2018.

Hata hivyo Lowassa amesema, umahiri wa Chadema na moto wake kwenye Uchaguzi Mkuu ujao hauzimwi.

Lowasa kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari ameeleza kuwa, CCM imebadili mbinu na kuamua kurubuni wabunge na madiwani wa upinzani kutokana na ‘moto’ wa upinzani uliowashwa mwaka 2015 kwenye kampeni za uchaguzi mkuu.

“Moto ule tuliouwasha 2015 hauwezi hata mara moja kuzimwa na mbinu hizi. Wataondoka kina Kalanga wengi tu lakini kasi ya moto ule jinsi ilivyo sasa ndani ya mioyo ya Watanzania ni ya moto wa kiangazi,” amesema Lowassa na kuongeza;

“Kalanga hakuwa na sababu za msingi za kujiuzulu nafasi yake hiyo ya heshima ya kuwatumikia wananchi wa Monduli nikiwemo mimi. Uamuzi huo umetuhuzunisha na kutuumiza.

“Lakini nawaomba msife moyo hata dakika moja zaidi, kitendo hicho cha Kalanga kizidi kutupa nguvu, ari, hamasa na mori zaidi wa kuendeleza mapambano ya kuitafuta demokrasia na mabadiliko ya kweli.”

Amesema kuwa, kuhama kwenye siasa sio tukio jipya kwenye dunia hivyo sio sababu ya kurudi nyuma kwenye mapambano, “hakuna jipya katika hili, ni kawaida kwa wana siasa duniani kuhama vyama vyao na kubadilishana vijiti.”

Lowassa alihama kutoka CCM na kujiunga Chadema mwaka 2015 kisha kupewa nafasi ya kukiwakilicha chama hicho kama mgombea urais ambapo aliungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Vyama vinavyounda UKAWA ni pamoja na Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha NCCR-Mageuzi, NLD na Chadema.

Lugumi maji ya shingo, asalimu amri

MFANYABIASHARA Said Lugumi amesalimu amri kwa kukubali kukamilisha kufunga mfumo wa mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole nchi nzima ndani ya miezi mine. Anaripoti Regina Kelvin…(endelea).

Lugumu ametakiwa kukamilisha mchakato huo kupitia kampuni yake ya Lugumi Enterprises.

Agizo la kukamilisha kazi hiyo limetolewa na Kangi Lugola, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola leo tarehe 31 Julai, 2018 jijini Dar es Salaam.

Lugola amesema, baada ya kukamilisha mfumo huo Lugumi anapaswa kuukabidhi rasmi kwa Jeshi la Polisi.

“Kampuni ya Lugumi mtakumbuka moja wapo ya jambo lilimkera rais wa nchi hii. Ni kwa namna ambavyo mkataba wa mfumo wa utambuzi wa alama za vidole katika udhibiti wa uhalifu ulivyoingiwa.

“…kazi hiyo Lugumi hajaimaliza, pesa za serikali haziwezi kupotea bure. Nimemuita na amekuwa muungwana, amekuja yeye mwenyewe na nimepata fursa ya kuzungumza kwamba mfumo huu ambao umelenga kudhibiti uhalifu unakamilika,” amesema Lugolana kuongeza;

“Lugumi amekubali na ameomba tumpe miezi minne ili ahakikishe mfumo huo anaukamilisha na kuukabidhi kwa jeshi la polisi ili uweze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.”

Lugola kwamba, Lugumi asipokamilisha mfumo huo ndani ya miezi minne kama alivyoomba, atamfikisha kwenye mahakama ya mafisadi.

“Lakini nimemuonya kwamba kazi yangu kubwa ni kuhakikisha ile mahakama ya mafisadi ambayo imeanzishwa na Rais John Magufuli bado ina uhaba wa wateja kwa maana ya mafisadi.

“Kwa hiyo hiyo miezi minne ikikamilika na hajafanya hivyo, haraka nitahakikisha anakuwa mteja wa mahakama hiyo, hatuwezi kukubali mahakama hiyo iliyoanzishwa na rais kwa ajili ya wale wanaochezea fedha za serikali ikawa na uhaba au ikakosa wateja ilhali watu kama hawa wanazurura mitaani,” amesema.

Zitto amgomea Kangi Lugola

ZITTO Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini amegomea wito uliotolewa na Kangi Lugola, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Waziri wa kujisalimisha kwa Mkuu wa Polisi Mkoa wa Lindi ndani ya siku mbili kuanzia sasa. Anaripoti Faki Sosi na Regina Kelvin … (endelea).

Katika ukurasa ukurasa wake wa Twitter Zitto ameandika kuwa, hatokwenda kujisalimisha polisi kama alivyoagiza Lugola.

Kabla ya kauli ya Zitto kutoa kauli hiyo, Waziri Lugola wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo alimtaka kujisalimisha kwa Mkuu wa Polisi Mkoa wa Lindi kwa madai ya kufanya uchochezi.

Lugola alidai kuwa, Zitto alitoa kauli za uchochezi kwenye mkutano wa hadhara alioufanya jana Julai 30 katika viwanja vya Mkapa Garden, Kilwa Masoko mkoani Lindi.

“Baadhi ya Watanzania wenzetu bado wanajihusisha na mambo ya kutoa kauli za uchochezi, kutukana viongozi, kukaidi agizo la rais hasa wabunge kutoka maeneo ya majimbo yao na kwenda kufanya mikutano kwenye majimbo yasiyo ya kwao,” amesema na kuongeza;

“…Wakifika kwenye majimbo yasiyo ya kwao wanajihusisha na kutukana viongozi na kutoa lugha za uchochezi.

“Nimekwisha kemea jambo hili na nimesema chaguzi zote zinazoendelea hivi karibuni na zitakazoendelea mwakani na milele na milele nimesema hakuna atakayepona kama ataendelea kutokana viongozi na kutoa lugha za uchochezi,” amesema.

Amesema, juzi (Julai 29) katika Jimbo la Saidi Bungara Zitto alikaidi agizo hilo na kwenda kufanya mikutano katika jimbo lisilo la kwake.

“Zitto mahali popote alipo ajisalimishe kwa Mkuu wa Polisi Mkoa wa Lindi na endapo asipojisalimisha ndani ya siku mbili, nitamulekeza IGP ili popote alipo akamatwe,” amesema Lugola.

Kutokana na kauli ya Lugola, Zitto ambaye ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo amesema waziri huyo hana mamlaka ya kumwagiza ajisalimishe polisi.

Zitto amesema, hatotii wito huo kwa kuwa ni kinyume cha sheria na kwamba, zipo taratibu za Jeshi la Polisi kinyume na zinazotumiwa na Lugola.

Kwenye ukurasa wake ameandika “Waziri hana hayo mamlaka. Kama polisi wananitaka watoe wito wa kisheria nitakwenda. Naendelea na kampeni za Mbunge wa Buyungu ambapo tunamwunga Mgombea wa Chadema na madiwani wa ACTwazalendo kwenye kata kadhaa. Nashauri Waziri ampate kwanza yule Mbwa
wa Polisi Bandari ”

Hata hivyo, Lugola Lugola amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kumchukulia hatua Mkuu wa Polisi Wilayani Kilwa(OCD) kwa kumruhusu Zitto kuendelea kufanya mkutano katika jimbo lisilo lake.

“ Na pia namulekeza IGP achukue hatua kwa mkuu wa polisi wa wilaya ya kilwa ocd, ya kwa nini hakuchukua hatua dhidi ya zitto kwa kuendelea kufanya yale tuliyoyakataza,” amesema.

Sheria ya PSSSF yaanza kufanya kazi kesho

SHERIA ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumsihi wa Umma (PSSSF) namba 2 ya mwaka 2018 kuanza kutumika rasmi kesho baada ya Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama kuitangaza rasmi. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumshi wa Umma (PSSSF) ni muunganiko wa mifuko minne ambayo ni PSPF, PPF, LAPF na GEPF.

Wakati sheria ikianza kutumika Mhagama ametangaza majina nane ya wajumbe wa bodi ya PSSSF ambao wameteuliwa kutokana na muundo wa sheria ya kuanzishwa kwa mfuko huo.

Sheria ya PSSSF imetangazwa kuanza rasmi kutumika baada ya bunge kupisha sheria hiyo Januari 31 na Rais John Magufuli kusaini sheria hiyo tarehe 8 Februari, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Waziri Mhagama amesema kuwa kuanzia sasa Watumishi wa umma watakaoajiriwa watasajiliwa katika mfuko huo na wale watakaoajiriwa katika sekta binafsi watasajiliwa katika mfuko wa NSSF.

Amesema kuwa wanachama wote ikiwa ni pamoja na wastaafu na warithi waliopo katika mifuko iliyounganishwa watahamishiwa katika mfuko wa PSSSF na haki na satahili zao zitaendelea kutolewa na mfuko huo bila kuathiriwa kwa namna yeyote ile.

“Vivyo hivyo rasilimali vitega uchumi, madeni, mifuko ya hiari na mikataba iliyokuwa chini ya mfuko iliyounganishwa itahamishiwa katika mfuko mpya wa PSSSF, hali kadhalika watumishi wote wa mifuko hiyo watahamishiwa katika mfuko mpya ambapo Uongozi wa mfuko huo utawapangia majukumu yao kwa kuzingatia muundo wa mfuko huo,” amesema
Mhagama.

Mhagama amesema kuwa bila kuathiri huduma kwa wanachama kwa namna yeyote ile serikali ilifanya mambo ya kutambua wanachama wastaafu na Wanufaika wote wa mifuko iliyounganishwa sambamba na haki na stahili zao katika mifuko hiyo.

“Kwa kuzingatia maandalizi hayo na jitihada nyingine mbalimbali zilizofanywa na serikali napenda kuwahakikishia na kuwaondoa wasiwasi wanachama wa mifuko iliyounganishwa, wadau wote wa sekta ya hifadhi ya jamii na wananchi wa ujumla kwamba serikali imelifanyia kazi jambo hili kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kwamba zoezi la kuunganishwa
mifuko halitakiwa na athari yeyote kwa uendelevu wa huduma kwa wanachama,” amesema Mhagama.

Wajumbe walioteuliwa kwa mujibu wa sheria ya kuanzishwa kwa mfuko huo ni kutoka katika chama cha wafanyakazi chenye wanachama wengi kwenye mfuko wa PSSSF walioteuliwa ni Leah Ulaya na Rashid Mtima.

Wawakilishi wa waajiri kutoka chama cha waajiri wenye uwakilishi mkubwa ni Dk. Agrey Mlimuka na Stella Katende, mwakilishi kutoka sekta binafsi aliyeteuliwa ni Thomas Manjati ambapo mwakilishi kutoka Tamisemi ni Hanry Katabwa.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Fedha na mipango ni Suzan Kabogo, mwakilishi wa wizara yenye dhamana (Owm- KVAU), ni Jacob Mwinuka na nafasi ya mjumbe mmoja kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali itatangazwa baadaye baada ya utaratibu kukamilika.

Naye Mkurugenzi kuu wa Mfuko wa PSSSF, Eliud Sanga amesema kuwa Mfuko huo umejipanga vizuri kwa ajili ya kuondoa kero za wanachama pamoja na kumaliza usumbufu kwa wanachama wa kucheleweshewa mafao yao.

Naye Mkurugenzi mkuu wa NSSF, William Erio amesema kuwa mifuko hiyo ya hifadhi za jamii imejipanga kutoa huduma bora zaidi kwa wanachama wake ikiwa ni pamoja na kutoa mafao yao kwa wakati kwa mujibu wa sheria mpya.

Mahakama yamuonya Mbowe kwa utoro

MWENYEKITI wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amepewa onyo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kosa la kutohudhuria mahakamani hapo kwa mara mbili. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Onyo hilo limetolewa leo tarehe 31 Julai, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wakati kesi inayomkabili Mbowe na wenzake ilipokuja kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali.

Hakimu Mashauri amesema iwapo Mbowe atarudia tena kutofika mahakamani kwa sababu zisizo na msingi, dhamana yake itafutwa.

Mbowe ametakiwa na mahakama kuheshimu masharti ya dhamana na kwamba asipofanya hivyo mahakama itamfutia dhamana yake sambamba na kutaifisha fungu la dhamana ambalo ameliweka.

Katika kesi hiyo, Mbowe na wenzake akiwemo Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Katibu wa Chadema, Dkt. Vicent Mashinji wanakabiliwa na mashitaka 13 ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki pamoja na kushawishi hali ya kutoridhika.

Serikali kupanga bei elekezi ya madini

SERIKALI imesema itapanga bei elekezi ya madini ili kundoa urasimu wanaofanyiwa wachimbaji wadogo wakati wa uuzaji. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alipotembelea kijiji cha Manda kilichopo Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ambapo kunachimbwa madini ya jasi (Gypsum).

“Kijiji cha Manda changamoto kubwa ni soko la gypsum, inaonekana wazi wachimbaji wanawaonewa kuna watu wanwalalia. Tumepanga tume tukae pamoja tutengeneze, tuziweke bei elekezi ili wanao nunua madini wafuate bei hizo.

“Sababu watu wetu wamewekeza kwenye madini hayo tumekuta malundo ya Gypsum yako sokoni bei wanayoambiwa watanunua hairidhishi,” alisema Pro. Kikula.

Prof. Kikula aliongeza kuwa “Hiyo hiyo gypsum inanunuliwa Itigi kwenda Mtwara kwa bei ya kutupwa, wananchi wanapata shida wanasafirisha kwa bei ndogo. Tutatengeneza bei elekezi ili iwe kigezo cha ununuzi na uuzaji wa madini sokoni.”

Katika hatua nyingine, Prof. Kikula aliwataka wachimbaji wadogo kuheshimu mamlaka za maeneo wanayochimba madini ikiwa pamoja na kuwa na mahusiano mazuri na viongozi wa serikali husika ili kuepusha migogoro.

“Katika ziara yetu tumekwenda kujua matatizo ya uchimbaji, tumekwenda Manzase njia ya kutoka Dodoma hadi Iringa kabla ya kuzungumza na wachimbaji tumezungumza na serikali ya kijiji kuhusu uchimbaji.

Wachimbaji lazima waheshimu mamlaka ya maeneo wanayochimba bila ya kuwa na mahusiano mazuri kunaleta migogoro,” alisema.

JWTZ wawaita madaktari kujiunga na jeshi

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kuandikishwa jeshini madaktari wa binadamu na fani nyingine za tiba. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 31, 2018 na Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano JWTZ, Kanali Ramadhan Dogoli wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

“Nafasi hizo zinatolewa ili kuongeza idadi ya wataalamu wa tiba watakaotoa huduma za afya katika hospitali zetu, vituo vya afya na Zahanati kulingana na mahitaji ya sasa na siku zijazo,” amesema Kanali Dogoli.

Kanali Dogoli ametaja sifa za watu wanaohitajika kuandikishwa ikiwemo, mhusika awe na umri kati ya miaka 18 hadi 28 na mzaliwa wa Tanzania, awe hajawahi kupatikana na hatia ya makosa ya jinai mahakamani na kufungwa jela, awe na cheti halisi cha kuziliwa.

Pia, kama ni daktari awe amemaliza mafunzo kwa vitendo na kutunukiwa vyeti pamoja na kusajiliwa na Bodi. Awe hajawahi kutumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo au Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo.

Kanali Dogoli amesema   wenye sifa tajwa na kuhitaji kujiunga na JWTZ waripoti katika kambi ya Jenerali Abdallah Twalipo, Mgulani Dar es Salaam tarehe 28 Agosti, 2018 kuanzia saa moja asubuhi.

Lugumi ajisalimisha kwa Kangi Lugola

MFANYABIASHARA Said Lugumi ametelekeza agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Kangi Lugola liliomtaka ajisalimishe ofisini kwake mara moja. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Taarifa ya Jeshi la Polisi inaeleza kuwa, Lugumi asubuhi ya leo tarehe 31, Julai 2018 amewasili katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ajili ya kuonana na Waziri Lugola.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa, kabla ya polisi kumpeleka Lugumi kwa Waziri Lugola, alipelekwa Makao Makuu ya Polisi Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai.

Waziri Lugola Julai 22, 2018 alimtaka Lugumi ajisalimishe ofisini kwake kabla ya Julai 31 mwaka huu.

Mbunge mwingine Chadema ang’oka

JINAMIZI la kukimbiwa na wabunge na madiwani linazidi kuitafuna Chadema, ambapo jana tarehe 30, 2018 Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga kupitia chama hicho ametangaza kujivua uanachama na kuhamia chama tawala CCM, Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Uamuzi huo wa Kalanga unakuja ikiwa zimepita siku mbili tangu aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara kutangaza kujivua ubunge, uanachama na nyadhifa zote alizokuwa nazo Chadema na kurudi CCM kwa kile alichodai kuwa Chadema hakuna demokrasia.

Taarifa iliyotolewa leo kwa umma na Idara ya Itikadi na Uenezi CCM, inaeleza kuwa, Kalanga amepokelewa rasmi na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole usiku wa kuamkia leo.

Hivi karibuni Polepole alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa kuna wabunge wawili kutoka Chadema watahamia CCM huku akisisitiza kwamba idadi ya wanaokiomba chama hicho tawala kujiunga nacho haihesabiki.

Polepole alidai kuwa, kukosekana kwa ushirikiano kutoka uongozi wa juu wa chama ni kati ya sababu zinazowakimbiza wanaohama Chadema.

Msako wa mashine za EFD waendelea

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema itaendelea kufanya ukaguzi wa matumizi za mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD), ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anatoa risiti za EFD na kulipa kodi stahiki. Anaripoti Regina Kelvin …. (endelea).

Hayo yalisemwa jana tarehe 31 Julai, 2018 na Kamishna wa kodi za ndani  Elijah Mwandumbya alipofanya ukaguzi wa kushtukiza katika maduka yaliyopo eneo la Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Mwandumbya aliwataka wafanyabiashara kuacha kutoa sababu ya ubovu wa mashine za EFD kwa kuwa mashine hizo sasa zinafanyakazi vizuri.

“TRA  haitakubali mfanyabishara anayeonesha barua kama sababu ya kutokutoa risiti ya EFD, tatizo la mashine lilikwisha, ni wajibu wa wafanyabiashara kutoa risiti,” amesema  Mwandumbya.

Kamishna Mwandumbya amesema wafanyabiashara wote wanaostahili kutoa Risiti za EFD wanapaswa kutoa kwa kila mauzo wanayofanya kwani tatizo la mashine lilishashughulikiwa na limekwisha.

Rais Magufuli awapa pole Waislam

RAIS John Magufuli ametuma pole kwa Waislam nchini kutokana na kifo cha aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Salum Hassan Fereji. Anaripoti Yusuph Katimba…(endelea).

Sheikh Fereji alifariki dunia usiku wa kuamkia Julai 28 alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza kutokana na kusumnuliwa na ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu

Hayati Sheikh Fereji alifanyiwa ibada ya swala Julai 29, 2018 katika msikiti wa Raudhwa uliopo Mtaa wa Lumumba, Mwanza na kuzikwa siku hiyo hiyo.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na dini akiwemo Mufti wa Tanzania, Aboubakary Zubeir.

Salamu za pole za Rais Magufuli pia alizielekeza kwa Mufti Zubeir ambapo amesema, anamkumbuka Sheikh Fereji kwa ucha Mungu wake, ukarimu, upendo kwa wananchi na namna alivyokuwa akiunga mkono juhudi za kudumisha amani na kusukuma mbele maendeleo.

“Nimesikitishwa sana na kifo cha Sheikh Fereji, nilipokuwa nikienda Mwanza alikuwa miongoni mwa viongozi wa dini waliokuja kunipokea.

“Amekuwa akifanya kazi ya Mwenyezi Mungu kwa mapenzi makubwa na nchi yake, pole sana Mufti wa Tanzania na nakuomba unifikishie salamu zangu za pole kwa familia yake, Waislamu wote wa Mkoa wa Mwanza na nchi nzima pamoja na wote walioguswa na msiba huu,” amesema Rais Magufuli.

Waziri Ummy: Serikali isiwe kikwazo

TAASISI za serikali zinazohusika na masuala ya ukaguzi na udhibiti wa bidhaa, zimetakiwa kutokuwa kikwazo kwa maendeleo ya wajasiriamali na ujenzi wa viwanda hapa nchini. Anaripoti Regina Kelvin…(endelea).

Agizo hilo limetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akihutubia kwenye mkutano wa wadau wa kujadili mchango wa taasisi za serikali katika kuanzisha na kuboresha viwanda vya chakula nchini.

Waziri Ummy amesema Shirika la Viwango nchini (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) na ofisi ya mkemia mkuu wa serikali kusikilizana katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuondoa vikwazo kwa wajasiriamali na ujenzi wa viwanda.

“TBS, TFDA na mamlaka nyingine inabidi msikilizane ili kuondoa vikwazo kwa wafanyabiashara na wawekezaji,” amesema.

Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema serikali itanedelea kuondoa changamoto za wajasiriamali na wawekezaji wa viwanda, lakini amewataka wajasiriamali hao kutobweteka katika uzalishajiwa bidhaa zenye ubora.

“Tunajenga vianda kwa ajili ya kutoa ajira, kuanzisha bishaa zenye ubora na viwango vya kukidhi matakwa ya watanzania na soko la nje ya nchi. Tunachopaswa kufanya tutengeneze viwango vya kiuhalisia. Tunawasaidia lakini Msibweteke,” amesema.

Kubenea: Hakuna wa kuning’oa Chadema

SAED Kubenea, Mbunge wa Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amesema kuwa, hakuna wa kumng’oa ndani ya chama hicho. Anaandika Faki Sosi…(endelea).

Kubenea ametoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na waandishi wa habari kuhusu taarifa za kutajwa kutaka kuondoka kwenye chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Hizi taarifa zimeenezwa na baadhi ya watu wakiwemo ndani ya Chadema kwa maslahi wanayoyajua wao na watu hao wanajulikana.

“Mimi niende CCM kwa lipi” amehoji na kuongeza; “mimi bana sitoki Chadema na hakuna wa kunitoa Chadema, nitabaki humo huko,” ameseam Kubenea.

Amesema kuwa, kuhusishwa kwake na kuhama kwa Mwita Waitara aliyekuwa Mbunge wa Ukonga aliyejiunga na CCM wiki iliyopita sio sahihi.

Ameeleza kuwa, hatua ya Mwita kuhamia CCM sio sahihi kwa kuwa wananchi wa Ukonga walimwamini na kumchagua kwa kura nyingi “hivyo alipaswa kupambana akiwa ndani ya Chadema.”

Kubenea amesema kuwa, atapambana ndani ya Chadema na akishindwa ataendelea na kazi yake ya uandishi.

MwanaHALISI huru, kurejea mtaani

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeamuru gazeti la kila wiki la MwanaHALISI ambalo lilifungiwa na serikali, liendelee kuchapishwa. Anaripoti Faki Sosi…(endelea). 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, tarehe 30 Julai, ofisini kwake, Kinondoni, mkurugenzi wa kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), Saed Kubenea amesema, mahakama imeridhia MwanaHALISI kurudi tena mtaani, kufuatia mamlaka iliyoifungia kutokuwa na nguvu za kisheria.

MwanaHALISI lilifungiwa na serikali, tarehe 19 Septemba 2017, kwa madai kuwa limekuwa “likiandika habari za uongo, kejeli, upotoshaji, uchochezi na zinazolenga kuwafanya wananchi waichukie serikali yao.”

Hukumu ya kuruhusiwa kuchapishwa kwa MwanaHALISI, imetolewa na Jaji Beatrice Mutungi, tarehe 24 Julai mwaka huu.

Amri ya kufungia MwanaHALISI, ilitolewa na aliyekuwa naibu waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, Anastazia Wambura, tarehe 19 Septemba2017.

Kubenea amesema, mahakama imethibisha kuwa gazeti lake, halikuwa na makosa; mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na naibu waziri Wambura, walijichukulia mamlaka wasiyokuwa nayo.

Amesema, hukumu hiyo imedhihirisha kuwa wapo watendaji ndani ya serikali wanaotumia mamlaka walizopewa “kushughulikia wenzao” kwa maslahi yao binafsi.

Amesema, kutokana na hali hiyo, wanatarajia gazeti hilo kuingiza mtaani Jumatano ya tarehe 8 Agosti na kwamba wamepanga kumchukulia hatua za kisheria Wambura.

Nani anaweza kuibadili CCM?

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kina mkondo ambao kila ajaye lazima aupite. Tusijidanganye kwamba, yupo anayeweza kubadili taswira na mfumo ndani ya CCM. Anaandika Ndoimba Nainda … (endelea).

Kinachoweza kubadilika ni sauti ya kiongozi, vitisho na ubabe-basi, lakini mengi yanayolalamikiwa huendelea kuwa yele yale.

Malilamiko yaliyoishi wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Benjamn Mkapa na Jakata Kikwete ndio haya haya ambayo leo watu wanayaishi.

Miongoni mwao ni msingi mibovu ya elimu, kukosekana kwa dawa, gharama za maisha kuwa juu, ubovu wa miundombinu ya maji, umeme, barabara na ufisadi.

Mwanzoni mwa utawala wa Rais Jakaya Kikwete wengi tulipata matumaini makubwa kuwa Tanzania inaingia awamu nyingine mpya ya kufagia uozo wa viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya.

Wananasiasa Basil Pesambili Mramba na Daniel Yona wakiambata na watendaji wawili serikalini Balozi Mahalu na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Gray Mgonja walifikishwa mahakamani.

Si mimi pekee bali Watanzania wengi tulifanya sala maalum ili kuiombea serikali ya Rais Kikwete kuendelea na kasi hiyo.

Kuwafikisha mahakamani wengine wengi waliofanya makosa ya ufujaji wa fedha za umma, na kutumia madaraka yao kwa maslahi binafsi kulileta hisia kuwa, maisha yetu yangepumua.

Inawezekana Mungu  hakukubali ombi la kumjaza Rais Kikwete nguvu ya kupambana na uovu huo au vita hivyo na kusababisha vita hiyo kupotelea mwituni.

Tuliomba kwa dhati kabisa kwa vile yeyote anayelitakia taifa hili mema alipaswa kuunga mkono hatua hii ya serikali iliyochelewa kuwadhibiti wanasisasa na watendaji wa ngazi za juu serikalini.

Mwimbo wa maisha magumu uliimbwa kwa minajili kuwa, watendaji wabovu ndani ya serikali ya CCM ndio waliotufikisha hapo. Waliokamatwa na kupelekwa mahakamani walitoka kwa mbwembwe.

Rais Mkapa naye, aliingia kwa gia ya kubinafsisha utajiri wa Watanzania, njia za uchumi zikakabidhiwa kwa wageni. Wakawa kama wao ndio wanaoendesha uchumi, Watanzania wakabaki kuwa washangiliaji.

Wanyama, Benki, migodi, viwanda na mashirika ya umma yanakabidhiwa kwa walioitwa wawekezaji, nao hawakufanya ajizi, wakakomba kila walichoweza na wengine wameacha magofu. Hakuna kilichovunwa.

Alhaji Mwinyi alifungua milango baada ya kibano cha muda mrefu kutoka kwa Mwalimu Nyerere, hapo napo mende, popo, inzi, kunguni nao walitumia dirisha hilo hilo kuingia nchini kwa kuwa, dhamira haikuendana na uangalizi kwa manufaa ya umma.

Serikali ya sasa nayo kama ilivyokuwa zilizopita, halmashauri nako kumeoza. Trilioni 1.5 zilizotajwa kutoweka haijulikani zilinyofioweje, hakuna aliyeshitakiwa ama kusimamishwa kazi.

Mfumo wa CCM unafanya kazi, kutwa kucha kuchwa, huwezi na hutasikia CCM wakipiga kelele kuhusu kupotea kwa kiwango hichokikubwa cha fedha.

Maalim Seif aichamba CCM

MAALIM Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) amesema kuwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) sio chama cha kukimbilia.  Anaripoti Regina Kelvin …(endelea).

Amesema, haoni sababu mtu mwenye msimamo imara kukimbilia kwenye chama hicho na kwamba, mfumo wa uendeshaji wake haukidhi wara kuridhisha.

“Siridhishwi hata kidogo na utendaji wa CCM” amesema Maalim Seif alipokuwa Kilimahewa visiwani Zanzibar wakati akizindua Jumuiya ya Wazee wa chama hicho (JUZECUF) jana.

Amesema kuwa, hana ndoto ya kujiunga na CCM ambayo utendaji wala mwelekeo wake kwa taifa hauelewiki.

Maalim Seif ameeleza kuwa, kinachotokea katika serikali inayoindwa na CCM hasa kukamatakamata hovyo hakijawahi kutokea hata wakati wa Ukoloni.

“CCM inatakiwa kuelewa haiwezi kutawala nje ya mfumo ambao Watanzania wanavyotaka nchi yao itawaliwe,” amesema na kuongeza;

“Mara kwa mara unasikia diwani ama mbunge kaingia CCM, tena kwa kutoa tamko maalumu. Haya mliyaona wapi?” amehoji Malim Seif.

“Imefika hatua sasa Mwenyekiti wa Kijiji kwa kuwa tu anatoka CCM basi anaweza kuamrisha Jeshi la Polisi likukamate na unakamatwa kweli na kuwekwa ndani,”amesema Maalim Seif.

Katika mazungumzo na wazee hao Maalim Seif amegawa kadi kwa wanchama wapya huku akiahidi kuendelea kuimarisha chama hicho.

Waitara atumwa kuinadi CCM Buyungu

ALIYEKUWA mbunge wa Ukonga, kupitia Chama cha Demokrasia (CHADEMA), Mwita Mwaikabe Waitara, anaelekea jimboni Buyungu, wilayani Kakonko, mkoani Kigoma, kukiongezea nguvu chama chake kipya (CCM). Anaripoti Yusuph Katimba…(endelea).

Waitara aliyetangaza kujiengua Chadema jana Jumamosi na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi, anatarajiwa kutua Kakonko, muda wote kuanzia kesho Jumatatu.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya CCM na zilizothibitishwa na Waitara mwenyewe zinasema, mwanasiasa huyo amesafiri leo asubuhi kwa ndege kuelekea Mwanza; tayari kujiunga na timu ya kampeni ya chama hicho iliyoko mkoani Kigoma.

Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Buyungu, unafanyika kufuatia kufariki dunia kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Mwalimu Samson Kasuku Bilago (Chadema).

Mwalimu Bilago (54), alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei mwaka huu.

Alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kuota kinyama sehemu ya haja kubwa unaofahamika kwa jina la hemorrhoids au piles – (bawasiri).

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza kuwa uchaguzi huo katika jimbo hilo utafanyika tarehe 12 Agosti.

Katika uchaguzi huu, ushindani mkali unatarajiwa kuwa kati ya Mhandisi Christopher Chiza (CCM) na Elias Kanjero (Chadema).

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI Online jana – Jumamosi – majira ya saa tatu usiku, Waitara alisema, “…mi kweli nimepanga kwenda Mwanza kwa shughuli zangu binafsi na baadaye nitakwenda kwenye kampeni Buyungu.”

Alisema, “ninakwenda Buyungu kukinadi chama changu na kuhakikisha kinapata ushindi katika uchaguzi huu. Ninakwenda Buyungu kueleza wananchi madhaifu ya Chadema na ambayo yamenisababishia mimi kuondoka.

“Ninakwenda Buyungu kueleza ukweli ambao baadhi ya wabunge na viongozi wakuu wa chama hicho, hawataki au wanaogopa kuusema.”

Akizungumzia kuondoka kwake ghafla Chadema na kujiunga na CCM, Waitara alisema, “nimeshindwa kuvumilia hila na ghiliba za Mbowe (Freeman Mbowe, mwenyekiti wa taifa wa chama hicho) na genge lake.”

Anasema, “hawa watu wamekuja Ukonga kuja kuvuruga Chadema. Mbowe na watu wake wamekuja Ukonga kwa ajili ya kuweka mtandao wao wa kuhakikisha anashinda uchaguzi mkuu ndani ya chama. Wamekuja Ukonga kunishughulikia.

“Hivyo basi, nimeona ni vema nikaondoka ili niweza kutimiza malengo yangu ya kuwatumikia wananchi wa Ukonga walionichagua kwa kura nyingi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.”

Waitara anadai kuwa ndani ya Chadema kuna matatizo makubwa yanayosababishwa na Mbowe kutaka kukigeuza chama hicho kuwa kampuni yake binafsi.

“Haya siyo maoni yangu binafsi. Wapo watu wengi ndani ya chama hicho wanaofikiri kama mimi, ingawa wao wameamua kubaki kuendeleza mapambano ndani,” ameeleza.

Waitara alitangaza kuondoka Chadema kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam na kuongeza, “nimeamua kuondoka kwa kuwa ndani ya Chadema hakuna demokrasia.”

Alipokelewa na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole.

Kabla ya kujiunga na Chadema, Waitara aliwahi kuwa katibu wa Umoja wa Vijana (UV-CCM), mkoani Tanga.

Alikuwa mmoja wa “wapinzani” wakuu wa Mbowe, kuendelea kugombea uenyekiti wa chama hicho, katika uchaguzi mkuu wa mwaka kesho.

Gonjwa hili, Ukimwi haugusi

UPUNGUFU wa Kinga Mwilini (Ukimwi) ndio unaoonekana kuwa tishio lakini Ugonjwa wa Homa ya Ini unatajwa kuuwa Ukimwi na hata Kifua Kikuu. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Prof. Muhammad Bakari wakati akihutubia wananchi katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani leo Julai 28, 2018.

Prof. Bakari ameeleza kuwa, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia ripoti ya Homa ya Ini ya mwaka 2017 zinaonesha kuwa, mwaka 2015 kulikuwa na vifo milioni 1.34 kutokana na Homa ya Ini ambavyo vilikuwa sawa na vifo vitokanavyo na Kifua Kikuu na zaidi ya vile vitokanavyo na ugonjwa wa UKIMWI ambavyo vilikuwa milioni 1.1.

Kwa hapa nchini, amesema takwimu kutokana na tafiti zilizopo zinaonesha uwepo wa maambukizi ya virusi vya Homa ya Ini aina ya B na C, na kwamba

kati ya wachangiaji damu 200,000 kwa mwaka 2016, asilimia 6 ambayo sawa na takriban watu 12,000 walikuwa na maambukizi ya Homa ya Ini aina ya B.

Wakati mwaka 2017, kati ya wachangiaji damu 233,953, 4.9% takriban watu 11,417 walikuwa na maambukizi ya Homa ya Ini aina ya B na 0.5% takriban watu 1,170 walikuwa na maambukizi ya Homa ya Ini aina ya C.

“ Aidha, utafiti mahsusi ujulikanao kama “THIS”, ulioratibiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, umeonesha kuwa maambukizi ya Homa ya Ini aina ya B ni 4.3% miongoni mwa watanzania wenye umri kati ya miaka 15-49, kwa mwaka 2017. Vilevile, miongoni mwa wanajamii, Homa ya Ini inayosababishwa na virusi aina ya C inakadiriwa kuwepo kwa 2%,” amesema na kuongeza.

“Wananchi wa Tanzania na Afrika Mashariki wapo katika hatari ya kupata maambukizi ya Homa ya Ini, hususan aina ya B na C, kutokana na kuwa njia za maambukizi ya Virusi hivi hufanana na zile za maambukizi ya VVU.”

Prof. Bakari amesema serikali ianendelea kuimarisha mikakati ya kuweza kudhibiti ugonjwa huo kwa kuongeza kuongeza juhudi za kutekeleza Mpango Mkakati wa kwanza wa Dunia wa Homa ya Ini (Global Health Sector Strategy on Viral Hepatitis) kwa mwaka 2016-2021.

Wanachojua ni kufoka, kutisha

BABA utufundishe kusema lakini kusema sawasawa. Kusema ni kukiri na kukana kwa wakati mmoja. Serikali ya watu husema na watu wake. Anaandika Mwalimu Wetu … (endelea).

Wakati mwingine tumekuwa tukisikia serikali ikisema hata pale pasipo na lazima ya kusema huku ikikaa kimya hata pale ilipotakiwa kusema. Serikali za kiimla zote ni serikali viziwi na ni serikali bubu.

Zinajua kufoka na kutisha basi. Hakuna timamu anayependa kufokewa ama kutishwa hivyo wananchi huzidharau serikali hizo. Viongozi wakishajua kuwa wanadharauliwa na wananchi, badala ya kujiuliza ni kwanini au wapi wamekosea, wao hudhani kufoka, kutisha watu na hata kuwatesa, ndiyo suluhisho.

Wanapofanya hivyo huwa hawaelewi kuwa wanafanya hivyo kwa hasara yao wenyewe. Na mara nyingi hayo huwa siyo yao. Hutokana na kuwasikiliza wapambe na wabangaizaji wao ambao aghalabu huwa ni watu
waliopuuzwa na jamii.

Kiongozi madhubuti hana wapambe. Ukiona kiongozi hawasikilizi wale anaowaongoza jua huyo hafai kuwa kiongozi wa watu. Kiongozi mhovyo tu ndiye hudhani anajua kila kitu.

Baba kitinda mimba wa tumbo la mama yangu ni mama mwenye familia na ni mwalimu kule Iringa. Anajua kuwa kama alivyokuwa baba yetu sipendi kuchapa mtoto hivyo sipendi viboko shuleni.

Akaniambia kaka watoto bila kiboko hawafundishiki. Katika kusoma kwangu kote, mara ya mwisho nilimwona mwalimu anamchapa mtoto shuleni kwetu, ni wakati namaliza shule ya msingi darasa la nne, mwaka 1964.

Tangu nilipoingia shule ya kati (middle school) darasa la tano katika Seminari ndogo ya Mlowo mpaka nilipomaliza masomo yangu katika Seminari kuu ya Filosofia, Ntungamo, katika shule zote nilizosoma, sikuwahi kuona mwalimu awe padri au mwalimu wa kawaida akiwa ameshika fimbo mkononi; sembuse kumchapa mwanafunzi.

Na shule hizo zote kwa wakati huo zilikuwa ni shule za mfano, kinidhamu na kitaaluma. Kumbe unaweza kuwatawala watu na wakatawalika bila kuwateka wala kuwatesa hata bila kuwapoteza wala kuwaua wengine.

Anayehitaji nguvu ili atawale, hatoshi! Baba ulifurahisha sana kule Morogoro ulipowalazimisha jamaa wamchangie fedha mama wa watu. Wananchi wako walikufurahia na wakakushangilia sana.

Na baba ulipendeza! Waliotia doa ni wale walioonekana kama ni walinzi. Wananchi hawakuona kilichokuwa kinalindwa.

Walijiuliza, hivi hawa jamaa wameyaona makosa gani ambayo wanadhani mkuu ameyafanya yanayoweza kumkusanyia maadui wengi kuliko wakuu wote waliomtangulia?

Ulimwita mwenyewe lakini kila aliposogea alizuiwa na mlinzi fulani mpaka uliposema mwacheni. Aliendelea kusogea na wao waliendelea kumzuia na wewe ukaendelea kusema mwacheni. Hata alipokusogelea kabisa ulinyoosha mkono umshike, lakini aliponyosha wake alizuiwa mpaka uliposema mwacheni nimshike mkono!

Baba umefanya nini mpaka hawa jamaa wadhani uko katika hatari kubwa hivi yakushambuliwa? Furaha ya kuishi na watu wa Mungu wenzako unaipataje?

Nilipoona yale nikamrejea Muumba wangu na kumshukuru kwa kunijalia maisha ya amani na furaha tele katika moyo wangu! Furaha yakuona wengi wanakujali, wakubwa kwa wadogo.

Masikini wanakupenda na wenye ukwasi pia! Abdulrahman aliniambia, “Mayega una amani kubwa sana katika kifua chako!” Nikayakumbuka maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alisema, “Mtakapoona tumejizidishia ulinzi jueni kuwa tunawaibia!”

Ulinzi huu ungekuwa na maana zaidi kama mtu angekuwa anazikwa nao. Lakini kaburini mtu hafukiwi hata na kisu cha mfukoni! Nimekutana na kushikana mikono na marais wangu wote wa awamu zilizotangulia.

Na Rais Mwinyi akiwa mlezi wa chama chetu tulikuwa tunamtembelea kama Baba, Ikulu, anakaa nasi kule nyuma, ‘tunachati’. Kwa marais wote hao walinzi walikuwapo.

Lakini hakuna kati yetu aliowahisi mwilini wakati wote tulipokuwa na Rais. Lakini kwanini uwe na maisha yaliyojaa wasiwasi muda wote na hofu nyingi mpaka uogope hata na hatari isiyokuwapo?

Baba Juni mosi mwaka huu Hamida Mapunda wa Kijiji cha Mugundeni, Tarafa ya Mang’ula Wilaya ya Kilombero, akiwa katika siku zake za mwisho za ujauzito wake, alikamatwa na polisi na kutiwa ndani.

Tuhuma ni kwamba mume wake Abdallah Mrisho alinunua kitanda ambacho nacho kinatuhumiwa tu kuwa ni cha wizi! Ni unyama wa kiasi gani kumshikilia katika mahabusu ya polisi kwa siku sita mwanamke aliyetayari kwa kujifungua wakati wowote?

Siku ya sita uchungu ulipomzidia huku maji ya uzazi yakimtoka alitolewa ndani na makatili wale mpaka kwenye majani. Na kama mnyama vile, akaachwa huko ajifungue mwenyewe!

Mtanzania mpya wa awamu ya tano (kichanga chake) kikaiona anga ya nchi yake kwa mara ya kwanza kikiwa katika majani sawa na vichanga vya mafisi na manyani vinavyozaliwa huko msituni. Inauma sana!

Halafu anasimama mwanaume mtu mzima ambaye mpaka umri ule hajawahi kupatwa na uchungu wa kuzaa, hatujui huko mbele, anasema wamefungua faili. Halafu?

Kusema gani huku? Baba utufundishe kusema! Nani kasema awamu yetu imepunguza rushwa? Tumbusi wa sasa wanadaiwa kuomba rushwa kwa kupiga, galagaza, wakikataa wanawatia ndani.

Mzazi mwingine Hamida anasema, “Mwanangu alifariki Mei 12 lakini nilizuiwa kutoka hospitalini nikamzike mwanangu. Ilinibidi nilale wodini huku mwili wa mwanangu ukiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti mpaka sh. 638,000 kama kikombozi zipatikane!”

Hamida ambaye alijifungua mtoto utumbo wake ukiwa nje na kulazimika kufikishwa Muhimbili anasema, “Binafsi nilishangaa kwasababu siku zote nimekuwa namsikia Waziri wa Afya anasema mtoto chini ya miaka mitano hutibiwa bure!”

Mpaka leo si Waziri si Naibu aliyesema kitu. Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano kwa umma cha MNH, Aminiel Aligaesha amesema, “Hii haijalishi kama ni mama mjamzito au mtoto. Hiyo ndiyo sera yetu na ipo wazi kabisa.”

Kusema gani huku? Baba utufundishe kusema! Baba kama utautaka tena urais mwaka 2020 utakapofika tena pale Morogoro na kwingine ulikofanya kama vile, utapokewa na umati mkubwa zaidi ya ule!

Lakini hao wote hushangilia kwa nguvu kubwa, lakini siyo wapiga kura. Hawajiandikishi na wakijiandikisha siku ya kupiga kura hawatokei.

Hayo tumeyaona kwa mwanamwema Augustino Lyatonga Mrema alipogombea urais. Hapo ndipo watu wazima watamkumbuka Abdulrahman, lakini nyakati zitakuwa zimeishapita!

Mtuhumiwa wa kesi ya Bilionea Msuya alivyohasiwa gerezani

SHWAIBU Jumanne, maarufu kwa jina la Mredii, amenusurika kifo, lakini amepata ulemavu wa maisha. Amehasiwa na hivyo hana uwezo tena wa kupata mtoto wala kufanya tendo la ndoa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Aidha, Mredii ameishi gerezani kwa miaka mitano mfululizo, bila kuwa na kosa; na sasa ametoka akiwa hana mtaji na hana nyezo za kufanyia kazi.

Mredii, alikuwa mmoja wa washitakiwa sita waliotuhumiwa kwa mauaji ya mfanyabiashara maarufu wa Mirerani, mkoani Manyara Erasto Msuya.

Kabla ya kukutwa na dhahama hiyo, alikuwa akijishughulisha na kazi ya uchimbaji madini. Washtakiwa wenzake watano wamehukumiwa na Mahakama Kuu, kunyongwa hadi kufa.

Mbela ya Jaji Maghimbi, Mredii alinukuliwa akisema, “niliteswa na polisi hadi kupewa ulemavu, ikiwamo kuhasiwa.”

Anasema, “kipigo nilichokipata mikononi mwa polisi, kimemsababishia kilema na maumivu makubwa. Kutokana na kuhasiwa, niliamua kumpa talaka mmoja ya wake zangu, aitwaye Zuhura Hassan kwa kuwa sikuwa na uwezo tena kama mwanamume.”

Anasema, aliamua kubakiza mkewe mmoja anayeitwa Adile Juma.

Mredii anasema, hakupata matibabu mazuri kutokana na kipigo hicho na kwamba kwa vile sasa yuko huru, moja ya vipaumbele vyake, ni kupata matibabu sahihi ya afya yake.

Akiongozwa na wakili wake Majura Magafu kutoa utetezi wake, Mredii alidai mbali na kuhasiwa, polisi walimvunja mara mbili mguu wa kushoto na mara moja mguu wa kulia.

Alisema wakati fulani walimfunga kamba na kumning’iniza kama mbuzi aliyebanikwa.

“Kwa hayo mateso niliyopata hapo kituoni nimekuwa mlemavu. Niliwekwa staili ya mbuzi anayechomwa nikiwa sina nguo,” alieleza.

Anasema, mtu unapokuwa gerezani unakuchukuliwa kama mhalifu na unapokuwa kwenye lile karandinga watu wanaona wewe ni mhalifu na wengine wanakuita mwizi bila kujua ni kosa gani limekupeleka gerezani.

Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa, ni Sharifu Mohamed, aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza, Musa Mangu (wa tatu), Karim Kuhundwa (wa tano), Sadik Mohamed (wa sita) na Ally Mussa (wa saba), ilitolewa Julai 23 na Jaji Salma Maghimbi.

Bilionea Msuya, aliuawa kwa kupigwa risasi, tarehe 7 Agosti 2013, maeneo ya Mijohoroni wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.

Akiongozwa na wakili wake Majura Magafu kutoa utetezi wake, tare 15 Mei mwaka huu, Mredil alitoa madai mazito mahakamani, akisema kuwa aliteswa na polisi hadi kupewa ulemavu ikiwamo kuhasiwa.

Kutokana na kuhasiwa huko, Mredil alisema, aliamua kuchukua uamuzi wa kumpa talaka moja mkewe aliyemtaja kuwa ni Zuhura Hassan kwa vile alikuwa hana uwezo tena kama mwanamme.

Alisema, mbali na kuhasiwa, lakini polisi walimvunja mara mbili mguu wa kushoto na mara moja mguu wa kulia.

Alisema, siku ya mauaji, yeye hakuwepo Arusha wala Kilimanjaro, bali alikuwa shambani kwake huko Babati akivuna mazao yake. Alisema alikuwa huko kuanzia tarehe 13 Julai hadi tarehe 7 Agosti 2013.

Shwaibu alidai alikamatwa na polisi baada ya kuitwa na mkuu wa kituo cha cha polisi (OCS) Mirerani, Ally Mkalipa, tarehe 17Agosti 2013, saa 2 usiku, na siku iliyofuata alimkabidhi kwa polisi wa Moshi.

Kutoka Polisi Mirerani, polisi walimfunga pingu na kumfunga kitambaa machoni na kupakizwa katika gari aina ya Toyota Landcruicer Hardtop na kulazwa kifudifudi hadi kituo cha polisi cha KIA.

Alidai walipofika hapo, hakuingizwa kituoni bali gari liliegeshwa nje na polisi mmoja alipotaka kumshusha, polisi mwingine alimtaka asimteremshe kwa kuwa kuna mtuhumiwa mwenzake.

Alisema kutoka kituoni hapo, polisi walimfunga pingu mikononi na kumuingiza kwenye gari na kumlaza kifudifudi na gari lilielekea hadi kituo kikuu cha polisi jijini Arusha.

Mshitakiwa huyo alidai walipofika kituoni, polisi walimfungua pingu na kumuingiza katika chumba kimoja kikubwa na walimtaka kueleza kila kitu kuhusu mauaji ya Msuya.

Kwa mujibu wa Mredil, aliwambia polisi hafahamu kitu na kwamba hakuwepo Arusha wala Kilimanjaro na hapo ndipo walipompeleka kituo cha Kisongo maarufu kwa jina la Guantaramo.

“Waliniambia hatutaki kitu kingine zaidi ya saini yako. Kwa hayo mateso niliyoyapata hapo kituoni, nimekuwa mlemavu. Niliwekwa staili ya mbuzi anayechomwa nikiwa sina nguo,” alidai.

Mredil alidaihakuwa anamfahamu mfanyabiashara Joseph Mwakipesile, maarufu kama Chussa kama maelezo ya kukiri kosa ya mshitakiwa wa kwanza, Sharifu Mohammed yaliyosomwa kortini.

“Sikuwa namfahamu kabisa Chussa zaidi ya kuona baishara zake zikiwa zimeandikwa Chussa Mining. Kwanza yeye kumuona mitaani ni vigumu kwa vile anatembea na walinzi wenye miili,” alidai.

Pia alikanusha maelezo ya onyo ya mshitakiwa wa tatu, Juma Mangu na wa saba Ally Mjeshi yaliyosomwa mahakamani yakimtaja yeye na wengine kuwa washiriki katika tukio hilo.

Mbali na maelezo hayo, mshitakiwa huyo alikanusha maelezo yaliyomo katika ungamo ya mshitakiwa wa tano, Karim Kihundwa yakidai siku ya mauaji alikuwepo eneo la tukio.

Alipoulizwa na wakili wake, Magafu kuwa anaiomba nini mahakama, ndipo shahidi huyo alipoiomba imuachie huru kwa vile hakuhusika na mauaji hayo na kesi hiyo imemtia ulemavu.

Jokate, Murro, Kafulila kumsaidia Rais Magufuli

RAIS John Magufuli amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, ambapo amemteua Mwanamitindo, Jokate Mwegelo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe huku aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila akimteua kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Rais Magufuli amefanya uteuzi huo leo tarehe 28 Julai, 2018 na Ikulu jijini Dar es Salaam.

Wengine walioteuliwa ni pamoja na Jerry Muro aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru wakati Patrobas Katambi akiteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma.

Vile vile, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ambapo Godfrey Chongolo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido akimteua kuirithi mikoba ya Hapi Kinondoni.

Na Lengay Ole Sabaya ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai. Pia, Rais Magufuli amemteua Moses Machali kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu.

Hapa chini orodha kamili ya mabadiliko yaliyofanywa na Rais Magufuli

Katibu tawala

Abubakar Musa – Dar es Salaam
David Kafulila – Songwe
Denis Bandisa – Geita
Happy William – Iringa
Abdallah Malela – Katavi
Rashid Chatta – Kigoma

Masaile Mussa – Manyara
Carolin Mpapula – Mara
Dk. Jerry Mareko – Mtwara
Christopher Kadio – Mwanza
Eric Chitindi – Njombe
Riziki Salas – Ruvuma

Makatibu katika Wizara
Andrew Masawe – Ofisi ya Waziri Mkuu
Lisante Gabriel – Wizara Uvuvi na Mifugo
Dk. Jimmy James – Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi
Edwin Muhede – Wizara Viwanda Biashara na Uwekezaji

Wakuu wa Wilaya
Jerry Murro- Arumelu
Patrobas Katambi – Dodoma
Jokate Mwegero – Kisarawe

Ujumbe wa Mbowe baada ya Waitara kuondoka

Wah. Viongozi na Wabunge!

Amani iwe kwenu wote!

Ujenzi wa Demokrasia ni safari ndefu yenye milima, mabonde, miiba, mawe na kila aina ya majaribu yenye vikwazo.

Waasisi wa Chama walifananisha na safari ya treni toka Dar kwenda Kigoma. Kwamba kuna watakaoshuka njiani kwa sababu mbalimbali, (halali na batili) hali kadhalika wengine wengi watapanda vituo mbalimbali kuungana na safari.

Hampaswi kushangaa baadhi yetu kuishia njiani. Nina hakika na imani kuwa hatakuwa wa mwisho kutoka.

Yumkini wako maelfu ambao wanapanda treni yetu kila siku.

Si kila atokaye ni hasara kwa Chama. Kutoka kwingine kwaweza kuwa baraka.

Wajibu huu wataka moyo Mkuu!! Shime wenye nia ya kufika Kigoma kwa umoja wetu tusonge mbele tukijiamini sana!!

Freeman Mbowe (MP)
Mwenyekiti & KUB

Zitto atoa neno zito kuondoka kwa Waitara

BAADA ya Mbunge wa Ukonga (Chadema) Mwita Waitara kutangaza kurudi CCM, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe  ametoa neno kuhusu hatua hiyo. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Kupitia ukurasa wake wa Twitter Zitto amemhoji Mwita kwa kuandika kuwa, amerudije CCM wakati viongozi waandamizi wa Chadema wana kesi mahakani  huku Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu yuko hospitalini takribani mwaka kwa majeraha ya risasi kutokana na jaribio la kuuawa.

Mbunge mwenzio yupo hospitali mwaka sasa kwa majeraha ya risasi kufuatia jaribio la kumwua. Viongozi wa Chama chako Karibu wote Ngazi ya Taifa wana kesi inayohatarisha kuwaweka jela. Watu wanauwawa na kupotea kila siku. Halafu unajiunga na hao wanaosababisha hayo? Kweli Mwita?” amehoji Zitto.

Waitara ametangaza uamuzi wa kurudi CCM mchana wa leo jijini Dar es Salaam mbele ya wanahabari baada ya kukaribishwa rasmi na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Hunphrey Polepole.

Chadema kwazidi kufukuta, Mbunge Waitara akimbilia CCM

KINYANG’ANYIRO cha uchaguzi mkuu ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza kukimega chama hicho. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Mbunge wa Ukonga (CHADEMA), Mwita Mwaikabe Waitara, ameamua kuondoka chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Waitara, alikuwa mmoja wa viongozi wandamizi ndani ya Chadema ambao wanapinga Freeman Mbowe, kuendelea kugombea uenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka kesho.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya chama hicho, tayari Mbowe ameunda “mtandao” kwa lengo la kumtetea na kuhakikisha anagombea kwa “gharama yeyote” nafasi hiyo na kushinda.

Akitangaza uamuzi wake wa kuondoka Chadema, leo Jumamosi, tarehe 28 Julai, ofisi ndogo ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam, Waitara amesema, “nimeamua kuondoka Chadema kwa kuwa hakuna demokrasia.”

Waitara amepokelewa ndani ya chama hicho ambacho aliwahi kuwa katibu wa Umoja wa Vijana (UV-CCM), mkoani Tanga na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole.

“Ugomvi wangu na Mbowe hivi sasa, ni uchaguzi wa ndani ya chama. Yeye anataka kuwa mwenyekiti na ameapa kumshughulikia yeyote anayepinga mradi wake huu,” ameeleza Waitara.

Amesema, “mimi nilisema huyu mtu ameongoza chama miaka 20. Anapaswa kupumzika. Lakini yeye amekusanya wapambe wanaomtetea; na ndani ya chama sioni demokrasia, bali kuna vitu vya kupachika pachika.”

Anaongeza, “lakini pili kuna matumizi mabaya ya ruzuku. Chadema kinapata ruzuku ya Sh. 360 milioni, kila mwezi. Lakini fedha zote zinaliwa na wakubwa pale makao makuu; na kwamba hakuna anayeruhusiwa kuhoji chochote.”

Kwa mujibu wa Waitara, akiwa mbunge wa Chadema, amepata changamoto mbili. Namna ya kufanya kazi na Chadema na jambo la pili, ni namna ya kushirikiana na serikali kuleta maendeleo.

CCM yamgeuka Lugola Buyungu

MAZINGIRA ya Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Buyungu yamekilazimisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumtosa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).

Ni kile kinachoelezwa kuwasakama vijana wa bodaboda na kudai ‘dawa yao inachemka’ ambapo Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Bashiru Ally amesema, Lugola anapaswa kuanza kwanza kutafakari utendaji wa Jeshi la Polisi.

CCM na vyama vingine vya upinzani vinaendelea na kampeni zake kwenye jimbo hilo ambapo uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mwaka huu.

Juzi akiwa wilayani Kakongo lilipo Jimbo la Buyungu ndani ya Mkoa wa Kigoma Dk. Bashiru amesema, polisi wamekuwa wakikamata bodaboda na kuzijaza kwenye vituo vya polisi kwa kile alichoeleza kutokuwepo kwa sababu za msingi.

Kiongozi huyo wa CCM amesema, lazima Lugola na timu yake wahakikishe wanakomesha vitendo vya kunyanyasa waendesha bodaboda.

Ameeleza zaidi kuwa, Jeshi la Polisi linapaswa kutenda haki na kuzingatia utu wa watu kwa kuwa, baadhi ya maeneo malalamiko ya kunyanyaswa yanajitokeza.

Dk. Bashiru ameeleza kuwa, hawako tayari kuwatetea bodaboda lakini kuna kila sababu ya Jeshi la Polisi kuata na kusimamia haki na si kuwanyanyasa vijana hao wa bodaboda.

“Hatuwatetei bodaboda…nataka Waziri wa Mambo ya Ndani kufanyia kazi suala hilo…” ameeleza Dk. Bashiru.

Kiswahili kimefika kiwango hiki

KUNA watumiaji wachache wa mtandao maarufu wa facebook wanaofahamu kwamba, mtandao huu unatumia lugha ya Kiswahili kuandaa mikataba ya kulinda taarifa zao za siri zinazoingizwa humo, japo mtandao huo unatumiwa na watu zaidi ya milioni 100 wanaoongea Kiswahili. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Haya yamefahamika tarehe 10 Aprili 2018 wakati Mark Zukerberg, mwasisi na Mkurugenzi Mkuu wa mtandao wa facebook, alipowekwa kitimoto na Kamati za Bunge la Marekani za sheria na biashara zinazosimamia masuala ya haki za watumiaji wa huduma. 

Katika mahojiano yaliyofanyika kwa siku mbili mfululizo kuanzia 10 Aprili 2018, Seneta wa Louisiana,John Kennedy, alimwambia maneno haya Zukerberg:

“Nataka kupendekeza kwamba, uende nyumbani na kumwambia mwanasheria wako unayemlipa Dola 1,200 kwa saa kuwa, mikataba hiyo inapaswa kuandikwa kwa Kiingereza na sio Kiswahili, kusudi kila Mmarekani wa kawaida aweze kuilewa.” 

Kauli hii ilizua hasira kutoka kona mbalimbali duniani, Seneta Kennedy akituhumiwa kwa ubaguzi wa lugha zisizo za Kiingereza, na hasa ubaguzi dhidi ya Waafrika wengi wanaotumia lugha ya Kiswahili.

Mtandao wa facebook unatumiwa duniani nzima, kiasi watumiaji wa Kiswahili wapatao milioni 100 hawawezi kuongelea intaneti bila kuutaja.

Japo watumiaji hawa wana kitovu chao katika Afrika Mashariki, wamesambaa duniani kote mpaka Oman, Afrika Kusini, Asia, Ulaya na ndani ya Amerika kwenyewe.

Kwa mujibu wa Profesa Ali Mazrui, lugha ya Kiswahili imegeuka lugha ya kimataifa ndani na nje ya Afrika kwa sababu ya kurithi misamiati yake kutoka katika vyanzo vitatu, yaani, lugha asilia za kibantu, mapokeo ya Mashariki kupitia Dini ya Kiislamu pamoja na wafanyabiashara kutoka Bara la Asia na mapokeo ya Magharibi kupitia Dini ya Kikristo pamoja na wakoloni wa kizungu. Kwa ufupi, Kiswahili ni kama lugha ya biashara ndani ya eneo kubwa ndani na nje ya Afrika.

Kwa siku mbili mfululizo, Zukerberg alihudhuria mahojiano kati yake na wabunge wa Marekani, kuhusu tuhuma kwamba kampuni moja ya Kompyuta kutoka Uingereza, iitwayo Cambridge Analytica, ilichota na kutumia taarifa binafsi za wateja waliojisajili katika mtandao wa facebook, lakini bila kuomba ridhaa ya watumiaji hao, na kuzitumia kumfanyia kampeni Rais Donald Trump kwenye uchaguzi mkuu wa 2016.

Mbali na kuingilia faragha ya watumiaji wa facebook bila ridhaa yao, kampuni ya Cambridge Analytica inatuhumiwa kutumia taarifa hizo kusambaza taarifa feki mtandaoni kwa lengo la kumfanya Trump ashinde.

Tuhuma kama hizo zimekuwa zinaukabili uongozi wa mtandao wa facebook kutoka nje ya Amerika pia, na hasa katika mataifa ambayo hayana ufundi wa kudhibiti taarifa zinazoeza kusababisha vurugu na vifo zinazosambazwa na watumiaji wenye nia ovu kupitia mtandao huu.

Kwa mfano, inaaminika kuwa, nchini Kenya mitandao ya facebook na whatsApp ilitumika kusambaza habari za uongo wakati wa uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa.

Na kwamba, hatua hiyo ilichangia katika kuchochea tukio la mauaji ya watu zaidi ya 100. Kampuni ya Cambridge Analytica inatuhumiwa kufanya jambo kama hilo huko Nigeria.

Huko nje ya Afrika, tatizo la usambazaji wa taarifa za uongo mitandaoni kupitia mtandao wa facebook na mitandao mingine, ni kubwa.

Tayari mtandao wa facebook unalaumiwa kusababisha chuki Waislamu wa Rohingya huko Myanmar. Katika nchi ya Ufilipino Rais Rodrigo Duterte anatuhumiwa kuutumia mtandao wa facebook kuwanyamazisha wapinzani wake.

Aidha, kuna tuhuma kuwa, facebook ilitumika kusambaza taarifa za uongo zilizochangia katika kuwafanya wapiga kura wa Uingereza kupiga kura ya kujitoa katika Jumuiya ya Ulaya kwa sababu ya kufuata mkumbo tu.

Ni katika mazingira haya, Mkurugenzi Zukerberg aliwekwa kiti moto, huku maseneta wakimwambia kuwa kama hawawezi kusimamia biashara yao vizuri Bunge litalazimika kuwasaidia kuisimia biashara hiyo kwa kutunga sheria mahususi kwa ajili ya kuratibu kazi za mtandao wa facebook.

Mwisho wa mahojiano, Seneta Long alisikika akisema, “Wewe ndiye mtu unayepaswa kuziba mianya ya matumizi mabaya ya mtandao wenu, na sio sisi. Unapaswa kuliokoa jahazi lako.”

Naye Seneta akahitimisha mahojiano kwa kusema, “Sitaki kupiga kura ya kutunga sheria ya kusimamia shughuli za facebook kadiri suala la kulinda haki ya faragha ya watumiaji linavyohusika, lakini Mungu akipenda nitafanya hivyo.”

Naye Zukerberg aliwaahidi wabunge wa Marekani kwamba atafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa, taarifa binafsi za watumiaji wa mtandao wake zinalindwa na kwamba mtandao huo unatumiwa vizuri.

“Tunao wajibu wa kulinda taarifa binafsi za watumiaji wa mtandao wetu, na kama tunashindwa hatustahili kuwahudumia,” alisema Zukerberg.

Jukumu la kulinda taarifa binafsi zinazopatikana kupitia mawasiliano binafsi yanayohusisha pande mbili, kati ya wakala na bosi wake, sio la sheria za Marekani pekee.  Hata sheria za Tanzania zinalitambua.

Taarifa binafsi zinazotolewa na mwajiriwa kwa mwajiri wake, mwanafunzi kwa mwalimu wake, mgonjwa na daktari au taarifa zinazotolewa na mshitakiwa kwa wakili wake, ni taarifa za siri. Zinatolewa katika mazingira ya kuaminiana.

Katika mazingira haya, mtoa taarifa anaitwa mtu wa upande wa kwanza (first party); mpokea taarifa anaitwa mtu wa upande wa pili (second party); na watu baki ambao hawakuhusika moja kwa moja katika muamala wa makabidhiano ya taarifa binafsi wanaitwa watu walio katika upande wa tatu (third party).

 Lakini, watu walio katika upande wa tatu wanagawanyika katika makundi mawili. Kwa upande mmoja, kuna watu walio katika upande wa tatu na ambao, kwa njia ya mzunguko, wanayo ruhusa ya kuziona na kuzifanyia kazi taarifa za siri, japo hawakushiriki katika muala wa makabidhiano yake.

Kwa mfano, bila kuomba upya ridhaa ya mgonjwa, mtaalam wa maabara anayo nafasi ya kuziona na kuzifanyia kazi taarifa za mgonjwa zinazotolewa kwa daktari.

Na kwa upande mwingine, kuna watu walio katika upande wa tatu na ambao, hata kwa njia ya mzunguko, hawana ruhusa ya kuziona na kuzifanyia kazi taarifa za siri, mpaka waombe upya na kupatiwa kibali au ridhaa ya mtoa taarifa wa kwanza.

Bunge la Marekani lilitaka kujua ni kwa kiasi gani uongozi wa mtandao wa facebook unasimamia sheria za aina hii.

Auawa kwa tuhuma za ujambazi

MTU mmoja anayefahamika kwa jina la Mussa Faustine (19) mkazi wa Bugarika wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza, ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa tuhuma za ujambazi. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Akizungumza na wanahabari leo tarehe 28 Julai, 2018, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Ahmed Msangi amesema Faustine amefariki dunia akiwa njiani kuelekea hospitali kutokana na majeraha ya kipigo cha wananchi,  baada ya kuhojiwa na askari polisi.

Kamanda Msangi amesema kabla ya mtuhumiwa huyo umauti kumfika aliutaja mtandao sugu wa ujambazi na kiongozi wake anayefahamika kwa jina la Hamza, ambao ulipanga kutekeleza matukio mengine ya ujambazi hivi karibuni.

“Kijana huyo alitoa ushirikiano vizuri kwa askari japo alikuwa katika hali ya kujeruhiwa sana, alitoa ushirikiano na kueleza kikundi chake ambacho wanashirikiana katika kufanya na kupanga matukio ambayo walikuwa wamepanga kufanya katika siku za hivi karibuni kisha alimtaja kiongozi wake aitwaye hamza maarufu mjomba,” amesema Kamanda Msangi.

Vile vile, Kamanda Msangi amesema marehemu Faustine aliwapeleka polisi maeneo wanakoficha silaha, ambapo polisi baada ya kufanya upekuzi walikuta silaha nne zilizotengenezwa kienyeji na risasi saba.

Kamanda Msangi amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya rufaa ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi na kwamba uchunguzi ukikamilika utakabidhiwa kwa ndugu zake.

Umoja wa Mataifa kununua tani mil 3 za chakula

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limewatangazia neema wakulima wa mazao ya chakula nchini, ambapo imewahakikishia kwamba itanunua chakula cha ziada kitakachozalishwa zaidi ya tani milioni 3. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Hayo yamesemwa leo terehe 27 Julai, 2018 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa WFP, Bw. David Beasley, jijini Dar es Salaam.

Waziri Majaliwa amesema Beasley amemhakikishia kwamba shirika lake litayanunua mazao hayo, na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa masoko kwa wakulima.

“Taarifa za Wizara ya Kilimo zinaonesha kuwa mavuno ya mazao ya chakula kama mahindi, maharage na mbaazi yatafikia tani milioni 16 wakati mahitaji ya chakula kwa Watanzania kwa mwaka ni tani milioni 13, hivyo tutakuwa na ziada ya tani milioni tatu,” amesema.

Vile vile, Waziri Majaliwa amesema ujio wa Beasley hapa nchini ni fursa itakayowawezesha Watanzania kunufaika kwa kiwango kikubwa katika kilimo, uhifadhi na uuzaji wa mazao ya chakula yanayolimwa hapa nchini.

Upasuaji wa kifua wafanikiwa JKCI

WATOTO tisa wenye umri kuanzia miezi mitatu hadi 17 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na Madaktari Bingwa wa upasuaji wa Moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Shirika la Chain of Hope la Uingereza kuanzia tarehe 23 hadi 27 Julai, 2018. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo kwa umma na Kitengo cha Uhusiano Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), na kusema kuwa, watoto waliofanyiwa upasuaji ni wale wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambapo madaktari hao wametengeneza valvu na kuziba matundu.

Pamoja na kurekebisha mishipa ya moyo ambayo imekaa vibaya, kurekebisha mfumo wa uzungukaji wa damu katika moyo na kuweka valvu za bandia kwa wale walio na valvu za moyo zilizoharibika.

“Wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji hali zao zinaendelea vizuri na sita kati yao wameruhusiwa kutoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Jamii yashauriwa usimamizi shirikishi wa misitu

JAMII imeshauriwa kuzingatia dhana ya usimamizi shirikishi wa misitu kibiashara yenye kulenga kuwapatia kipato kufuatia utunzaji wa misitu na uvunaji endelevu. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Afisa wa Kujenga Uwezo kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Simon Lugazo amesema hayo kwenye mkutano wa madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mvomero, wakati umefika kwa jamii kutambua umuhimu wa kujenga mfumo mzuri wa kuhakikisha mapato yanaleta faida kwenye halmashauri zao.

Amesema usimamizi wa misitu kibiashara unawezekana kama kijiji kikiwa na mipango ukiwemo wa matumizi bora ya ardhi uliopitishwa katika ngazi zote.

Ametaja mpango mwingine kuwa ni mpango wa uvunaji wa msitu husika, mpango wa usimamizi wa msitu uliopitishwa ngazi ya kijiji halmashauri na sheria ndogo za usimamizi wa misitu zilizopitishwa ngazi ya kijiji na halmashauri.

Lugazo ameishauri jamii inayojihusisha na masuala ya uvunaji misitu katika kunufaika na usimamizi wa misitu kibiashara lazima ufuate njia endelevu za uhifadhi ili uvunaji ulete faida bila kuwa na matokeo hasi kwenye mazingira.

Lugazo amesema mauzo ya hewa ukaa na malipo kwa makampuni yanayotumia maji yanayotoka msituni mfano TANESCO na idara ya maji yanapaswa kuzingatiwa na kwamba sekta hizo zilipaswa kulipa asilimia 2 kwa watunzaji misitu.

Afisa huyo wa TFCG, alitolea mfano Halmashauri za wilaya ya Kilwa mkoani Lindi na Tunduru mkoani Ruvuma ambazo zimenufaika kwa kukusanya kiasi cha sh bil 1.4 kutokana na uvunaji endelevu wa mbao ambao ulifaidisha watu wapatao 33,868.

Pia amesema matumizi ya teknolojia bora inayozalisha mazao ya kutosha inapaswa kutumika ikiwemo ya kupanga kuni kwa ajili ya kupata mkaa kitaalamu kwa njia inayopendezwa na wajasiliamali na wanamazingira.

Lugazo amesema maeneo yaliyosimamiwa vizuri yakitoa mapato na asilimia 10 ikarudishwa halmashauri itasaidia kuboresha miradi mingine ikiwemo ujenzi wa madarasa kwenye vijiji husika huku pesa iliyokusudiwa ikaenda kwenye mambo mengine.

Naye Diwani wa kata ya Homboza Nelson Joseph ameushukuru mradi huo kwa kutoa elimu inayoonesha kuwa jamii nayo inaweza kunufaika na misitu baada ya kusimamia.

Joseph amesema kuwa awali jamii ilikuwa ikijitahidi katika kuhifadhi misitu lakini wamekuwa hawapati faida yoyote jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa.

Iran yajibu mapigo ya Marekani

NCHI ya Irani imejibu tishio la Rais wa Marekani, Donald Trump kwa kumuonya kwamba atapoteza kila anachomiliki iwapo ataruhusu nchi yake kulishambulia Taifa hilo. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Mnamo terehe 23 Julai, 2018 kupitia akaunti yake ya Twitter, Rais Trump aliitaka Iran kutotishia taifa lake na kwamba ikifanya hivyo ataiangamiza kupitia vita.

Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Iran, Meja Jenerali Qassem Soleiman amesema iwapo Trump ataanzisha vita dhidi ya nchi yake, vita hiyo itaharibu kila anachokimiliki.

Jenerali amemuonya Trump kwamba Jeshi la Iran lina nguvu na uwezo, pia liko tayari kumfikia popote alipo, huku akiapa kuwa iwapo Rais huyo wa marekani ataanzisha vita wako tayari kuimaliza.

Chanzo: BBC Swahili.

Biashara yampeleka Ally Kiba Coastal Union

NI wazi kuwa klabu ya Coastal Union imemsajili Msanii maarufu nchini Ally Kiba kwa sababu za kibiashara zaidi na uwezo wa staa huyo uwanjani. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Coastal imesajili Kiba katika kikosi chake kilichorejea Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kucheza ligi daraja la kwanza kwa misimu kadhaa iliyopita.

Mengi yameibuka baada ya Coastal kutangaza kikosi chake cha msimu huu, lakini swali la kujiuliza kocha wa kikosi hicho alimuihitaji staa huyo? Kiba atakuwa na muda wa kushiriki vizuri msimu mzima na kikosi hicho? Staa huyo yupo tayari kupumzika muziki na kujikita uwanjani? Uongozi wa Coastal utakuwa na majibu ya maswali hayo.

Ukichana maswali hayo, lakini inawezekana uongozi wa Coastal wameangalia kibiashara kwa kumtumia Staa huyo maarufu ‘Celebrity Marketing’ ambazo zinaweza kuinufaisha klabu kwa siku za mbele kutokana na ukubwa wa jina alilonalo mchezaji huyo ambaye pia ni mwanamuziki.

Uwepo wa Kiba unaweza kuwanufaisha Coastal kwenye upande wa mapato ya uwanjani, kutokana na mwanamuziki huyo kuwa na mashabiki wake binafsi, ambao wanampenda kutokana na kazi yake ya muziki hivyo watakuwa wanavutiwa zaidi kumuona uwanjani akicheza.

Lakini pia klabu yenyewe kama taasisi inaweza kuvutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza kibiashara kutokana na kuwa na mchezaji mwenye ushawishi mkubwa ndani ya nchi na bara la Afrika kiujumla kutokana na yeye mwenyewe kuwa ni ‘Brand’ inayojitegemea.

Kama kungekuwa na utaratibu mzuri wa mapato wa haki za matangazo za televisheni basi Coastal Union ingenufaika kwenye hili kutokana na watu wengi watatamani kuifuatilia na kuitazama kwa njia ya televisheni timu hiyo kila inapo shuka dimbani kama zilivyokuwa Simba na Yanga.

Kwa upande wa mauzo ya jezi, Coastal wanaweza kutengeneza kiasi kikubwa cha fedha, kama kungekuwa na mifumo rasmi ya kibiashara ndani ya klabu za Ligi Kuu, sema kwa kuwa bado hatujajitambua na kujua tunataka nini kwenye soka, huu utajiri utaendelea kutupita tu.

Licha ya hayo yote lakini wadau wengi wa mchezo wa soka wanajiuliza ni namna gani Kiba ataweza kufanya kazi zote mbili kwa pamoja, kutokana na asilimia kubwa na umaruufu alioupata umetokana na kazi yake ya muziki ambayo ameifanya kwa zaidi ya miaka 10.

Na ukizingatia mchezo wa mpira unahitaji muda ‘Time Mnagement’ nguvu pamoja na mazoezi na muda huo huo aendelee kufanya shughuli zake za muziki ambazo naamini zinamuingizi kipato kikubwa kutokana na uhodari aliokuwa nao.

Mrema: Rais Magufuli kuwa makini na unaowateua

AUGUSTINO Mrema, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha TLP,  amemtaka Rais John Magufuli kuwa macho anapofanya uteuzi wa viongozi wa umma, huku akimshauri kufuata nyayo za Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Mrema ametoa ushauri huo leo terehe 27 Julai, 2018 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea nchini, ambapo amesema Rais Mkapa wakati wa utawala wake alikuwa anateua watu wenye sifa stahiki.

Mrema amesema kitendo ambacho amekiita kuwa ni cha ‘kuokoteza okoteza’ kimepelekea baadhi ya watu kwenye wizara mbalimbali kufanya mambo ya ajabu ambayo Rais Magufuli hayajui.

“Rais awe macho sana, hawa watu wa kuokoteza okoteza hawafai, ujifunze kwa Rais Mkapa,” amesema Mrema.

Katika hatua nyingine, Mrema amesema amependezwa na utendaji kazi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ambapo amesema yuko tayari kumuonyesha njia alizopitia katika kuiongoza wizara hiyo miaka kadhaa iliyopita wakati akiwa Waziri.

“Lugola amenipendeza kwa kile kitendo cha kufuatilia mbwa wa polisi, si jambo dogo sababu watu wengi wanajiuliza inakuaje mbwa wa polisi anatumika kulinda majumba ya watu,” amesema.

Serikali yazindua mpango wa Jiji la Dar es Salaam

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amezindua Master Plan (Mpango Mji) wa jiji la Dar es Salaam. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mpango huo utakaotumika kwa kipindi cha miaka 20 ijayo, umezinduliwa leo Ijumaa, terehe 27 Julai; unalenga kuwapa wadau fursa ya kutoa mapendekezo bora ya jinsi ya kuutekeleza.

Kwa sasa, jiji la Dar es Salaam linatumia master plan iliyoandaliwa mwaka 1979 na ambayo muda wake umeisha mwaka 1999.

Akizungumza na wadau wa jiji la Dar es Salaam, waziri Lukuvi amesema, mpango huo hauna lengo la kuvunja makazi ya watu wakati wa utekelezaji, lakini ametaka waananchi kutonunua maeneo wala kuendeleza ujenzi bila kuwasiliana na wataalamu wa ardhi.

“Ukinunua eneo bila kuwasiliana na wataalamu wa ardhi, unaweza kujikuta unaingizwa mjini. Hii ni kutokana na ukweli kuwa unaweza kununua eneo kwa ajili ya kujenga baa, wakati eneo hilo limetengwa kwa ajili ya shule,” ameeleza.

Ameongeza, “kwa hiyo, mapendekezo haya yasiwashtue. Mpango huu ukianza kutumika, utataka kila kitakachojengwa, kifuate mpango ulivyo.”

Amesema mpango huo ulianza kuandaliwa tangu mwaka 2012, lakini ulicheleweshwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo upigaji wa picha za uchambuzi zinazoonyesha kila eneo, hali halisi ya ukuaji wa jiji na dira ya jiji kuwa endelevu.

Wakati huo huo, Lukuvi amepiga marufuku urasimishaji holela wa ardhi kwa dhumuni la kuzidhibiti kampuni za kitapali zilizojitokeza.

Lukuvi ameeleza kuwa utaratibu wa kulipa fedha kwa kampuni zinazoibuka mitaani na kupewa tenda bila kufuata utaratibu na kupitishwa na wataalamu wa ardhi kutoka wilayani.

Amesema, amepata taarifa kuwepo kampuni tatu zilizoibuka kama warasimishaji bila kufuata utaratibu hatimaye walitokomea na pesa za wananchi.

Amesema, ili kuepuka utapeli huo, waziri Lukuvi amepiga marufuku kwa viongozi wa kata na mitaa kuruhusu tenda kwa kampuni zisizopitia ngazi ya wilaya kwa ajili ya kushindanishwa na kuridhiwa kuwa wanasifa ya kurasimisha makazi.

Ameagiza kuwa gharama za upimaji na urasmishaji wa makazi hazitazidi Sh. 250,000 (laki mbili na nusu).

Augustino Mrema ampa kazi Kangi Lugola

AUGUSTINO Mrema, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole,  amesema kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amedhamilia kuwashughulikia wanaowabambikizia watu kesi, basi aanze na waliombambikia kesi ya kumkashifu Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ya mwaka 1996. Anaripoti Khalifa Abdallah … (endelea).

Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) amesema kama yeye alishika nafasi mbalimbali nchini ameweza kubambikiwa kesi kuwa amemtukana Rais Mkapa basi haitashindikana kwa mtanzania wa kawaida kubambikiwa kesi yoyote.

“Watu wanaposema wanabambikiwa kesi siyo uongo. Mimi niliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Naibu Waziri Mkuu nilifanyiwa hivyo, itakuwaje kwa mwananchi wa kawaida,” amesema Mrema na kuongeza:

“Jinsi Waziri Kangi Lugola alivyoanza kazi yake amenitia moyo pamoja na watanzania kwa ujumla, naweza nikasema akiendelea hivi anaweza akavaa viatu vyangu.”

Aidha, amesema Lugola ana kazi kubwa ya kufanya kwa sababu Wizara ya Mambo ya Ndani ndiyo kioo na uchafu wowote unaotaka kuuondosha katika nchi, wizara hiyo inahusika kwa kiasi kikubwa kutekeleza jukumu hilo.

Amesema yeye kama Mwenyekiti wa Bodi ya Parole bado hajajua ni asilimia ngapi ya waliokuwepo jela wamebambikiwa kesi lakini ni watu wengi.

Yanga yawatema makinda, mafaza

BAADA ya dirisha la usajiri kufungwa jana majira ya saa sita usiku, klabu ya Yanga imetoa orodha ya wachezaji tisa ambao hawatotumikia timu hiyo kwa msimu ujao wa mashindano unaotarajiwa kuanza 23, Agosti 2018. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea)..

Wachazaji hao ambao ni mlinda mlango Youthe Rostand, Hassani Kessy, Yohana Mkomola, Geofrey Mwashiuya, Said Bakari, Baruani Akilimali, Said Makapu, Obrey Chirwa na Donald Ngoma.

Baadhi ya wachezaji hao wakitolewa kwa mkopo kwenda kwenye baadhi ya timu za Ligi Kuu, huku wengine wakiondoka kama wachezaji huru ambao mikataba yao imeisha toka msimu wa ligi ulipomaliza.

Mpaka sasa Yanga imeshasajili jumla ya wachezaji saba, huku wakijiandaa na mchezo wao wa marudiano dhidi ya Gor Mahia siku ya Jumapili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

‘CCM inamvua nguo Chiza’

CHRISTOPHER Chiza, mgombea mteule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Buyungu, Kigoma anakwenda kuumbuka. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

“CCM imeamua kumvua nguo Chiza. Kwanza kaishachoka na wananchi wanajua kachoka hoi.

“Kama haki itasimama huku matumizi ya mabavu na uhuni mwingine ukiwekwa kando, Chiza ataanguka mapema.

“Yale ya kuiba masanduku ya kura kule Kinondoni, Dar es Salaam huku hatuyataki, tunaamini Buyungu ni ya amani na wananchi wanataka uchaguzi wa amani. Ni matarajio yetu Chiza ataendelea kupumzika mililele kwenye uso wa dunia,” amesema Elias Michael.

Michael ndio aliyeteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kugombea ubunge kwenye jimbo hilo.

Akizungumza na MwanaHALISI Online Michael amesema kuwa, CCM ni chama pinzani kwenye jimbo hilo kutokana na kuachwa na Mbunge wa Chadema, Kasuku Biloga aliyefariki 26 Mei mwaka huu.

Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, 2018 kwenye jimbo la Buyungu sambasamba na kata 79.

Michael amedai, Chiza ni mchovu na hana jipya kwa kuwa, wananchi wanamjua kutokana na kuhudumu jimbo hilo kwa miaka 10.

“Mgombea wa CCM hakuwatendea haki wananchi wa Buyungu wakati akihudumu kama mbunge kwenye awamu ya nne na bahati nzuri alipata nafasi ya kuwa waziri kwa miaka 7 na nafasi ya naibu waziri kwa miaka 3 bila kuwanufaisha wananchi wa Buyungu” amesema Michael.

Michael ambaye ni kijana mbichi kabisa ameeleza kuwa, hasira za wananchi hao zipo kwenye vifua vyao kwa sababu CCM imemrejesha mtu aliyesababisha kuzorota kwa maendelo kwenye jimbo hilo.

Amedai kwamba, wakati Chiza akiwa Waziri wa Kilimo aliwachukiza wananchi wa eneo hilo kwa kuhusika na kuuza pembejeo nchi jirani ya Burundi ihali wananchi wake hawakuwa na mbolea .

Na kwamba, Chiza aliwahi kushindwa kufanikisha mradi wa maji uliogharimu bilioni 2 zilizopotea bila kufanikisha mradi huo.

Michael ameweka wazi kuwa, yeye ni zao la vijana waliosoma kwenye shule za kata na mwenye kujua umuhimu wa elimu hivyo wakati wananchi walipo mkabidhi kijiti cha udiwani ilikuwa ni fursa kwake ya kufanya mabadiliko kwenye kata yake ya Gwarama.

Michael alipoinga kwenye udiwani alikopeshwa shilingi 8 Milioni ambazo zote aliziingiza kwenye ujenzi wa vyumba vinne vya shule ya msingi kwenye kata hiyo ambapo wanafunzi 320 wa Darasa la I na II.

Amesema kuwa, tayari amepatiwa Sh. Mil 60 kutoka Ufaransa kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Muhange.

Amesema, kwa kipindi cha miaka 3 ya udiwani wake ameshughulikia suala la amani kwenye kata hiyo ambayo hapo awali kulikuwa na matukio ya ujambazi.

“Wananchi wa Buyungu wanajua thamani ya kula zao na nikihujumiwa mimi watahujumiwa wao, kwa hiyo wapiga kura wangu wanajitambua na hawatakubali kunyangwanywa haki yao,” amesema.

Nondo akamatwa tena na Polisi

MWENYEKITI wa Mtandao wa Wanafunzi nchini (TSNP), Abdull Nondo ametiwa mbaroni na jeshi la Polisi usiku kuamkia leo. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI Online Hellen Sisya Ofisa Habari wa Mtandao huo amethibitisha kushikiliwa kwa kiongozi huyo.

Sisya amesema kuwa Nondo alikamatwa akiwa viunga vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam usiku wa jana Julai 26 na askari wa chuo hicho.

Paul Kisabo, Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa TSNP, amesema kuwa Nondo amekamatwa akiwa eneo la Mgahawa wa chuo na
askari wa auxiliary.

“Tumefika kituo cha polisi chuo tumekuta Abdul Nondo anachukuliwa maelezo lakini alikataa kuyasaini sababu hakuwa na msaada wa kisheria akiwa anachukuliwa maelezo.

“Sababu ya kukamatwa ni eti amefanya criminal tresspass chuoni, tumeongea na mkuu wa kituo ili tuweze kuondoka na Nondo, imeshindikana kwa sababu za kiusalama,” amesema Kisabo.

Yanga yazinduka jioni

IKIWA yamebakia masaa machache kabla ya dirisha la usajiri la Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na ligi daraja la kwanza hatimaye klaba ya Yanga imefanikiwa kunasa saini ya kipa Klaus Nkinzi na mshambulia Heritier Makambo ambao wote ni raia wa Congo DRC. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Yanga ambayo ilionekana kusuasua hapo awali katika mchakato wa usajili toka dirisha hilo kufunguliwa kutokana na hali ya kiuchumi wanayopitia kwa sasa toka alipojiuzuru mwenyekiti wao na mfadhili mkuu wa klabu hiyo

Wawili hao wanaongeza idadi ya kuwa wachezaji saba mpaka sasa waliosajiriwa na klabu ya Yanga kuelekea msimu mpya wa mashindano wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza 23 Agosti, 2018.

Mange kubeba tuzo Marekani

MANGE Kimambi, raia wa Tanzania anayeishi Marekani, ni miongoni mwa wanawake wanaharakati wa kisiasa wanaotajwa kwenye orodha ya kugombea tuzo ya mwanamke mhamasishaji zaidi kisiasa Afrika. Anaandika Mwandishi Wetu…(endelea).

Tuzo hiyo imeandaliwa na Shirika la Black Entertainment Film Fashion Television and Art (BEFFTA) –Burudani, Filamu, Mitindo, Televisheni ya Watu Aweusi.

Taarifa za kuwania tuzo hizo zilitolewa na shirika hilo la BFFTA kupitia ukurasa wao unaopatikana kwenye mtandao wa kijamii wa instagram.

Shirika hilo lengo lake kuu ni kuangaza maslahi ya watu weusi katika nchi za Uingereza, Canada, Marekani, Carribbean na nchi za bara la Afrika.

Wengine waliojuimushwa katika kipengele hicho ni Elie Johson Sirleaf wa Liberia, Joice Majuru kutoka Zimbabwe, Diane Shima Rwigara raia wa Rwanda, Mbali Ntuli kutoka South Afrika na Alengot Oromait kutoka nchini Uganda.

Mange amejipatia umaarufu katika mitandao ya kijamii hasa instagram kutokana jumbe zake za ukosoaji kwa viongozi wa serikali na hata viongozi wa dini nchini Tanzania.

Pia aliongeza ‘presha’ zaidi Tanzania kutokana na kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha maandamano aliyopanga kufanyika Aprili 26 mwaka huu.

Hatua hiyo hiyo iliwalazimu viongozi mbalimbali Tanzania kujitokeza na kupinga maandamano hayo yaliyoonekana kushika kasi kupitia mitandao hiyo.

Waziri wa Madini afunga mgodi Pwani

SERIKALI imesimamisha shughuli za mgodi unaochimbwa madini ya Kaolin unaomilikiwa na kampuni ya RAK Kaolin kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa uendeshaji wake na biashara ya madini hayo viwandani. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji madini ya ujenzi Julai 25,2018.

Waziri Nyongo alitoa agizo hilo baada ya kutoridhishwa na shughuli za mgodi huo uliopo katika Kijiji cha Kimani wilayani Kisarawe mkoani Pwani, ikiwemo umiliki wa ardhi, leseni ya mgodi, uchimbaji pamoja na biashara ya madini hayo viwandani.

Waziri Nyongo alisema shughuli za uchimbaji na biashara ya madini katika mgodi huo hazioneshi wazi taratibu za ulipaji serikalini, mrabaha na tozo mbalimbali zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha, alimtaka mmiliki wa leseni ya mgodi huo kuwasilisha wizara ya madini nakala ya mkataba walioingia kati yake na wachimbaji wa madini ya Kaolin katika mgodi huo, na namna ambavyo aliweza kumiliki eneo husika.

Tukio kubwa kuikumba dunia kesho (Julai 27)

KARNE ya 21 inatarajiwa kushuhudia tukio kubwa na la muda mrefu la kupatwa kwa mwezi Ijumaa ya Julai 27, 2018. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Ni tukio kubwa kutokana na kupatwa huko kutachukua muda mrefu zaidi tofauti na matukio yaliyowahi kutokea awali. 

Kwa mujibu wa mtandao wa bbc, Shirika la Usimamizi wa Anga za Juu (NASA) limeeleza kuwa, tukio hilo litakuwa la muda mrefu zaidi katika karne hii ya 21.

Tukio hilo linatarajiwa kudumu kwa muda wa dakika 103 ambapo katika awamu tofauti kupatwa huko kwa mwezi kutafanyika kwa saa tatu na dakika 55.

Kupatwa kwa mwezi hutokea wakati jua, dunia na mwezi zinapokua kwenye mstari mmoja kwa maana ya kuwa dunia inakuwa katikati ya jua na mwezi hatua inayoziba mwanga wa jua.

Kupatwa huko hutokea wakati mwezi unapoingia katika kivuli cha dunia.

BBC imeeleza kuwa, kupatwa huko kwa mwezi Julai 27 kutaonekana Ulaya, Afrika, Mashariki ya Kati, katikati mwa Asia na Australia ikiwa ni maeneo yote isipokuwa Kaskazini mwa Marekani.

Eneo zuri la kulitazama tukio hilo ni eneo nusu ya Mashariki mwa Afrika, Mashariki ya Kati na katikati mwa bara Asia. Tukio hilo halitaonekana katika maeneo ya kati na Marekani Kaskazini.

Kusini mwa Marekani unaweza kuonekana kiasi katika maeneo ya mashariki hususani miji ya Buenos Aires, Montevideo, Sao Paulo na Rio de Janeiro.

Katika miji mingine ya karibu utaonekana wakati mwezi utakapokuwa ukiondoka katika eneo hilo.

Watakaobadili matumizi ya kanisa kulaaniwa

WAUMINI wa Kanisa la Mama Maria Mkuu wa Kanisa la Kigurunyembe Manispaa ya Morogoro mkoani hapo wameaswa kutobadili matumizi ya kanisa hilo na na endapo watabadilisha matumizi watalaaniwa. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki jijini Dar es Salaam, Mwadhama Polycard Kardinaly Pengo wakati akiweka wakfu baada ya kuzindua kanisa hilo jipya lilijengwa kwa thamani ya shilingi mil 860.

Kardinary Pengo alisema kuwa kanisa ni hekalu la Mungu ambapo ni mahali patakatifu panapotakiwa kuheshimiwa kwa utakatifu wake sambamba na utakatifu wa waumini wenyewe.

“Kanisa hili ni mahali patakatifu kuanzia leo na mkibadilisha mawazo mkafanya kuwa mahali pa matumizi mengine na lisiwe kanisa hata na Askofu wenu Mkude, hapo mtakuwa mmelaaniwa, nitawashitaki” alisema Kardinary Pengo.

Alisema uzuri na ukubwa na uzuri wa jengo hilo ungefanya watu wengine wasio na mioyo ya utakatifu kulibadilisha matumizi na kuwa kumbi ya starehe na kwamba utakatifu wao ndio umejidhihirisha kulifanya kuwa kanisa.

Naye Mkuu Mkoa wa Morogoro Dk. Kebwe Steven Kebwe aliwaagiza waumini wa kanisa hilo kuhakikisha wanalitunza kanisa hilo ili liweze kudumu zaidi ya miaka 100.

Aidha Dk. Kebwe alisema kuwa huduma za kijamii zimekuwa zikibebwa kwa sehemu kubwa chini ya dini zote ikiwemo elimu, maji, na malezi ya kiroho sambamba na amani ya nchi.

Dk. Kebwe alisema katika kuonesha dhamira hiyo ya kuanzisha huduma za kijamii anatoa shilingi laki tano kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Paroko hali ambayo ilichangia kupatikana zaidi ya sh Mil 1.75 na mifuko 100 ya saruji ambayo iliahidiwa kutolewa na Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete.

Aidha, Kikwete alisema familia yao haitaweza kuisahau dini ya Kikristo hasa Roma kwa kuweza kuwa njia ya kuinuka kielimu na kimaisha kufuatia ndugu wengi kupata elimu katika shule za kimisionari.

Mil 46 zatengwa kusimamia misitu

JUMLA ya shilingi mil 46 zimetengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani hapa kwa mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (CBFM) katika vijiji  vitatu wilayani humo. Anaripoti Christina Haule, Kilosa … (endelea).

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Idara ya Maliasili, Ardhi na Misitu wilaya ya Kilosa, Ibrahim Ndembo wakati akizungumza na waandishi wa habari wilayani humo.

Ndembo amesema halmashauri imekubali kutenga fedha hizo ili kuweza kuendeleza jitihada ambazo zimefanywa na Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) katika vijiji 20 vya wilayani hapo.

Amesema halmashauri katika kutekeleza dhana ya CBFM iliyoanza kutekelezwa na Mradi wa CBFM  katika vijiji hivyo vya New Mamboya, Inyunywe na Nyangala kutasaidia kuokoa misitu ambayo inaharibiwa kwa wingi na wavunaji misitu wasiofuata usimamizi wa shirikishi wa misitu.

Mkuu huyo wa idara amesema lengo ni kutekeleza dhana ya CBFM katika vijiji vitano kila mwaka wa fedha ila kutokana na uhaba wa fedha wataanza na vijiji hivyo vitatu.

Ndembo amesema matarajio yao ni kupitia Baraza la Madiwani katika mwaka wa fedha 2019/2020 watatenga fedha nyingine kwa ajili vijiji vingine vya Kaskazini hasa Dumila ili kufikia vijiji 20 mwaka 2021.

Mkuu huyo wa idara amesema Kilosa ina vijiji 139 na vijiji ambavyo vinatekeleza CBFM ni 20 na vyote vipo Kusini.

Amesema watatumia wana vijiji kutoka Kusini kutoa elimu ya CBFM na mkaa endelevu katika vijiji vipya vya mradi, wanachofanya ni kusimamia Sheria na Sera ya Misitu ambayo inahitaji kuwepo kwa CBFM.

Akizungumzia CBFM, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilosa Hassan Mkopi amesema madiwani wote wameridhia utengaji wa fedha hizo kwa ajili ya CBFM hivyo kuwataka watendaji kutekeleza kwa ufanisi.

Mkopi amesema mradi wa TTCS umekuwa mkombozi mkubwa katika utunzaji mazingira na uchumi wa wana vijiji wao hivyo ni lazima uwe endelevu.

Naye Kaimu Meneja wa Mradi wa TTCS, Simon Lugazo amesema mradi huo unatarajia kufikia mwisho hivyo wamelazimika kuwaita wadau wa Serikali na madiwani ili kujua wamejipangaje kuendeleza mradi huo.

Amesema mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) na Shirika la Kuendeleza Nishati Asilia Tanzania (TaTEDO) kupitia Ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswis (SDC), umefanikiwa kuokoa uharibifu wa misitu kwa zaidi ya asilimia moja kwa miaka michache ya uwepo wake.

Lugazo amesema mradi wa TTCS umesaidia usimamizi misitu shirikishi, utawala bora na sheria huku pia zaidi Sh.Mil 800 zikikusanywa wilayani Kilosa katika mauzo ya maliasili za misitu.

Rais Magufuli apongezwa  

SERIKALI inayoongozwa na Rais John Magufuli imepongezwa kwa kufanya vizuri katika utekelezaji wa kutoa na kuchukua hatua hasa katika magonjwa ya mlipuko. Anaandika Khalifa Abdallah… (endelea). 

Pongezi hizo zimetolewa na Kituo cha Kimataifa cha Kufuatilia, Kutathimini, Kutoa Taarifa na Kuchukua Hatua (CDC) kilichopo nchini Marekani.

Hayo yamesemwa na Ummy Mwalimu ambaye ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati wa kikao cha kuangalia hali ya utendaji katika sekta ya afya nchini.

“Wenzetu wa CDC kutoka Marekani wanatusaidia kujenga uwezo wa kufuatilia, kutoa taarifa na kuchukua hatua juu ya magonjwa ya mlipuko kama vile Ebola na Kipindupindu na wameridhika kwa utendaji wetu hapa nchini,” amesema Waziri Ummy.

Amesema kuwa, Tanzania imeimarika katika kufanya uchunguzi, kutathimini,  kutoa taarifa na kuchukua hatua juu ya magonjwa mbalimbali.

Mbali na hayo amesema  kuwa, magonjwa hayana mipaka hivyo ni lazima kuwa waangalifu na  kuchukua hatua mda wote kwa kujenga mifumo imara ya ufuatiliaji.

Inmi Petterson, Kaimu Balozi wa Marekani nchini amesema kuwa, wamefurahishwa na kazi ya wataalamu wa afya waliowekwa hapa nchini katika kupambana na magonjwa na kuahidi kuongeza nguvu kubwa ikiwemo vitendea kazi.

Aidha Balozi Inmi amesesema kuwa, Serikali ya Tanzania inatakiwa kushirikiana na wananchi wake katika kupata taarifa sahihi za magonjwa na kujenga nchi yenye wananchi wenye afya bora.

DART yabadili ratiba ya mabasi

KUFUATIA ujenzi wa daraja la juu kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na Mandela, Kampuni ya UDA Rapid Transport (UDART)  inayotoa huduma kwenye mfumo wa mabasi yaendayo haraka imetangaza kubadili ratiba ya huduma zake. Anaripoti Khalifa Abdallah … (endelea).

Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa UDART, Deus Bugaywa amesema mabadiliko hayo yataanza 30 Julai, 2018 ambapo asubuhi mabasi yanayotoa huduma ya Express kutoka Ubungo- Kivukoni na namba 005 ya Ubungo- Gerezani yataanzia safari zake katika kituo cha Ubungo Terminal badala ya Ubungo Maji.

Bugaywa amesema wakati wa mchana na jioni mabasi hayo yataendelea na huduma zake kama kawaida zisizokuwa Express badala ya kuishia Ubungo Maji sasa yataishia Ubungo Terminal.

“Kutokana na mabadiliko haya tunawashauri abiria wetu waliokuwa wakitumia kituo cha Ubungo Maji hasa nyakati za asubuhi watumie zaidi kituo vha Ubungo Terminal,” amesema.

Hata hivyo amesema wakati ujenzi huo ukiendelea mabasi ya mwendo wa haraka yatatumia njia moja tu (Single lane) ambapo ndio sababu kubwa ya mabasi hayo kuishia Terminal kwa lengo la kupunguza msongamano katika kituo wakati wa kushusha abiria hivyo UDART inaomba radhi abiria wake kwa usumbufu huo.

Sethi, Rugemalira kuwaumbua vigogo mahakamani

JAMES Rugemalira (74), bado anasota kwenye gereza la Segerea, jijini Dar es Saalaam. Anashitakiwa kwa kuhujumu uchumi. Anaripoti Saed Kubenea … (endelea).

Anadaiwa kujipatia kinyume cha taratibu, mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow, kupitia kampuni yake ya VIP Engineering and Marketing Limited.

Rugemalira alikuwa akimiliki asilimia 30 ya hisa katika kampuni ya kigeni ya IPTL kupitia kampuni yake hiyo.

Alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, tarehe 19 Juni 2017 na kusomewa mashtaka sita, yakiwamo ya uhujumu uchumi.

Mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo, ni Harbinder Sigh Seth (Singasinga). Seth anadai kumiliki kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), kupitia kampuni yake ya Pan African Power Tanzania Limited (PAP).

Mabilioni ya shilingi yaliyokuwa yamehifadhiwa katika akaunti ya Escrow yalikwapuliwa na Singasinga huyo aliyejiita mmiliki wa IPTL kwa msaada mkubwa wa viongozi wakuu wa serikali na kile kilichoitwa, “amri ya mahakama.”

Hata hivyo, kinachoitwa amri ya mahakama, kilikuwa ni kumaliza mzozo wa wanahisa wa IPTL na mbia mwenzake kampuni ya Rugemalira na kampuni ya MECHMAR ya Malaysia.

MECHMAR ilikuwa inasisitiza na mpaka sasa, bado inasisitiza, kuwa mtambo wa IPTL uliyopo eneo la Tegeta, Salasala, jijini Dar es Salaam, ni mali ya Benki ya Standard Chartered ya Malaysia.

Benki ya Standard Chartered ilikuwa inadai na mpaka sasa bado inadai kuwa mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL na fedha zilizopo kwenye akaunti ya Escrow, ni mali yake.

Inadai kuwa kampuni ya MECHMAR ya Malasia ilishindwa kurejesha mkopo iliochukua benki na kwamba hilo ni jambo linalosababisha mitambo ya IPTL iliyopo Tegeta Salasala, jijini Dar es Salaam, kuwa mali yake.

Standard Chartered inaeleza kuwa ilikabidhiwa mamlaka ya kumiliki, kusimamia na kuendesha, mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL na mahakama, kufuatia MECHMAR kushindwa kulipa mkopo.

Mkataba huo ulipa benki ya SCB haki za IPTL ndani ya mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na kumiliki mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL.

Benki ya Standard Chartered inaidai Tanesco dola za Marekani 258.7 milioni kama deni linalotokana na gharama za umeme uliozalishwa na IPTL na dola za Marekani 138 milioni zinazotokana na mkopo pamoja na riba.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na kimataifa, wanasheria waliobobea kwenye mikataba na mawakili wanaotetea Shirika la umeme la taifa (Tanesco), IPTL na serikali, madai hayo ni halali kwa mujibu wa sheria.

Akihutubia taifa kupitia walioitwa, “wazee wa mkoa wa Dar es Salaam,” wiki tatu baada ya Bunge kuagiza waliohusika katika wizi wa fedha za Escrow kuchukuliwa hatua, Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema, “…fedha za Escrow siyo mali ya umma.”

Kwa mujibu wa Kikwete, “Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wakati wa ukaguzi wa mahesabu ya Tanesco, ameeleza kuwa fedha za Escrow ni mali ya IPTL. CAG aliagiza fedha hizo ziondolewe kwenye hesabu za Tanesco kwa kuwa siyo mali yake.”

Hata hivyo, Rais Kikwete alikiri kuwapo udanganyifu katika kufikia utoaji wa fedha za Escrow.

Alikiri baadhi ya nyaraka kughushiwa. Akakiri kuwa kampuni ya PAP imekwepa kodi ya serikali na kudai kuwa serikali yake bado inaendelea kuitafuta kampuni ya MECHMAR iliyodaiwa kuuza asimia 70 ya hisa zake ndani ya IPTL.

Aidha, Rais Kikwete alikiri kuwa aliyepewa fedha na serikali – PAP – hakuwa na sifa; serikali yake haikufanya uchunguzi yakinifu kuhusu historia, uhalali, sifa na uwezo wa kampuni ya PAP katika uwekezaji wa umeme, ununuzi wa mitambo na mtaji.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya serikali, Sethi alitokea ikulu kabla ya kukwapua zaidi ya Sh. 321 bilioni kutoka akaunti ya Escrow katika Benki Kuu ya taifa (BoT).

Aidha, anayejiita na kuitwa na serikali kuwa ni “mmiliki mpya wa IPTL/PAP,” Harbinder Singh Sethi, aliletwa nchini na mmoja wa wanafamilia wa Rais Kikwete.

Mara baada ya kutoka ikulu jijini Dar es Salaam na kukutana na “wakubwa;” na kutoka hapo singasinga alikwenda moja kwa moja kukwapua mabilioni ya shilingi BoT hata bila kumfahamisha Rugemalira – mbia mwenzake.

Katika hili la IPTL, taarifa zinasema, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Benno Ndullu alichukua tahadhari zote juu ya fedha hizo, ikiwamo kumjulisha aliyekuwa Waziri wa Fedha, umuhimu wa kumjulisha Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu malipo hayo.

Gavana alikwenda mbali zaidi. Alitaka kupata uhakika kwamba utekelezaji wa uamuzi wa mahakama, pamoja na makubaliano ya kukabidhi fedha, unapata baraka za wakuu wa nchi kama vile Rais na Waziri Mkuu.

Pia BoT ilihakikisha kwamba mahitaji yote ya msingi kama vile, makubaliano ya kuhamisha fedha, kinga dhidi ya madai au mashitaka baada ya malipo, na suala la kodi ya ongezeko la thamani (VAT), vinapata ufafanuzi, baraka na mwongozo unaostahili.

BoT iliamua kuchukua hatua hizo ili kujinasua na madai mapya ambayo yangeweza kuibuka baada ya fedha kuhamishwa kutoka benki.

Kwa mujibu wa nyaraka, BoT ilihamishia mabilioni hayo ya shilingi kwa PAP kupitia akaunti yake iliyoko benki ya Stanbic baada ya Sethi, anayedai kuwa mmiliki wa IPTL, kumuelekeza gavana.

Waraka wa Sethi kwenda kwa gavana Ndulu ulielekeza fedha hizo kulipwa kwa akaunti Na. 9120000125324, iliyopo benki ya Stanbic, tawi la Tanzania.

Sethi alimwandikia gavana tarehe 28 Novemba 2013, zikiwa siku 37 (21 Oktoba hadi 28 Novemba 2013) tangu mkataba kati ya serikali na PAP kufungwa.

Mkataba wa upelekaji fedha katika akaunti ya Escrow ulifungwa tarehe 21 Oktoba 2013.

Malipo hayo kwa PAP yalifanyika bila Waziri wa Nishati, Prof. Sospeter Muhongo, wala BoT kuhakiki uhamishaji wa hisa kutoka Mechmar kwenda PAP; bila PAP kusajili hisa zake nchini; bila PAP kuthibitisha kujisajili Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC); na bila kuwa na hati ya mlipa kodi (TIN).

Mkataba kati ya serikali na IPTL ulielekeza fedha zilizohifadhiwa katika akaunti ya Escrow, zilipwe kwa kampuni ya PAP kupitia tawi la Tanzania la United Bank Limited (UBL) – yenye matawi zaidi ya 1,300 katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Qatar, Yemen, Marekani, Pakistani, Uingereza, Uswisi, Oman, China na Tanzania.

Mkataba huo uliagiza fedha hizo zilipwe kupitia akaunti mbili za PAP; ambazo ziko katika benki ya UBL. Akaunti hizo ni zile zenye Na. 010-0016-0 – ambayo ni ya fedha za Tanzania na 060-0016-7 ya dola za Marekani.

Katika moja ya maandishi yake, Rugemalira anahoji: “Tanesco inaweza kununua huduma ya umeme kutoka IPTL na badala ya kuilipa IPTL ikajilipa yenyewe?”

Alikuwa akimueleza rais Kikwete kile alichoita, “maswali yanayoombewa majibu kwenye sakata la TEGETA ESCROW.”

Rugemarila alifanya mawasiliano na Kikwete  tarehe 29 Novemba 2015.

Akiandika kwa rais Kikwete, mmiliki huyo wa IPTL alisema, “kama kuna madai au makosa, kwenye mchakato wa kumaliza suala la IPTL, walalamikaji wamepewa ruhusu na Jaji John Utamwa, tarehe 5 Septemba 2014, kupeleka malalamiko yao mahakamani.

Akahoji, “ni busara Bunge liamrishe serikali kufuta hukumu ya mahakama?” Rugemalira alikuwa akieleza rais jinsi maamuzi ya Bunge yaliyoagiza serikali kutaifisha mtambo wa IPTL yasivyoweza kutekelezeka.

Alisema, “…serikali inayo mamlaka ya kutaifisha mali ya mtu binafsi bila kupitia njia za sheria? Je, Bunge halina wajibu wa kuheshimu na kuimarisha utawala wa sheria nchini?”

Akaongeza, “tangu lini likawa jukumu la Bunge kudai pesa kwa niaba ya kampuni binafsi wakati kampuni hiyo imefungua madai mahakama za nje kwa kisingizio cha kutokuwa na imani na mahakama zetu?”

Alisema, “tuelewe kwamba sasa Bunge letu linapiga kura ya kutokuwa na imani na mahakama iliyoanzishwa kwa mujibu wa Katiba?”

Rugemalira alihoji, “ni halali kwa watu wa nje pamoja na mashirika ya nje na wengine kutoka ndani, kutoa misaada, lakini ni haramu kwa kampuni yake ya VIP au yeye binafsi kufanya hivyo?”

Anasema, kama tozo ya uwekezaji wa IPTL ni wizi, serikali imejiridhisha kuwa tozo za makampuni mengine, ikiwamo Songas, Symbion na Aggreko kama siyo wizi mkubwa zaidi.

Anashauri kama kuchunguza IPTL, serikali inapaswa kuchunguza kwanza makampuni hayo ya kigeni.

Anasema, “kama fedha za IPTL ni haramu, kwa nini TRA wametoza kodi kwenye fedha ambazo zinadaiwa kuwa ni za wizi?”

Kampuni ya IPTL – Independent  Power Tanzania Limited –   ilijifunga katika mkataba na serikali wa miaka 20 wa kuzalisha megawati 100 za “umeme wa dharura” na kisha kuuza umeme huo kwa shirika la umeme la taifa (TANESCO).

Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa mwaka 2004 baada ya serikali kushuku udanganyifu katika gharama za ununuzi wa umeme na mtaji wa IPTL.

Kampuni hiyo binafsi ilidai kuwa gharama za umeme zilikuwa asilimia 22.3; na gharama za mtaji asilimia 30 zilikuwa dola za Marekani 38.16 milioni. Hata hivyo, mahakama ilithibitisha kuwa gharama halisi za mtaji wa IPTL, zilikuwa chini ya dola za Marekani 1,000.

Hadi Novemba 2014, akaunti hiyo ilikuwa imehifadhi zaidi ya dola 120 milioni. Mamilioni hayo ya dola yaligawanywa mithili ya “shamba la bibi” kwa aliyejiita mwekezaji mpya wa IPTL, kampuni ya Pan African Power (PAP).

Mabilioni ya shilingi yalilimbikizwa na Tanesco, katika akaunti hiyo, baada ya kuibuka mgogoro juu ya malipo ya gharama ya uwekazaji wa mitambo na gharama za kuweka mitambo (Capacity Charge), kati ya IPTL na Tanesco.

Lakini fedha hizo zilichotwa kabla mgogoro huo haujapatiwa ufumbuzi na katika mazingira ya udanganyifu; na kwa kutumia baadhi ya nyaraka ambazo zilikuja kugundulika kuwa ni za kugushi.

Sethi aliwasilisha serikalini nyaraka zinazomuonesha kuwa ndiye mmiliki mpya wa IPTL. Hata hivyo, Sethi alishindwa kuweka uthibitisho wowote kuwa kampuni hiyo inamiliki hisa za kampuni ya Mechmar Limited ya Malaysia ndani ya IPTL.