Mch. Msigwa ayamwaga bungeni aliyoyaona Segerea

MBUNGE wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) amedai Tanzania kwa sasa kuna msongamano mkubwa wa wafungwa ambapo amehoji Serikali inachukua hatua gani kupunguza msongamano huo. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Akiuliza swali la nyongeza jana bungeni Msigwa alidai kuwa gereza la Segerea limezidiwa na mahabausu ambapo lina uwezo wa kuchukua mahabusu 700, lakini waliopo kwa sasa ni mahabusu na wafungwa  2400.

“Ukienda katika Magereza zetu kuna msongamano mkubwa sana kwa mfano Gereza la Segerea ambalo nililipitia juzi lina uwezo wa kuchukua mahabusu 700 lakini sasa hivi lina mahabusu na wafungwa 2400.

“Wanalazimika watu kulala upande mmoja mmoja kwa zamu baada ya muda inapigwa ‘alarm’ kisha mnageukia upande mwingine huu ni ukiukwaji kabisa wa haki za binadamu na watoto wengi wapo pale chini ya umri wanatakiwa waende shule.

“Ni kwanini Serikali imekuwa ikipeleka wanasheria kutetea kesi za Serikali ambao wamekuwa wakilazimisha wale ambao wanaweza kupata dhamana waende kukaa mahabusu kama ambavyo kesi zetu zilikuwa zina dhamana lakini mawakili wa Serikali walikuwa wanalazimisha tuende kule tukaongeze msongamano,” ameuliza Msigwa.

Akijibu kwa niaba ya Serikali, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema kuwekwa ndani kwa muda mrefu kwa mahabusu siyo kweli kwamba Serikali haitaki kesi hizo zimalizike haraka.

“Sababu za msingi ni sababu ya usalama wao, wakienda nje wanaweza wakapata matatizo ikiwemo Serikali kuwalinda pili kuna watuhumiwa wakitoka nje wataenda kuharibu ushahidi,” amesema

Naye, Mbunge wa Tarime Mjini Ester Matiku (Chadema) katika swali lake la nyongeza aliitaka serikali iwaachie kina mama ambao wamefungwa huku wakiwa wanaumwa.

“Nimekuwa Segerea Mheshimiwa Spika kule kuna wamama wamefungwa wanadaiwa mathalani 150,000 lakini amefungwa miezi sita kwa gharama ambazo amezitoa Naibu Waziri zinavuka mpaka 200,000.

“Kwanini Serikali isitumie busara kwa kina mama ambao wengine wana watoto wachanga wanafungwa kwa kesi ya shilingi 100,000 mpaka 200,000 na Serikali inatumia gharama kubwa katika gharama za chakula,” amehoji Matiko.

Akijibu swali hilo, Ole Nasha amesema suala hilo ni la kisheria hivyo kama Mbunge anaona hoja hiyo inamashiko apeleke hoja binafsi bungeni.

Akiongezea majibu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba, alisema hawawezi kuwaacha wahalifu nje kutokana na kuogopa Magereza kujaa.

“Niweke kumbukumbu sawa sio kila Magereza yana msongamano tuna baadhi ya Magereza katika mikoa ile ambayo kiwango cha uhalifu ni mdogo mfano Lindi na kule Mlalo,” amesema

Mfungwa mmoja kutumia laki moja kwa siku

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema gharama za chakula kwa mfungwa mmoja kwa siku ni wastani wa shilingi 1,342. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Hayo yalielezwa leo bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamadi Masauni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Njombe Mjini, Edward Mwalongo (CCM).

Katika swali hilo Mwalongo alitaka kujua Serikali inatumia kiasi cha shilingi ngapi kuhudumia mfungwa mmoja kwa siku kwa ajili ya chakula.

 “Vitendo kama kulala chini, kulala bila blanketi au shuka vimekuwa vya kawaida kabisa katika Magereza yetu. Je hii nayo ni sehemu ya adhabu ambayo wafungwa wanapewa kwa mujibu wa sheria,” alihoji Mbunge huyo.

Akijibu, Masauni amesema Jeshi la Magereza katika kutekeleza majukumu yake pia hutoa huduma ya chakula kwa wahalifu kupitia bajeti iliyotengwa na Serikali kila mwaka wa fedha.

Naibu Waziri huyo amesema gharama za chakula kwa mfungwa mmoja kwa siku ni wastani wa shilingi 1,342.

Amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za wafungwa na mahabusu kwa kununua vifaa mbalimbali vya malazi ikiwemo, magodoro shuka, mablanketi na madawa ya kuua wadudu.

Mbunge Chadema amvaa waziri wa mifugo

MBUNGE wa Tarime Mjini, Ester Matiko (Chadema) amehoji serikali ni kwanini Mnada wa Magena umefungwa licha ya kuwa na miundombinu yote. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Akiuliza swali jana bungeni,Mbunge huyo alidai kuwa mnada huo uliopo halmashauri ya Mji wa Tarime una miundombinu yote licha ya kufungwa na Serikali bila sababu maalumu.

Mbunge huyo alidai mwaka 2016 aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, alitembelea mnada huo na kuagiza ufunguliwe.

“Je ni kwanini mnada huo haujafungiliwa mpaka sasa ili kutoa fursa za ajira na kuokoa mapato yanayopotea,” amehoji Matiko.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema mnada wa Magena ulikuwa kati ya minada 10 ya mipakani.

Amesema mnada huo ulikamilika kujengwa mwaka 1995 na kufunguliwa mwaka 1996 ambapo ulifanya kazi kwa takribani mwaka mmoja ambapo ng’ombe 104,000 waliuzwa na jumla ya Sh. 260 milioni zilikusanywa kama maduhuli ya Serikali.

Naibu Waziri huyo amesema kutokana na changamoto zilizojitokeza ikiwemo wizi wa mifugo na sababu za kiusalama kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Mara mwaka 1997 iliagiza mnada huo ufungwe.

“Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Mkoa wa Mara uliiomba Wizara ya Maendeleo ya Mifugo ya wakati huo ifute mnada wa Magena na Kirumi Check Point iteuliwe kuwa mnada wa mpakani kwa kuwa tayari kuwa kizuizi cha Mto Mara,” amesema.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amesema Wizara ilikubali ombi la uongozi wa mkoa wa Mara na hivyo ikaanza kujenga mnada eneo la Kirumi sehemu ambayo kuna kizuizi asili cha Mto Mara.

Amesema ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 80 na unatarajiwa kufunguliwa mwaka huu mara baada ya kukamilika ujenzi wa kituo cha Polisi cha kuweka umeme.

Wanachuo waaswa kutotegemea kuajiriwa na Serikali

VIJANA wengi wanaomaliza elimu ya juu wanatakiwa kuachana na fikra za kutaka kuajiriwa na serikali na badala yake wafikirie kutumia elimu yao kwa lengo la kubuni miradi mbalimbali ambayo itawawezesha kujiajiri wenyewe. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Mbali na hilo imeelezwa kuwa bila wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kupatiwa elimu ya stadi za maisha ni vigumu kufikia mapinduzi ya kiuchumi kwenye jamii inayowazunguka.

Kauli hiyo imetolewa mara baada ya kubainika idadi kubwa ya wanafunzi wa elimu ya juu pindi wanapohitimu masomo wanashindwa kutumia taaluma yao kuanzisha miradi ya kiuchumi badala yake wanasubiri kuajiriwa.

Akizungumza juzi mjini hapa kwenye mafunzo maalum ya stadi za maisha yaliyotolewa kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Taasisi ya Green Hope, Manjala Makongoro kwa ushirikiano wa kampuni ya simu za mkononi Vodacom, amesema elimu kuhusu stadi za maisha itamwezesha mwanafunzi kujitambua.

Amebainisha kuwa lazima mwanafunzi wa elimu ya juu kujitambua thamani yake kwenye jamii, hivyo anapaswa kuitumia taaluma yake kama njia ya kuondokana na utegemezi wa kiuchumi.

“Mwanafunzi mwenye kujitambua anapaswa kuwa na tabia ya kujitathimi kwa kila jambo analolifanya kama lina maslahi kwake na kwenye jamii.

“Pia lazima awe mwenye uthubutu wa kufanya maamuzi ya kuachana na jambo ambalo anaona halina maslahi kwake na kutafuta njia bora za kumwezesha kufikia malengo aliyoyakusudia,” ameeleza.

Mwezeshaji huyo amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom, imeamua kutoa mafunzo hayo ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwajengea uelewa vijana waweze kutumia fursa zilizopo kuleta mapinduzi ya kiuchumi.

“Serikali imekuwa ikisisitiza mapinduzi ya viwanda lakini kama wanafunzi wa vyuo vikuu wakikosa ufahamu kwenye stadi za maisha zitakazowawezesha kujiajili, kundi hilo litaachwa nyuma, ” amesema.

Naye Meneja wa Vodacom mkoani Dodoma, Balikulile Mchome, amesema mafunzo hayo yameonyesha kufanikiwa kwani wanafunzi wamekuwa na shauku ya kutaka kufahamu masuala mbalimbali yatayowawezesha kujitegemea kiuchumi baada ya kuhitimu masomo.

“Vijana wameonyesha kuwa na shauku ya kuwa wajasiliamali. Kwetu sisi ni mafanikio kwani kile tulichokilenga kimeonyesha mafanikio,” amesisitiza.

Naye Mooren Minja, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza anayesomea shahada ya elimu chuoni hapo, amesema mafunzo hayo yamewawezesha kujijengea uwezo wa kujitathimi na kubaini namna ya kukabiliana na changamoto za kiuchumi.

Amesema elimu ya stadi za maisha ni muhimu kwa wanafunzi kwani itamjengea wigo wa kuchanganua mambo yatakayowezesha kufikia lengo alilolikusudia hususan kufikia hatua fulani ya maendeleo.