Serikali watilia shaka uraia wa Abdul Nondo

MWENYEKITI wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo ameitwa Makao Makuu ya Uhamiaji kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu uraia wake. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Sheria wa TSNP, Paul Kisabo imeeleza kuwa Nondo ametakiwa kwenye ofisi hizo ili kuhojiwa kuhusu uraia wake na ndugu zake.

”Kwa muda wa takribani wiki moja mpaka sasa Nondo amekuwa akihitajika Uhamiaji ili akahojiwe kuhusu taarifa za uraia wake pamoja na za ndugu zake,” imeeleza taarifa hiyo.

Leo Nondo alifika katika ofisi hizo na kuhojiwa baada kutoka kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam alipokwenda kusikiliza kesi yake anayowashataki Mkuu wa Upelelezi, Mwanasheria Mkuu pamja na Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa kuchelewa kumpeleka makahamani.

Mnamo saa sita mchana tuliweza kumfikisha Abdul Nondo Makao Makuu ya ofisi za Uhamiaji mkoa (makao makuu ya wizara ya mambo ya ndani)
Tulipata kuhoji alichoitiwa na anachotakiwa kujaza katika fomu aliyopatiwa.

”Tuliambiwa wanataka kupata taarifa zake binafsi, za wazazi wake, babu na bibi zake pande zote mbili (upande wa baba na upande wa mama)
pamoja na za ndugu zake, kwani Afisa uhamiaji mkoa alitamka kuwa sheria inawaruhusu kumuhoji mtu yeyote wanaotilia mashaka uraia wake na kuwa wanamashaka na uraia wa Abdul Nondo, hivyo awathibitishie kuwa yeye ni Raia wa Tanzania”

Baada ya hapo afisa uhamiaji aliyekabidhiwa jukumu la kumhoji Abdul Nondo alisema kwamba Apliri 20, 2018 Abdul Nondo anapaswa kupeleka cheti chake cha kuzaliwa, cheti cha kuzaliwa cha baba yake, mama yake, cha bibi na babu mzaa baba na mzaa mama.

Dk. Abbasi: Waandishi msiogope, kosoeni serikali

DAKTARI Hassan Abbasi, Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO amewataka waandishi wa habari nchini kufanya kazi zao kwa uhuru, bila uoga kwani serikali ipo tayari kupokea maoni ya ukosoaji. Anaripoti Charles William … (endelea).

Dk. Abbasi amesema hayo hii leo jijini Dar es Salaam, katika sherehe za waandishi wa habari waliohitimu mafunzo chini ya ufadhili wa taasisi ya Tanzania Media Foundation (TMF), ambapo alikuwa mgeni rasmi.

“Wakati tunatengeneza Sheria ya Huduma za Habari, miongoni mwa vifungu nilivyopigania kiwepo kilikuwa ni kifungu cha 52 (2) kinachosema hakuna kosa kwa mtu anapokosoa serikali.

“Msiogope kukosoa, tuambieni tunakosea wapi, semeni tunakosea wapi labda kwenye sekta ya viwanda au kwingine na sisi tutafanyia kazi. Usitukane wala kukashifu mtu, usikosoe lakini kwa kusema uongo. Pia kuna mambo yanayohusu usalama wa Taifa lazima yazingatiwe.”

Dk. Abbasi ameipongeza TMF kwa kutoa mafunzo kwa waandishi ili waweze kubobea katika habari za uchunguzi za maendeleo pamoja na eneo la usalama wa barabarani, na kuwataka kutumia ujuzi waliopata kuisaidia serikali kwa kukosoa na kufichua mambo mbalimbali.

Fausta Musokwa, Kaimu Mkurugenzi wa TMF amesema taasisi hiyo itaendelea kutoa mafunzo na ruzuku kwa waandishi na vyombo vya habari ili waweze kuandika habari zitakazosaidia uwazi na uwajibikaji serikalini.

“Taasisi yetu ilianza mwaka 2008 kama mfuko wa wanahabari, mpaka sasa tumetoa mafunzo ya ubobezi (fellowship) kwa waandishi zaidi ya 120 na tutaendelea kufanya hivyo.”

Halima Shariff, mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya TMF amewataka waandishi kutochoka kufanya uchunguzi na kuibua mambo mbalimbali kwa maslahi ya nchi na wananchi pamoja na changamoto zinazowakabili.

Jumla ya waandishi 14 wamehitimu mafunzo yaliyokuwa yakiendeshwa na TMF kwa miezi sita kutoka Juni mpaka Januari mwaka 2018. Waandishi tisa wamehitimu mafunzo ya ubobezi ya kuandika habari za maendeleo na watano wamebobea katika uandishi wa habari za usalama barabarani.