Mbunge wa CCM aikaba serikali

MBUNGE wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) ameihoji serikali na kutaka ieleze ni lini itaana ujenzi wa kituo cha polisi na nyumba za askari. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Nkamia aliihoji serikali leo bungeni wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa kutaka kujua serikali ina mpango gani wa kujenga kituo cha polisi wilayani chemba pamoja na nyumba za askari.

“Wilaya ya Chemba haina Kituo cha Polisi, Je ni lini serikali itaanza ujenzi wa kituo cha polisi na nyumba za askari,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masaun, amesema kuwa ni kweli jeshi la polisi lina uhaba wa vituo vya polisi pamoja na nyumba za kuishi askari kote nchini ikiwemo wilaya ya Chemba.

“Ili kutatua changamoto hiyo jeshi la polisi linashirikisha wananchi wa eneo husika pamoja na wadau wengine wa maendeleo ili kufanikisha azma ya serikali ya kujenga vituo vya serikali vya kisasa vya polisi pamoja na nyumba za kuishi za askari hao,” amesema Masaun.

Naibu Waziri huyo amesema Wilaya ya Chemba jeshi la polisi ka kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, wananchi na wadau wengine wapo kwenye hatua za awali za kuanza ujenzi wa kituo cha polisi.

“Kwa sasa mchoro wa ramani ya kituo na gharama za ujenzi (BOQ) vimeisha kamilika na ukusanyaji wa mahitaji ya ujenzi unaendelea,” ameeleza Masaun.

Wafanyabiashara wa ng’ombe watishia kugoma

WAFANYABISHARA wa mifugo wanaopeleka katika machinjio ya kisasa ya Kizota mkoani Dodoma wametishia kuacha biashara hiyo baada ya kuibuka kwa faini kubwa mbalimbali kutoka Wizara ya Uvuvi na Mifugo zinazotozwa kwao. Anaripoti Christina Haule … (endelea).

Wakizungumza na waandishi wa habari, wafanyabiashara hao wamesema kuwa kumekuwa na faini mbalimbali wanazotozwa kutoka kwa watumishi wa wizara hiyo ambazo ni kati ya sh. 500,000 hadi sh. milioni moja au zaidi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mmoja wa wafanyabiashara hao, Joseph Mazengo ambaye husafirisha mbuzi kutoka Singida kuleta katika machinjio hiyo amesema kuwa yeye binafsi alitozwa sh. milioni moja kwa kukosa kibali cha kusafirishia mbuzi kati ya 100 na 120.

Amesema kuwa fani hizo hutozwa katika kituo cha mifugo Kizota ambako mifugo yote inayoingia katika mkoa wa Dodoma inalazimika kupitia katika kituo hicho.

Amesema mbali ya kutozwa kiasi hicho cha fedha bado alitozwa faini nyingine kabla ya kufikisha mbuzi hao kwa ajili ya kuchinjwa katika kiwanda hicho.

Mfanyabiashara huyo amesema wao ununua mbuzi vijijini na kisha kuwaleta kiwandani hapo ambako kuna mwekezaji ambaye ununua na kisha kuchinja na kusafirisha nyama hiyo nje ya nchini kwa oda maalum.

“Sisi tunanunua mbuzi ili kuja kuwauza kwa makampuni ya wawekezaji ambao nao uchinja na kuuza nje lakini sasa kumekuwa na faini hata kama namba ya gari imekosewa katika kibali unatozwa hadi sh. laki tano hii si sahii sisi wenyewe hatuna mitaji hata hawa mbuzi tunachukua kwa mali kauli,

“Sisi hatukatai kama kuna utaratibu kama huo tungepewa taarifa mapema ili nasi tujitayarishe na si kutukurupusha sasa tusipo leta hawa mbuzi huyu mwekezaji atapata wapi mbuzi wa kuchinja na kila siku mna sema kuwa mnaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji sasa haya ni mazingira mazuri kweli,’’ amesema.

Mfanyabiashara mwingine aliyejulikana kwa jina la Anthony Methew amesema inashangaza kwani hata wakitaka kuuliza swali kwa wahusika hao wamekuwa wakali na kuhitiwa askari na kukemewa kuwa hakuna swali hapa ni fani tu.

Amesema hali hiyo iliwafa baadhi yao kwenda hadi kwa katibu Mkuu wa Wizara hiyo naye alituombea tupunguziwe faini jambo ambalo wanahoji kama ni kweli faini hiyo ipo kisheria suala la kuonewa huruma linatoka wapi.

Mfanyabiashara huyo amesema kuwa jambo kubwa linalowashangaza mara baada ya kulipa faini hiyo wamekuwa wakiandikiwa risiti za serikali zile za zamani za karatasi na siyo za kieletroniki kama serikali ilivyo sema hivi karibuni kuwa malipo yote yawe katika mfumo wa kieletroniki.

Katika machinjio yao kuna jumla ya makampuni matano ya wawekezaji ambao ununua mbuzi hao na kuchinja kisha kuunza nyama nchi za nje ikiwemo kampuni ya Mkonga A, Bongo Export, Sunchoice, Saudi Park. na Smartfedha Export.

Akizungumzia hali hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mary Mashingo amesema kuwa Wizara yake haitamfumbia macho mtumishi wake yeyote atakayeenda kinyume na taratibu zilizowekwa katika ukaguzi wa mifugo.

Amesema wizara yake itafuatilia kama kuna malalamiko yeyote ili kubaini tatizo ni nini lakini aliwaasa wafanyabishara nao kuzingatia taratibu katika kusafirisha mifugo ili kuepuka faini zisizo za lazima.

Vifaa tiba visivyofaa vyakamatwa mitaani

SERIKALI imesema kuwa imefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali ambavyo ni dawa na vifaa tiba ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu, katika vituo vya tiba za asili. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Mafanikio hayo yalitokanana Operesheni iliyoandalikwa kutokana na kuwepo kwa taarifa za matumizi ya vifaa tiba aina ya Magnetic Quantum Analyzer na vingine vinavyofanana na hivyo kwenye vituo vya tiba asili na tiba mbadala kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa na matangazo ya vifaa hivyo yanayopotosha umma.

Amesema kuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliandaa na kufanya ukaguzi maalum wa kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219 na Sheria ya Dawa Asili na Mbadala ya mwaka 2002 hususan uuzaji, usambazaji, matumizi na matangazo ya vifaa tiba vinavyotumika katika tiba ya kuchua, uchunguzi wa magonjwa na vifaa vingine vinavyodaiwa kuondoa sumu mwilini.

Akitoa taarifa hiyo Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia na Watoto Dk. Faustin Ndungulile amesema kuwa Kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219 vifaa tiba kwa ajili ya matumizi nchini, ni lazima viwe vimesajiliwa au kutambuliwa na Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) baada ya kufanyiwa tathmini ya taarifa za kisayansi za kuthibitisha ubora, usalama na ufanisi wake.

Amesema Operesheni hiyo ilifanyika sambamba katika mikoa kumi na moja ambayo ni Dar es salaam (Kinondoni, Ilala, Temeke, Ubungo, Kigamboni), Morogoro (Kilombero), Singida (Manispaa), Arusha (Manispaa), Kilimanjaro (Moshi), Mbeya (Jiji, Mbalizi, Tukuyu), Rukwa (Manispaa), Kigoma (Kasulu, Manyovu), Mwanza (Nyamagana, Ilemela), Kagera (Bukoba) na Mtwara (Manispaa) kwa muda wa siku mbili, kuanzia 6 hadi 7 Machi, 2018.

“Operesheni ililenga kukagua vituo vyote vilivyosajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na vituo vingine kadri ilivyopatikana kwa kuzingatia taarifa za kiintelijinsia zilizofanyika awali,” amesema Dk. Ndungulile.

Amesema jumla ya maeneo 115 yalikaguliwa wakati wa operesheni hiyo ambapo vituo 39 vikiwa vya mkoa wa Dar Es Salaam, 6 Morogoro, 6 Singida, 10 Arusha, 5 Kilimanjaro, 15 Mbeya, 5 Rukwa, 6 Kigoma, 14 Mwanza , 3 Kagera na 6 Mtwara.

Akiendelea kutoa ufafanuzi wa Operesheni hiyo Dk. Ndungulile amesema jumla ya vifaa tiba 395 vyenye thamani ya shilingi 51,116,000/- na dola za kimarekani 2,768 vilikamatwa.

Amevitaja vifaa hivyo vilivyokamatwa kuwa ni Quantum Magnetic Analyser 53, Massagers 40, Detoxifier 18, Cybrow Urinary Stick 1, BP Machine 19, Blood Glucose Meter 2, Ultrasound 1, Acupuncture needles 176, Ion Cleanse 2, Elecromagnetic Bed 20, Homeopathic Electronic Radionic Machine 4, Stetoscope 2 na vifaa vingine 57.

Amesema sambamba na bidhaa hizo kukamatwa operesheni hiyo imebaini kuwepo kwa mapungufu makubwa katika utekelezaji wa Sheria ya Tiba Asili na Tiba mbadala ya mwaka 2002 pamoja na Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219 katika vituo vingi vilivyokaguliwa.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa ukaguzi huo umebaini kuwepo kwa matumizi makubwa ya vifaa vinavyojulikana kama Quantum Magnetic Analyzer katika kupima magonjwa mbalimbali na Detoxifier inayodaiwa kuondoa sumu mwilini.

Aidha, kupitia matangazo yanayotolewa kwenye vituo husika, ukaguzi umebaini upotoshaji mkubwa kwa jamii, kuwa vifaa husika vina uwezo wa kupima au kutibu magonjwa makubwa kama vile saratani, hepatitis, ovarian cysts.

Alisema katika baadhi ya maeneo yaliyokaguliwa, wakaguzi walibaini huduma za upimaji wa HIV, Malaria, Sukari na Pressure zikitolewa huku kukiwa hakuna wataalamu wenye fani husika.

Amesema kutokana na matokeo ya Operesheni hiyo, hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ambapo jumla ya majalada 52 ya kesi tayari yamefunguliwa katika vituo mbalimbali vya polisi dhidi ya watuhumiwa na vituo 50 vimefungwa.

Dk. Ndungulile amevitaja idadi ya vituo, idadi ya kesi na vituo vilivyofungiwa kwa mkoa wa Dar es Salaam idadi ya vituo vilivyofungwa ni 16 na idadi ya madalada ya kesi ni 16.

Amesema mkoa wa Singida vituo vilivyofungwa ni vitatu na majarada ya kesi ni matatu kwa mkoa wa Arusha vituo vilivyofungiwa ni saba na majarada ya kesi saba, mkoa wa Kilimanjaro hakuna kituo kilichofungiwa lakini majarada ya kesi ni vituo mbili.

Vituo vingine alivitaja kuwa ni Mbeya vituo vilivyofungwa ni 11 na vyenye majarada ya kesi ni 11, katika mkoa wa Rukwa vituo vilivyofungiwa ni vinne na vyenye majarada ya kesi ni manne, mkoa wa Kigoma kituo kimoja kimefungiwa huku vituo vitatu vikiwa na majarida ya kesi, katika Mkoa wa Mwanza vituo vitatu vimefungiwa na hakuna kituo chenye jarida la kesi, mkoa wa Kagera vituo vilivyofungiwa ni viwili na vyenye majarida ya kesi ni mawili na Mkoa wa Mtwara vituo vilivyofungiwa ni vitatu na vituo vyenye majarida ya kesi ni manne na kufanya jumla ya vituo vyote vilivyofungiwa ni 50 na vyenye majarada ya kesi kuwa 52.

Aidha amesema baada ya uchunguzi wa makosa kukamilika hatua mbalimbali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani watuhumiwa na kutoa adhabu kulingana na Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219 na Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya mwaka 2002.

Amesema adhabu hizo zinajumuisha kufuta leseni ya biashara, kuwafutia usajili wataalamu, kuondoa kwenye soko na kuharibu vifaa husika.

“Napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa taasisi zilizoshiriki kwenye operesheni hii ikiwemo Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Chakula na Dawa, kwa kutambua umuhimu wa zoezi hili kwa maslahi ya Taifa.

“Aidha, napenda kuchukua nafasi hii kupiga marufuku uingizaji, usambazaji na matumizi ya vifaa vinavyodaiwa kupima magonjwa mbalimbali kama Quantum Magnetic Analyzer, Detoxifier n.k kutokana na ukweli kuwa usalama na ufanisi wa vifaa hivyo haujathibishwa. Waingizaji wanaagizwa kuwasilisha TFDA taarifa za kisayansi za kuthibitisha ubora, usalama na ufanisi kupitia mfumo wa usajili ili ziweze kutathminiwa,” amesema Dk. Ndungulile.

Katika taarifa hiyo Dk. Ndungulile alitoa wito kwa umma na wananchi kwa ujumla kuwa makini na taarifa za upotoshaji zinazotolewa hususan matumizi ya vifaa hivyo ambavyo havijathibitishwa na TFDA ili kulinda usalama wa afya zao.