Kesi ya Mawio yamponza Mwendesha Mashtaka

KWA mara nyingine Mahakama imehoji sababu ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoa kauli nyepesi za kushawishi kutoendelea kwa kesi ya tuhuma za uchochezi inayowakabili wahariri wawili. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hakimu Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alimtaka Wakili wa Serikali kutilia umuhimu haja ya kuondokana na kauli zinazochelewesha kesi ambayo tayari imechukuwa muda mrefu.

Hakimu Simba anasikiliza kesi Na. 208/2016 inayowakabili mwandishi wa Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL), Jabir Idrissa na Mhariri Mtendaji wa MAWIO, Simon Mkina.

Tarehe 30 Aprili, siku ya kutajwa kwa kesi hiyo, upande wa mashtaka kupitia mwanasheria wake alifika mahakamani bila ya jalada la kesi kasoro ambayo Hakimu Simba kaliihoji akisema, “inakuaje tunakuja hapa lakini nyinyi hata jalada la kesi hamnalo?”

Hakimu Simba alisema mtindo huo ni uzembe usiokuwa na sababu na kutaka DPP awe makini kushughulikia kesi anazofungua mahakamani.

Kesi Na: 208 iliyoanza Juni 2016, pia inamkabili mwanasheria na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (mshtakiwa wa nne) na Ismail Mehboob mshtakiwa wa tatu.

Wakati Mehboob, meneja wa Flint Priting Co, anashtakiwa kwa kosa la kuchapa gazeti lililobeba makala za uchochezi, Lissu anatuhumiwa kutoa maelezo yanayodaiwa kuchochea wananchi waichukie serikali yao.

Lissu alikuwa mmoja wa watu mashuhuri walionukuliwa katika maoni yaliyohusu namna ya kutatua mgogoro wa kisiasa Zanzibar uliozuka baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2015.

Hatua ya kufutwa uchaguzi ilizusha hofu na Lissu katika maoni yake alimtaka Rais John Magufuli kuchukua hatua ya kushughulikia mgogoro huo kabla ya kutokea maafa nchini.

Washitakiwa wote ambao wamekana mashtaka, wako nje kwa dhamana. Kesi itatajwa tena Mei 23.

Kesi ambayo imeanza usikilizaji kwa kutolewa ushahidi na mashahidi wawili, imekuwa ikitajwa tangu Septemba mwaka jana baada ya Lissu kujeruhiwa kwa risasi mjini Dodoma na kulazimika kukimbizwa nje ya nchi kwa matibabu.

Yuko nchini Ubelgiji anakoendelea kutibiwa majeraha yaliyosababishwa na risasi 10 hivi zilizoingia mwilini.

Lissu ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 Septemba 7 mwaka jana akiwa anawasili nyumbani kwake Area D Dodoma alikokuwa anashiriki vikao vya Bunge.

Gazeti ambalo lilitumika kufungua mashtaka ya Uchochezi ni MAWIO la Januari 14, 2016 na makala husika kutajwa ni iliyobeba gazeti kwa maneno “Maafa yaja Z’bar.”

Mabalozi nao kuhamishiwa Dodoma

JUMLA ya Mabalozi 63 wameshakabidhiwa maeneo ya kujenga ofisi zao Katika Jiji la Dodoma lakini Ubalozi wa Zambia tayari umeshaanza mchakato huo kwa kuanza ujenzi wa nyumba ya Mkandarasi wake. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi wakati akitambulisha mpango wa maonyesho ya wajenzi katika mkakati wa ‘Tunajenga Dodoma.’

Kunambi amesema mabalozi hao walikwenda wiki mbili zilizopita lakini juzi balozi wa Zambia akamuomba kumpatia kiwanja cha kununua haraka kwa ajili ya kujenga nyumba ya mkandarasi atakayekuwa akisimamia jengo la ubalozi.

Amesema mkakati umewekwa kwa ajili ya kuijenga Dodoma mpya itakayolingana na miji ya Abuja (Nigeia), Pretoria (Afrika ya Kusini) au Mji wa Nairobi nchini Kenya na kwamba Serikali imekwishatoa kiasi cha Sh 1.2 bilioni kwa ajili ya mapitio ya ramani ambayo hata hivyo hayataruhusu nyumba za watu kubomolewa isipokuwa kama kuna umuhimu zaidi.

Akizungumzia kuhusu vifaa vya ujenzi kwamba havitoshelezi, Meneja wa Tawi wa mabati ya Alaf Grayson Mwakasege, amesema dhata kuwa vifaa vya ujenzi kwa Dodoma ni vichache si ya kweli na kuwa imepitwa na wakati kwani bidhaa ipo ya kutosha isipokuwa watu wanatumia mwanya huo kutaka kuhalalisha manunuzi nje ya mkoa.

Mwakasege amesema ujenzi wa jiji hilo jipya hauwezi kumaliza malighafi iliyopo ambayo kila soko linavyopanuka ndivyo ambavyo wafanyabiashara wanavyoendelea kuongeza mitaji yao na kupeleka bidhaa hitajika.

Serikali yapiga stop kuagiza mita za luku

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amesema kuanzia Julai mwaka huu, serikali itasitisha uagizaji wa mita za luku ya umeme kutoka nje ya nchi ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa ndani. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Dk. Kalemani amesema nia ya serikali ni kutoa nafasi kwa wawekezaji nchini kuanza kuzalisha vifaa hivyo ili kuendana na kasi ya Tanzania wa viwanda.

Waziri huyo amesema kuwa usitishwaji wa kuagiza mita za luku unaenda sambamba na ule wa nguzo za umeme kutoka Afrika Kusini na transfoma kutoka nchini India.

Hans Poppe aongezwa kwenye kesi ya Aveva, Kaburu

MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Pope, ameongezwa katika kesi ya tuhuma za kughushi nyaraka na kujipatia fedha inayowakabili Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva na Makamu wa wake, Godfrey Nyange ‘Kaburu’. Anaripoti Jabir Idrissa … (endelea).

Waendesha mashtaka leo wamesoma upya mashtaka manane mbele ya Hakimu Mkazi, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Prosecution wameomba mahakama itoe hati ya kumkamata Hans Poppe kwa kuwa hakuwepo mahakamani wakati akijumuishwa katika kesi hiyo.

Hakimu Simba ameridhia ombi na kuelekeza hati itolewe na mahakama. Upelelezi wa kesi umekamilika.

Mtuhumiwa mwingine aliteongezwa katika kesi hiyo ni Franklin Lauwo ambaye anatuhumiwa kuitumia kampuni ya ukandarasi isiyosajiliwa ikapitishiwa pesa Dola 40,000 kama vile imelipwa kwa kazi wakati si kweli.

Haya ameyaeleza Leonard Swai, Mwanasheria wa TAKUKURU, wakati akiongeza washitakiwa na kusoma upya mashtaka.

Wahitimu SUA waomba fedha kununulia vifaa

SERIKALI imeombwa kuweka utaratibu wa upatikanaji wa fedha za kununua visanduku vya tiba kwa wanyama na kuweza kumkabidhi kila wanafunzi ili wanafunzi wanaomaliza elimu ya juu ya mifugo waweze kuwa navyo kufuatia kushindwa kufanya kazi vizuri wanapomaliza masomo kutokana na kukosekana kwa visanduku hivyo mahali wanapokwenda. Anaripoti Christina Haule … (endelea).

Ombi hilo lilitolewa jana na mwanzilishi wa kitivo cha tiba ya mifugo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Prof. Beda Kessy wakati wa sherehe za siku ya tiba ya wanyama duniani iliyofanyika katika viwanja vya hospitali ya wanyama katika ndaki ya tiba ya wanyama na sanyansi za Afya SUA.

Prof. Kessy amesema kuwa mara nyingi wanafunzi hao wamekuwa wakitayarishwa vizuri kielimu wawapo chuoni hapo lakini wanapotoka hapo wakiwa na digrii zao na kuajiriwa kwenye wilaya au maeneo mengine hushindwa kufanya kazi zenye ubora kwa tiba za wanyama kufuatia kukosekana kwa visanduku hivyo.

Hivyo amesema ni vema serikali ingeliona hilo na kutenga bajeti kwa ajili ya manunuzi ya visanduku hivyo kwa manufaa ya wanyama na Taifa kwa ujumla.

Naye Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. Raphael Chibunda amewataka wamiliki wa wanyama kutambua kuwa wao daktari wa mifugo ni muhimu sana kwao na kwa wanyama wao pia.

“Kwa mfugaji iwe ni mbwa, paka, farasi au kuku nafahamu kuwa mnawapenda wanyama wenu lakini kwenu daktari wa mifugo ni muhimu sana kwenu kama alivyo kwa wanyama wake,” amesema.

Amesema kuwa kwa Ndaki ya tiba ya wanyama kujitolea kujitolea kufanya matibabu na ushauri wa bure kwa wamiliki wa wanyama ni nafasi muhimu ya kuzidi kuimarisha mahusiano yao na wanyama na madaktari wao.

Hivyo aliwaomba wamiliki hao kuwa mabalozi wa tiba ya wanyama mahali wanapokaa na kwamba wataalam na vifaa vilivyopo kwa sasa SUA kwa ajili ya Tiba ya mifugo havitumiki kiasi cha kutosha, huku afya za wanyama zikiwa haziko nzuri sana sambamba na magonjwa ya hatari kama kichaa cha mbwa kuendelea kutishia uhai wa binadamu hapa nchini.

Alishauri watanzania wanaoifahamu fursa hiyo kuitua vyema na kuitumia kuwaelimisha watanzania wengi ambao hawajui juu ya uwepo wa taaluma na huduma hizo hapa nchini.

Amesema, ifahamike kwamba uboreshaji wa maisha ya wanyama sit u utawasaidia wanyama na wamiliki wao bali pia itasaidia kuboresha ajira, kuboresha mazao ya wanyama nchini na hivyo kuongeza kipato na uchumi wa nchi.

Wafanyakazi watakiwa kupeleka vilio vyao Mei Mosi

WAFANYAKAZI nchini wametakiwa kuendelea kuhamasika kujitokeza kwa wingi wakati wa maandamano kwenye siku ya maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ili kuweka bayana changamoto zinazowakabili sehemu zao za kazi na kuweze kupatiwa ufumbuzi. Anaripoti Christina Haule … (endelea).

Wito huo ulitolewa jana na Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi (TPAWU), Nicholaus Ngowi wakati akizungumzia sherehe za Mei Mosi zinazotarajiwa kufanyika kimkoa katika viwanja vya Jamhuri mkoani Morogoro.

Ngowi amesema kuwa wafanyakazi wanapaswa kutambua kuwa Maadhimisho hayo ni sehemu ya kutoa changamoto zao ikiwemo masuala ya mahusiano yaliyopo sehemu zao za kazi. Aidha aliwataka waajiri kuendelea kutoa haki kwa wafanyakazi hasa pale wanapotimiza wajibu wao.

Naye Mratibu wa sherehe za Mei Mosi Mkoani hapa Mgassa Chimola amewaomba waajiri wilayani na mkoa mzima wa Morogoro kuwaruhusu watumishi kuhudhuria maadhimisho hayo huku wakileta bidhaa mbalimbali kwa ajili ya maonesho na elimu kwa jamii.

Chimola ambaye pia ni Katibu wa Chama Cha wafanyakazi (TUICO) mkoa, amesema kuwa maadhimisho hayo kimkoa yatafanyika katika uwanja wa Jamhuri Manispaa ya Morogoro ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa ni mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Kebwe Steven Kebwe.

Amesema, maadhimisho hayo yataanza na maandamano yatakayoanzia ofisi za TUICO mkoa zilizoko barabara ya stesheni Manispaa ya Morogoro ambapo kauli katika maadhimisho hayo ni “kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi za jamii kulenge kuimarisha maslahi ya wafanyakazi”.

Naye Mwenyekiti wa maandalizi ya sherehe hizo kimkoa, Mohamedi Simbeye amewaasa wafanyakazi kujiunga kwenye vyama vya wafanyakazi ili waweze kuwa na umoja wa kuwatetea hasa kwenye masuala yanayohusu maslahi yao.

Aidha Simbeye ambaye pia ni Mwenyekiti wa TUCTA mkoa wa Morogoro amesema kuwa maandalizi ya mwaka huu yamejitahidi kuondoa dosari ndogondogo zilizokuwa zikijitokeza kwenye maadhimisho ya nyuma ikiwemo waajiri kutofikisha zawadi kwa mshindi kama ilivyokusudiwa.

“Kwa sasa changamoto zimetatuliwa, tunapokea zawadi mapema za washindi wote kabla hatujaingia uwanjani, na mshindi anakabishiwa zawadi yake papo hapo kuanzia kwa viongozi wa wilaya hadi mkoani,” amesema.

Nondo apewa tuzo kwa kuwatetea vijana

MWENYEKITI wa Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo amepata tuzo kama mtetezi kijana chipukizi wa haki za binadamu (wanafunzi) Tanzania, tuzo aliyopewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Nondo amesema kuwa tuzo hiyo kwake imekuwa na maana kubwa na kuweza kuinua hari mpya ya kuzidi kuwatetea wanafunzi katika haki zao katika masuala mbalimbali nchini na kudai tuzo hiyo imezidi kumuimarisha zaidi na kutokana tamaa na changamoto mbalimbali anazopitia katika kutetea haki za wanafunzi.

“Kwanza namshukuru Mwenyezimungu kwa kunipa Afya njema, pia wazazi wangu na viongozi wenzangu wa TSNP na watanzania wote kwa ujumla kwa faraja zao na matumaini yao kwangu. Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mtandao wa THRDC kwa kutambua mchango wetu TSNP kwa kunizawadia tuzo kama mtetezi kijana chipukizi wa haki za binadamu (wanafunzi) Tanzania nimefarijika saana,” amesema Nondo.

Nondo amesema kuwa kwa kushirikiana na baadhi ya taasisi za serikali na taasisi hizo zimekuwa zikipokea na kusikia na kufanyia kazi baadhi ya mambo ambayo wamekuwa wakiyasemea.

 

Meya wa Chadema aliyejiuzuru Iringa, avuliwa uanachama

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Iringa kimemvua uanachama Dady Igogo aliyekuwa diwani wa Kata ya Gangilonga na Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa baada ya kukutwa na kosa la kukisaliti chama. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii huku ikionesha imetolewa na Katibu wa Chadema Jimbo la Iringa Mjini, Suzana Mgonokulima, imeeleza kuwa Kamati Tendaji ya Jimbo imechukua uamuzi huo baada ya kumkuta mtuhumiwa kwa makosa ya kukisaliti chama, kujivua nafasi ya Unaibu Meya na baadaye Udiwani.

Taarifa kamili iliyotolewa na Chadema Jimbo la Iringa Mjini hii hapa:-

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) JIMBO LA IRINGA MJINI :

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA.

YAH: KUFUKUZWA UANACHAMA NDUGU DADY JOHANES IGOGO:

Dady Igogo aliyekuwa Diwani wa CHADEMA kata ya Gangilonga na Naibu Meya Manispaa ya Iringa; alikisaliti Chama na kujivua nafasi ya Unaibu Meya na baadaye Udiwani kwa kile alichokiita “Sababu zilizoko moyoni mwake.”

Katiba ya CHADEMA 2006 , Toleo la 2016 Ibara 5.4. Inaeleza na kufafanua juu ya “kukoma kwa uanachama.”

Vile vile Ibara 5.4. (1 , 2, na 3) inaeleleza kuwa mwanachama atakoma uanachama wake kwa kujiuzulu , kufariki , kuachishwa ama kufukuzwa.

Ndugu Igogo kwa muda mrefu amekuwa na mwenendo usioendana na Itikadi, Falsafa, Madhumuni, Kanuni, Maadili na Sera za Chama.

Kamati tendaji ya Jimbo katika kikao chake cha dharura kilichoketi Tar.24/04/2018 kiliazimia yafuatayo:

1. Dady Igogo avuliwe ujumbe wa kamati tendaji ya Jimbo kwa mujibu wa Ibara 7.4.10 (x) na Ibara 7.7.8 (k) kwa kwenda kinyume na katiba ya chama, kanuni na maadili ya chama.

2. Dady Igogo afukuzwe uanachama kwa mujibu wa Ibara 5.4.3 kwa kuwa amekosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama wa CHADEMA.

Hivyo kuanzia leo tar 28/04/2018 Chama kinatoa taarifa kwa wanachama na umma kuwa Dady Igogo sio mwanachama wa CHADEMA tena.

Imetolewa na;

Suzana Mgonokulima.

Katibu wa CHADEMA.

Jimbo la Iringa Mjini.

27/04/2018.

Makao Makuu ya Mahakama Dodoma yaiva

JAJI Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma amezindua zoezi la upandaji miti katika kiwanja ambacho itajengwa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania mkoani Dodoma. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Akizindua zoezi la upandaji miti katika kiwanja hicho Jaji mkuu Prof. Juma amesema kuwa miti inazofaida nyingi katika maisha ya mwanadamu hivyo watumishi wa Mahakama Kuu Tanzania hawana budi kuitunza.

Amesema kiwanja hicho ambacho wamepatiwa na Manispaa ya Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu kitapendeza kama kitakuwa cha mafano katika suala la utunzaji wa mazingira.

Aidha amesema kuwa tafiti zinaonyesha kuwa mtu akipanda heka moja ya miti atakuwa ametoa hewa ya Oxygen kwa watu 18 kwa mwaka mzima.

Awali akisoma taarifa za kiwanja hicho Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango Mahakama ya Tanzania, Erasmus Uisso amesema kuwa eneo hilo linaukubwa wa hekta 18.9 sawa na hekari 45.

Amesema katika eneo hilo wanatarajia kujengwa jengo la mahakama kuu, mahakama ya Rufani na masjala kuu na ujenzi unaanza ndani ya mwaka huu.

Amesema kuwa tayari wameshapatiwa hati ya eneo hilo ya miaka 99 na hivi sasa wapo katika mchakato wa kumtafuta mtaalam kwa ajili ya michoro pamoja na gharama za ujenzi.

“Tayari eneo hili tulishalifanyia utafiti wa kisayansi kubaini hali ya miamba pamoja na athari za matetemeko lakini wataalam wa masuala ya jiolojia walituambia kuwa hapa hakuna athari ya matetemeko hivyo tunaweza kuendelea na ujenzi kwani athari ya matetemeko ni kilomita 10 kutoka hapa,” amesema Uisso.

Aidha amesema kuwa pia katika eneo hilo kipo kiwacha chenye mita za mraba 9,000 kwa ajili ya ujenzi majengo ya mahakama kuu kanda ya kati, mahakama ya mkoa, Mahakama ya wilaya pamoja na mahakama ya mwanzo.

Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi aliipongeza Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kupata eneo hilo ambalo litajengwa makao makuu ya moja katia ya mihiri ya taifa.

Prof. Kabudi aliwataka kulitumia vizuri eneo na kujenga mahaka ambayo itakuwa ya mfano na inayoendana na makao makuu ya nchi.

Waliokula Bil 1.5 kukiona cha moto

RAIS John Magufuli ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinawachukulia hatua kali watu wote waliohusika katika kufanya ubadhilifu wa zaidi ya Sh. 1.5 bilioni ya mradi wa maji wa Ntomoko. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Agizo hilo alilitoa wakati wa ufunguzi wa barabara ya Dodoma Manyara yenye urefu wa kilometa 251 iliyozinduliwa katika eneo la Bicha wilayani Kondoa mkoani hapa ambayo itaongeza fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa hiyo miwili.

Akiwahutubia wananchi wa Kondoa na Manyara, muda mfupi baada ya kupatiwa taarifa ya mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhandisi Bilinithi Mahenge, kuelezea kuwa kuna ubadhirifu wa zaidi ya Sh. bilioni moja na nusu zilizopotea katika mradi wa maji wa Ntomoko na kuwakosesha huduma ya maji wananchi wa wilaya ya Kondoa na Chemba.

Mradi huo wa kutandika mabomba ya kusambazia maji kuwafikia wananchi ambapo waliopewa dhamana hiyo badala ya kutandika mabomba ambayo yanauwezo mkubwa wa kufikisha maji wao wakaweka mabomba madogo ambayo hayana uwezo.

“Kama ni kuchomoka basi wachomoke wale wote waliofanya ubadhirifu wa mradi huu kwani wanawapa shida wananchi wanyonge ambao walikuwa wapate huduma ya maji tokea mwaka 1980,” alisisitiza Rais Magufuli.

Aidha kwa upande mwingine Rais Magufuli akawataka viongozi wa wilaya hiyo kuacha migogoro ya wao kwa wao na kuwa migogoro inachangia kushindwa kuwapelekea wananchi huduma za maendeleo kwa wakati na yeye hakuwatuma kwenda kuibua migogoro hiyo.

Kwa upande wake Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Akinwim Adesina aliahidi neema kwa jiji jipya la Dodoma na serikali kwa ujumla kwamba atatoa ushirikiano kuhakikisha serikali na jiji hilo wanapata fedha za miradi.

Amesema kuwa barabara hiyo itafungua milango ya kiuchumi kwa lango la Kaskazini mwa Afrika na Kusini ambapo hiyo itakuwa fursa pana kwa wananchi wa mataifa nane barani humo ambayo barabara hiyo inapita kutoka Cape Town hadi Cairo nchini Misri.

Nae Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa barabara hiyo yenye urefu wa km. 251 imejengwa kwa jumla ya Sh. 378.4 bilioni kati ya hizo fedha za ndani Sh. 107.6 bilioni na zilizobakia zimechangiwa na wafadhili Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) na Shirika la Maendeleo la Japani (JICA).

Pauline Gekul amchokonoa JPM

Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekuli amemtaka Rais John Magufuli kuingilia kati mgogoro uliopo kati ya wananchi na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusiana na stendi ya mabasi.

Amesema pamoja na kujengwa barabara ambayo inaunganisha Dodoma na Babati ambayo itafungua fursa kubwa kwa wananchi lakini bado kuna changamoto ya stendi ambayo imekuwa ikileta utata kati ya wananchi wa CCM kwa kudai kuwa eneo hilo ni la kwao.

“Mheshimiwa Rais kwanza kabisa nishukuru kwa maendeleo ya barabara hii ambayo unaizindua leo ambayo wananchi wa Babati watajiongezea kipato kwa kutumia barabara hiyo.

“Na kama unavyosema kuwa maendeleo hayana vyama hivyo naomba uingilie kati na kutatua mgogoro wa stendi kwa sasa najua magari yatakuwa mengi lakini hakuna stendi kwani hiyo kwa sasa imeonekana kuwa ni ya chama cha mapinduzi badala ya halmashauri.

“Sasa naomba utuachie stendi hiyo ili wananchi waendelee kuitumia na kuongeza kipato kwa halmashauri hiyo na badala yake wanachama wa CCM watapatiwa kiwanja kingine ili waweze kujenga wanachokitaka,” amesema Gekul.

Mdogo wa Heche adaiwa kuuwawa mikononi mwa Polisi

MDOGO wa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche aitwaye Chacha Heche Suguta, adaiwa kuuwawa akiwa chini ya Jeshi la Polisi baada ya kukutwa akiwa jeraha la kuchomwa kisu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Ndugu wa marehemu wanasema wakati alipokamatwa na Polisi alikuwa mzima kabisa. Muda huu mabomu ya machozi na risasi vinafurumushwa kuwafukuza wananchi kutoka kituoni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, RPC Mwibambe amekiri askari wake kuhusika na mauaji hayo ya kijana huyo aliyezaliwa mwaka 1989. Chacha Suguta ni mdogo (upande wa Baba mdogo) wa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema).

John Heche anasema kuwa kijana huyo alikamatwa na Askari wa Jeshi la Polisi usiku wa jana akiwa Baa akiwa mzima kabisa.

Heche amesisitiza kuwa baada ya kufariki, Askari wa Polisi walitaka kuutupa mwili wake lakini ilishindikana kwa sababu eneo walilotegemea kuutupa kulikuwa na Mlinzi aliyewafukuza, ndipo walipoamua kuupeleka mwili wake kwenye chumba cha kuhifadhia maiti (Mortuary) ya Tarime.

Kesi ya Lema yafutwa, akamatwa tena

JESHI la Polisi Mkoani Arusha limemkamata Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema kwa kile kinachodaiwa “uchochezi” dhidi ya Rais kuhusiana na ndoto aliyowahi kuota. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili Lema kutokana na ndoto alizoota miaka miwili iliyopita, ilifutwa lakini muda mchache baadaye polisi walimkamata tena na kumfungulia kesi upya kwa mashtaka yale yale.

Kesi hii ni mwendelezo wa kesi iliyokua ikimkabili Lema na ambayo ilimsotesha mahabusu (Magereza) kwa zaidi ya miezi mnne mwaka juzi kabla ya kuachiwa kwa dhamana mapema mwaka jana.

Magufuli atangaza Dodoma kuwa jiji

RAIS John Magufuli jana katika sherehe za Muungano, ametumia sherehe hizo kutangaza Dodoma kuwa jiji badala ya kuwa Manispaa na kumtangaza aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi na kuwa Mkurugenzi wa Jiji. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Mbali na kutangaza kuwa Dodoma ni Jiji ametangaza vita kwa mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kutaka kuvunja au kuruvuga Muungano kuwa yeye (Magufuli) pamoja na rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kuwa watamshughulikia kwa gharama yoyote.

Akihutubia umati wa watu Mafufuli alisema kuwa licha ya kuwa siku ya leo (jana) siyo siku ya hotuba bali ni siku ya sherehe alisema kuwa hatahakikisha analinda muungano kwa gharama yoyote na atakayejaribu kutaka kuvunja muungano huo atashughulikiwa kwa nguvu zote.

Alisema kuwa serikali anayoiongoza haitamfumbia macho mtu yoyote awe wa ndani ya nchi au nje ya nchi ambaye atajaribu au kutaka kuvuruga muungano ambao umeasisiwa na viongozi waliokuwa marais wakati huo kwa maana ya Juliasi Kambarage na Abeid Amani Karume.

“Mtu yoyote sichezee Muungano, Mimi na Dk. Shein tutahakikisha tunalinda Muungano kwa gharama yoyote, Muungano wetu ndiyo ngao yetu kamwe hatutamwonea aibu mtu yoyote atakaye jaribu kuchezea Muungano wetu,” alisema Dk. Magufuli.

Akizungumzia changamoto mbalimbali za Muungano alisema kupitia kwa makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan changamoto nyingi za mashirikiano zimepungua kutoka 22 hadi kufikia 11.

Alisema kutokana na hali hiyo alisema Muungano uweweza sauti hata kimataifa na ni kati ya muungano uliodumu kuliko nchi nyingine ambazo zilikuwa na muungano .

Alisema Juhudi za Muungano zimeweza kuwa mkombozi wa utatuaji wa migogoro katika maeneo mengi Tanzania bara na Visiwani huku akieleza kuwa muungano ni lazima ueshimiwe na kulindwa kwa gharama yoyote.

Dodoma kuwa Jiji

Akizungumzia Dodoma kuwa jiji alisema kuwa amejaribu kuangalia maeneo mbalimbali ambayo ni majiji na kubaini kuwa lipo jiji la Dar es salaam, jiji la Tanga, Jijij la Mbeya, Jiji la Mwanza na kutafakari na kuona kama anayo mamlaka ya kufanya jambo lolote na kueleza kuwa ameweza kujiridhisha na kuamua kutangaza Dodoma kuwa Jiji badala ya kuendelea kuwa Manispaa.

“Nimejaribu kuangalia majiji yaliyopo nikaona kuna jiji la Dar es salaam, jiji la Tanga, Jijij la Mbeya, Jiji la Mwanza,na kwammlaka niliyonayo kuanzia leo natangaza kuwa Dodoma siyo Manispaa tena bali linakuwa jiji na kuanzia leo tarehe 26 mwezi huu na mwaka huu aliyekuwa mkurugenzi wa Manispaa atakuwa mkurugenzi wa Jiji la Dodoma” alisema Dk. Magufuli.

Alisema kutokana na Dodoma kuwa jiji baada ya sherehe za Muungano atakwenda kukutana na rais wa Benki ya Maendeleo ili aweze kumchomekea kwa ajili ya kupata hela za kufanya miradi ya maendeleo kwa bajeti ya jiji badala ya kupata pesa za miradi yenye sura ya Manispaa.

Uchumi kukua 

RAIS Dk. Magufuli alisema kuwa kwa sasa serikali awamu ya tano inaendelea kupambana na kuhakikisha inafanya vizuri ikiwa ni pamoja na kupandisha uchumi wan chi.

Alisema kuwa kwa sasa uchumi umekua kwa asilimia 7 na anategemea baada ya mwaka mmoja uchumi utaendelea kukua hadi kufikia asilimia 7.1 huku akisema hata ali ya kiafya imeimarika ikiwa ni pamoja na kupambana na hali ya malaria kushuka kutoka asilimia 14.3 hadi kufikia asilimia 7.3.

Viongozi washindwa kufika 

Pamoja na kusherehe hizo kupambwa na maonesho mbalimbali lakini baadhi ya viongozi mbalimbali hawakuweza kufika katika sherehe hizo licha ya kutotangazwa sababu yoyote licha ya kuwa ni lazima wafike au wasifike katika sherehe hizo.

Viongozi ambao hawakufika katika sherehe hizo ni pamoja na Rais wa awamu ya pili All Hasani Mwinyi, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, mawaziri wastaafu ni Mizengo Pinda, Dk. John Malecella, Edward Lowasa huku rais wa awamu ya tatu William Mkapa akiwa ni kati ya viongozi wastaafu waliohudhuria sherehe hizo.

RC Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge alisema kitendo cha Manispaa kuwa jiji kitaongeza ari ya kimaendeleo lakini pia ni hshima kwa wakazi wa Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalum alisema wanchi wa Jiji la Dodoma wanatakiwa sasa kujituma kufanya kazi ili kuweza kujiongezea kipato na kubadilika na kuona kuwa sasa wanatakiwa kubadilisha mfumo wa maisha na kuishi katika mfumo mwingine.

Mbali na hilo alisema hata hivyo serikali ya mkoa inaro jukumu zaidi katika kuhakikisha inasimamia miundombinu mbalimbali pamoja na mipango ya kimaendeleo ili kukithi mahitaji ya wananchi ambao wanaishi katika jiji la Dodoma.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa

Naye aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa na sasa kupandishwa hadhi kuwa jiji Godwini Kunambi alisema kitendo cha Manispaa kuwa jiji kinapelekea zaidi kuendelea kutekeleza mipango kabambe ili kuweza kukidhi matakwa ya jiji.

Alisema pamoja na mambo mengine lakini kwa sasa wakati ikiwa Manispaa aliweza kufanya makusanyo kuwa na kiwango cha juu hadi kufika asilimia 66 ambapo alitakiwa kukusanya asilimia 50.

Alisema kuwa katika manispaa pekee Tanzania ambayo inamzidi kwa makusanyo ni manispaa ya Ilala wakati yeye akiwa anamakusanyo akubwa zaidi .

Alisema kitendo cha manispaa kuwa makao jiji itawafanya wananchi kuhakikisha wanafanya kazi ya kujipatia kipato kama pale wataweza kufanya mambo mbalimbali kwa ajili ya kujiongezea kipato cha mtu mmoja mmoja.

Wananchi 

Baadhi ya wananchi ambao waliozungumza na gazeti hili alisema kitendo cha Manispaa kutangazwa kuwa jiji kitasaidia sana wananchi kujiongeza na kufanya shughuli za kimaendeleo na kuachana na tabia za kubweteka.

Mmoja wa wananchi ambaye pia ni mjasiliamali Lilian Sambu, alisema kuwa kila mtu sasa ataweza kupata fursa ya kuongeza juhudi katika ufanyaji wake wa kazi sambamba na kuboresha shughili anazozifanya.

“Kuna watu ambao wanaweza kubeza kuwa Manispaa hajafikia kiwango cha kuitwa jiji lakini kama hautaweza sasa na kuanza kuzoea lini tutaweza kuanza na kuzoea,” alihoji Lilian

Katika hatua nyingine mjasiliamali huyo aliwataka wananchi ambao ni wajasiliamali wenzake kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa viwango na ubora ambao unakubalika kwa kuzingatika kuwa kwa sasa jiji la Dodoma litakuwa na wageni wengi na waaina mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Ujumbe mzito wa kifo cha Masogange

JULIUS Mtatiro, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF ameandika ujumbe mzito wenye kufikirisha wengi juu ya msiba wa Agnes Gerrald “Masogange.’

Mtatiro ameandika ujumbe huo kwenye ukurasa wake wa Facebook, akieleza maisha ya mrembo huyo huku akiwataja baadhi ya watu ambao walimtumia vibaya binti huyo na kumwacha anafariki bila kula matunda yake.

Soma kwa kina ujumbe huo mzito wa Mtatiro:-

KWAHERI MASOGANGE … HATUKUKUTENDEA HAKI!

Ndugu zangu, uvumilivu umenishinda na nikaona lazima niandike jambo. Ni kawaida yetu kwenye taifa letu kuandika kurasa nyingi za wasifu wa wanasiasa, watumishi wa umma “waliotukuka”, matajiri na watu tunaodhani waligusa maisha ya jamii kwa njia sahihi kila wanapofariki.

Ni kawaida yetu pia kuwahukumu marehemu wengine, bila kuwajua, wakifa tunaishia kutangaza yale tuliyodhani ni maovu yao bila kujiuliza tuliweka mchango gani kwao.

Wapo watu wengine hufa, tukadhani hawana maana, ni wadhambi, hawana mchango kwenye jamii na hawapaswi kuigwa hata kidogo. Kumbe vifo vyao ni kioo kikubwa cha maisha yetu, ni funzo kubwa na ni tafakari halisi ya sisi ni nani.

Tangu dada yetu Agnes Gerald (Agnes Masogange) afariki, nimeona kwenye mitandao mingi watu wakimzungumzia vile watakavyo. Hiyo ni kawaida. Sehemu kubwa ya wanaomzungumzia wanaeleza namna ambavyo hakuishi maisha mema na hakuwa kioo cha jamii.

Mimi sikuwahi kukutana na Agnes zaidi ya kumuona mitandaoni, mara ya kwanza kupitia video ya mwanamuziki “Bele 9”, tangu hapo nilimuona kama msichana mwenye vituko na visa vingi, tangu kuchezesha viungo vyake bila nguo hadi kuhusishwa na tuhuma za madawa ya kulevya.

Katika safari yote hiyo binafsi sikuwahi kumhukumu, maana nilijua chanzo cha yote hayo ni kukosa elimu bora (ya darasani), elimu bora ya uraia na elimu bora ya maadili. Chanzo cha kukosa vitu hivyo ni familia yake, ndugu zake, marafiki zake, serikali yake na wote tuliomzunguka.

Kwa kipaji cha Agnes, tangu kinachomozwa kwenye wimbo wa Bele 9, umbo lake na haiba yake – kama tungelikuwa na taifa lenye maandalizi na vijana walioandaliwa, Agnes tumuagaye na kuelekea kumzika labda angelikufa akiwa Agnes mshindi wa tuzo ya Oscar kwenye Muziki, Uigizaji, Uhamasishaji Jamii, Uburudishaji n.k.

Lakini tunaenda kumzika Agnes na vipaji vyake sahihi ambavyo aliwahi kuvichomoza, vikageuzwa kuwa faida kwa wengine kwa njia nyingine, vikaharibiwa, akavishwa taswira ya picha chafu mitandaoni na madawa ya kulevya.

Naamini, kipaji cha Agnes kilipochomoza tu, wajanja walimuwahi, wengine wakiwa watu wakubwa tu, wengine wakiwa na nyadhifa kubwa tu, wengine wakiwa na elimu kubwa tu, wengine wakiwa na fedha nyingi tu na wengine wakiwa na vipaji vikubwa zaidi.

Dada yetu huyu najua alikimbiliwa na kutumiwa na sisi sisi, kila mmoja wetu akimtumia kwa maslahi yake.

Agnes aliwahi kukutwa na kemikali ambazo haziruhusiwi kusafirishwa, alikamatiwa Afrika Kusini, baadaye aliachiwa. Zile kemikali zilikuwa ni za nani? Kwa alimpa Agnes? Je tulimfuatilia (maana naambiwa yuko hapa Tanzania) na ni mtu mkubwa tu, ana hela nyingi tu na ana elimu ya kutosha! Taifa zima likamhukumu Agnes, tukamuita muuza madawa; mtu mwenye mamlaka (mmiliki wa kemikali hizo) hadi leo anatembea barabarani akitamba, Agnes yuko kwenye jeneza na jamii ikihukumu matendo yake!

Kuna wakati video ya Agnes ilionekana mitandaoni akiwa anacheza na nguo za ndani tu. Aliyekuwa anarekodi video ile alikuwa anampa maelekezo “…bebi sogea hivi, cheza hivi, fanya vile…” Agnes anatekeleza!

Video ile ikazua gumzo, bila shaka aliyeilikisha mitandaoni kwa sababu zozote zile ni huyu mwanaume ambaye anaweza kuwa mpenzi wa wakati huo wa Agnes. Kwa kutojali na kutotambua umuhimu wa vijana wetu (serikali/taifa), hatukuwahi kusikia mwanaume huyo amehojiwa, hatukuwahi kusikia akihukumiwa na hatukuwahi kuona Agnes akilipwa fidia ya udhalilishaji ule uliomuonesha kama msichana mdhambi. Sana sana ambaye alitukanwa na kuhukumiwa na taifa ni Agnes, huyo mwanaume yuko “SALAMA!” na huenda anaendelea kurekodi wasichana wengine.

Tumo kwenye taifa ambalo halijui kulinda vijana wake kwa kutatua mizizi na vyanzo vya matatizo yao. Tumo kwenye taifa ambalo, vijana wanakamatwa kwa tuhuma za kutumia madawa ya kulevya huku wasambazaji na wenye mitaji ya uingizaji wa madawa hayo wakiwa ni wafadhili wakubwa wa vyama vyetu na kutusaidia kuingia serikalini. Sisi ni wapumbavu sana!

Upumbavu wetu ndiyo unafanya vijana wetu wanakufa na vipaji vyao huku sisi kama taifa tukiendelea kushindwa kuwanyanyua na kuwasaidia, sana sana tukiingilia vipaji vyao, tunavitumia kwa maslahi yetu, waje kuimba kwenye matamasha na wawe wanachama wa vyama vyetu, na huko tunawatumia tutakavyo, mwisho wa siku hawatambuliki.

Ndiyo maana kwa hawa wasanii wetu, ni wachache mno ndiyo wana mafanikio, wengi wamo kwenye sanaa kuwanufaisha watu wengine. Angalia wachezaji wetu, wengi hustaafu michezo yao wakiwa hawajui watakula nini. Sababu ya yote haya ni taifa letu kutokuwa na mpango unaotekelezeka wa kuwasaidia vijana kuinuka kutoka chini ni kung’arisha vipaji vyao.

Kifo cha Masogange kimeniumiza kwa sababu kinajenga taswira za maisha ya ndani ya vijana wengi wa taifa letu, taswira ya kutwishwa mizigo mizito wakiwa wadogo, kuharibiwa, kutelekezwa, kujitafutia maisha, kuonesha vipaji vyao na vipaji hivyo kutumiwa na watu wengine kwa manufaa ya watu hao huku vijana wetu wakibaki na taswira hasi na kuonekana ni wavunja maadili.

Namheshimu Binti Agnes kwa sababu naamini hakupaswa kufa akiwa Masogange huyu atafsiriwaye na watu wenye mitizano hasi. Naamini Agnes alinyimwa fursa na usimamizi wa kila mtu (familia, marafiki, ndugu na taifa).

Nimemuona Baba ya Agnes akisema alikosana na mwanaye tangu alipopata ujauzito na kuacha shule akiwa kidato cha 2. Baba ya Masogange alijua kuwa “…mtoto wako akipata mimba shuleni suluhisho ni kumfukuza nyumbani”, ndivyo mababa wengi wa zamani waliamini na ndivyo hata baadhi ya viongozi wakubwa wa sasa wanaamini. (Yupo kiongozi amesema mwanafunzi akipata mimba asisomeshwe tena).

Pamoja na kuishia kidato cha pili na kutelekezwa na familia yake naambiwa ya kuwa, hata baba ya mwanaye alimtelekeza. Masogange akaanza kupambana kivyake.

Video ya Bele 9 ikamtambulisha kwa watanzania, alirudi na kusimama kwa msaada wa watu wema lakini tokea hapo akakosa usimamizi na menejimenti.

Kama kipaji cha Diamond kisingepata usimamizi, Diamond angelikuwa anaomba dua kupata nauli ya daladala, yeye mwenyewe Diamond mara kadhaa amesema kuna watu wamemnyanyua sana.

Lakini Agnes najua kuna watu wamemdidimiza sana, wamemuumiza sana, wamemtumia sana na wamempa matatizo makubwa sana – wengine kati ya watu waliomuumiza watakuwa msibani kwake wakishughulikia usafiri, chakula, matangazo….wengine watafika kuchangia maziko yake lakini walimuumiza sana na ama walifurahi sana wakati walidhani anazama alipokuwa hai. Ni kawaida yetu!

Wako watu wanaamini “wewe binafsi ndiye wa kulaumiwa kwa maisha yako”, ni kweli kabisa, lakini wanasaikolojia wanajua “wewe ni wewe hivi sasa kwa sababu ya jinsi ulivyoathiriwa na mazingira uliyomo.” Watu ulionao, familia uliyonayo, ndugu zako, taifa lako, marafiki zako n.k ni vyanzo vikubwa vya kukufanya wewe uwe nani.

Dada yetu Masogange ni matokeo ya yote niliyoyataja hapo juu. Yeye ni tunda letu, ni dada yetu, mtoto wetu, mwenzetu.

Agnes ni taswira yetu halisi. Kama tunadhani yu mdhambi, basi sisi ni wadhambi mara 100. Kama tunadhani hafai, basi sisi hatufai mara 100 – yeye ni zao letu sisi, ni zao la mazingira yetu, zao la mipango yetu kwa vijana wetu, zao la roho zetu.

Wakati tunamzika Agnes tukumbuke maisha aliyokuwa anaishi ndiyo wanaishi vijana wetu wengi kwenye taifa letu, mapito aliyopitia hadi mwisho ndiyo safari ya maisha ya vijana wetu wengi, tabu, mateso, usumbufu, shida, kutengwa, kutwezwa, kudhalilishwa, kuumizwa, kutumiwa na kulaumiwa kwa yote hayo – ndiyo maisha wanayopitia vijana wetu wengi na hasa wasichana wa taifa hili.

Nimemsikia baba ya Agnes akisema mwaka jana na hadi mwaka huu binti yake alimweleza kuwa anajipanga kumfanyia mambo makubwa. Agnes akamsisitiza baba yake kuwa siku hizi (yeye Agnes) amebadilika mno, ameachana na maisha ya hovyo na ana shabaha ya kulinda nidhamu na kutafuta mafanikio.

Kwa mtizamo wangu, Agnes amekufa kifo cha amani na matumaini makubwa kwake na kwa Mungu wake. Halafu naamini Agnes alikuwa mdhambi kama sisi woote, na labda sisi wengine tumewahi kufanya dhambi kubwa kumshinda, yeye anahukumiwa sana kwa sababu alikuwa maarufu kiasi chake, alikuwa socialite, video queen na msanii.

Wasanii wetu (hasa wa kike) wajifunze kupitia maisha ya Agnes, wajipange, wajenge nidhamu, wachague marafiki wenye faida, wakuze sanaa zao ndani ya menejimenti imara, wasikubali kutumiwa na watu wenye fedha, wanasiasa wenye mamlaka yoyote na hasa wanaume.

Familia zetu, ndugu, jamaa, marafiki, taifa zima..sote tujifunze na tusikimbie majukumu yetu, tusitose wajibu wetu.

Nawapa nukuu hii kutoka Yohana.8:7-9
“Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. ”

Nawakumbusha ya kwamba, wale wanaodhani Agnes alikuwa mwovu wajichunguze mara 7 zaidi, watagundua wao ni wadhambi kuliko marehemu. Agnes ni tunda letu, na kama kuna makwazo aliipa jamii yetu basi hayo ni malezi yetu.

Binti huyu amemaliza safari yake, ametuachia mafunzo makubwa sana. Taswira yake ya ndani ya yeye na Mungu wake inaweza kuwa utukufu mkuu ambao binadamu hatuna jicho la kuuona. Kifo chake kimenigusa mno ndiyo maana nimempa heshima hii.

Mungu wa Mbinguni ampokee, amsamehe dhambi zake! Sisi tuliobaki tunajua wajibu wetu, tumsitiri, na kama hapo kabla ulisambaza picha zisizo na maadili, kama umemaliza kusoma andiko hili, zifute, maana Yesu angelikuuliza “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe”.

Mtatiro J,
(+255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com),
22/04/2018.

Wakulima wadogo wapigiwa debe kuhudhuria 88

MKUU wa Idara ya mazao ya Utafiti wa kilimo Kanda ya Mashariki, Salvatory Kundi ameiomba Serikali kutafuta njia mbadala ya kuwawezesha wakulima wadogo kufika kwa wingi katika maonesho ya wakulima ya 88 kutokana na wakulima wakubwa kufika kwa wingi tofauti na kusudio la maonesho. Anaripoti Christina Haule … (endelea).

Kundi amesema maandalizi ya sherehe za wakulima Nanenane Kanda ya Mashariki 2018 yatakayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vya Maonesho ya wakulima 88 vilivyopo Tungi nje kidogo ya mji wa Morogoro, yamekamilika.

Amesema kuwa kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakiona wakulima wakubwa na wakati kwa wingi wakifika kupata elimu katika mabanda yao tofauti na wakulima wadogo ambao ndio wengi na ndio lengo hasa la dhana ya kilimo kumyanyua mkulima mdogo.

Kundi amesema kuwa hali ya wakulima wadogo kutoonekana wengi kwenye maonesho hayo na kujipatia ujuzi wa kilimo bora inatokana na kuwepo kwa viingilio kwenye maonesho getini na gharama za usafiri kutoka mahali walipo hadi kwenye maonesho hayo.

“Utakuta mkulima anatoka kijijini na ili aweze kujifunza na kupata uelewa itabidi atumie muda kuwepo uwanjani sasa atalala wapi, atafikaje uwanjani kulingana na changamoto za usafiri na kiingilio,” amehoji Kundi.

Akizungumza kwenye upandaji vipando hivyo Mkurugenzi wa utafiti na maendeleo Kanda ya Mashariki kutoka Wizara ya Kilimo, Dk. Geoffrey Mkamilo amewataka wakulima nchini kuhakikisha wanapofika kwenye maonesho hayo wanazitumia vyema taasisi za utafiti wa kilimo zinazowekeza katika kujifunza teknolojia mbalimbali za uzalishaji wa mazao ya kilimo zinazotolewa ili waweze kuzalisha kwa tija na kuachana na kilimo cha kizamani.

Dk. Mkamilo amesema kuwa Wizara ya Kilimo ina idara ya utafiti na maendeleo ambapo inafanya shughuli za utafiti wa mazao mbalimbali ili kumwezesha mkulima kuweza kuzalisha kwa tija ambapo katika Kanda ya Mashariki yapo mazao yanayoratibiwa kitaifa na kikanda.

Ameyataja mazao ya kitaifa yanayoratibiwa na Ilonga kuwa ni pamoja na zao la mahindi katika ukanda wa chini na wakati, mazao ya jamii ya mikunde huku ya kitaifa yakiwa ni mtama ,uwele ,ulezi ,mihogo na jamii ya viazi.

Amesema kuwa katika kazi za utafiti wanaainisha teknolijia mbalimbali kwa ajili ya wakulima na wadau katika kujua teknolojia ya mbegu bora za mazao husika na pia kuwafundisha teknolojia ya usindikaji wa mazao mbalimbali ili kuweza kuwa na bidhaa mbalimbali kupitia mazao wanayozalisha.

“Teknoloji hizi zina faida kubwa kwa wakulima endapo watazizingatia kwani mbegu zinauwezo wa kuzaa kwa wingi na pia zina sifa ya kuzaa kwa muda mfupi na kuvumilia ukame na ili mkulima aweze kuona ubora wa elimu hiyo ni lazima mazao hayo yaweze kupandwa maelkezosahihi ya watafiti kulingana na muda wa upandaji,” amesema Dk. Mkamilo

Naye Mratibu wa usambazaji wa teknolojia za kilimo Kanda ya Mashariki, Margaret Mchomvu amesema kuwa wanaotesha mazao ya aina mbalimbali ili inapofika kipindi cha maonyesho ya Nanenane mazao hayo yaweze kuwa tayari yamekomaa ili kuwawezesha wakulima kujifunza kwa uhalisia sambamba na kuona namna mazao yanavyosindikwa katika mabanda yao.

Joseph Selasini aanza kusakamwa

MBUNGE wa Chadema katika jimbo la Rombo, Joseph Selasini, naye ameanza kuonja “machungu ya utawala wa Rais John Magufuli.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Taarifa zinasema, jana Selasini aligundua gari yake kufunguliwa nati zote za tairi zake mbili za nyuma.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi leo Jumapili mjini Dodoma, Selasini amethibitisha kunyofolewa nati kwenye tairi zake zote mbili.

Alisema, “ni kweli tairi zangu zimefunguliwa nati. Hili limenitokea juzi pale Africa Dream hapa Dodoma.”

Selasini amewatahadharisha wabunge wenzake kuwa makini kwa kuangalia na kuyachunguza magari yao kabla ya kuwasha na kuanza safari.

Anasema, “juzi gari yangu ilifunguliwa. Mhe Anna Gidery na Mama Roze Kamili waliniona nilipoondoka pale African Dream tairi ikicheza sana kiasi cha kutaka kutoka wakafikiri ni bearing. Walinipigia sana sikuweza kushika simu kwa kuwa huwa sipokei simu nikiwa naendesha.”

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja huku mjadala juu ya upotevu wa Sh. 1.5 trilioni ukiwa umepamba moto.

Selasini ni miongoni mwa wabunge wa upinzani nchini wanaosisitiza kufanyika kwa uchunguzi thabiti na kuitaka serikali kutolea majibu madai ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali (CAG).

Amesema, “jana sikulitumia gari hilo kwa kuwa nilikuwa katika ziara ya kamati na nilikutana na Anna akaniambia walichukuwa wameona ili niwahi garage.

“Leo nimegundua stud(nati) zote za tairi zilikuwa zimefunguliwa kiasi cha kuzizungusha kwa mkono. Hii ni hatari na inathibitisha kuwa tunatafutwa kwa njia nyingi.”

Wadau, wawekezaji watakiwa kutoilalamikia Serikali

SERIKALI imewataka wawekezadi na wadau mbalimbali kuachana na tabia ya kulalamika serikali na badala yake watoe ushauri kwa serikali ni jinsi gani ya kutatua changamoto mbalimbali. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Biashara Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Mwijage alitoa kauli alipokuwa akifungua mkutano wa wadau na wawekezaji wa pamba, bidhaa za nguo na mavazi katika ukumbi wa mikutano wa Hazina mjini hapa.

Amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazokabiliana na wizara hiyo lakini ni wakati wa wadau kutoa maoni yao ya kuishauri serikali pamoja na kuisaidia ili iweze kufanikiwa badala ya kuendelea kulalamika.

Hata hivyo amesema kwa kuzingatia kuwepo kwa sera ya serikali ya viwanda ni wakati sasa wa waekezaji kujenga viwanda ambavyo vitaweza kuzalisha malighafi ambazo zinazalishwa nchii badala ya kuuza nje na kununua bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi.

Akizungumzia zao la pamba amesema kwa kuwa wananchi na wakulima wamehamasishwa zaidi kulima pamba katika maeneo ya ukanda wa pamba ni lazima pamba inayozalishwa nchini isiuzwe nje ya nchi na badala yake ichakatwe na kuzalisha nguo na nyuzi ambazo zinaweza kutumiwa na kuzalisha bidhaa bora.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro, Siriel Mchembe, ameitaka serikali kuhakikisha inaweka mikakati ambayo inaeleweka kwa lengo la kujua soko la pamba pamoja na bei ambayo itakuwa inamanufaa kwa wakulima.

Akichangia katika mkutano huo mkuu huyo wa wilaya ambaye alikuwa amemwakilisha mkoa wa Morogoro, amesema kwa sasa wananchi wamehamasishwa zaidi kulima zao la pamba na kufikia hatua ya kuachana na kilimo cha mahindi hivyo wanatakiwa kuhakikishiwa kama pamba yao itakuwa na soko la uhakika.

“Kwa sasa wakulima wamehamasishwa sana kulima pamba imefikia hatua wapo wakulima ambao wameachana na kulima mahindi wakijua kuwa pamba itakuwa na bei nzuri, sasa ikitokea pamba ikaa haina soko au kuonekna ni chafu je wakulima hao tutawaambia nini,” alihoji mkuu huyo wa wilaya.

Naye mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Kigoma Malima amesema haiweze, mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya pamoja na wetendaji wengine wakaishi kwa kulalamika badala ya kutafuta suluhusho.

Amesema suala la uwepo wa viwanda unatakiwa kuwa na mikakati ya pamoja nadala ya kuishi kwa malalamiko na kukosa ufumbuzi na maazimio ya pamoja na kwa hali hiyo haiwezekani pakawepo na maendeleo.

ACT, CCM wameendelea kuparuana juu ya ripoti ya CAG

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeeleza kuwa uchambuzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) juu ya ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kimepotosha na kimewaahaada watanzania juu ya upotevu wa Sh. 1.5 trilioni. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Katibu Itikadi na Uenezi, Ado Shaibu amesema msimamo CCM ndio msimamo wa serikali kutokana na kuwa hicho ndicho chama tawala.

Shaibu ameeleza kuwa CCM miaka ya nyuma kilikuwa na kazi ya kuwafichua mawaziri mizigo lakini sasa kimekuwa kikisikia ripoti kama hizi kimekuwa kikumbatia maovu yanayotendwa na serikali.

Akitoa hoja tano za kukosoa uchambuzi ulifanywa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,  Humphrey Polepole.

Shaibu amesema kuwa uchambuzi wa CCM ulikuwa una kejeli na matusi dhidi ya ACT-Wazalendo, ambapo hoja dhaifu ya kuwa ni chama kidogo hakiwezi kufanya uchambuzi.

“Uchambuzi wa Ripoti ya CAG ni suala la kitalaamu halihitaji ukubwa wa chama Uchambuzi wa Ripoti hiyo unahitaji Weledi, Ujuzi na Uzoefu na sivyo kama ilivyoelezwa na Polepole,” amesema Shaibu.

Amesema kuwa Polepole amedanganya kuwa ukaguzi wa CAG ulihusu fedha zilizokusanywa na siyo mapato yaa fedha ghafi na sio fedha tarajiwa.

“CAG ameonesha kuwa Serikali ilikusanya Sh. 25.3 trilioni na kushindwa kukusanya Sh. 4.2 trilioni sawa na asilimia 14.33 ya bajeti yote ya mwaka 2016\2017.”

Shaibu amesema kuwa hakuna pesa ya Zanzibar kwenye ripoti ya CAG na kwamba ingekuwa ingeripotiwa hivyo huo ni upotoshaji kwa umma.

TCAA watakiwa kufuata kanuni za kazi

SERIKALI aimeitaka Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria za nchi katika utendaji wake wa kazi. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Hayo yalisemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasailiano Prof. Makame Mbarawa, wakati alipokuwa akizindua Baraza la wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) mjini Dodoma.

Amesema ili kufikia malengo na mafaniko ya shirika hilo ni lazima wafanyakazi wote wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria za nchi katika kutimiza majukumu yao ya kila siku.

Aidha amesema kuwa TCAA haiwezi kufanikiwa kama hapatakuwepo na uwajibikaji wa wafanyakazi wake katika kusimamia sheria na kanuni za nchi zilizowekwa.

“Kwa mwaka uliopita tu anga yetu ilitumiwa na wasafiri zaidi ya milioni 4.1 ambao walitumia anga yetu kwa maana hiyo basi kama tunataka kuongeza watu ambao wanatumia naga yetu kusafiri basi tuhakikisha tuanaendelea kusimamia kazi zetu kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi,” amesema Makame.

Vilevile aliwataka wafanyakazi wa shirika hilo kuacha kulalamikia maslahi yao binafsi wakati wanashindwa kutimiza majukumu yao waliyopewa katika nafasi zao.

“Leo hii hamuwezi kulalamikia kutaka kupandishiwa mishara wakati nyinyi wenyewe mmeshindwa kuzalisha wala hamkusanyi mapato ya kutosha,” amesema.

Amesema kama watumishi hao wa TCAA wataweza kufanya kazi kwa kujituma na kusiamamia mapato katika maeneo yao hakuana anatakeye pinga wao kupandishiwa mishahara.

“Leo hii mshindwe kukukusanya mapatao ya kutosha halafu nisikie kuwa mmepandishiwa mishara yenu nitamuondoa mara moja kwenye nafasi yake Mkurugenzi wenu mkuu Bwana Hamza maana atakua ahafai, fanyeni kazi hakuna anataye wanyima maslahi yenu,” amesisitiza Prof. Makame

Pia amelipongeza shirika hilo kwa kufanikiwa kununua Rada mpya kwa fedha zake bila kukopa benki hali ambayo katika kipindi cha nyuma ilikuwa ni vigumu.

“Rada ya mwisho kununuliwa ilikuwa ni mwaka 2002 lakini niwapongeze kwa kununua nyingine kwani mlikuwa mkitegemea serikali ndio itoe fedha kwajili ya hii rada lakini kumbe hata nyine mnaweza kwa kutumia mapato yenu wenyewe,” amesema.

Naye Mkurugenzi mkuu wa TCAA Hamza Johari amesema kuwa lengo la kuwa na baraza hilo la wafanyakazi ni kuhakikisha kuwa wanaibua mikakati mikubwa ya kimaendeleo katika sekta ya usafiri wa Anga.

Hata hivyo amesema pia katika chuo kinacho toa mafunzo ya usafiri wa anga wameendelea kupokea wanafunzi wengi kutoka nje ambao wanasaidia kuongeza mapato.

ATCL watakiwa kubadilika

WATUMISHI wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) wamewashauriwa kuchukua hatua ya kubadilika kuendana na mabadiliko yaliyopo katika usafiri wa ndege kwa sasa ili kujenga msingi thabiti wa kuonesha ushindani kwa viwango vya kimataifa. Anaripoti Christina Haule … (endelea).

Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Mkoa wa Morogoro, Lucas Mwaisaka amesema hayo kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe wakati akifunga kikao cha pili cha baraza la wafanyakazi wa shirika hilo kilichofanyika mjini hapa.

Mwaisaka amesema kuwa ni ikiwa hawatabadilika mambo yote waliyojifunza yatakuwa ni kazi bure ambapo aliyataja mambo hayo kuwa ni mbinu za kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na mbinu za kushindana kwa viwango vya kimataifa.

Aidha amesema kuwa kufuatia kauli mbiu ya ATCL kuwa ni “Tunaweza, Tubadilike” hivyo hawana budi kuchukua hatua ya kubadilika.

Hivyo ameuomba uongozi wa baraza na menejimenti ya shirika hilo kuchukua hatua za makusudi ya kuendelea kujenga uwezo wa wafanyakazi katika utekelezaji wa mambo muhimu yaliyotokana na mafunzo yaliyotolewa kwa ajili ya ustawi wa kampuni hiyo.

Hata hivyo amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha jinsi ilivyokusudia kuimarisha usafiri wa anga ili uchangie ukuaji wa utalii na uchumi wa nchi kwa kuongeza usafiri wa ndege na kufikisha ndege sita mpaka sasa ambapo aliwataka wajumbe hao kutumia fursa hiyo kuonesha kwamba wanaweza.

Naye Mkaguzi mkuu wa ndani wa ATCL Khamis Mambo amesema azma ya Rais John Magufuli imeweza kuwafanya kupiga hatua ya usafirishaji ambapo kabla ya ujio wa ndege mbili za mwanzo kampuni ilikuwa na asilimia 9.2 ya usafirishaji lakini baada ya kufikishwa wameweza kuwa na asilimia 24%.

Aidha Mambo amesema kuwa ATCL kwa sasa imeweza kubadilika na kuona namna ya kuhudumia wateja vizuri ili waweze kurudi huku ikihakikisha gharama za uendeshaji zinakuwa za chini ili wapate wateja.

Hata hivyo aliiasa jamii licha ya kutambua kuwa shirika hilo ni mali ya Umma inapaswa kutambua kuwa lazima liwe na mikakati ya kibiashara ili liweze kujiendesha.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Mawasiliano na Uchukuzi (COTWU) Taifa, Musa Mwakalinga aliiomba Serikali kuongeza mishahara kwa wafanyakazi wa shirika hilo ili kuendelea kuwajengea moyo wa kizalendo waliouonyesha tangu zamani.

Mwakalinga amesema kuwa wafanyakazi wa ATCL wamekuwa wakilalamikia kutopanda kwa mishahara yao licha ya ndege kuongezeka huku watumishi wakibaki wale wale.

“Haya ni malalamiko yao kwetu, nasi tunaelekeza kwa Serikali, nampongeza kwanza Mheshimiwa Rais kwa kuongeza na kuboresha usafiri wa ndege Tanzania lakini wafanyakazi wanaomba kuongezewa misharaha, ndege nyingi wafanyakazi wachache lakini waongezewe mishahara” alisema.

Naye Mfanyakazi wa kwenye ndege, Magreth Makwaia amesema, kufuatia mafunzo waliyopata wanaweza kuleta ufanisi mzuri katika kazi zao ikiwemo kutoa huduma nzuri kwa wateja wao na kuongeza wateja wengi zaidi ili wasiweze kwenda kwenye makampuni mengine kufuatia ushindani wa kibiashara uliopo wa sasa.

Waliotekwa Pemba wapatikana, waelezea kilichowakuta

VIJANA sita wa kijiji cha Mtambwe Mtambuuni, wilayani Wete Pemba, waliokuwa wametekwa mapema mwezi huu na watu wanaodhaniwa ni wa dola, wamepatikana. Anaripoti Jabir Idrissa … (endelea).

Vijana hao wamepatikana hai lakini hoi kwa uchovu na maumivu yatokanayo na kuteswa na watekaji wao.

Baada ya vijana watatu kupatikana wiki moja tangu walipotoweka kwao wakiwa wazima ingawa wanaonesha kufadhaika na kilichowakuta, wenzao watatu walipatikana jana wakiwa hawajitambui na waliojaa michubuko mgongoni inayoonesha walipigwa kwa kitu kama waya.

Taarifa kutoka kijijini Mtambwe Mtambuuni, zinasema hawa wa jana walikutwa maeneo tofauti msituni; wapo waliokutwa eneo la Mzambarauni, kilomita tano hivi kufika njiapanda ya Piki yalipo makutano ya barabara ya Chake-Wete na njia kuu ya kwendea Mtambwe.

Kiongozi wa Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) jimboni Mtambwe, Mohammed Khatib amesema vijana wawili ambao ni Thuweni Nassor Hemed na Khamis Abdalla Mattar walikutwa Mzambarauni.

Mwenzao aitwaye Khalid Khamis Hassan alikutwa Likoni, kando ya barabara I iendayo kisiwa kidogo cha Kojani, kilichoko kaskazini mashariki mwa kisiwa kikuu cha Pemba.

“Tumewapata hai lakini hali zao zi taabani, bila ya shaka, kutokana na mateso. Wamevimba miguu na mgongoni wana mavilio ya damu yatokanayo na kupigwa kitu kama waya,” alisema Khatibu.

“Tumewapeleka Hospitali ya Wete kwa uchunguzi na matibabu,” alisema.Taarifa za kupatikana vijana hao zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, ACP Haji Khamis Haji.

“Ninazo taarifa kuwa wamepatikana lakini kwa sasa wanafanyiwa uchunguzi hospitali ya Wete. Nitakuwa na taarifa zaidi kuhusu hali zao tukionana nao na kupata maelezo yao,” alisema.

Hospitali hiyo iliyopo mjini Wete, ni ya hadhi ya mkoa na inamilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mafanikio ya kuwapata yamekuja kwa ufuatiliaji uliofanywa na kikosi maalum cha vijana wa CUF.

“Tukiwa kwenye mizunguko ya kuwatafuta majira ya saa 8 usiku kuamkia Jumapili, tulimuona mtu kapanda baiskeli amepita kwa kasi na ghafla akatoweka tusimuone alikoelekea.

“Tulipofuata upande aliokimbilia ndipo tukakuta watu wawili wamelala kwenye majani kama wametupwa hivi. Kumbe ndio wenzetu waliotekwa,” alisema Khatibu kwa lugha nyepesi akionesha huzuni.

“Wamechoka na wamejeruhiwa na kudhoofika miili. Hawawezi kuzungumza kitu na miguu yao imevimba kiasi cha kutoweza kusimama,” alisema.

Thuweni Nassor Hemed, alikutwa Likoni, karibu na njia ya kwenda Kojani kisiwani.Kaka yake, Said Nassor Hemed, amesema haki ya ndugu yake “si nzuri. Hawezi kuongea; amepoteza uzito na mgongoni amejaa michubuko ya kupigwa kwa kutumia waya.”

“Yeye na wenzake wanatoka damu wanapojisaidia haja kubwa na ndogo. Hatujajua hasa kilichowasibu,” alisema.

Watu waliodhaniwa ni askari wa Usalama wa Taifa wakitumia gari mahsusi za serikali walifika Mtambwe Mtambuuni usiku wa saa 4 tarehe 4 Aprili mwaka huu na baada ya kuufunga mtaa na kupekua nyumba baada ya nyumba walitoweka na vijana sita wenye umri wa kati ya miaka 16 na 31.

Vijana watatu walipatikana pamoja siku nne baadaye kwenye kijiji cha Kengeja, Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba. Hali za vijana hao ambao wadogo kwa umri kuliko wenzao watatu, si mbaya.

“Hatukuteswa mwilini lakini tulihojiwa mara kwa mara masuala yasotuhusu kabisa. Waliotuhoji walijificha usoni na wakati mwengine sisi tulifungwa vitambaa usoni ili tusi wajumbe,” alinukuliwa mmoja wao akisema.

Hili ni tukio la kwanza la utekaji wa staili hiyo kwa Zanzibar katika kipindi cha karibuni cha kushamiri kwa matukio kama hayo Tanzania Bara. Matukio maarufu kwa Zanzibar ni yale yanayohusu askari wa vikosi vya SMZ kushambulia kqa vipigo wananchi nyakati za usiku.

Katikati ya mwaka jana, askari hao waliopachikwa jina la mazombi, walimuua Ali Juma, aliyekuwa ofisa habari na uenezi wa CUF wilaya ya Magharibi B.

Mazombi walimchukua baba huyo wa watoto 19 mkaazi wa Maoni Kidatu mjini Zanzibar chumbani kwake baada ya kuvunja mlango wa nyumba yake na kuingia ndani usiku.

Walimshambulia mbele ya familia yake na kuondoka naye huku wakimtupia matusi. Ali alipata fahamu alfajiri akiwa msitu wa Masingini, nje kidogo ya mji. Alipata msaada kwa kuchukuliwa na wachunga ng’ombe waliomkuta akilalama kwa maumivu.

Alifariki dunia siku iliyofuata kutokana na majeraha. Alipata kujieleza akisema alihujumiwa makusudi kwa sababu za kisiasa. “Tunadhulumiwa kwa kweli lakini nawaambia wenzangu tusikubali dhulma namna hii,” ilikuwa kauli ya mwisho akiwaeleza viongozi wa CUF waliofika nyumbani kwake kumkagua.

Polisi walisema hawakuripotiwa rasmi tukio hilo.

CCM wamtelekeza Mzee Makamba

JANUARY Makamba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira ametoa madai mazito kwa chama chake, kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemtelekeza baba yake Mzee Yusuph Makamba akiwa mgonjwa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Makamba ameandika ujumbe huo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, akielezea hali ya baba yake kiafya na kusema pamoja na kupitia hali hiyo lakini CCM hakimpi stahiki zake kama mstaafu wa chama hicho.

Mzee Makamba ameshika nafasi mbalimbali katika chama lakini kikubwa zaidi ni kuwa Katibu Mkuu cha chama hicho, pamoja na nafasi mbalimbali serikalini ikiwemo Mkuu wa mikoa mbalimbali ukiwemo Dar es Salaam.

Katika taarifa hiyo ya January pia imeeleza tuhuma za wanasiasa aliowalea Mzee Makamba ambao mmoja wao kwa sasa anasema maneno mabaya dhidi ya mzee huyo.

Soma andiko la January hapa chini:

Majuzi nilienda kumjulia hali Mzee Makamba ambaye anaumwa. Mazungumzo yake yalihusu watoto wake aliowalea kisiasa, ambapo mmoja wapo, pamoja na kumhifadhi na kumfariji wakati kasahaulika, sasa anasema maneno mabaya dhidi yake.

Tukazungumzia subira na uvumilivu kwenye siasa. Akaamua kunipa kisa kifuatacho:

Mwaka 1980, baada ya kutoka vitani, alipangwa kuwa Katibu Msaidizi wa CCM Dodoma. Mwaka 1982, wakati wa kuadhimisha miaka 5 ya kuzaliwa kwa CCM kimkoa kule Mvumi, alitumwa mnadani Mwitikira kununua kitoweo (ng’ombe na mbuzi) kwa ajili ya sherehe.

Baada ya muda, akiwa kahamishiwa Monduli, akapewa barua ya kusimamishwa utumishi na uongozi (u-NEC) wa CCM kwa tuhuma kwamba wale ng’ombe na mbuzi wa sherehe aliwaswaga kwetu Bumbuli badala ya kuwapeleka Mvumi.

Tukafungasha mizigo na kurudi kijijini. Wakati Mzee anaendelea kutafuta maisha kijijini alikuwa anaandika barua kila siku Ikulu kwa Mwalimu Nyerere kueleza kwamba ameonewa. Baada ya barua kadhaa, Mwalimu akaagiza aitwe kwenye kikao cha Kamati Kuu Chamwino Dodoma. Mzee aliwasili Dodoma akiwa kachoka sana, amebeba makabrasha yake kwenye mfuko wa rambo.Makambazzz

Kikao kilipoanza, Mwalimu akampa nafasi Mzee Makamba ya kujieleza. Mzee akaanza kwa kusema ana hoja nyingi kuonyesha kaonewa lakini angependa kuanza na swali dogo: “Kwenye ile sherehe, Ndugu Moses Nnauye alikuwa mgeni rasmi na alikula ubwabwa. Ndugu Mwenyekiti, naomba aulizwe iwapo ubwabwa ule aliokula ulikuwa na nyama au la.” Mwalimu akamgeukia Nnauye na kumuuliza “Moses, Yusuf anauliza iwapo ubwabwa uliokula ulikuwa na nyama.” Nnauye akasimama na kujibu “Mwenyekiti, ubwabwa ulikuwa na nyama.” Mzee akaendelea “iwapo niliswaga ng’ombe kijijini kwetu, hiyo nyama kwenye ubwabwa ilitoka wapi?” Mwalimu akawageukia watendaji waliotengeneza mashtaka ili watoe majibu. Kukawa hakuna jibu. Baada ya Mzee kujieleza tena kwa kifupi ikadhihirika wazi kabisa kwamba kulikuwa na uonevu mkubwa. Akarudishwa kazini.

Wakati Mzee ananipa kisa hiki, alikuwa anajichoma sindano ya “insulin” kudhibiti kisukari, huku akigusa jicho lake moja ambalo linakaribia kuwa pofu. Amegoma kabisa kutibu jicho akisema “hata likiacha kuona, sio tatizo kabisa; limeshaona mengi humu duniani”

Kwa sasa Mzee hali yake kiafya sio nzuri chama cha mapinduzi hakimpi stahiki zake kama mstaafu.
January Makamba

Mbunge wa Chadema ang’ang’aniwa Polisi

MBUNGE wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema) ameshikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam (Central) kwa madai amebakishwa kwa ajili ya upelelezi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Bulaya aliripoti leo kituoni hapo baada ya kutakiwa kufanya hivyo, akiongozana na Viongozi wengine wa Chadema akiwemo Mwenyekiti, Freeman Mbowe ikiwa ni moja ya sharti la dhamana yao katika kesi inayowakabiri.

Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji amesema kuwa baada ya kuripoti kituoni hapo viongozi wote waliruhusiwa kuondoka lakini Bulaya alitakiwa kubaki kwa sababu ya upelelezi.

“Mbunge Bulaya amebaki mahabusu kwa sababu za kiupelelezi lakini tumeambiwa ataunganishwa katika shauri letu lililokuwa mahakamani Kisutu,” amesema Mashinji.

 

Hata hivyo ameeleza kuwa upelelezi utakapokamilika Bulaya atafikishwa mahakamani na kuunganishwa katika shauri la viongozi wengine ambao walishafikishwa mahakamani.

Kuripoti kwa viongozi hao ni moja ya sharti la dhamana katika kesi yao namba 112/2018 katika mahakama ya Kisutu Dar es Salaam.

Lissu kupasuliwa kwa mara nyingine

TUNDU Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), muda huu atafanyiwa upasuaji mwingine katika mguu wake wa kulia, ikiwa ni mara ya 20 tangu alipoanza kutibiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Lissu amesambaza ujumbe katika mitandao ya kijamii ulioeleza: “Napenda kuwajulisha kwamba ndani ya nusu saa ijayo ninaingia kwenye operesheni nyingine tena.”

Amesema madaktari wamebaini bakteria katika mguu wake wa kulia ambao uliumizwa sana, hivyo wameamua kumfanyia upasuaji ili kuwaondoa.

Operesheni hiyo inayofanyika nchini Ubelgiji ni ya 20 baada ya ile ya 19 ilifanyika mwezi Machi mwaka huu ikiwa ni mwendelezo wa matibabu aliyokuwa akifanyiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikopelekwa akitokea Dodoma baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7, mwaka jana.

Lissu amesema baada ya operesheni huo atafanyiwa upasuaji mwingine baadaye wa kuunga mfupa. “Niseme tu naendelea vizuri sana. Ninawashukuru Watanzania kwa kunitibu, kwani wenye jukumu la kufanya hivyo wamekataa lakini Watanzania hawajanitupa.”

Wanamichezo Jumuiya ya Madola ‘wazamia’

WANAMICHEZO nane wa Cameroon hawaonekani katika makazi yao katika michezo ya Jumuiya madola nchini Australia, maafisa wa timu hiyo wamethibitisha. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Afisa wa habari wa timu ya Cameroon, Simon Molombe amesema kutoonekana kwa wanariadha hao wanaamini wametoroka na kwamba wameripotiwa kwa maafisa wa polisi nchini humo.

Amesema wanyanyua vyuma vya uzito watatu na mabondia watano walionekana mara ya mwisho katika muda tofuati Jumatatu na Juamnne.

Cameroon imesema kundi la wanariadha hao wana viza halali za kudumu hadi Mei 15.

Wanamichezo waliotoweka kambini ni pamoja na Olivier Matam Matam, Arcangeline Fouodji Sonkbou na Petit Minkoumba, wanaonyanyua vyuma vya uzito na mabondia Christian Ndzie Tsoye, Simplice Fotsala, Arsene Fokou, Ulrich Yombo na Christelle Ndiang.

Serikali ya Australia imewaonya wanariadha dhidi ya kukaa zaidi ya muda walioruhusiwa.

Shirikisho la michezo hiyo ya Jumuiya ya madola limesema litaikagua hali hiyo, lakini limeongeza kwamba wanariadha wana “haki ya kusafiri kwa uhuru” kwa viza walizo nazo.

Polisi ya Australia imejulishwa kuhusu hali inavyoendelea, kwa mujibu wa Kate Jones, waziri katika jimbo la Queensland.

Mch. Msigwa aweka rehani ubunge wake kisa Makonda

MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amesema yupo tayari kujiuzuru ubunge wake kama itathibitika kuwa amemtelekeza mtoto kwa mwanamke mmoja jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwanadishi Wetu … (endelea).

Mch. Msigwa ametajwa na mwanamke mmoja kati ya walioripoti katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa ametelekeza mtoto.

Makonda ametoa nafasi kwa wanawake waliotelekezwa na wanaume waliowazalisha, ndipo mwanamke huyo ambaye hajatajwa jina lake alifika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa na kueleza kuwa amezalishwa na mbunge huyo na kumtelekeza bila matunzo yoyote.

Katika taarifa yake, Mch. Msigwa amesema kinachoelezwa kuwa ametelekeza mtoto jijini na mwanamke huyo ni propaganda za makusudi zenye lengo la kujaribu kumchafua.

Msigwa amesema: “Kama huyo mama ambaye jina lake limehifadhiwa yupo, nataka ajitokeze pamoja na mtoto niliyemtelekeza. Kwa sasa nipo Dodoma Bungeni; anaweza kunipata kupitia Spika wa Bunge au Katibu wa Bunge au Kiongozi wa Upinzani Bungeni.”

Mbunge huyo amesema kama ikithibitika kuna mtoto amemtelekeza yupo tayari kujiuzuru Ubunge.

 

Mbunge wa CCM aikaba serikali

MBUNGE wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) ameihoji serikali na kutaka ieleze ni lini itaana ujenzi wa kituo cha polisi na nyumba za askari. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Nkamia aliihoji serikali leo bungeni wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa kutaka kujua serikali ina mpango gani wa kujenga kituo cha polisi wilayani chemba pamoja na nyumba za askari.

“Wilaya ya Chemba haina Kituo cha Polisi, Je ni lini serikali itaanza ujenzi wa kituo cha polisi na nyumba za askari,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masaun, amesema kuwa ni kweli jeshi la polisi lina uhaba wa vituo vya polisi pamoja na nyumba za kuishi askari kote nchini ikiwemo wilaya ya Chemba.

“Ili kutatua changamoto hiyo jeshi la polisi linashirikisha wananchi wa eneo husika pamoja na wadau wengine wa maendeleo ili kufanikisha azma ya serikali ya kujenga vituo vya serikali vya kisasa vya polisi pamoja na nyumba za kuishi za askari hao,” amesema Masaun.

Naibu Waziri huyo amesema Wilaya ya Chemba jeshi la polisi ka kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, wananchi na wadau wengine wapo kwenye hatua za awali za kuanza ujenzi wa kituo cha polisi.

“Kwa sasa mchoro wa ramani ya kituo na gharama za ujenzi (BOQ) vimeisha kamilika na ukusanyaji wa mahitaji ya ujenzi unaendelea,” ameeleza Masaun.

Wafanyabiashara wa ng’ombe watishia kugoma

WAFANYABISHARA wa mifugo wanaopeleka katika machinjio ya kisasa ya Kizota mkoani Dodoma wametishia kuacha biashara hiyo baada ya kuibuka kwa faini kubwa mbalimbali kutoka Wizara ya Uvuvi na Mifugo zinazotozwa kwao. Anaripoti Christina Haule … (endelea).

Wakizungumza na waandishi wa habari, wafanyabiashara hao wamesema kuwa kumekuwa na faini mbalimbali wanazotozwa kutoka kwa watumishi wa wizara hiyo ambazo ni kati ya sh. 500,000 hadi sh. milioni moja au zaidi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mmoja wa wafanyabiashara hao, Joseph Mazengo ambaye husafirisha mbuzi kutoka Singida kuleta katika machinjio hiyo amesema kuwa yeye binafsi alitozwa sh. milioni moja kwa kukosa kibali cha kusafirishia mbuzi kati ya 100 na 120.

Amesema kuwa fani hizo hutozwa katika kituo cha mifugo Kizota ambako mifugo yote inayoingia katika mkoa wa Dodoma inalazimika kupitia katika kituo hicho.

Amesema mbali ya kutozwa kiasi hicho cha fedha bado alitozwa faini nyingine kabla ya kufikisha mbuzi hao kwa ajili ya kuchinjwa katika kiwanda hicho.

Mfanyabiashara huyo amesema wao ununua mbuzi vijijini na kisha kuwaleta kiwandani hapo ambako kuna mwekezaji ambaye ununua na kisha kuchinja na kusafirisha nyama hiyo nje ya nchini kwa oda maalum.

“Sisi tunanunua mbuzi ili kuja kuwauza kwa makampuni ya wawekezaji ambao nao uchinja na kuuza nje lakini sasa kumekuwa na faini hata kama namba ya gari imekosewa katika kibali unatozwa hadi sh. laki tano hii si sahii sisi wenyewe hatuna mitaji hata hawa mbuzi tunachukua kwa mali kauli,

“Sisi hatukatai kama kuna utaratibu kama huo tungepewa taarifa mapema ili nasi tujitayarishe na si kutukurupusha sasa tusipo leta hawa mbuzi huyu mwekezaji atapata wapi mbuzi wa kuchinja na kila siku mna sema kuwa mnaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji sasa haya ni mazingira mazuri kweli,’’ amesema.

Mfanyabiashara mwingine aliyejulikana kwa jina la Anthony Methew amesema inashangaza kwani hata wakitaka kuuliza swali kwa wahusika hao wamekuwa wakali na kuhitiwa askari na kukemewa kuwa hakuna swali hapa ni fani tu.

Amesema hali hiyo iliwafa baadhi yao kwenda hadi kwa katibu Mkuu wa Wizara hiyo naye alituombea tupunguziwe faini jambo ambalo wanahoji kama ni kweli faini hiyo ipo kisheria suala la kuonewa huruma linatoka wapi.

Mfanyabiashara huyo amesema kuwa jambo kubwa linalowashangaza mara baada ya kulipa faini hiyo wamekuwa wakiandikiwa risiti za serikali zile za zamani za karatasi na siyo za kieletroniki kama serikali ilivyo sema hivi karibuni kuwa malipo yote yawe katika mfumo wa kieletroniki.

Katika machinjio yao kuna jumla ya makampuni matano ya wawekezaji ambao ununua mbuzi hao na kuchinja kisha kuunza nyama nchi za nje ikiwemo kampuni ya Mkonga A, Bongo Export, Sunchoice, Saudi Park. na Smartfedha Export.

Akizungumzia hali hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mary Mashingo amesema kuwa Wizara yake haitamfumbia macho mtumishi wake yeyote atakayeenda kinyume na taratibu zilizowekwa katika ukaguzi wa mifugo.

Amesema wizara yake itafuatilia kama kuna malalamiko yeyote ili kubaini tatizo ni nini lakini aliwaasa wafanyabishara nao kuzingatia taratibu katika kusafirisha mifugo ili kuepuka faini zisizo za lazima.

Vifaa tiba visivyofaa vyakamatwa mitaani

SERIKALI imesema kuwa imefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali ambavyo ni dawa na vifaa tiba ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu, katika vituo vya tiba za asili. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Mafanikio hayo yalitokanana Operesheni iliyoandalikwa kutokana na kuwepo kwa taarifa za matumizi ya vifaa tiba aina ya Magnetic Quantum Analyzer na vingine vinavyofanana na hivyo kwenye vituo vya tiba asili na tiba mbadala kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa na matangazo ya vifaa hivyo yanayopotosha umma.

Amesema kuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliandaa na kufanya ukaguzi maalum wa kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219 na Sheria ya Dawa Asili na Mbadala ya mwaka 2002 hususan uuzaji, usambazaji, matumizi na matangazo ya vifaa tiba vinavyotumika katika tiba ya kuchua, uchunguzi wa magonjwa na vifaa vingine vinavyodaiwa kuondoa sumu mwilini.

Akitoa taarifa hiyo Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia na Watoto Dk. Faustin Ndungulile amesema kuwa Kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219 vifaa tiba kwa ajili ya matumizi nchini, ni lazima viwe vimesajiliwa au kutambuliwa na Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) baada ya kufanyiwa tathmini ya taarifa za kisayansi za kuthibitisha ubora, usalama na ufanisi wake.

Amesema Operesheni hiyo ilifanyika sambamba katika mikoa kumi na moja ambayo ni Dar es salaam (Kinondoni, Ilala, Temeke, Ubungo, Kigamboni), Morogoro (Kilombero), Singida (Manispaa), Arusha (Manispaa), Kilimanjaro (Moshi), Mbeya (Jiji, Mbalizi, Tukuyu), Rukwa (Manispaa), Kigoma (Kasulu, Manyovu), Mwanza (Nyamagana, Ilemela), Kagera (Bukoba) na Mtwara (Manispaa) kwa muda wa siku mbili, kuanzia 6 hadi 7 Machi, 2018.

“Operesheni ililenga kukagua vituo vyote vilivyosajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na vituo vingine kadri ilivyopatikana kwa kuzingatia taarifa za kiintelijinsia zilizofanyika awali,” amesema Dk. Ndungulile.

Amesema jumla ya maeneo 115 yalikaguliwa wakati wa operesheni hiyo ambapo vituo 39 vikiwa vya mkoa wa Dar Es Salaam, 6 Morogoro, 6 Singida, 10 Arusha, 5 Kilimanjaro, 15 Mbeya, 5 Rukwa, 6 Kigoma, 14 Mwanza , 3 Kagera na 6 Mtwara.

Akiendelea kutoa ufafanuzi wa Operesheni hiyo Dk. Ndungulile amesema jumla ya vifaa tiba 395 vyenye thamani ya shilingi 51,116,000/- na dola za kimarekani 2,768 vilikamatwa.

Amevitaja vifaa hivyo vilivyokamatwa kuwa ni Quantum Magnetic Analyser 53, Massagers 40, Detoxifier 18, Cybrow Urinary Stick 1, BP Machine 19, Blood Glucose Meter 2, Ultrasound 1, Acupuncture needles 176, Ion Cleanse 2, Elecromagnetic Bed 20, Homeopathic Electronic Radionic Machine 4, Stetoscope 2 na vifaa vingine 57.

Amesema sambamba na bidhaa hizo kukamatwa operesheni hiyo imebaini kuwepo kwa mapungufu makubwa katika utekelezaji wa Sheria ya Tiba Asili na Tiba mbadala ya mwaka 2002 pamoja na Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219 katika vituo vingi vilivyokaguliwa.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa ukaguzi huo umebaini kuwepo kwa matumizi makubwa ya vifaa vinavyojulikana kama Quantum Magnetic Analyzer katika kupima magonjwa mbalimbali na Detoxifier inayodaiwa kuondoa sumu mwilini.

Aidha, kupitia matangazo yanayotolewa kwenye vituo husika, ukaguzi umebaini upotoshaji mkubwa kwa jamii, kuwa vifaa husika vina uwezo wa kupima au kutibu magonjwa makubwa kama vile saratani, hepatitis, ovarian cysts.

Alisema katika baadhi ya maeneo yaliyokaguliwa, wakaguzi walibaini huduma za upimaji wa HIV, Malaria, Sukari na Pressure zikitolewa huku kukiwa hakuna wataalamu wenye fani husika.

Amesema kutokana na matokeo ya Operesheni hiyo, hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ambapo jumla ya majalada 52 ya kesi tayari yamefunguliwa katika vituo mbalimbali vya polisi dhidi ya watuhumiwa na vituo 50 vimefungwa.

Dk. Ndungulile amevitaja idadi ya vituo, idadi ya kesi na vituo vilivyofungiwa kwa mkoa wa Dar es Salaam idadi ya vituo vilivyofungwa ni 16 na idadi ya madalada ya kesi ni 16.

Amesema mkoa wa Singida vituo vilivyofungwa ni vitatu na majarada ya kesi ni matatu kwa mkoa wa Arusha vituo vilivyofungiwa ni saba na majarada ya kesi saba, mkoa wa Kilimanjaro hakuna kituo kilichofungiwa lakini majarada ya kesi ni vituo mbili.

Vituo vingine alivitaja kuwa ni Mbeya vituo vilivyofungwa ni 11 na vyenye majarada ya kesi ni 11, katika mkoa wa Rukwa vituo vilivyofungiwa ni vinne na vyenye majarada ya kesi ni manne, mkoa wa Kigoma kituo kimoja kimefungiwa huku vituo vitatu vikiwa na majarida ya kesi, katika Mkoa wa Mwanza vituo vitatu vimefungiwa na hakuna kituo chenye jarida la kesi, mkoa wa Kagera vituo vilivyofungiwa ni viwili na vyenye majarida ya kesi ni mawili na Mkoa wa Mtwara vituo vilivyofungiwa ni vitatu na vituo vyenye majarida ya kesi ni manne na kufanya jumla ya vituo vyote vilivyofungiwa ni 50 na vyenye majarada ya kesi kuwa 52.

Aidha amesema baada ya uchunguzi wa makosa kukamilika hatua mbalimbali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani watuhumiwa na kutoa adhabu kulingana na Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219 na Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya mwaka 2002.

Amesema adhabu hizo zinajumuisha kufuta leseni ya biashara, kuwafutia usajili wataalamu, kuondoa kwenye soko na kuharibu vifaa husika.

“Napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa taasisi zilizoshiriki kwenye operesheni hii ikiwemo Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Chakula na Dawa, kwa kutambua umuhimu wa zoezi hili kwa maslahi ya Taifa.

“Aidha, napenda kuchukua nafasi hii kupiga marufuku uingizaji, usambazaji na matumizi ya vifaa vinavyodaiwa kupima magonjwa mbalimbali kama Quantum Magnetic Analyzer, Detoxifier n.k kutokana na ukweli kuwa usalama na ufanisi wa vifaa hivyo haujathibishwa. Waingizaji wanaagizwa kuwasilisha TFDA taarifa za kisayansi za kuthibitisha ubora, usalama na ufanisi kupitia mfumo wa usajili ili ziweze kutathminiwa,” amesema Dk. Ndungulile.

Katika taarifa hiyo Dk. Ndungulile alitoa wito kwa umma na wananchi kwa ujumla kuwa makini na taarifa za upotoshaji zinazotolewa hususan matumizi ya vifaa hivyo ambavyo havijathibitishwa na TFDA ili kulinda usalama wa afya zao.

Mch. Msigwa ayamwaga bungeni aliyoyaona Segerea

MBUNGE wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) amedai Tanzania kwa sasa kuna msongamano mkubwa wa wafungwa ambapo amehoji Serikali inachukua hatua gani kupunguza msongamano huo. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Akiuliza swali la nyongeza jana bungeni Msigwa alidai kuwa gereza la Segerea limezidiwa na mahabausu ambapo lina uwezo wa kuchukua mahabusu 700, lakini waliopo kwa sasa ni mahabusu na wafungwa  2400.

“Ukienda katika Magereza zetu kuna msongamano mkubwa sana kwa mfano Gereza la Segerea ambalo nililipitia juzi lina uwezo wa kuchukua mahabusu 700 lakini sasa hivi lina mahabusu na wafungwa 2400.

“Wanalazimika watu kulala upande mmoja mmoja kwa zamu baada ya muda inapigwa ‘alarm’ kisha mnageukia upande mwingine huu ni ukiukwaji kabisa wa haki za binadamu na watoto wengi wapo pale chini ya umri wanatakiwa waende shule.

“Ni kwanini Serikali imekuwa ikipeleka wanasheria kutetea kesi za Serikali ambao wamekuwa wakilazimisha wale ambao wanaweza kupata dhamana waende kukaa mahabusu kama ambavyo kesi zetu zilikuwa zina dhamana lakini mawakili wa Serikali walikuwa wanalazimisha tuende kule tukaongeze msongamano,” ameuliza Msigwa.

Akijibu kwa niaba ya Serikali, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema kuwekwa ndani kwa muda mrefu kwa mahabusu siyo kweli kwamba Serikali haitaki kesi hizo zimalizike haraka.

“Sababu za msingi ni sababu ya usalama wao, wakienda nje wanaweza wakapata matatizo ikiwemo Serikali kuwalinda pili kuna watuhumiwa wakitoka nje wataenda kuharibu ushahidi,” amesema

Naye, Mbunge wa Tarime Mjini Ester Matiku (Chadema) katika swali lake la nyongeza aliitaka serikali iwaachie kina mama ambao wamefungwa huku wakiwa wanaumwa.

“Nimekuwa Segerea Mheshimiwa Spika kule kuna wamama wamefungwa wanadaiwa mathalani 150,000 lakini amefungwa miezi sita kwa gharama ambazo amezitoa Naibu Waziri zinavuka mpaka 200,000.

“Kwanini Serikali isitumie busara kwa kina mama ambao wengine wana watoto wachanga wanafungwa kwa kesi ya shilingi 100,000 mpaka 200,000 na Serikali inatumia gharama kubwa katika gharama za chakula,” amehoji Matiko.

Akijibu swali hilo, Ole Nasha amesema suala hilo ni la kisheria hivyo kama Mbunge anaona hoja hiyo inamashiko apeleke hoja binafsi bungeni.

Akiongezea majibu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba, alisema hawawezi kuwaacha wahalifu nje kutokana na kuogopa Magereza kujaa.

“Niweke kumbukumbu sawa sio kila Magereza yana msongamano tuna baadhi ya Magereza katika mikoa ile ambayo kiwango cha uhalifu ni mdogo mfano Lindi na kule Mlalo,” amesema

Mfungwa mmoja kutumia laki moja kwa siku

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema gharama za chakula kwa mfungwa mmoja kwa siku ni wastani wa shilingi 1,342. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Hayo yalielezwa leo bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamadi Masauni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Njombe Mjini, Edward Mwalongo (CCM).

Katika swali hilo Mwalongo alitaka kujua Serikali inatumia kiasi cha shilingi ngapi kuhudumia mfungwa mmoja kwa siku kwa ajili ya chakula.

 “Vitendo kama kulala chini, kulala bila blanketi au shuka vimekuwa vya kawaida kabisa katika Magereza yetu. Je hii nayo ni sehemu ya adhabu ambayo wafungwa wanapewa kwa mujibu wa sheria,” alihoji Mbunge huyo.

Akijibu, Masauni amesema Jeshi la Magereza katika kutekeleza majukumu yake pia hutoa huduma ya chakula kwa wahalifu kupitia bajeti iliyotengwa na Serikali kila mwaka wa fedha.

Naibu Waziri huyo amesema gharama za chakula kwa mfungwa mmoja kwa siku ni wastani wa shilingi 1,342.

Amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za wafungwa na mahabusu kwa kununua vifaa mbalimbali vya malazi ikiwemo, magodoro shuka, mablanketi na madawa ya kuua wadudu.

Mbunge Chadema amvaa waziri wa mifugo

MBUNGE wa Tarime Mjini, Ester Matiko (Chadema) amehoji serikali ni kwanini Mnada wa Magena umefungwa licha ya kuwa na miundombinu yote. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Akiuliza swali jana bungeni,Mbunge huyo alidai kuwa mnada huo uliopo halmashauri ya Mji wa Tarime una miundombinu yote licha ya kufungwa na Serikali bila sababu maalumu.

Mbunge huyo alidai mwaka 2016 aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, alitembelea mnada huo na kuagiza ufunguliwe.

“Je ni kwanini mnada huo haujafungiliwa mpaka sasa ili kutoa fursa za ajira na kuokoa mapato yanayopotea,” amehoji Matiko.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema mnada wa Magena ulikuwa kati ya minada 10 ya mipakani.

Amesema mnada huo ulikamilika kujengwa mwaka 1995 na kufunguliwa mwaka 1996 ambapo ulifanya kazi kwa takribani mwaka mmoja ambapo ng’ombe 104,000 waliuzwa na jumla ya Sh. 260 milioni zilikusanywa kama maduhuli ya Serikali.

Naibu Waziri huyo amesema kutokana na changamoto zilizojitokeza ikiwemo wizi wa mifugo na sababu za kiusalama kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Mara mwaka 1997 iliagiza mnada huo ufungwe.

“Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Mkoa wa Mara uliiomba Wizara ya Maendeleo ya Mifugo ya wakati huo ifute mnada wa Magena na Kirumi Check Point iteuliwe kuwa mnada wa mpakani kwa kuwa tayari kuwa kizuizi cha Mto Mara,” amesema.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amesema Wizara ilikubali ombi la uongozi wa mkoa wa Mara na hivyo ikaanza kujenga mnada eneo la Kirumi sehemu ambayo kuna kizuizi asili cha Mto Mara.

Amesema ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 80 na unatarajiwa kufunguliwa mwaka huu mara baada ya kukamilika ujenzi wa kituo cha Polisi cha kuweka umeme.

Wanachuo waaswa kutotegemea kuajiriwa na Serikali

VIJANA wengi wanaomaliza elimu ya juu wanatakiwa kuachana na fikra za kutaka kuajiriwa na serikali na badala yake wafikirie kutumia elimu yao kwa lengo la kubuni miradi mbalimbali ambayo itawawezesha kujiajiri wenyewe. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Mbali na hilo imeelezwa kuwa bila wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kupatiwa elimu ya stadi za maisha ni vigumu kufikia mapinduzi ya kiuchumi kwenye jamii inayowazunguka.

Kauli hiyo imetolewa mara baada ya kubainika idadi kubwa ya wanafunzi wa elimu ya juu pindi wanapohitimu masomo wanashindwa kutumia taaluma yao kuanzisha miradi ya kiuchumi badala yake wanasubiri kuajiriwa.

Akizungumza juzi mjini hapa kwenye mafunzo maalum ya stadi za maisha yaliyotolewa kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Taasisi ya Green Hope, Manjala Makongoro kwa ushirikiano wa kampuni ya simu za mkononi Vodacom, amesema elimu kuhusu stadi za maisha itamwezesha mwanafunzi kujitambua.

Amebainisha kuwa lazima mwanafunzi wa elimu ya juu kujitambua thamani yake kwenye jamii, hivyo anapaswa kuitumia taaluma yake kama njia ya kuondokana na utegemezi wa kiuchumi.

“Mwanafunzi mwenye kujitambua anapaswa kuwa na tabia ya kujitathimi kwa kila jambo analolifanya kama lina maslahi kwake na kwenye jamii.

“Pia lazima awe mwenye uthubutu wa kufanya maamuzi ya kuachana na jambo ambalo anaona halina maslahi kwake na kutafuta njia bora za kumwezesha kufikia malengo aliyoyakusudia,” ameeleza.

Mwezeshaji huyo amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom, imeamua kutoa mafunzo hayo ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwajengea uelewa vijana waweze kutumia fursa zilizopo kuleta mapinduzi ya kiuchumi.

“Serikali imekuwa ikisisitiza mapinduzi ya viwanda lakini kama wanafunzi wa vyuo vikuu wakikosa ufahamu kwenye stadi za maisha zitakazowawezesha kujiajili, kundi hilo litaachwa nyuma, ” amesema.

Naye Meneja wa Vodacom mkoani Dodoma, Balikulile Mchome, amesema mafunzo hayo yameonyesha kufanikiwa kwani wanafunzi wamekuwa na shauku ya kutaka kufahamu masuala mbalimbali yatayowawezesha kujitegemea kiuchumi baada ya kuhitimu masomo.

“Vijana wameonyesha kuwa na shauku ya kuwa wajasiliamali. Kwetu sisi ni mafanikio kwani kile tulichokilenga kimeonyesha mafanikio,” amesisitiza.

Naye Mooren Minja, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza anayesomea shahada ya elimu chuoni hapo, amesema mafunzo hayo yamewawezesha kujijengea uwezo wa kujitathimi na kubaini namna ya kukabiliana na changamoto za kiuchumi.

Amesema elimu ya stadi za maisha ni muhimu kwa wanafunzi kwani itamjengea wigo wa kuchanganua mambo yatakayowezesha kufikia lengo alilolikusudia hususan kufikia hatua fulani ya maendeleo.

Rais Magufuli amtumbua Mkurugenzi

RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa, Mohamed Maje kuanzia leo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Akitoa taarifa ya utenguzi huo mjini Dodoma, Katibu Mkuu wa Tamisemi, Alhaji Mussa Iyombe amesema kuwa Maje ameisababishia serikali hasara ikiwemo kushindwa hata kukusanya mapato ya serikali.

Utenguzi wa Maje umetokana na taarifa iliyotolewa na tume iliyoundwa kukagua utendaji wake wa kazi nakubaini kuwa ameshindwa kusimamia na kudhibiti mapato ya halmashauri hali iliyopelekea upotevu wa fedha.

“Hadi kufikia robo tatu ya mwaka wa fedha halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa imekusanya mapato kwa asilimia 24 tu pamoja nakuwa halmashauri hiyo ni kongwe na yenye vyanzo vingi vya mapato,” amesema Iyombe.

Hatua hii imekuja baada ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk. Bilineth Mahenge kuagiza kuundwa kwa tume ya mkoa kuchunguza ubadhilifu wa fedha zaidi ya Sh. 500 milioni katika halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa pamoja na kubaini sababu za halmashauri hiyo kuwa ya mwisho katika ukusanyaji wa mapato.

Akizungumza katika kikao cha ushauri wa mkoa (RCC) Mahenge alionyesha kusikitishwa na matokeo hayo pamoja na kuwa wilaya Kongwe nayenye vyanzo vingi vya mapato kukusanya asilimia 24 pekee ya mapato hivyo kupelekea kuchukuliwa hatua kwa watendaji wote wanaokwamisha ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Hata hivyo Mahenge alisisitiza uadilifu kwa watendaji ikiwa ni pamoja na kupeleka mashine za kukusanyia mapato katika kata.

“Ukusanyaji wa mapato ya ndani ni muhimu sana katika halmashauri kwani ndio hutumika katika shughuli za maendeleo,ukuaji na ustawi wa halmashauri,” amesema Mahenge.

Wambura ashindwa rufaa, sasa kuburuzwa mahakamani

KAMATI ya Rufaa za Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetupilia mbali rufaa ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura, hivyo adhabu aliyopewa na Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo itaendelea. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Wambura alifungiwa kutojihusisha na kujishughulisha na masuala ya mpira wa miguu maisha yake yote na Kamati ya Maadili ya TFF kwa makosa matatu ikiwemo la kupokea au kuchukua fedha za shirikisho hilo kwa malipo ambayo hayakuwa halali.

Akisoma hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa za Maadili ya TFF, Ebenezer Mshana amesema wamesikiliza pande zote mbili za mrufani na mjibu rufani na kuzitupilia mbali rufaa zote za Wambura kutokana na kutokuwa na hoja za msingi.

Mshana amesema rufaa ya Wambura iliyopelekwa mbele ya kamati yao haina mashiko hivyo wameridhia adhabu aliyopewa katika Kamati ya Maadili kama ilivyoamuliwa ya kufungiwa maisha kujihusisha na soka.

Pia Mshana ameshauri TFF kupeleka tuhuma zilizomtia hatiani Wambura zipelekwe katika vyombo husika ili hatua nyingine zaidi zichukuliwe.

Mshana amesema mawakili wa mrufani walijikita zaidi katika hoja za mteja wao kutopewa nafasi ya kusikilizwa lakini hawakuwa na hoja hata moja ya kupinga mashtaka yaliyomtia hatiani katika Kamati ya Maadili.

Makosa mengine yaliyomtia hatiani Wambura mbali na kuchukua fedha za TFF, ni kugushi barua alipwe fedha za kampuni ya Jeck System na kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya shirikisho hilo.

 

Shule, Vyuo binafsi walalamikiwa rushwa ya ngono

SERIKALI imesema kuwa baadhi ya Mameneja, Wakurugenzi pamoja na wamiliki wa shule binafsi na vyuo wanalalamikiwa kwa vitendo vya rushwa ya ngono hasa wakati wa kutoa ajira kwa walimu hususani jinsia ya kike. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Elimu, Joseph Kakunda alipokuwa akifunga mkutano wa Shilikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali (TAMONGSCO) uliofanyika kitaifa mjini hapa.

Kakunda amesema kwamba licha ya kuwa shule za binafsi pamoja na vyuo vinamchango mkubwa katika jamii pamoja na serikali kuzitambua lakini yapo maeneo yanayolalamikiwa ikiwa ni pamoja na masuala ya rushwa.

“Yapo maeneo ya rushwa hasa katika rushwa ya ngono ni jambo la aibu hata hivyo wanaume wengi ndio wanaoongoza kuomba rushwa ya ngono,wanawake wengi wa Afrika hasa wa Kitanzania wanajiheshimu sana hivyo wanaume igeni mfano wa wanawake wengi.

“Rushwa ya ngono imekuwa ikilalamikiwa hasa wakati wa kipindi cha uombaji wa ajira najua siyo shule zote wala vyuo vyote vya binasi lakini kwa baadhi ya wanaofanya hivyo wanatakiwa kuacha mara moja kwani ni aibu kuwepo kwa vitendo hivyo,” amesema Kakunda.

Akizungumzia kuwepo kwa shule binafsi Kakunda amesema kuwa wapo baadhi ya Mameneja na Wamiliki ambao wanaendesha shule hizo kama biashara kwa kutoza ada kubwa na kusababisha hata wale waliopakana na shule hizo kushindwa kujiunga na shule hizo kutokana na kiwango kikubwa cha ada.

Kutokana na hali hiyo amewataka mameneja na wamiliki kurudi katika mwongozo wa sera ya elimu na mazingira ya usawa na uwezeshaji na isiwe katika misingi ya kibiashara.

“Zipo shule zenye majina makubwa kalini watoto wa jirani na shule hizo hawasomi hapo, hata mameneja na wamiliki hawatembelei wazazi na kuwaelezea mikakati ya shule zao na bei za ada wanazotoza hata kuwashawishi kuwa wanaweza kutoa ada kwa awamu ngapi ili kuwashawishi wazazi hao kuwa na mwamko wa kusomesha watoto katika shule hizo,” amesema Kakunda.

Katika hatua nyngine hakusita kuzungumzia baadhi ya shule binafsi kushindwa kutoa mikataba ya ajira kwa watumishi wao ikiwa ni hatua moja wapo ya kutowaingiza katika mifuko ya jamii watumishi hao jambo ambalo amesema ni ukiukwaji wa misingi ya utoaji wa ajira.

Amesema kutokana na hatua hiyo serikali haitasita kuwachukulia hatua wamiliki na mameneja watote ambao watakiuka utoaji wa mikataba kwa watumishi wao ikiwa ni pamoja na kutowapa fursa ya kujiunga katika mifuko ya kijamii.

Kakunda pia amekemea baadhi ya shule pamoja na vyuo binafsi ambavyo vinajiendesha bila kuwa na bodi ikiwa ni pamoja ya kuwafukuza wanafunzi bila kufuata utaratibu alisema kuwa pia zipo ambazo hazifuhati mihura rasmi ya serikali jambo ambalo kiongozi huyo alisema kuwa halikubaliki.

Shonza aitwa mahakamani kesho

MAHAKAMA ya Hakim Mkazi mkoani Dodoma imemuagiza naibu waziri wa utamaduni, Sanaa na michezo, Juliana Shonza, kufika mahakamani kwa “hiari kesho” Ijumaa, vinginevyo itatoa amri ya kukamatwa na kufikishwa mbele ya mahakama kwa nguvu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Agizo hilo limetolewa kufuatia Shonza kushindwa kufika mahakamani
kutoa ushahidi kwenye kesi ya jinai aliyoifungua dhidi ya mbunge mwenzake, Saed Kubenea.

Katika kesi hiyo Na.8 ya mwaka 2018, Kubenea anatuhumiwa kumshambulia Shonza kwa kinachoitwa, “kitu chenye bapa,” jambo ambalo amedai limemsababishia maumivu makali na kuteguka viongo.

Kubenea amekana madai hayo na kuongeza, “yote yaliyoelezwa yamesheheni siasa za maji taka.”

Serikali watilia shaka uraia wa Abdul Nondo

MWENYEKITI wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo ameitwa Makao Makuu ya Uhamiaji kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu uraia wake. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Sheria wa TSNP, Paul Kisabo imeeleza kuwa Nondo ametakiwa kwenye ofisi hizo ili kuhojiwa kuhusu uraia wake na ndugu zake.

”Kwa muda wa takribani wiki moja mpaka sasa Nondo amekuwa akihitajika Uhamiaji ili akahojiwe kuhusu taarifa za uraia wake pamoja na za ndugu zake,” imeeleza taarifa hiyo.

Leo Nondo alifika katika ofisi hizo na kuhojiwa baada kutoka kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam alipokwenda kusikiliza kesi yake anayowashataki Mkuu wa Upelelezi, Mwanasheria Mkuu pamja na Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa kuchelewa kumpeleka makahamani.

Mnamo saa sita mchana tuliweza kumfikisha Abdul Nondo Makao Makuu ya ofisi za Uhamiaji mkoa (makao makuu ya wizara ya mambo ya ndani)
Tulipata kuhoji alichoitiwa na anachotakiwa kujaza katika fomu aliyopatiwa.

”Tuliambiwa wanataka kupata taarifa zake binafsi, za wazazi wake, babu na bibi zake pande zote mbili (upande wa baba na upande wa mama)
pamoja na za ndugu zake, kwani Afisa uhamiaji mkoa alitamka kuwa sheria inawaruhusu kumuhoji mtu yeyote wanaotilia mashaka uraia wake na kuwa wanamashaka na uraia wa Abdul Nondo, hivyo awathibitishie kuwa yeye ni Raia wa Tanzania”

Baada ya hapo afisa uhamiaji aliyekabidhiwa jukumu la kumhoji Abdul Nondo alisema kwamba Apliri 20, 2018 Abdul Nondo anapaswa kupeleka cheti chake cha kuzaliwa, cheti cha kuzaliwa cha baba yake, mama yake, cha bibi na babu mzaa baba na mzaa mama.

Dk. Abbasi: Waandishi msiogope, kosoeni serikali

DAKTARI Hassan Abbasi, Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO amewataka waandishi wa habari nchini kufanya kazi zao kwa uhuru, bila uoga kwani serikali ipo tayari kupokea maoni ya ukosoaji. Anaripoti Charles William … (endelea).

Dk. Abbasi amesema hayo hii leo jijini Dar es Salaam, katika sherehe za waandishi wa habari waliohitimu mafunzo chini ya ufadhili wa taasisi ya Tanzania Media Foundation (TMF), ambapo alikuwa mgeni rasmi.

“Wakati tunatengeneza Sheria ya Huduma za Habari, miongoni mwa vifungu nilivyopigania kiwepo kilikuwa ni kifungu cha 52 (2) kinachosema hakuna kosa kwa mtu anapokosoa serikali.

“Msiogope kukosoa, tuambieni tunakosea wapi, semeni tunakosea wapi labda kwenye sekta ya viwanda au kwingine na sisi tutafanyia kazi. Usitukane wala kukashifu mtu, usikosoe lakini kwa kusema uongo. Pia kuna mambo yanayohusu usalama wa Taifa lazima yazingatiwe.”

Dk. Abbasi ameipongeza TMF kwa kutoa mafunzo kwa waandishi ili waweze kubobea katika habari za uchunguzi za maendeleo pamoja na eneo la usalama wa barabarani, na kuwataka kutumia ujuzi waliopata kuisaidia serikali kwa kukosoa na kufichua mambo mbalimbali.

Fausta Musokwa, Kaimu Mkurugenzi wa TMF amesema taasisi hiyo itaendelea kutoa mafunzo na ruzuku kwa waandishi na vyombo vya habari ili waweze kuandika habari zitakazosaidia uwazi na uwajibikaji serikalini.

“Taasisi yetu ilianza mwaka 2008 kama mfuko wa wanahabari, mpaka sasa tumetoa mafunzo ya ubobezi (fellowship) kwa waandishi zaidi ya 120 na tutaendelea kufanya hivyo.”

Halima Shariff, mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya TMF amewataka waandishi kutochoka kufanya uchunguzi na kuibua mambo mbalimbali kwa maslahi ya nchi na wananchi pamoja na changamoto zinazowakabili.

Jumla ya waandishi 14 wamehitimu mafunzo yaliyokuwa yakiendeshwa na TMF kwa miezi sita kutoka Juni mpaka Januari mwaka 2018. Waandishi tisa wamehitimu mafunzo ya ubobezi ya kuandika habari za maendeleo na watano wamebobea katika uandishi wa habari za usalama barabarani.

Mbowe na wenzake wakamilisha dhamana, waachiwa huru

MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake sita akiwemo Halima Mdee, Mbunge wa Kawe aliyeunganishwa katika kesi hiyo leo, wamekamilisha masharti ya dhamana hivyo wakati wowote wanaweza kuachiwa huru. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imejiridhisha na nyaraka walizoziwasilisha wadhamini kwa ajili ya dhamana ya washtakiwa hao na imewakubalia kuwadhamini huku ikiwapa maelekezo kuhakikisha kuwa wanapatikana mahakamani kila wanapohitajika.

Masharti ya dhamana yao ni kusaini bondi ya Sh 20 milioni  kuwa na wadhamini wawili wenye barua kutoka ofisi za Serikali za mitaa au vijiji na kuripoti kituo kikuu cha Polisi kila Alhamisi.

Mbali ya Mbowe wengine ni Katibu Mkuu Dk Vicent Mashinji, manaibu katibu wakuu John Mnyika (Bara), Salum Mwalimu (Zanzibar), Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa na Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake wa chama hicho, Ester Matiko  na Mwenyekiti wake, Halima Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe, wanaokabiliwa na kesi ya jinai, wakidaiwa pamoja na mambo mengine ikiwamo kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali.

Kabla ya Mdee kupata dhamana pamoja na wenzake mawakili wa Serikali wapinga mahakama kumpa dhamana Mdee kwa sababu kabla hajafikishwa mahakamani alipewa dhamana Polisi lakini hakukidhi masharti kwa kushindwa kuripoti polisi wasema wanahofu akipewa dhamana ya mahakama hataweza kutimiza wajibu wake.

Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri hakukubaliana na madai ya mawakili wa Serikali kwani Mahakama haiwezi kumnyima mshtakiwa dhamana kwa sababu aliruka dhamana ya polisi kwa kuwa hizo ni taasisi mbili tofauti na haziwezi kuingiliana.

Kesi hiyo itatajwa tena Aprili 16, 2018. Watuhumiwa hao walikuwa mahabusu tangu walipopandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo Machi 27 mwaka huu, 2018.

Tume huru itasaidia kuepusha uhasama, visasi baada ya uchaguzi

MJADALA juu ya umuhimu wa katiba mpya na “tume huru ya uchaguzi nchini,” bado ungali mbichi. Anaandika Saed Kubenea … (endelea).

Ubichi huu unatokana na ukweli kwamba serikali ilipuuza ushauri wa tume tatu tofauti zilizoundwa na marais Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, na Jakaya Kikwete, kuwashauri juu ya masuala mbalimbali ya kikatiba.

Tume iliyoongozwa na Jaji Mkuu Francis Nyalali kuhoji Watanzania kama wanataka chama kimoja au vyama vingi vya siasa mwaka 1991, katika moja ya mapendekezo yake ilizungumzia umuhimu wa katiba mpya na “tume huru ya uchaguzi.”

Katika ripoti hiyo, Jaji Nyalali alitoa mifano ya nchi kadhaa ambazo zilizokuwana tume za uchaguzi zisizo huru.

Alionya kuhusu madhara yanayoweza kutokea iwapo taifa lingekosa chombo huru cha kusimamia uchaguzi. Alisema tume huru ya uchaguzi ingeweza kuepusha mauaji, machafuko, kudidimia kwa uchumi wa taifa, njaa na maradhi.

Katika ibara ya 591 ya ripoti yake, Jaji Nyalali alisisiza: “Ni lazima muundo wa tume ya taifa ya uchaguzi ubadilike, ili kukidhi haja ya demokrasia ya vyama vingi.” Hakusikilizwa.

Jaji Robert Kisanga, aliyeongoza tume ya rais ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu maeneo mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi mwaka 1998, naye alitaja katiba mpya na tume huru ya uchaguzi kama moja ya mambo ya lazima.

Alisema uteuzi wa wajumbe wa tume, kwamba si sahihi wao kuteuliwa na rais – ambaye ni kiongozi wa chama cha siasa kinachotawala.

Mantiki ni kwamba kwa kuwa wengi wanaoteuliw anaye ni wafuasi wa chama wake, ama watakuwa na upendeleo kwa chama chake au watalipa fadhila kwa aliyewateuwa.

Aliseme kuwa wakati mwingine, rais anakuwa mmoja wa wagombea katika uchaguzi unaofuata. Chama chake kina wagombea kwenye nafasi mbalimbali. Hakuna shaka kuwa wasimamizi hao watajiegemeza kwenye chama cha aliyewateua. Hawakumsikiliza.

Katika mchakato wa katiba mpya ulioshinikizwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mwaka 2011, hatimaye Rais Kikwete akaunda tume ya mabadiliko ya katiba, suala hili lilijitokeza tena.

Soma makala kamili kwenye gazeti lako la SMATI la kesho Jumanne – MHARIRI

Polisi wamshikilia Halima Mdee na ugonjwa wake

JESHI la Polisi limemkamata Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na kuendelea kumshikiria hadi sasa pamoja na kuwa mgonjwa. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mdee alikamatwa leo alfariji akitokea Afrika Kusini alipokuwa amelezwa. Pamoja na daktari kuwathibitisha Polisi kuwa Mdee ni mgonjwa.

Polisi wanamshikiria Mdee wakitaka kumjumuisha katika kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine watano ambao watafikishwa mahakamani kesho kutwa.

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA KWA UMMA-KUKAMATWA KWA MHE. HALIMA MDEE (MB)

Leo Jumapili tarehe 01 Aprili 2018, majira ya saa tisa alfajiri Mhe. Halima Mdee (Mb) alikamatwa akiwa uwanja ndege wa Dar Es salaam alipokuwa amerejea nchini akitokea Nchini Afrika Kusini alipokuwa anapatiwa matibabu.

Mpaka mchana wa leo tarehe 01 Aprili, 2018 Jeshi la Polisi wameendelea kumshikilia Katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam na hajapatiwa dhamana pamoja na daktari wake kuwathibitishia polisi kuwa Mheshimiwa Halima ni mgonjwa.

Tunasikitishwa na kulaani kitendo hiki cha Polisi kuendelea kumshikilia mgonjwa ambaye alikuwa amelazwa hospitalini.

Tunatoa mwito kwa Jeshi la Polisi limpatie dhamana ili aweze kuendelea na matibabu yake, Kwani dhamana ni haki yake na zaidi ni kuwa huyu bado ni mtuhumiwa na ni Mgonjwa ambaye ametoka hospitalini.

Mwisho Jeshi la Polisi litawajibika kwa watanzania endapo afya ya Mhe. Halima Mdee ikitetereka au ikidhoofu zaidi na lawama zote zitakuwa juu yao.

Imetolewa Leo Jumapili tarehe 01 Aprili, 2018

John Mrema – Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje – CHADEMA