Majaliwa: Bakwata acheni kugombania vyeo

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Kasimu Majaliwa, amewataka viongozi na waumini wa dini ya Kiislamu nchini kuacha kugombania vyeo na misikiti badala yake waimalishe umoja, amani na mshikamano ndani ya dini ya Uisamu. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Majaliwa alitoa kauli hiyo leo wakati alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa kikatiba wa Baraza la Waislamu Tanzania  (Bakwata) uliofanyika mjini Dodoma.

Amesema kuwa ni wakati wa viongozi pamoja na waumini wa dini ya kiislamu kukaa pamoja na kujipanga katika kufanya masuala ya kimaendeleo badala ya kutumia muda mwingi kugombania vyeo na umiliki wa misikiti jambo ambalo alisema aliufanyi uislamu kuwa na afya.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, amesema kuwa pia viongozi wa dini hiyo kwa kushirikiana na viongozi wa dini nyingine wanatakiwa kukemea baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakifisadi mali ya Umma au mali za dini.

Amesema jukumu kubwa la viongozi wa kidini ni kuhakikisha wanawafundisha waumini wao kuwa na hofu ya kimungu ili kufanya kazi bila kufisadi mali za Umma au mali za dini zao na badala yake wawe na uzalendo wa nchi na mali zao.

Katika hatua nyingine Majaliwa aliitaka Bakwata kuhakikisha inahakiki mali zake zote ili ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Suleiman Jafo, amewata viongozi wa dini hiyo kuhakikisha wanasaidia serikali pamoja na wananchi kwa ujumla kwa kufanya shughuli za kimaendeleo.

Jafo amesema ni wakati sahihi kwa dini ya kiislamu kuwekeza katika masuala mazima ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na sekta ya Afya, elimu na kiuchumi.

“Kutokana na serikali kujikita katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wote, ni wajibu sasa wa viongozi wa dini kuwaimiza waumini wao kutunza miundombinu ya barabara, rasilimali fedha pamoja na kulinda umoja wa dini zote za kiislamu,” amesema Jafo.

Naye Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Ali amesema kwa sasa wamejaribu kuirudisha Bakwata kwa waumini wa dini ya kiislamu tofauti na ilivyokuwa hapo awali kwa maana ya kuwa mbali na waumini wa dini hiyo.

Amesema kwake ni mara ya kwanza kufanyika kwa mkutano mkuu wa Bakwata ambao ni mkutano wa kikatiba na hiyo inatokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali ambazo zilikuwepo.

Mufti amesema licha ya kuwepo kwa changamoto ya kifedha lakini baraza liionekana kuwa mbali na waumini wa dini hiyo jambo ambalo lilimewafanya viongozi pamoja na waumini kutokuwa tayari katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo.

Akizungumzia kuhusu mali za Bakwata amesema kuwa kwa sasa baraza hilo linaendelea kufuatilia mali zake na kuzirejesha huku wakiendelea kutatua migogoro mbalimbali ya ndani na kuendelea kujienga mahusiano mazuri katika dini zote ndani ya uisilamu pamoja na mahusiano mazuri kwa nchi rafiki ya Morocco.

“Mwelekeo wa Bakwata katika siku za usoni ni kufanya kila linalowezekana ili kuongeza imani ya waislamu kwa Bakwata na viongozi wake kwa ngazi zote, kukuza uwezo wa Baraza kutoa huduma za afya, elimu ya dini na sekula kwa kutengeneza mtandao mpana wa mashule, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu.

“Kuongeza uhusiano mwema na nchi na taasisi za kitaifa na kimataifa ili tusaidiane nao kukuza uwezo wa kiuchumi na kitaaluma, kujenga uwezo wa kudumu kiichumi ili kuiwezesha Bakwata kukidhi mahitaji ya wafanya kazi na waislamu kwa ujumla, kujenga tawi la chuo kikuu cha Al azhar shariif kwa kushirikiana na taasisi ya Alaz har Sharif ya nchini misri pamoja na kusambaza mtandao wa vyuo vya Darul maarif kila mkoa na wilaya nchi nzima,” amesema Mufti Mkuu.

Bavicha wajitosa kulinda hatma ya Chadema

BARAZA la Vijana la  Chadema (Bavicha) limejiapiza kukulinda chama chao kwa gharama yeyote kwa kile walichodai ni hujuma za kutaka kukifuta na kufungwa kwa viongozi wa chama hicho. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi amesema kuwa vijana wa Chadema ndiyo walinzi wa chama hicho ambapo ameahidi kupitia vijana hao chama kitalindwa dhidi ya hujuma.

Amesema kuwa chama hicho kipo kwenye hujuma zilizopangwa makusudi ili chama tawala ambacho ndicho chama dola ambacho kimetani kibaki chama kimoja.

Ole Sosopi amesema kuwa kushikiliwa kwa viongozi wa juu wa chama hicho ni sehemu ya mkakati huo ambapo ameeleza jinsi viongozi hao walivyokamatwa na kufikishwa mahakamani kimya kimya ikiwa muda umeenda hadi kukosa dhamani kuwa ni mkakati wa kuwafunga.

Amesema kuwa hujuma hizo zimemuibua msajili wa vyama vya siasa ambaye amekuwa akitumia mwamvuli huo kutaka kukihujuma chama kwa kutishia kukifuta.

Amemtaja Cyprian Musiba ambaye amekuwa akiwatukana na kukashifu viongozi wa chama hicho bila kuchukuliwa hatua yoyote kisheria ilhali anavunja sheria ambapo anaonekana kuwa sehemu ya mkakati huo.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa hawatarudi nyuma kwenye uamuzi watakao uwelekeza kwa wafuasi vijana wa chama hicho.

“Bavicha iliyopo chini yangu sio ile ya Katambi (Patrobas) lakini hata kipindi kile mimi ndiye niliyekuwa nikihamasisha hatua kadhaa kwenye chama. Bavicha hii haitarudi nyuma,” amesema Ole Sosopi.

Wakati huohuo, Ole Sosopi amesema viongozi na wafuasi wa chama hicho wataenda mahabusu kuwafariji na kusherehekea pamoja Sikukuu ya Pasaka kwenye gereza la Segerea jijini Dar es Salaam na gereza la Ruanda Mbeya alikofungwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.

Wabunge wanusurika kifo katika ajali ya gari

WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamepata ajali ya gari jana usiku mkoani Morogoro wakati wakitokea Dodoma kuelekea Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Baada ya kutokea ajali hiyo saa 2 usiku katika barabara kuu ya Morogoro-Dodoma eneo la Bwawani, wabunge hao waliumia maeneo mbalimbali ya miili yao na kukimbizwa hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

Wabunge hao ambao wote ni kutoka Zanzibar ni Haji Ameir Haji (Makunduchi), Khamis Ali Vuai (Mkwajuni), Bhagwanji Maganlal Meisuria (Chwaka), Makame Mashaka Foum (Kijini), Juma Othman Hija (Tumbatu).

Mganga mfawidhi hospitali ya rufaa Mkoa wa Morogoro, Dk Rita Lyamuya amesema majeruhi hao walipokelewa saa 3 usiku na kupatiwa huduma za awali.

“Jana tumepokea majeruhi sita walioumia sehemu mbalimbali na mmoja wao alilazimika kulazwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) lakini hali yake inaendelea vizuri,” amesema.

“Leo asubuhi tayari tumewapa rufaa kwenda hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi  zaidi.” Dk Rita amesema Kimbe na May ndio wameumia zaidi, kupata maumivu makali.

Mbowe na wenzake wapata dhamana, kuachiwa Machi 3

HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Wilbard Mashauri amewapa dhamana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake watano bila ya kuwepo mahakamani. Anaripoti Jabir Idrissa … (endelea).

Hakimu Mashauri ametoa maamuzi hayo bila ya washitakiwa kuwepo mahakamani kutokana na kushindwa kuletwa kutoka gereza la Segerea walipokuwa mahabusu kwa madai gari liliharibika.

Mashauri amesema dhamana kwa watuhumiwa hao ipo wazi kwa masharti ya kusaini bondi ya Sh. 20 milioni kila mmoja pamoja na wadhamini wawili.

Viongozi hao waliokuwa mahabusu pamoja na Mbowe, ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Kabla ya kutoa uamuzi huo Hakimu Mashauri alipinga madai ya magereza ya kushindwa kuwaleta washtakiwa mahakamani kwa madai ya kuharibikiwa na gari, hivyo alilazimika kutoa uamuzi bila ya yao kuwepo na taratibu nyingine zitafuata.

Baada ya Hakimu Mashauri kusikiliza hoja za upande wa Serikali na utetezi katika kesi inayowakabili viongozi wa Chadema, amesema washtakiwa hao kuletwa mahakamani hapo Aprili 3, 2018 ili kutimiza masharti ya dhamana.

Chadema waishtaki Serikali ya JPM Umoja wa Ulaya

WABUNGE na Madiwani wa Chama cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameishitaki SErikali ya Tanzania kwa Umoja wa Ulaya juu ya hali ya kisiasa na kushinikiza kupatiwa dhamana viongozi wa chama hicho pamoja na kutahadhalisha usalama wa viongozi hao. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Viongozi hao waliongozwa na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbles Lema, Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, Joseph Haule mbunge wa Mikumi. Wengine ni Boniface Jacob, Meya wa Ubungo, Patrick Ole Sosopi, Mwenyekiti wa Bavicha na wengine zaidi ya 30.

Viongozi wa chama hicho walikosa dhamana Machi 27, 2018 baada ya viongozi serikali kuzuia dhamana zao.
Lema aliyeongoza msafara huo alisema kuwa wataomba hati tahadhari kwenye ubalozi huo.

Amesema kuwa chama hicho kitawaomba ubalozi huo kusiishie tu kutoa matamko ya kupinga kinachoendelea nchini bali waende mbele zaidi na kwa kuchukua hatua stahiki.

Wabunge na Madiwani wa Chadema wakiwa katika mkutano na Ubalozi wa Umoja wa Ulaya
Wabunge na Madiwani wa Chadema wakiwa katika mkutano na Ubalozi wa Umoja wa Ulaya

Lema amesema kushikiliwa kwa viongozi wao kunatoa tafsiri kuwa chama chote kimefungwa gerezani licha kuwepo mkakati wa serikali kukifunga chama hicho.

Wakati Wabunge na Madiwani wa Chadema wakiwa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya, kesi ya viongozi wao inaendelea Makahama ya Kisutu bila ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani hapo.

Hakimu Mkazi, Wilbard Mashauri anasikiliza kesi hiyo na kutoa uamuzi wake juu ya dhamana yao. MwanaHALISI Online itawajuza kinachoendelea.

Mawakili, Hakimu kutoa hatima ya kutoletwa Mbowe na wenzake

MAWAKILI wa pande zote mbili wa kesi zinazowakabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake wamekutana na Hakimu Mkazi, Wilbard Mashauri kujua hatma ya watuhumia hao kutofika mahakamani mpaka sasa. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mbowe na viongozi wengine watano walitarajiwa kufikishwa mahakamani leo asubuhi ili kutolewa maamuzi juu ya dhamana yao ikiwa pamoja na kupangwa tarehe ya kuanza kusikilishwa mashtaka yao yanayowakabili, lakini mpaka mchana walikuwa hawajafikishwa mahakamani hapo.

Pamoja na Mbowe, viongozi wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko

Baada ya kutokea mkanganyiko juu ya kutofikishwa mahakamani kwa viongozi hao sita wa Chadema, mawakili wa upande wa mashtaka na wale wanaowatetea watuhumiwa, walilazimika kumfuata hakimu anayesikiliza kesi hiyo, ambaye ametoa ahadi ya kutoa maamuzi muda mchache ujao.

Mawakili wa pande zote mbili wamekubaliano na mahakama, kuwasiliana na Magereza ili kujua sababu ya kushindwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao na kujua kama wanaletwa leo au hawaletwi, au mahakama iendeleea kusoma uamuzi wa dhamana hiyo.

Pande zote mbili zimekubaliana kukutana baada ya kufanya mawasiliano hayo ili kupata mrejesho na kujua hatua gani zinafuatwa.

Mahakamani hapo kulifurika umati wa watu wengi wakiwemo wafuasi wa Chadema waliokuwa na kiu ya kusikiliza kesi ya viongozi wao, hali iliyosababisha ulinzi kuimarishwa huku wakiwazuia wafuasi hao kuingia mahakamani.

baadhi ya viongozi wa Chadema waliofika mahakamani hapo ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa na Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, pamoja na wabunge na madiwani wa chama hicho.

Kutokana na kuchelewa kwa watuhumiwa hao kuwasilishwa mahakamani hapo baadhi ya viongozi walilazimika kuondoka ambapo Lowassa na Sumaye walielekea katika mazishi ya mmoja wa waasisi wa chama hicho, Victor Kimesera, wakati wabunge na madiwani wakielekea ofisi za Umoja wa Ulaya.

Watoto wa Rungwe wapatikana

WALE watoto wa Mzee Hashim Rungwe akiwemo mpwa wake wa kike, waliokuwa hawaonekani kwao, “wameachiwa.” Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Rungwe, mfanyabiashara mkubwa nchini na kiongozi wa Chama cha Umma, amesema vijana hao wamerudi nyumbani.

“Aah… wamewaachia. Naona wameturidhia na kutusikiliza,” ni maneno machache aliyoyatoa punde hivi kwa Mhariri wa MwanaHALISI, Jabir Idrissa, kwenye vipenu vya Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.

“Wamewaachia tayari. walikuwa nao huko,” alikazia kauli yake. Hakueleza zaidi mazingira ya kupatikana kwa watu wake,” amesema Rungwe.

Rungwe ni wakili wa kujitegemea nchini na amefika Mahakama ya Kisutu kikazi.

Aliulizwa na Idrissa baada ya kuchomoza ghafla mahakamani Kisutu ambako Mhariri alikwenda kuhudhuria kesi ya tuhuma za uchochezi kuhusu alichokiandika katika gazeti la MAWIO Januari mwaka juzi.

Kesi hiyo iliyokwama kusikilizwa kwa sababu ya kutokuwepo kwa Tundu Lissu ambaye ni mtuhumiwa wa nne, inawahusu pia Simon Mkina, Mhariri Mtendaji na Ismail Mehboob Meneja wa kiwanda cha uchapaji magazeti cha Flint.

Kwa mara nyingine leo kesi hiyo imetajwa na kuahirishwa kwa ombi la upande wa mashtaka ambao unaeleza mtuhumiwa Lissu yuko nje ya nchi anaumwa.

Wakili wa Serikali ameiambia mahakama leo kuwa wanawasiliana na DPP ili “kuona njia nzuri ya kufanya kumaliza shauri hili.”

Hakimu Thomas Simba alisema hiyo ni hatua nzuri kufuatwa kwani kesi ina mazingira yanayoelezeka. Itatajwa tena tarehe 30 Aprili mwaka huu.

Sakata la kina-Mbowe, Chadema kukutana, kutoka na mazito

KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wabunge na Madiwani wa chama hicho wanakutana kujadili sakata la Mwenyekiti na viongozi waandamizi wa chama hicho kukamata na kahidi kutoka na maamuzi mazito. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Lengo la mkutano huo ni kujadili mustakabali wa demokrasia nchini pamoja na kukamatwa kwa viongozi waandamizi wa chama hicho ikiwa pamoja na mipango iliyosukwa na Serikali kuhusiana kesi inayowakabiri.

Jana Mwenyekiti, Freeman Mbowe, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara, Vincent Mashinji, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salimu Mwalimu, Mch. Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa na Ester Matiko, Mbunge wa Tarime walishtakiwa na kupelewa rumande baada ya kukosa dhamana hadi kesho hakimu atakapotoa uamuzi wa dhamana yao.

Makamo Mwenyekiti wa Chadema, Prof. Abdallah Safari amesema kesho wakitoka mahakamani kusikiliza hatma ya dhamana ya viongozi wao watakutana kujadili mustakabali wa demokrasia ndani ya nchi yao.

Prof. Safari amesema kikao hicho kitajumuisha Kamati Kuu ya Chadema, Wabunge na Madiwani na baadaye watatoa uamuzi mzito kama chama nini cha kufanya kwa kile kinachoendelea nchini kuhusasi demokrasia nchini.

“Kushikiliwa kwa viongozi wa ngazi za juu wa chama pinzani imevunja rekodi ya historia ya siasa Afrika. Sidhani katika Afrika ilishawahi kutokea tukio kama hili, ukiacha lile la mwaka 1999. Hii ni rekodi mbaya tunaiweka Tanzania,” amesema Prof. Safari.

Prof. Safari amesema wanajua malengo ya serikali kwa viongozi wao, lakini wao hawatakubaliana na mipango inayoendelea, mkutano wao utatoka na maamuzi magumu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amesema kuwa kushikiliwa kwa viongozi hao wa juu kabisa wa chama chao ni makakati wa kuwafunga kama Mbunge wa mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.

Lema amesema kuwa zipo taarifa kuwa viongozi hao kesho wanawaweza wakakosa dhamana na baadaye kesi hiyo kuendeshwa haraka haraka ili wafungwe.

Hiki ndicho kilichowakwamisha Mbowe na wenzake

VIONGOZI wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaendelea kusota rumande kwa hoja kwamba, wanaweza kuhatarisha usalama wa jamii. Anaandika Faki Sosi…(endelea).

Hoja hiyo imewasilishwa jana na mawakiwa wa Jamhuri mbele ya Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam dhidi ya viongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema; Vincent Mashinji, Katibu Mkuu; John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara; Salumu Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar; Easter Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini; Pater Msigwa, Mbunge Iringa Mjini walifikishwa katika Mahakama ya Kisutu jana kwa madai ya kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT), Akwilina Akwiline na kurudishwa rumande.

Madai mengine ni pamoja na kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali, uchochezi na kusababisha chuki katika jamii, uchochezi wa uasi, pia ushawishi wa utendekaji wa kosa la jinai.

Hatua ya kunyimwa dhamana kwa viongozi hao kumesababisha kuendelea kukaa mahabusu kwa siku mbili.

Hatua hiyo imetokana na mawakili hao wa serikali kuwasilisha hoja kwamba, wakiachwa kwa dhamana, watuhumiwa hao wanaweza kuhatarisha usalama wa jamii.

Hata hivyo, pingamizi hilo lilipingwa na jopo la mawakili wa utetezi liliongongozwa na Mwanasheria mwandamizi wa Chadema, Pater Kibatala.

Hakimu Wilbard alisikiliza hoja za pande zote mbili kwenye kesi hiyo ambapo alisema kuwa, atatoa uamuzi wa kupewa dhamana au kutopewa kwa watuhumiwa hao kesho Machi 29 mwaka huu.

“Kifungu cha 392 (A) cha mwenendo wa makosa ya jinai kinaturuhusu kuomba kuzuiliwa kwa dhamana ya washtakiwa kwa kuzingatia maslahi ya jamii na haki zao,” alisema Dk. Zainabu Mango, Wakili wa Serikali na kuongeza;

“Dhamana ni haki yao lakini hakuna haki isiyokuwa na wajibu, kila mtu anawajibu wa kutii sheria za nchi kutumi haki ya mtu mmoja kunapaswa kuzingatie haki za watu wengine.”

Amedai kuwa, makosa wanayoshtakiwa nayo viongozi hao yanaweza kuhatarisha usalama wa jamii na taifa kwa ujumla na kwamba, kupewa kwao dhamana kunaweza kuhatarisha usalama wa umma wa Tanzania.

Wakili huyo amedai kwamba, kupewa dhamana viongozi hao kunaweza kusababisha hatari ya kuendelea kufanya makosa kama hayo.

Faraja Nchimbi ambaye pia ni Wakili wa Serikali alisema, matamshi yaliyotolewa na viongozi hao yalisikika na yanaendelea kusikika ambapo yanaweza kuhatarisha amani.

Nchimbi amedai kuwa, zipo taarifa za kiupelelezi kuwa, matamko ya viongozi hao yamesababisha kutekelezwa kwa matukio ya uhalifu.

Wakili Kibatala anayetetea watuhumiwa ameieleza Mahakama kuwa, hakuna hoja ya kisheria kutoka kwa mawakili wa serikali inayoweza kuzuia dhamana za watuhumiwa.

Kibatala amakitaja kifungu cha 148 (5) cha mwenendo wa makosa ya jinai kinachoweka mipaka ya dhamana kwa mtuhumiwa na hakisemi kuhusu suala la usalama wa jamii.

“Kitu pekee kinachoweza kuzuia dhamana ni usalama wa mtuhumiwa ambapo sijamsikia mwasheria yeyote wa serikali akidai,” alisema Kibatala.

Amedai kuwa, kifungu hiko kinaitaka mahakama kujua kama kweli mtuhumiwa usalama wake upo mashakani. Amehoji kwanini Jeshi la Polisi liisukumie mahakama mzigo wake kwa kutaka liwafunge watuhumiwa kwa kulinda usalama wa jamii ilhali wanalipwa mishahara kwa kodi za wananchi ili kulinda usalama wao?

“Hakuna nyaraka yoyote hapa mahakamani inayofanya mahakama ifanye ulinganifu wa maslahi ya umma na washtakiwa.

“Hakuna wakili yoyote wa serikali aliyejitolea kuieleza Mahakama kwamba tangu Frebeuari 16 watuhumiwa walikuwa wapi na walifanya nini kinachohatarisha usalama wa jamii?” alihoji Kibatala.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo ambapo aliahidi kutoa uamuzi wa pingamizi hilo la serikali Machi 29 mwaka huu.

Taifa Stars yazinduka kwa DR Congo

TIMU ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’ imezinduka usingizi baada ya kuitandika DR Congo kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki wa Kimataifa. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Huu ni mchezo wa pili wa kirafiki Taifa Stars kucheza baada ya wiki iliyopita kukubali kipigo dhidi ya Algeria cha mabao 4-1 uliochezwa ugenini.

Bao la kwanza kwa Taifa Stars lilipachikwa kwa kichwa na nahodha wa timu hiyo Mbwana Samatta katika dakika ya 74 ya mchezo kabla ya Shiza Kichuya kupachika bao la pili dakika ya 87.

Ushindi huo utaisaidia Taifa Stars kuweza kupanda katika viwango vya ubora wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kutokana na kushinda dhidi ya timu iliyokuwa juu kwa viwango zaidi yao.

DR Congo inashika nafasi ya tatu kwa ubora katika viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Africa (CAF) huku ikiwa nafasi ya 39 Fifa wakati Tanzania ipo nafasi ya 149 duniani na 46 Afrika.

 

Mbowe na wenzake wapewa kesi ya Akwilina, wanyimwa dhamana

FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na viongozi watano wa chama hicho wamesomewa mashtaka nane katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu likiwemo la kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT), Akwilina Akwiline na kurudishwa rumande. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mbowe na wenzake Dk. Vicent Mashinji, Salum Mwalim, Mchungaji Peter Msigwa, John Mnyika na Esther Matiko, wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri na kukosa dhamana hadi Machi 29, mwaka huu, uamuzi wa dhamana utakapotolewa.

Wakili Nchimbi amedai kuwa kosa la kwanza ni kufanya mkusanyiko ama maandamano yasiyo na uhalali, siku ya Februari 16, 2018 katika barabara ya Mkwajuni kwa lengo la kuwaogopesha watu waliokuwepo eneo hilo kwa kuona maandamano ya kuvunja amani.

Amesema kosa la pili ni kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali, ambapo linawakabili washtakiwa wote wakidaiwa kutenda kosa hilo Februari 16, 2018 Barabara ya Kawawa maeneo ya Kinondoni Mkwajuni.

Viongozi hao kwa pamoja na watu wengine 12 ambao hawajafikishwa mahakamani wakiwa katika maandamano na mkusanyiko wa vurugu waligoma kutii amri ya kusambaratika na kuvunja mkusanyiko huo uliosababisha kifo cha Akwilina Akwiline na majeraha kwa maofisa wa Polisi.

Wakili Nchimbi amedai kuwa kosa lingine ni kuhamasisha chuki kwa wanajamii isivyo halali, ambalo linamkabili Mbowe, siku Februari 16, 2018 akiwa viwanja vya Buibui Kinondoni, Dar es Salaam akihutubia wakazi wa maeneo hayo alitoa matamshi ambayo yangesababisha chuki kwa jamii.

Kosa lingine linalomkabili Mbowe ni uchochezi na kusababisha chuki katika jamii, ambapo inadaiwa amelitenda Februari 16, 2018, akiwa Uwanja wa Buibui Kinondoni, Dar es Salaam akihutubia wakazi hao alitoa matamshi ambayo yangepelekea chuki katika jamii.

Pia kosa lingine linalomkabili Mbowe ni uchochezi wa uasi, ambapo inadaiwa amelitenda Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui, Kinondoni, Dar es Salaam alipotoa matamshi ambayo yangepandikiza chuki na dharau kwa wananchi wa Tanzania dhidi ya uongozi uliopo madarakani.

Kosa la saba linamkabili Mbowe ambalo ni ushawishi wa utendekaji wa kosa la jinai, ambalo amelitenda Februari 16, 2018 maeneo ya Buibui Kinondoni, Dar es Salaam, akiwa amejumuika na watu wengine aliwashawishi wakazi wa maeneo hayo na DSM kutenda kosa.

Wakili Nchimbi amedai kosa la nane, linamkabili Msigwa ambalo ni kushawishi raia kutenda kosa la jinai, alilotenda Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui Kinondoni, Dar es Salaam, ambapo aliwashawishi wakazi wa maeneo hayo na DSM kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana ambapo Wakili Nchimbi amedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaomba tarehe kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.

Hata hivyo, Wakili Nchimbi aliwasilisha maombi kwa mahakama hiyo ili washtakiwa wanyimwe dhamana kwa sababu ya usalama wa umma wa Watanzania.

Mbowe na wenzake wafikishwa mahakamani Kisutu

MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusomewa mashtaka yanayowakabiri. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Viongozi hao walioripoti Kituo cha Polisi cha Kati jijini Dar es Salaam kama walivyotakiwa mapema leo, lakini walipofika waliondolewa dhamana na kuwekwa mahabusu.

Mchana huu viongozi hao akiwemo Mbowe na Katibu Mkuu Dkt. Mashinji,  Salum Mwalim, Msigwa, Mnyika na Esther Matiko wamefikishwa katika Mahakama ya Kisutu mchana huu baada ya kutolewa Kituo Kikuu cha Polisi walipokuwa wameshikiliwa. 

MwanaHALISI Online itaendelea kuwajulisha kinachoendelea mahakamani hapo

Waganga wamtuhumu Katibu kutumia madaraka vibaya

BAADA ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa Umoja Chama Waganga wa Tiba Asilia, Wakunga (UWAWATA “T”) kukutana na kufanya mageuzi kwa kuondoa uongozi uliopita kwa kumtuhumu Katibu Mkuu wa Chama hicho Dk. Daud Nyaki kwa kufanya ubadhilifu na kuiganganya serikali naye ameibuka na kuwatukana wanachama hao kuwa ni wafu wa akili. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Hali hiyo ya Katibu Mkuu Dk. Nyaki kuwatukana wenzake ni kutokana na mkutano mkuu wa kitaifa wa chama hicho ulioketi jana ya kata Kibaigwa kwa lengo la kujadili mwenendo wa viongozi hao waliokaa miaka kumi bila kufanya maendeleo yoyote na badala yake wamekisababishia chama hicho hasara.

Katika mkutano huo uliowakutanisa viongozi wa chama hicho kutoka mikoa mbalimbali wamesema kuwa uongozi ambao ulikuwa ukiendeshwa na katibu Mkuu Dk. Nyaki, umeshindwa kufanya kazi kwa zaidi ya miaka kumi na badala amekuwa akitumia madaraka yake vibaya kwa kuwalazimisha viongozi wa chama hicho kuchanga fedha kwa ajili ya matumizi yake binafsi.

Mmoja wa Makatibu wa chama hicho Kutoka Shinyanga aliyejitambulisha kwa jina la Shidula Mapalala, amesema Dk. Nyaki amechangisha kiasi cha zaidi ya Sh. 18 milioni kwa lengo la kuwanunulia walemavu wa ngozi (Albino) magari lakini hakuweza kufanya hivyo.

“Huyu aliyekuwa katibu mkuu wa chama hiki Dk. Nyaki alikuja Shinyanga na kulazimisha kila mganga kuchangia fedha kwa ajili ya kuwanunulia wengetu maalubino magari na hiyo ilitokana na kuwepo kwa mahusiano mazuri kati ya waganga wa tiba asilia na maalbino.

“Awali waganga wa tiba asilia tulishambuliwa sana na serikali pamoja na watu binafsi kuwa tnahusika katika mauaji ya maalbino na vikongwe kwa kuona hivyo tukajenga mahusiano mazuri ya waganga wa tiba asilia na watu wa jamii hiyo,kwa nafasi hiyo Dk.Nyaki alitumia nafasi hiyo kujikusanyia pesa nyingi kutoka kwa waganga wa tiba asilia kwa madai kuwa anataka kuwanunulia gari jambo ambalo halikufanyika.

“Zaidi ya Sh. 18 milioni zilichangwa lakini hakuna jambo lolote lililofanyika hakuna pesa iliyotumiwa, amezitumia kwa faida yake mwenyewe na unapojaribu kuhoji anakuja juu na kutishia kukufukuza kazi jambo hili sasa linakera sana na serikali inatakiwa kutambua kuwa mtu huyu anawavuruga waganga wa tiba asilia na kuonekana hawafahi,” amesema Mapalala.

Naye Mwenyekiti wa kanda ya ziwa na mwenyekiti wa uongozi wa mpito wa chama hicho, Bujukano Mahungu John lengo la kikao kilichofanyika ni kujadili mwenendo wa viongozi wa chama hicho waliovuka muda wao.

Bujukano amesema kuwa viongozi hao wakiongozwa na katibu mkuu wa chama hicho Dk. Nyaki kwa sasa hawana sifa ya kuendelea kuwa viongozi kwani wameisha vunja katiba ya chama hicho kwani uongozi ni wa miaka mitano na baada ya hapo kunafanyika uchaguzi.

Jambo lingine amesema kuwa kiongozi huyo amekuwa akilazimisha viongozi kuchangisha fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali vya watu wenye ulemavu wa ngozi lakini amekuwa akikusanya fedha hizo bila kufanya jambo lolote na kueleza kuwa mbaya zaidi ni kuwatishia viongozi pale wanapojaribu kuhoji mabo ya msingi.

Aidha amesema kuwa Dk. Nyaki kwa uongozi wake wote a miaka 10 hajawahi kutoa taarifa ya mapato na matumizi na kuongeza kuwa kutokana na hali hiyo mkutano mkuu huo uliohsisha mikoa 11 ya Tanzania bara wamefanya mageuzi na kuweka viongozi wapya pamoja na kuunda kamati ya kufuatilia mali za chama na kuchukua hatua kali za kisheria.

Viongozi wa mpito waliochaguliwa ni Bujukano Mahungo John ambaye ni mwenyekiti, Licas Mlipu- Katibu, Maiko Salali- Mratibu, Mwanahamisi Kapera –Mratibu ukaguzi, Shida Twahibu –Katibu Mwenezi, Mrumba Abdul, Mkurugenzi Mashitaka, Mwajabu Mgaza-Mhasibu na Alex Raymond-Mjumbe.

Kwa pamoja viongozi hao paamoja wajumbe wametangaza rasmi kwa kutowatambua viongozi waliopita na kuitaka serikali kutowakumbatia viongozi hao kwani wamekuwa wakipaka matope chama.

Kwa upande wake katibu wasiyemtambua Dk. Nyaki alipoulizwa juu ya kukaa kwa mkutano mkuu na kumkataa yeye pamoja na uongozi wake amesema watu hao wameisha kufa na akili zao.

Amesema kinachofanyika ni unafiki na chuki na wala hajawahi kuchukua fedha za chama na wala kuchangisha fedha kwa mtu yoyote.

“Kwanza kabisa futa kauli yako mimi bado ni katibu mkuu hao waliokaa ni wahuni tu na wanafiki mimi sijawahi kuchangisha fedha wanaozungumza hivyo ni wale ambao walishafukuzwa kazi kutokana na utovu wa nidhamu ndani ya chama.

“Kuhusu hizo pesa mimi likaa Shinyanga zaidi ya miezi 4 na nlikuwa nadaiwa zaidi ya sh.Milioni 1.8 na nilienda nkalipa sikucangisha fedha, uongozi wa Shinyanga ulishindwa, lakini kama suala ni kutoa zawadi kwa Albino mimi ndiye niliyekuwa napendekeza kutoa zawadi hivyo silazimishwi kutoa misaada kwa Maalbino ila nilitoa sehemu mbalimbali,” amesema Dk.Nyaki.

Wakulima watakiwa kutowaogopa maofisa ugani

AFISA kilimo wa mkoa wa Dodoma, Benard Abraham amewataka wakulima kuwasiliana na maofisa ugani pale wanapoona mimea yao au mazao inashambuliwa na wadudu. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Ofisa huyo alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na Tanzania baada ya wakulima wa mahindi wa Kibaigwa wilayani Kongwa mkoani Dodoma kulalamikia mahindi yao kushambuliwa na wadudu.

Mmoja wa wakulima wa Mahindi wilayani Kongwa, Machite Mgulambwa amesema zaidi ya heka 50 za mahindi zimeharibiwa.

Amesema licha ya kujibidisha katika kilimo na mvua kunyesha vizuri lakini wadudu wamevamia mahindi na kuyaharibu na kuwasababishia hasara kubwa wakulima.

“Tunaomba serikali iwahimize wataalamu wa kilimo kuwatembelea mara kwa mara wakulima ili kubaini changamoto wanazokumbana nazo.

“Wataalamu wa kilimo wasiwe watu wa kukaa maofisini badala yake waende mashambani kwa lengo la kuwasaidia wakulima ili waweze kulima kilimo chenye tija badala ya kilimo cha mazoea,” amesema Machite.

Mbali na hilo amesema kuwa kama serikali haitawahimiza wataalamu wa kilimo kuwa karibu na wakulima ni wazi hata sera ya Tanzania ya viwanda itakuwa ndoto.

Akizungumzia malalamiko hayo ofisa kilimo wa Mkoa, Benard Abrahamu amesema serikali imepeleka maofisa kilimo kuanzia ngazi ya kijiji.

Amesema wakulima wanatakiwa kuwasiliana na maofisa kilimo mara kwa mara pale wanapoona mimea yao au mazao pale yanapokuwa na dalili tofauti ambayo inatia shaka.

Amesema yeye kwa ngazi ya mkoa wanatakiwa kupata taarifa za mara kwa mara ili kukabiliana na matatizo na changamoto zinazowakumba wakulima.

Mbowe, viongozi Chadema wafutiwa dhamana

MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wengine wandamizi wa chama hicho, “wameswekwa rumande,” kwenye kituo cha polisi kati jijini Dar es Salaam. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Taarifa zilizothibitishwa na Casimil Mabina, katibu wa chama hicho Kanda ya Pwani, Mbowe na wenzake wameswekwa rumande, kwa maelekezo ya mkuu wa upelelezi wa Kanda ya Dar es Salaam.

“Muda huu tumeingia kwa Deputy ZCO (naibu mkuu wa upelelezi wa Kanda). Faili analo mmoja wa askari. Dalili zote ni kwamba wanawekwa mahabusu,” anaeleza Mabina katika taarifa yake kwa wanachama wa chama hicho kwenye Kanda hiyo.

Viongozi walioshikiliwa polisi ni pamoja na Mbowe, Katibu Mkuu Dk. Vincent Mashinji, John Mnyika, Salum Mwalim, Peter Msigwa na Ester Matiko.

Mabina anasema, awali kulikuwa na maelekezo ya kuwapeleka mahakama ya Hakim Mkazi Kisutu, ili kijibu tuhuma zinazowakabili.

Katibu huyo amesema wamefutiwa dhamana na mpango kesho watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yao.

Mbowe na viongozi wenzake wanatuhumiwa kuhamamisisha wafuasi wao kufanya maandamano ya tarehe 16 Februari mwaka huu.

Deni la Taifa lazidi kupaa

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali (CAG) ya mwaka 2016/17 imeonyesha deni la Taifa limezidi kupaa kwa asilimia 12 ukilinganisha na ripoti ya mwaka 2015/16. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad amesema ongezeko hilo la deni la Taifa linatia wasiwasi hivyo serikali inatakiwa kuchukua hatua kupunguza ukubwa wa deni hilo.

Prof. Assad amesema kuwa deni hilo limeongezeka kwa Sh. 5 trilioni kwa mwaka huu, kutoka Sh 41trilioni mpaka kufikia Sh 46 trilioni ikiwa ni mwaka mmoja baadaye.

Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa leo kwa Rais John Magufuli Ikulu, Dar es Salaam imebaini mapungufu mengi katika Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma.

Baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Magufuli ameahidi kuchukua hatua za haraka kwa sekta zilizokuwa na mapungufu hayo huku akiomba azidi kuombewa kwani kutekeleza hayo ni kazi kubwa sana.

Pia Rais Magufuli amemwagiza Waziri wa TAMISEMI kuwasimamisha kazi mara moja Wakurugenzi wa Halmashauri ya Kigoma Ujiji na Pangani kwa kukutwa na hati chafu ya ukaguzi.

Moil yafunga biashara Tanzania, yahamia Uganda, DR Congo

KAMPUNI ya mafuta ya Moil, inadaiwa kuwa imeanza kuondoa biashara zake za uuzaji wa mafuta nchini na kuzihamishia katika nchi za Uganda na Congo kwa kile kinachotajwa kuwa kwa sasa Tanzania mazingira ya uwekezaji sio mazuri. Anaripoti Mwandishi wetu … (endelea).

Moil inatajwa kumilikiwa na mbunge wa Jimbo la Kwimba mkoani Mwanza, Shanif Mansoor (CCM) na Altaf Mansoor (Dogo), ambao wanamiliki vituo vya mafuta kadhaa hapa nchini.

Taarifa za ndani kutoka katika kampuni hiyo zinaeleza kuwa wamiliki wa kampuni hiyo wamelazimika kuondoa biashara nchini kutokana na mazingira ya kiuwekezaji kwa sasa nchini siyo rafiki.

Chanzo hicho cha ndani kutoka katika kampuni hiyo kinameueleza mtandao huu kuwa, kwa sasa tayari magari makubwa ya mafuta ya kampuni hiyo yamebadilishwa usajili wa namba za Tanzania na sasa zimesajiliwa kwa usajili wa nchi za Uganda na DR Congo.

“Wakurugenzi wao wanasema Tanzania sasa hivi biashara siyo nzuri na ufanyaji wake umekuwa mgumu na faida hakuna hivyo wamelazimika kuanza kuondoa biashara zao na kuzihamishia katika nchi za Uganda na DR Congo,” kilisema chanzo hicho.

Pia chanzo hicho kimebainisha kwamba uongozi wa kampuni hiyo ulikuwa umeanza kuondoa biashara zake nchini kwa muda mrefu lakini kwa gari hizo kumi za usafirishaji mafuta, usajili wa namba zake ulianza Februari 27 mwaka huu.

Kampuni ya Moil, ambayo ina vituo vya mafuta vitatu jijini Mwanza, inadaiwa kwa sasa gari inayosambaza mafuta kwenda jijini humo ni moja tofauti na awali zaidi ya gari kubwa za mafuta kuanzia 10 zilikuwa zikisambaza kwenye vituo hivyo.

Aidha chanzo hicho kimeendelea kudai kuwa pamoja na wanahisa wengine kushinikiza kuondolewa kwa biashara zao nchini pia mbunge wa sasa wa jimbo la Kwimba amekuwa akidai kuwa hana mpango wa kugombea tena ubunge mwaka 2020.

Kutoendelea kwa Mansoor katika nafasi hiyo pia kunadaiwa kuchangia kuhamishwa kwa Biashara za kampuni hiyo kwenda nchi hizo.

Mmoja wa wakurugenzi hao, Shanif Mansoor alipotafutwa kwa njia ya simu zaidi ya mara nne kwa nyakati tofauti ili kuzungumzia suala hilo, simu yake ya mkononi iliita bila majibu.

Maalim Seif amdhibiti Prof. Lipumba, amshika pabaya

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimepiga marufuku uanzishaji wa matawi mapya na kuagiza viongozi wake ngazi ya majimbo kuwa macho na nyendo zozote za “watu fulani” kutaka kufungua matawi kwa nia ya kumfanikisha mipango ya kukihujumu chama. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Agizo hilo limetolewa kwa uongozi wa chama hicho kupitia vikao vya kamati tendaji vya matawi na majimbo nchini kote vilivyofanyika wiki mbili zilizopita, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya CUF.

Matawi yatakayoruhusiwa kufunguliwa ni yale yaliyopata idhini ya ofisi ya Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad. Agizo hili limeanza kutekelezwa Unguja na Pemba ambako inasemekana ndiko nguvu ya wasaliti wa CUF inakoelekezwa kwa sasa.

Salim Bimani, mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano na umma wa CUF, ameiambia Mwanahalisionline kwa njia ya simu kuwa chama kina haki ya kuchukua hatua mbalimbali za kujilinda dhidi ya mbinu za kukihujumu.

Viongozi wa matawi kadhaa wameithibitishia Mwanahalisionline kwamba wamepewa agizo hilo wakati wa mikutano maalum ya wajumbe wa kamati tendaji na viongozi wa ngazi ya juu wakiwemo wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama.

“Kwa hili hakuna shaka yoyote ni agizo halali tulilopewa na uongozi wa juu wa chama chetu. Tumejuilishwa rasmi kwamba ni katika kukabiliana na njama za kuzidi kukihujumu chama. Waliotueleza walisema ni agizo kutoka ofisi ya Katibu Mkuu wa chama,” mtandao huu umeelezwa.

Baadhi ya viongozi waliohojiwa na mtandao huu, wamesema agizo hilo limetokana na ukweli kwamba Profesa Ibrahim Lipumba hajachoka kutumika kukihujumu chama hicho.

“Viongozi wetu wametueleza mengi lakini kubwa ni kwamba wanajua namna ambavyo profesa Lipumba anaendelea kuvuruga chama,” ameeleza kiongozi mmoja anayetoka moja ya majimbo yaliyoko ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Profesa Lipumba, aliyevuliwa uanachama wa CUF tangu Septemba mwaka 2016, kwa tuhuma za kukisaliti chama kwa kuandaa na kutekeleza mpango wa kukihujumu chama, ikiwemo kuvunja mkutano mkuu maalum wa Ubungo Plaza wa tarehe 21 Agosti 2016, anatuhumiwa na uongozi wa juu wa chama kutaka kukiangamiza akisaidiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Msajili Francis Mutungi ambaye pia anakabiliwa na tuhuma hizo hadi kuwa mmoja wa maofisa waandamizi wa serikalini wanaoshitakiwa mahakamani na CUF, aliamua kumtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti halali hata baada ya kuwa alivuliwa uanachama.

Msimamo wake huo ulikuja baada ya Profesa Lipumba kushikilia ofisi kuu za CUF za Buguruni jijini Dar es Salaam licha ya kuwa alijiuzulu wadhifa huo kwa hiari yake kupitia barua ya tarehe 5 Agosti 2015 aliyomkabidhi katibu mkuu.

Miezi kumi baadaye, profesa alitangaza kutengua uamuzi huo na kutaka aruhusiwe kuingia ofisini na kuanza tena kufanya kazi za mwenyekiti.

Mkutano mkuu wa Ubungo Plaza uliridhia kujiuzulu kwake lakini ulikwama kuchagua mwenyekiti mpya. Kazi za mwenyekiti tangu hapo zimekuwa zikifanywa na Kamati ya Uongozi inayoongozwa na Julius Mtatiro.

Kwa mujibu wa taarifa za agizo la uongozi wa juu, viongozi wa matawi na majimbo wametakiwa kutoa taarifa haraka wanapoona watu wanaojitambulisha kama wanachama wa CUF wakitaka kufungua matawi popote pale nchini.

“Ukiona tu kuna bendera mpya ya chama karibu na eneo lako la uongozi au ndani ya eneo lako, piga ripoti kwa uongozi wa juu yako hadi wilaya.

“Ni jukumu la viongozi wote wa ngazi zote na jukumu mahsusi kwa walinzi wote wa chama chetu kusimamia agizo hili,” kiongozi mwingine ameiambia Mwanahalisionline akimnukuu kiongozi aliyewahutubia katika mkutano maalum wa viongozi wa matawi na majimbo ya Wilaya ya Magharibi A, mjini Unguja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Maalim Seif amesema hatua mbalimbali zinachukuliwa na chama katika kukabiliana na mkakati mpya wa kukihujumu chama.

Maalim Seif ambaye juzi alihutubia viongozi na wanachama walioshiriki kongamano la CUF wilayani Kinondoni, alisema hatua hizo zimeidhinishwa na Kamati ya Utendaji ya chama iliyokutana tarehe 25 Machi.

Zipo taarifa kuwa kundi linaloongozwa na profesa Lipumba linajitahidi kutaka kupata akidi ya wajumbe ili kuitisha watakachokiita “mkutano mkuu” ambao moja ya maazimio yanayolengwa ni kumfukuza Maalim Seif.

Mapema mwezi huu, profesa alisafiri kwa ndege kwenda kisiwani Pemba ambako aliandaliwa mkutano wa ndani kwenye ukumbi wa kiwanda cha Makonyo, eneo la Wawi, nje kidogo ya mji wa Chake Chake, na kuondoka mara baada ya mkutano huo.

Hakufanikiwa kukagua tawi lolote wala kukutana na viongozi wa wilaya kama ilivyokusudiwa awali. Walioshuhudia profesa akipokewa uwanja wa ndege wa Chake Chake, walisema ziara yake hiyo iligubikwa na ulinzi mkali wa polisi wenye sare na wasiovaa sare.

CUF inamtuhumu kiongozi mmoja katika Baraza la Mapinduzi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kushirikiana na profesa Lipumba katika mpango mpya wa kumaliza chama hicho.

Nondo aachiwa kwa dhamana Iringa

MWENYEKITI wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo ameachiwa kwa dhamana leo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Nondo ameachiwa baada ya Hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, John Mpitanjia kutoa maamuzi kuwa dhamana ipo wazi na mtuhumiwa huyo kutimiza masharti ya dhamana.

Masharti ya dhamana ni kudhaminiwa na watu wawili ambao ni wakazi wa Iringa, huku mmoja awe mfanyakazi wa serikali, na wanatakiwa waweke bondi ya Sh. 5 milioni sambamba na kuwa na mali isiyohamishika, ambayo Nondo ameyatimiza na kupata dhamana.

Kesi imehairishwa mpaka Aprili 4, 2018 itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Nondo anatuhumiwa kwa makosa mawili, la kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni Machi 7, 2018 akiwa Ubungo na kusambaza kwa kutumia mtandao wa WhatsApp kuwa yupo hatarini.

Shitaka la pili ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma mjini Mafinga alipokuwa akitoa taarifa katika kituo cha Polisi Mafinga kuwa alitekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam na kupelekwa Kiwanda cha Pareto cha Mafinga.

Kubenea atinga kwa Lissu

MBUNGE wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, leo Jumapili amekutana na madiwani wa jimbo la Singida Mashariki, linaloongozwa na Tundu Lissu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea). 

Katika mkutano huo uliofanyika mjini Ikungi, Kubenea alikutana pia na viongozi wa Kamati tendaji jimbo na wilaya, pamoja na diwani pekee wa Chadema kwenye jimbo la Singida Magharibi, Emmanuel Jingu.

Kwenye ziara hiyo, Kubenea aliongozana na Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kati, Alphonce Mbasa; katibu wa Kanda, Iddi Kizota na mbunge wa Viti Maalum, mkoani Singida, Jessica Kishoa.

Mkutano kati ya mbunge huyo na viongozi hao, ulilenga kusikiliza matatizo ya madiwani hao yaliyotokana na kutokuwapo kwa mbunge wao.

Aidha, mkutano huo ulilenga kupanga mikakati ya kukabiliana na hujuma za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na madiwani kupata taarifa sahihi ya maendeleo ya Lissu.

Hatua ya Kubenea kufika jimboni jimboni Singida Mashariki, imefuatia kuombwa kwake na Lissu kukutana na madiwani wake na viongozi wake wa chama.

Kubenea na viongozi wenzake waliwaeleza madiwani na viongozi hao wa kata kuwa wanalo jukumu kubwa la kukilinda chama na kumtetea mbunge wao kwa gharama yeyote ile.

Naye Lissu akizungumza kwa njia ya simu ya video, aliwaeleza madiwani na viongozi wake maendeleo ya afya yake na kutokubali kughiribiwa.

Alisema, “kwa kweli, ninaendelea vizuri. Afya yangu inazidi kuimarika. Nawahakikishia, nitarudi nikiwa mzima na ninayetembea.”

Aliongeza: “Ninawaamini sana. Sina mashaka yeyote na ninyi. Naomba pigeni kazi ili kulinda heshima yenu na hadhi zenu mlizopewa na wananchi.”

Lissu alitumia mkutano huo kumshukuru Kubenea kwa upendo wake kwake na kumuomba yeye na viongozi wengine kufika kwenye jimbo hilo mara kwa mara kuongea na wananchi wake.

Naye Mbasa – mwenyekiti wa Kanda hiyo – alimshukuru Kubenea kwa uamuzi wake kutembelea jimbo hilo.

Alisema, “uamuzi huu ni mzuri na unapaswa kupigiwa mfano. Ninakushukuru wewe na nawashukuru wote uliongozana nao katika safari hii.”

Kwa upande wake, katibu wa Kanda alisema, ziara ya Kubenea imeleta faraja kubwa kwa wananchi wa Singida Mashariki na Kanda ya Kati kwa ujumla.

Jessica Kishoa – akizungumza katika mkutano wa madiwani na viongozi hao wa jimbo, wilaya, mkoa na Kanda, alimhakikishia Kubenea kuwa mbegu aliyoipanda leo watailinda na hivyo itadumu.

Nao baadhi ya madiwani wamemshukuru Kubenea kwa hatua yake ya kufika jimboni humo na kumhakikishia kuwa watailinda heshima hiyo waliyopewa.

Lowassa, Mbowe waufuata waraka wa Maaskofu KKKT

MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe na Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chama hicho, Edward Lowassa wameshiriki kwenye ibada ya Jumapili ya matawi kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Azania Front,  Dar es Salaam. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Ujumbe waliotoka nao viongozi hao ni amani inayotakwenda sambamba na haki kwa pande zote.

Akizungumza nje ya Kanisa hilo baada ya ibada hiyo, Mbowe amesema kuwa viongozi wa dini wamehubiri amani na kusisitiza kutenda haki kutokana na kushabihiana kwa masuala hayo.

“Neno la leo ni amani na amani inapatikana kwa kutoa haki hivyo wachungaji wetu wamesema kuwa haki itendeke kwenye familia hadi kwa viongozi,” amesema Mbowe.

Mbowe amesema kuwa Pasaka ni Sikukuu muhimu kwa waumini wa dini ya kikristo  na ni siku inaazimisha kuteswa kufa, kuzikwa na kufufuka Yesu.

“Ni siku ambayo wakiristo tunaiona kuwa ni chanzo ukombozi na amani ya mwadamu ni chanzo cha kukoshwa kwa zambi zetu na damu ya kristo,” amesema Mbowe.

Mipango ya Jaji Mutungi, Lipumba kumng’oa Maalimu Seif yafichuka

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa Msajili wa vyama siasa nchini Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi yake Profesa Ibrahimu Lipumba wamepanga njama ya kukisambatisha chama hiko pamoja na kumfukuza Katibu mkuu huyo. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Maalimu Seif ameyasema hayo leo alipokutana na wanachama wa chama hicho wa Tandale Jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa umesukwa mpango mahususi wa kung’oa ili kukisambaratisha chama hicho.

Amesema kuwa ziara ya Lipumba ya wiki iliyopita ilikuwa ni sehemu ya mpango huo uliosukwa na Msajili wa vyama vya siasa na kushirikiana na Balozi Seif Ali Iddi Makomo wa pili wa Rais Zanzibar ili kupatikane kwa wazanzibar wanaomuunga mkono Lipumba ili kupatikane uhalili wa kikatiba wa kuwa na wanachama Tanzania bara na visiwani ili kuweza kupora chama hicho.

Amesema kuwa Balozi Seif Ali Idd amekuwa mstari wa mbele kwenye mpango huo ili kuifukia haki ya wananchi wa Zanzibar ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Maalim Seif amesema kuwa Lipumba alipofika Zanzibar hakuna Mwanachama yoyote wa CUF aliyekwenda kumpokea Zaidi ya askari Polisi waliokuwa wakimlinda.

“Waliompokea ni askari waliovaa kiraia na wanachama wa chama cha Mapinduzi CCM na ADC”

Amesema ni wazi Lipumba hawezi kupata wafusi Zanzibar wa kuweza kukidhi matakwa yta kikatiba lakini Msajili Mutungi amemuahidi atampitisha hivyo hivyo.

“Msajili kashamwambia kuwa yeye atafute watu angalau 15 ili wapitishe …..Lipumba anafanya kazi na Seif ali Idd anyejita Makamo wa pili wa Rais anafanyakazi na Hamadi Rashidi …. Kwa lengo la kuisambratisha CUF Zanzibar.

“Wanajua kwa mazingira ya unguja na pemba kupata idadi ya kikatiba wanancha 5o haiwekani lakini wanaambizana kuwa nendeni kwa vile msajili amewaambia wajumbe 15 wanatosha”.amesema Maalimu Seif.

Maalimu Seif ameeleza kuwa Lipumba amekuwa akiinga Zanzibar kama mwizi na hukuitana na viongozi waandamizi wa CCM.

Maalimu seif amesititiza kutokuinga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo amesema kuwa serikali hiyo ni haramu.

Maaskofu wa KKKT watoa waraka mzito kwa serikali

MAASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wametoa waraka mzito waliouta ‘Ujumbe wa Sikukuu ya Pasaka’ ambao utasomwa kesho katika makanisa yote nchini kwa waumini wake. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Ujumbe huo wa Pasaka ambao umegusia mambo makubwa matatu ambayo ni Jamii na Uchumi, Maisha ya Siasa na Masuala Mtambuka na kusainiwa na maaskofu 27 wa KKKT waliokutana Machi 15, 2018 jijini Arusha.

Soma waraka wenyewe wa Maaskofu hao hapa chini.

KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA (KKKT)

UJUMBE WA PASAKA KUTOKA BARAZA LA MAASKOFU WA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA (KKKT)

TAIFA LETU, AMANI YETU

A. UTANGULIZI

“Fumbua Kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao; Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; uwapatie maskini na wahitaji haki yao” (Mithali 31: 8-9).

Wapendwa wana KKKT,
Watukuka, watu wote na familia ya Mungu katika Taifa letu, “Amani iwe kwenu!; Kristo Amefufuka (Yohana 20:19).

Bwana wetu Yesu Kristo mfufuka, alipowatokea wanafunzi wake wakiwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, aliwasalimu na kujifunua kwao kwa salaamu ya kuwatakia amani. Wapendwa watu wa Mungu, katika umoja wetu, sisi maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), tunawasalimuni nyote kwa kuwatakia amani. Bwana wetu Yesu Kristo Amefufuka kweli kweli – Haleluya!. Yeye ni amani yetu, na pia ni amani kwa watu wote wenye mapenzi mema. Kwa kufufuka kwake, upendo umeishinda chuki; unyenyekevu umeushinda ubabe; nuru imelishinda giza; haki imeshinda udhalimu; msamaha umeshinda visasi; ujasiri umeshinda hofu; na kwa hiyo uzima umeshinda kifo.

Mwaka 2017, Kanisa letu limeadhimisha miaka 500 ya Matengenezo ya Kanisa. Tukiwa wana Matengenezo tumekumbushwa tena kuwa mwanadamu anaokolewa kwa Neema ya Mungu tu: Wokovu Hauuzwi; Mwanadamu Hauzwi wala kununuliwa; na Uumbaji hauuzwi. Kanisa zima na dunia kwa ujumla tunaitwa kusimama pamoja na kuueleza ukweli huu unaoziweka huru dhamiri zetu (Yohana 8:31-32).

Matengenezo (Reforms) ni dhana ya kibiblia. Tangu zama za Agano la Kale, Mungu kwa nyakati mbalimbali aliteua wajumbe wake kuwasilisha ujumbe wake kwa jamii na kwa watawala wa dunia. Kwa Umungu wake, aliwainua wanawake na wanaume kwa makusudi ya kutoa unabii yaani, ujumbe wa Mungu kwa jamii au watawala. Wakati mwingine aliinua manabii kuwasemea wasiokuwa na sauti. Unabii na Matengenezo ni njia ya Mungu katika kusimika utawala wa haki na unaostawisha uhuru na amani.

Kwa namna ya pekee, manabii kama Daniel, walionya juu ya uongozi unaojenga uhalali wake katika wingi wa watu wanaokubaliana na uongozi huo hata kama ni katika makosa. Haikuwa rahisi kibinadamu kuukosoa mfumo kama huo lakini Mungu alitumia manabii kuzungumza na mfumo wa namna hiyo. Unabii wa Daniel 3:7 unasema, “Kwa hiyo watu WOTE, mara waliposikia sauti za baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari, na sauti za ala nyingine za muziki, walianguka kifudifudi na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebkadneza aliisimamisha.”

Hapa tunaona kosa la kiongozi kutengeneza sanamu, linasababisha kosa la watu wanaokubali kuiabudu hiyo sanamu. Tumetafakari na kusadiki kuwa, kosa la kiongozi au mfumo, haliwaondolei hatia wanaomfuata kiongozi au kuufuata mfumo, hata kama watu hao walikula kiapo cha kutii maongozi ya kiongozi huyo na mfumo wake. Mbele ya Mungu hakuna ile kanuni ya kuwajibika kwa pamoja. Kila mtu kwa dhamiri yake anawajibika mbele za Mungu. Kwa upande mwingine, pamoja na uwajibikaji wa mtu binafsi, Nabii Ezekieli anatukumbusha na kutuonya kuwa tusipoonya na kusimama katika zamu yetu, hatia na damu ya wasio na hatia, itadaiwa mikononi mwetu (Ezekiel 33: 8-9).

Adhimisho la kufufuka kwa Yesu Kristo (Pasaka) na maadhimisho ya miaka 500 ya Matengenezo ya Kanisa, yanatusukuma kutafakari utume wa Kanisa katika jamii kwa nyakati zetu. Tunaalikwa kupeleka ujumbe wa amani kwa watu wote na kusimama kwa ujasiri katika kuwasemea wasio na sauti katika jamii ili kuenzi roho ya Pasaka na Matengenezo katika nyakati zetu. Kama Kanisa na kwa nafsi zetu mmoja mmoja, tunaitwa kwa upande mmoja, kufundisha, kushauri na kutia moyo. Kwa upande mwingine, tunaitwa kuonya, kukaripia, kukemea na kuelekeza kwa uvumilivu wote na upendo (2 Timotheo 4: 1-5).

Wajibu huu kwetu sisi maaskofu ni wito na utume usiokwepeka; na kwa watu wote wa imani, wajibu huu hauna mbadala. Tunaagizwa kuchochea ujenzi wa madaraja ya maridhiano katika upendo na amani, na kuwa kinyume na mifumo yote inayoendeleza chuki na marafakano. Kwa kufanya hivyo, imetupasa kusema wazi wazi ujumbe wa amani, upendo, heshima, utu, ustahimilivu na maelewano. Mfumo wowote unaojengwa katika utii wa sheria bila upendo; heshima bila uhuru; na amani bila haki, unajengwa katika msingi usio imara. Kupuuza wito huu kuna madhara kwa jamii yetu. Ni sawa na kujenga nyumba juu ya mchanga (Mathayo 7: 26).

Tunasihi kwa machozi mengi, tuwe wajenzi wenye akili wajengao nyumba zao juu ya mwamba (Mathayo 7:24). Mwamba tunaotakiwa kujenga taifa letu lenye dini mbalimbali, vyama mbalimbali, na makabila mbalimbali, umetajwa katika sala kuu ya taifa letu, yaani, “DUMISHA UHURU NA UMOJA”. Bila Uhuru hakuna umoja uwezao kuleta maendeleo; na bila umoja wa kitaifa, uhuru wetu hauleti amani endelevu. Kwa sababu ya nguvu ya dhamiri safi iliyo dira ya taifa letu, tunalazimika kumtii Mungu kuliko mwanadamu (Matendo 5:29).

B. TAIFA LETU NA AMANI YETU

Tunapoadhimisha sikukuu ya kukumbuka kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, tunatambua kuwa utume wa Kanisa letu katika taifa letu, unafanyika katikati ya changamoto kadhaa. Kwa kuwa Kanisa ni sehemu ya jamii, linaguswa na changamoto hizo. Katika kukaa pamoja na kuliombea taifa letu, sisi maaskofu wa KKKT, tumetafakari na kubaini changamoto hizo. Kwa njia ya salaam za Pasaka, tunaleta kwenu changamoto tatu ili ziongeze mzigo wa kuliombea taifa letu na viongozi wake.

1. Jamii na Uchumi
Kiini cha Utume wetu katika jamii kinatuingiza kwa nia njema katika maisha ya uchumi na mshikamano wa kijamii. Neno la Mungu linatufundisha kuwa “Mwanadamu hawezi kuishi kwa mkate peke yake” (Luka 4:4). Pia neno la Mungu linatuhakikishia kuwa Bwana wetu Yesu Kristo alikuja ili tuwe na uzima tele (Yohana 10:10).

Tunawiwa katika umoja wetu wa ubaba, kuipongeza serikali yetu kwa jitihada inazofanya kuboresha maisha ya wananchi. Tumeshuhudia jitihada na nia njema kuhusu uvunaji na umilikaji wa rasilimali za nchi kwa manufaa ya taifa zima. Aidha, tunapongeza jitihada za ukusanyaji wa kodi ili kuiwezesha serikali kugharamia huduma za jamii. Hata hivyo, bila kukatisha tamaa jitihada hizo, tunawiwa kushauri yafuatayo:

I. Sekta binafsi na mashirika ya dini ni wadau wa maendeleo, si washindani wa serikali katika kuchangia maendeleo ya taifa. Mazingira yasiyo rafiki kuhusu wadau hawa, ni kikwazo kisicholeta mshikamano kati ya serikali na sekta binafsi na mashirika ya dini katika kuleta maendeleo. Jitihada za makusudi na za mara kwa mara zifanyike kuondoa dhana ya ushindani kati ya serikali na wadau hawa ili kuimarisha mahusiano mema kati ya serikali na sekta binafsi.

II. Ili mfumo wa ukusanyaji wa kodi uwe endelevu; jitihada za kukusanya kodi ziendane na elimu kwa mlipa kodi. Msisitizo wa uzalendo wa kulipa kodi uende sambamba na ustawi wa walipa kodi katika shughuli zao za biashara. Mivutano isiyo na tija kati ya walipa kodi (wafanya biashara) na mamlaka ya ukusanyaji wa kodi, inastawisha uadui unaopunguza makusanyo ya kodi na kujenga ushawishi wa rushwa. Mfumo wa kodi unaowafilisi wafanya biashara, haulengi kujenga uchumi wa viwanda.

III. Kutokana na ongezeko kubwa la vijana wasio na ajira; jitihada za wazi na za makusudi zifanyike ili msukumo wa uchumi wa viwanda ufikie matumaini yanayoshikika miongoni mwa vijana wasio na ajira. Sekta binafsi, wawekezaji na wadau wengine, wahakikishiwe usalama wa mitaji yao kisheria. Hili likifanyika ni kichocheo kizuri cha ujenzi wa viwanda.

IV. Uchumi wa viwanda (vidogo na vikubwa) uendane na uwekezaji katika sekta ya kilimo maeneo ya vijijini. Kilimo na ufugaji ndizo sekta zenye wigo mpana wa viwanda vinavyogusa maisha ya watanzania walio wengi. Utozaji holela wa kodi na ushuru wa mazao unakatisha tamaa wadau wa kilimo. Migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja, na wakulima/wafugaji na wawekezaji kwa upande wa pili, si kivutio cha uwekezaji katika sekta ya kilimo.

2. Maisha ya Siasa
Kwa umoja wetu katika utume, tunatambua siasa safi na uongozi bora kuwa ni misingi iliyoongoza maisha ya siasa katika taifa letu. Ujio wa vyama vingi mnamo 1992, haukuondoa umuhimu wa misingi hii bali ulipanua matumizi ya demokrasia iliyojengwa katika uhuru wa mawazo. Taifa ni mkusanyiko wa taasisi na watu mbalimbali, wenye lengo moja lakini kwa njia mbalimbali. Kutokana na wingi huu, taifa letu daima ni juu ya vyama, taasisi na makundi.

Taifa huongozwa na katiba iliyo kiini cha sheria zote. Taifa haliongozwi na ilani za vyama. Serikali haiongozwi na ilani za vyama. Serikali huongozwa na katiba, sheria, kanuni na mapokeo mema (misingi na tunu za taifa). Serikali husimamiwa na bunge huru lililo sauti ya wananchi. Wananchi ndilo chimbuko la madaraka ya bunge. Bunge halisimamiwi na ilani, chama chochote wala mtu awaye yote. Kwa umoja wetu na kwa nyakati zetu, hivi sasa tunashuhudia matukio yaliyo kinyume na tunu na misingi iliyolilea taifa letu. Baadhi ya matukio hayo ni:

 1. Hofu iliyojengwa katika matukio halisi yakiwamo utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.
 2. Kupungua na hatimaye kutoweka kwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na kupata habari. Kwa mwenendo huu, kuna hofu kuwa hata uhuru wa kuabudu uko mashakani.
 3. Kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi. Hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.
 4. Kukosekana kwa mazingira ya haki na uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi zote zimeghubikwa na ubabe, vurugu, hila, na vitisho.
 1. Utekelezaji wa mipango ya maendeleo wenye mwelekeo wa kiitikadi. Hatua hii imeimarisha ubaguzi wa kiitikadi katika taifa letu na kukuza migawanyiko.
 2. Kushamiri kwa chuki mioyoni mwa watu ambalo ni chimbuko la visasi, kukata tamaa, na ushiriki mdogo wa wananchi katika chaguzi na maisha ya siasa.
 3. Udhalilishaji wa kauli njema isemayo “Maendeleo hayana chama”. Udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya kutumia fedha nyingi katika chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama ili kuleta maendeleo. Tunajiuliza, kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu anajiuzuru chama fulani, eti kwenda kuleta maendeleo katika chama kingine? Mchezo huu unagharimu fedha nyingi na maisha ya watu wanaokufa, kujeruhiwa na uharibifu wa mali. Mambo haya ni tishio linalohatarisha umoja na amani ya nchi yetu.

3. Masuala Mtambuka
Kanisa ni alama ya uwepo wa utume wa kuleta na kutunza matumaini katika jamii. Ukimya wa Kanisa katika masuala yanayoigusa jamii ni ukwepaji wa wajibu wake. Lakini pia sauti ya Kanisa isiyomilikiwa na mtu isipokuwa Mungu tu, ni chachu ya amani na matumaini. Kwa dhamiri safi inayotokana na utambuzi wa “Wakati wa Mungu”(Kairos) katika taifa letu, tunawiwa kutambua masuala mtambuka yanayogusa maisha ya watu kipekee na kwa njia nyingi na kuyatolea ushauri ufuatao:

 1. Kuhitimisha mabadiliko ya mara kwa mara katika mfumo wa elimu nchiniili kuondoa mwanya wa kila mtendaji mkuu wa wizara kuja na sera yake. Elimu ni kitovu cha ustawi wa taifa, kisiwe kinachokonolewa chokonolewa kila wakati. Sekta zote nchini hujenga mafanikio yake katika mafanikio ya mfumo thabiti wa elimu.
 2. Uwezeshaji wa vijana kupata mikopo ya elimu ya juu uwe shirikishi na usiokuwa na “ubaguzi” kati ya wanafunzi wa vyuo binafsi na wale wa serikali; sayansi na sanaa; wazazi maskini na wenye nafasi; waliosoma shule binafsi na wale wa shule za serikali, n.k. Kwa kuwa huu ni mkopo, jitihada ziwekwe zaidi katika urejeshaji wa mkopo huo kwa kuzingatia kuwa huu ni mkopo kwa mtoto siyo kwa mzazi.
 3. Vyombo vya usimamizi wa sheria na utoaji haki vionekane vinatenda haki sawa kwa watu wote na makundi yote bila kuacha ishara za fadhila au kukomoana.
 4. Wajibu wa serikali kikatiba katika kulinda uhai wa raia wake, uonekane unatekelezwa bila kuacha mwanya wa kuituhumu serikali. Ukiachwa mwanya katika ulinzi wa uhai wa raia, waweza kutumiwa na mamluki kujichukulia sheria mkononi kwa niaba ya serikali. Damu isiyo na hatia ina madhara kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo. Mpaka sasa tumeshuhudia umwagaji wa damu unaotusuta sisi sote na mamlaka zote. Mungu anatusuta watanzania kama alivyomsuta Kaini: “Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi” (Mwanzo 4:10).
 1. Uhai wa mtu una thamani isiyopimika. Ni wajibu usiokwepeka kuulinda na kuutunza uhai kwa vitendo halisi. Endapo uhai umepotea katika mazingira yoyote, uchunguzi huru na wa haki ufanyike na taarifa zitolewe kwa wakati muafaka ili kujenga jamii yenye imani kwa serikali na vyombo vyake. Matukio ya mauaji ya askari wetu, mauaji ya raia, majaribio ya kuwaua wanasiasa, utekaji, na uteswaji visipochunguzwa na kutolewa taarifa, ni shina la hofu na uchungu katika jamii. Jamii iliyojaa hofu na uchungu, haiwezi kuwa na maendeleo wala kuwa na roho ya uzalendo.
 2. Ili kulipatia taifa letu ufumbuzi wa mambo yote tuliyotaja na kushauri kwa wakati huu na ujao; tunaisihi serikali ya awamu ya tano, kurejea mchakato wa upatikanaji wa KATIBA MPYA ya wananchi, iliyopendekezwa na wananchi kupitia Tume ya Warioba. Watanzania wengi wanaona na kuamini kuwa KATIBA MPYA ina majibu ya kukidhi mahitaji ya taifa letu kwa sasa na baadaye. KATIBA MPYA ni zao la utashi wa Watanzania kupitia tume ya Warioba iliyokuwa na uwakilishi mpana wa taifa letu.
 3. Aidha, tunawashauri raia wema, kwa njia za kidemokrasia kupitia majukwaa ya kikatiba yaliyo katika maeneo yao, kudai upatikanaji wa KATIBA MPYA. Itapendeza ikiwa KATIBA MPYA itapatikana kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Mambo mazuri yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano yatadumu iwapo kuna KATIBA MPYA inayolinda mazuri. Kiongozi mzalendo si mbadala wa KATIBA MPYA. Tanzania yenye amani na maendeleo ni tunda la itikadi zote, dini zote, makabila yote na makundi yote chini ya KATIBA MPYA.

C. HITIMISHO

Kufufuka kwa Yesu Kristo ni kiini cha Matengenezo ya Kanisa. Kwamba, katikati ya jamii iliyokata tamaa na kutawaliwa na hofu, Kristo alifufuka na kuleta matumaini mapya. Kwamba, katikati ya wasiwasi wa Kanisa kupoteza nguvu ya utume wake, Roho Mtakatifu aliongoza Matengenezo ya Kanisa. Kwa hiyo Matengenezo ni endelevu katika jamii ya watu na taasisi zao. Muasisi wa Matengenezo Dr. Martin Luther yungali analiwajibisha Kanisa kuzingatia utume wake unaoleta matumaini mapya kila siku. Waliobatizwa wote ni wamisionari tunaotumwa na Bwana wetu Yesu Kristo (Yohana 20:21). Imetupasa kuwa nuru na chumvi ya jamii na kuwa mawakala wa uhuru, umoja na amani.

Taifa letu lilipata uhuru mwaka 1961 bila kumwaga damu. Roho ile ile ya majadiliano na maridhiano iliyokuwamo ndani ya waasisi wa taifa letu, inatakiwa kila wakati. Uhuru ulioletwa kwa majadiliano, utunzwe na kulindwa bila ulazima wa kumwaga damu ya watanzania. Uhuru na Umoja ndizo ngao zetu zilizolitunza taifa kwa zaidi ya miaka 50.

Sisi tulio maaskofu kwa neema ya Mungu, tunaleta wito kwenu wenye imani katika dini mbalimbali, kuliombea taifa letu. Kuwaombea wote wenye madaraka ili wajaliwe hekima, busara na upendo kwa taifa na watu wake. Kupitia jumuia ndogo ndogo na sharika zote, waombee viongozi wetu ili Mungu awajalie na kuwatunuku kiu ya kutenda haki, kusikiliza kuliko kusema, kuelekeza kuliko kuamrisha, kuunganisha kuliko kutawanya, kupenda watu kuliko kutamani kupendwa na watu, kutamani kutumika kuliko kutumikiwa (Marko 10:45), kuheshimu kuliko kuheshimiwa.

Ujumbe wa Pasaka unatuhimiza kuthamini uhai. Bwana wetu Yesu Kristo alikubali kufa ili kuhifadhi uhai wetu. Kwa kufa kwake na kufufuka, amekomesha kifo na mawakala wake. Tunaitwa kuthamini uhai na kutoruhusu tena watu kuteswa na kuuawa. Kwa hekima yote na unyenyekevu, tunasihi tena, kwamba ikubalike kuwa hitaji la watanzania walio wengi kwa sasa ni KATIBA MPYA. Katiba Mpya ipatikane ili kukuza na kuimarisha mfumo wa utawala utakaolinda uhai wa watu, raslimali za nchi, tunu za taifa, uhuru wa mihimili ya dola, na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi.

Tunawatakia Pasaka njema ya mwaka 2018, na Mungu awabarikini nyote.

Ni sisi

 1. Askofu Dkt. Fredrick O. Shoo, Mkuu, KKKT na Dayosisi ya Kaskazini
 2. Askofu Dkt. Benson K. Bagonza, Dayosisi ya Karagwe
 3. Askofu Dkt. Stephen I. Munga, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki
 4. Askofu Dkt. Alex S. Mkumbo, Dayosisi ya Kati
 5. Askofu Blaston Gaville, Dayosisi ya Iringa
 6. Askofu Dkt. Abednego N. Keshomshahara, Dayosisi ya Kaskazini Magharibi
 7. Askofu Andrew P. Gulle, Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria
 8. Askofu Dkt. Emmanuel Makala, Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria
 9. Askofu Chediel E. Sendoro, Dayosisi ya Mwanga
 10. Askofu Charles R. Mjema, Dayosisi ya Pare
 11. Askofu Elias Kitoi Nassari, Dayosisi ya Meru
 12. Askofu Dkt. Solomon Massangwa, Dayosisi ya Kaskazini Kati
 13. Askofu Jacob Mameo Ole Paulo, Dayosisi ya Morogoro
 1. Askofu Michael Adam, Dayosisi Mkoani Mara
 2. Askofu Isaya Mengele, Dayosisi ya Kusini
 3. Askofu Job Mbwilo, Dayosisi ya Kusini Magharibi
 4. Askofu Renard Mtenji, Dayosisi ya Ulanga Kilombero
 5. Askofu Ambele Mwaipopo, Dayosisi ya Ziwa Tanganyika
 6. Askofu Dkt. Alex G. Malasusa, Dayosisi ya Mashariki na Pwani
 7. Askofu Dkt. Edward Mwaikali, Dayosisi ya Konde
 8. Askofu Levis L. Sanga, Dayosisi ya Kusini Kati
 9. Askofu Amon Mwenda, Dayosisi ya Ruvuma
 10. Askofu Lucas Y. Mbedule, Dayosisi ya Kusini Mashariki
 11. Askofu Amon Kinyunyu, Dayosisi ya Dodoma
 12. Askofu Nicolaus Nsanganzelu, Dayosisi ya Mbulu
 13. Askofu Mteule Isaack Kissiri Laiser, Dayosisi Teule ya Magharibi Kati
 14. Askofu Mteule Wilson Sanga, Dayosisi ya Kusini Kati

Arusha, 15 Machi 2018

ACT-Wazalendo waikaba Polisi

MAHAKAMA Kuu kanda ya Dar es Salaam imekiruhusu chama cha ACT-Wazalendo kulishtaki Jeshi la Polisi Tanzania kwa kuzuia ziara za chama hicho. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Kesi hiyo namba 8 ya mwaka 2018 imepangwa kuanza kusikilizwa Aprili 4, mwaka huu mbele ya Jaji Ferdinand Wambari, Jaji Rehema Sameji, na Jaji Rose Teemba.

Chama hicho kimefunga shauri hilo kwa lengo la kulishtaki jeshi hilo kuacha kuingilia shughuli za chama hicho isivyo halali.

Frebruari 23 mwaka huu Kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe alitiwa mbaroni na jeshi la Polisi mkoani Morogoro kwa kudaiwa kufanya ziara kinyume na sheria.

Mkurugenzi awataka watendaji wake wajitathimini

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Sengerema mkoani Mwanza, Magesa Mafuru amewataka watendaji katika ofisi ya Ofisa maendeleo ya jamii kujitathimini katika utendaji wao wa kazi kutokana na kutuhumiwa kutoa mikopo kwa vikundi kwa upendeleo kinyume na utaratibu. Anaripoti Moses Mseti … (endelea).

Mkurugenzi huyo ametoa kauli hiyo leo wakati akitoa hundi ya mikopo yenye thamani ya Sh. 42 milioni kwa vikundi 30 vya akinamama wilayani humo, fedha ambazo zinatokana na mapato ya ndani.

Amesema Halmashauri ya Sengerema ina kata 26 vijiji 71 vitongoji 419 na kila sehemu kuna akinamama ambao nao wanatakiwa kunufaika na mikopo inayotolewa na serikali ili wajikwamue kimaisha.

Amesema anashangazwa kuona kila mwaka vikundi vinavyopewa mikopo ni vile vile huku akidai watu walipewa dhamana hiyo ya kusimamia utoaji mikopo wakitoa kinyume na utaratibu.

Mafuru amesema utendaji kazi wa mratibu wa mfuko wa wanawake unatia mashaka hivyo anatakiwa kubadilika na kutoa fursa sawa kwa wanawake wote wilayani humo na kumtaka kujitathimi utendaji kazi wake.

”Siwezi kutoa mkopo tena, endapo hakutakuwa na vikundi vya akinamama wengine kutoka kata zingine, kila mikopo inatolewa hapa mjini tu inanitia mashaka tunapaswa kubadirika,” amesema Mafuru.

Mwenyekiti wa wanawake wajasiliamali, Halmashauri ya Sengerema, Daline Matonange amekiri kuwepo kwa madhaifu hayo huku akiwataka watendaji kubadilika juu ya suala hilo na kufuata maelekezo waliyopewa na mkurugenzi huyo.

Mratibu wa Mfuko wa Wanawake wajasliamali wilayani humo, Noela Yamo alipotakiwa kujibu tuhuma hizo, amesema yeye ni sehemu ya watumishi wa halmashauri hiyo anayetakiwa kuzungumzia swala hilo ni afisa maendeleo ya jamii na siyo yeye licha ya baadhi ya vikundi kumtupia lawama kuwa anatoa mikopo kwa upendeleo.

Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Sengerema, Boniphace Kasasilo amesema maelekezo yote waliyopewa watayazingatia na kuyafanyia kazi na kuondoa dosari zilizojitokeza na kuvitaka vikundi vinavyodaiwa kurejesha mikopo kwa haraka.

Wananchi Mwanza wajutia kumchagua Mbunge

WAKAZI wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, wamejikuta wakizilaumu nafsi zao na kujutia kumchagua Mbunge wa jimbo hilo, Angelina Mabula kutokana na kile walichodai ameshindwa kutatua kero mbalimbali ikiwemo za migogoro ya ardhi. Anaripoti Moses Mseti … (endelea).

Wananachi hao wamesema kitendo cha mbunge huyo kushindwa kutatua migogoro ya ardhi katika kata za jimbo hilo, kimesababisha kujutia kumchagua na kwamba maamuzi waliyoyafanya mwaka 2015, hawawezi kuyarudia tena katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020.

Hatua ya wananchi hao inakuja kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi ya mara kwa mara ambayo inaonekana imeshindwa kupatia ufumbuzi na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya wilaya hadi Taifa.

Wananchi hao wametoa kilio chao siku chache zilizopita mbele ya mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella, ambaye alitembelea katika maeneo ya Shibula kwa lengo la kuzungumza na wananchi hao kuhusu mgogoro wa ardhi uliopo.

Mmoja wa wananchi hao, Maduhu Daud amesema kuwa tangu mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aingie madarakani hajawahi kutatua mgogoro wa ardhi katika wilaya hiyo.

Amesema kuwa wilaya hiyo, kila kona kumeshamiri migogoro ya ardhi lakini viongozi wenye dhamana, wameshindwa kuchukua hatua na kusababisha wananchi hao kuzurumiwa ardhi zao na watu wenye fedha na baadhi ya viongozi wa serikali.

Daud ameyataja baadhi ya maeneo yenye migogoro kwa muda mrefu ni Kitangiri katika maeneo ya jiwe kuu, mhonze, Busweru, maeneo yote yanayozunguka uwanja wa ndege wa mwanza, Kahama na Igombe.

“Mimi binafsi najuta sana kumchagua Mabula (Angelina Mabula) kwa sababu nilitarajia baada ya kuteuliwa kuwa waziri atasaidia kutatua migogoro ya ardhi kumbe ndio kabisa migogoro inazidi kushamili.

“Hawa wananchi wote unaowaona hapa, wanakabiliwa na migogoro ya ardhi kwa muda mrefu na chanzo cha migogoro hii inachangiwa na watumishi wa idara ya ardhi na baadhi ya viongozi (anawataja majina) na sasa hatuji hatima yetu,” amesema Daud.

Hata hivyo, Daud amesema wamekuwa wakifikisha malalamiko yao kwa mbunge huyo na wakati mwingine kuyafikisha kwa mkuu wa mkoa wa Mwanza lakini hakuna ufumbuzi wowote unaopatikana.

Neema Elias ni mkazi wa Kahama yeye kwa upande wake amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa migogoro ya ardhi kwa muda mrefu katika wilaya hiyo, pia kuna kero ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Amesema nusu ya wakazi wa wilaya hiyo wanatumia maji ambayo sio safi na salama na kwamba walio wengi maji wanayotumia ni ya visima na ziwa Victoria ambayo ni hatari kwa afya zao.

Elias amesema pamoja na ukosefu huo wa maji kwa muda mrefu lakini mbunge huyo hajawahi kuwaeleza ni lini wananchi hao watapata huduma ya maji safi na salama.

“Sisi ambao hatupati maji safi na salama tulishazoea hali hiyo na kuna tatizo lingine kwenye wilaya hii kuna tatizo la mgao wa maji watu wanakaa wiki hadi wiki mbili bila maji lakini tatizo hili hatufahamu litaisha lini,” amesema Elias.

Kutokana na hali hiyo, Elias ameiomba serikali kuangalia suala hilo na kuchukua hatua za haraka kwa kuwa migogoro ya ardhi na ukosefu wa maji safi na salama katika wilaya hiyo ni vya muda mrefu.

Mtandao huu, ulipomtafuta mbunge huyo ili kuzungumzia suala hilo, amesema amejitahidi kutatua migogoro katika jimbo lake kadri alivyoweza na kwamba hawezi kuchukua hatua za kutatua mgogoro kinyume cha sheria.

“Wananchi walio wengi wanataka nivunje sheria na mimi kuwa mbunge sio mpaka nivunje sheria nafanya kazi kulingana na sheria za nchi, tayari nimetatua migogoro kwa asilimia 90 kwa migogoro yote iliyonifikia kwenye jimbo langu,” amesema Mabula.

Mnyika, Heche wang’ang’aniwa Polisi, Mdee asakwa

JOHN Mnyika, Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, John Heche wamezuiliwa polisi kwa madai ya kuwa wameshindwa kufuata taratibu za dhamana. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Viongozi hao wa Chadema pamoja na wengine walifika Kituo Kikuu cha Polisi kuitikia wito kama walivyotakiwa na jeshi hilo.

Walioachiwa kwa dhamana ni Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu na Dk. Vicent Mashinji.

Mwalimu amesema Mnyika na Heche wamebaki polisi kwa maelezo kuwa wamekuwa wakikwepa taratibu za dhamana.

Heche na Mnyika hawakuripoti polisi Machi 16, 2018 huku chama hicho kikieleza kuwa moja ya sababu ya wabunge hao kutoripoti ni kutokana na kuhudhuria vikao vya kamati za Bunge mjini Dodoma.

Mbali na kina Mnyika na Heche kuzuiliwa kutokana na kutoripoti polisi kama walivyotakiwa, leo Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Ester Matiko hawajafika kutokana na kupata dharura.

“Mdee yupo nje ya nchi kwa matibabu na Ester Matiko yuko Dodoma kwa shughuli za kibunge amechelewa usafiri,” amesema Dk. Mashinji.

Jeshi la Polisi wametoa amri ya kukamatwa kwa Mdee na Matiko popote walipo kwa kosa la kutoripoti polisi leo kama walivyotakiwa kufanya hivyo.

Machozi ya Mbowe kwa JPM

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, ametoa waraka maalumu kwa Watanzania kuonesha kilio chake kwa nchi ilipo na inapoelekea. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Waraka Maalum wa Freeman Aikaeli Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai kwa Taifa

Leo tarehe 22 Machi 2018, mimi na viongozi wenzangu waandamizi wa Chadema tumetakiwa tena kuripoti Polisi.

Tunaokabiliwa na usumbufu huu ni pamoja na: Mhe Vincent Mashinji (Katibu Mkuu), Mhe. John John Mnyika, Mb na Naibu Katibu Mkuu Bara, Mhe. Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar; Mhe Halima J. Mdee, Mb, Mwenyekiti wa Bawacha, Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Mhe. John W. Heche, Mb, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti (Mara, Simiyu na Shinyanga) na Mjumbe wa Kamati Kuu; Mhe. Esther N. Matiko, Mb, Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Mara na Mweka hazina wa Bawacha Taifa.

Tuna taarifa pia ya kusudio la kumuunganisha Mhe. Peter Msigwa, Mb, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa (Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa) na Mjumbe wa Kamati Kuu katika shauri hili.

Historia ya wito:

Kwa muda wa wiki tano sasa, kufuatia sintofahamu kadhaa zilizojitokeza katika uchaguzi wa marudio wa Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam na Siha, Kilimanjaro, tumekuwa tukisumbuliwa kuripoti Polisi kila wiki kwa mashtaka ambayo hayajawahi kuwekwa bayana.

Katika kampeni na chaguzi hizi, palijitokeza mambo mengi ya ukiukwaji wa Haki za binadamu, ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, matumizi mabaya ya madaraka ya kiserikali, udhalilishaji na unyanyapaa dhidi ya Vyama vya Upinzani, mauaji na mateso kwa viongozi wa vyama vya Upinzani na hata Wananchi wasio na hatia.

Wakati nenda rudi hii ikiendelea, tuna taarifa (asante teknolojia) kuwa zinapangwa njama mahususi za kutubambikia viongozi wa Chadema kesi za Mauaji au Uhaini ili kuhalalisha azma ya Watawala kutuweka mahabusu kwa muda mrefu, wakidhani kwa kufanya hivyo watakuwa wamefanikisha ku sha na hata kuua kabisa uwepo wa Upinzani katika Taifa.

Jitihada hizo ni pamoja na kujaribu kuhusisha viongozi, wanachama na wapenzi wa chama chetu na tuhuma aidha za Kigaidi, Mauaji na hata Uhujumu wa Uchumi.

Mkakati huukKitaifa unashinikizwa na Rais John Pombe Magufuli na kuratibiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Dk Modestus Kipilimba, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, Jeshi la Polisi, na O si ya DPP.

“Viongozi” hawa, wasaidizi na washirika wao wamejazana matumaini hewa kuwa vuguvugu la mabadiliko na uhitaji wa demokrasia ya kweli na vita dhidi ya udikteta katika taifa hili litazimwa kwa “kuwa cha, kuwapoteza na hata kuwaua” viongozi wa Chadema na wanaharakati wengine wanaoamini katika uhalisia huu.

Naam, njama hizi zaweza kuua baadhi, kujeruhi baadhi na hata kupoteza kadhaa! Lakini kamwe, hazitazima njozi za Watanzania wema kupigania haki na ustawi katika nchi yao.

Naamini kwa kuzima uongozi wa Chadema uliopo leo, siyo tu kutaruhusu kuchipua kwa kasi kwa uongozi mbadala, bali pia kutaamsha ari ya taifa kuongeza juhudi katika harakati ili hatimaye kutokomeza udikteta na uongozi wa kiimla katika nchi yetu.

Taifa lina msiba! Wanasiasa, wanaharakati, wanahabari na hata wasanii wanateswa, wanafungwa, wanajeruhiwa na wengine kuuwawa! Wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje wanalia! Viongozi wa dini wanachanganyikiwa! Wakulima, wafugaji na wavuvi wako hoi! Hata watoto na wanafunzi nao ni tishio kwa watawala!

Taifa limejazwa hofu. Wengi hawasemi, lakini wanataabika rohoni. Wanaisubiri fursa iwavyo vyovyote vile.

Nguvu, majeshi na silaha zao, magereza na mifumo kandamizi haziwezi kuwa suluhu ya uimla huu. Tuimarishwe badala ya ku shwa.

Hatukimbii!! Tuko tayari kwa lolote, popote!

Shime Watanzania! Msitulilie! Lilieni watoto wenu na Taifa la kesho.

Na iwe vyovyote iwavyo! Damu, mateso, dhihaka dhidi ya maisha yetu iwe chachu ya dhati katika kutafuta Tanzania aliyoikusudia Mwenyezi Mungu yenye kusimamia haki, demokrasia, usawa, utu na ustawi kwa wote!!

Aluta Continua!!!

Freeman Aikaeli Mbowe

ATC yaleta taharuki Dodoma

NDEGE ya shirika la ndege la taifa (ATC), iliyokuwa imetokea Dar es Salaam kuja Dodoma leo Jumatano, imeshindwa kutua kwenye uwanja wa ndege mjini hapa kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa. Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Dodoma … (endelea).

Taarifa zilizothibitishwa na meneja wa ATC mkoani Dodoma, Harrieth Rutihinda zinesema, ndege hiyo iliyokuwa imewasili majira ya saa moja na nusu asubuhi, ililazimika kurejea Dar es Salaam, baada ya rubani kushindwa kuona njia za kutua.

“Ndege ilifika hapa katika muda wake wa kawaida. Lakini rubani alishindwa kutua kutokana na anga kugubikwa na ukungu. Akalazimika kurejea Dar es Salaam, ambapo baada ya hali ya hewa kutulia, ndipo ilipoanza tena safari ya kuja Dodoma,” ameeleza.

Kwa mujibu wa meneja huyo, pamoja na kwamba suala la ndege hiyo kushindwa kutua kwenye uwanja wa Dodoma kama lilivyopangwa limeleta usumbufu kwa abiria, lakini uamuzi wa rubani wa kurudisha ndege Dar es Salaam, ni uamuzi sahihi na wa kupongezwa.

Amesema, “kulikuwa hakuna namna. Uamuzi wa rubani wa kurudisha ndege Dar es Salaam, ni sahihi kuliko kama angeamua kuirudisha chini wakati njia hazioni kutokana na giza lililotanda.”

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wetu ambaye alikuwa abiria kwenye ndege hiyo anasema, rubani alitumia muda mwingi kuzunguuka eneo la uwanja wa ndege wa Dodoma, kwa lengo la kutafuta njia bora na salama ya kutua.

“Wakati wote rubani alipokuwa anazunguuka uwanja, roho zetu zilikuwa zikitweta kwa hofu. Tunashukuru Mungu kuwa aliongozwa na maombi na hivyo kuamua kurejea Dar es Salaam,” ameeleza.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo ambaye ni mbunge wa Bunge la Muungano, ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria kadhaa wakiwamo viongozi na mizigo lukuki, jambo ambalo lilimfanya rubani “kutua kwa riski.”

Shirika la ndege la ATC ambalo lilikuwa moja ya mashirika makubwa ya ndege katika ukanda huu wa Afrika Mashariki kabla ya kuteteleka, sasa limeanza kuimarika baada ya serikali kununua ndege zake yenyewe.

Kwa muda mrefu, ATC lilikuwa linaendeshwa kwa ndege za kukodi, jambo ambalo limeingiza shirika na serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.

Watengeneza pombe feki, wakwepa kodi wagunduliwa

IMEBAINIKA kuwa hadi sasa kuna kampuni 11 ambazo zinadaiwa kujihusisha na utengenezaji pombe kali zisizokuwa na viwango ambazo zimekuwa zikisambazwa sokoni kinyume na sheria. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Mbali ya kampuni hizo kutokutengeneza pombe ambayo hazina viwango hazilipi kodi kama ambavyo zinapaswa kufanya kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa nyaraka kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo mwandishi amefanikiwa kuziona, zimeonyesha kampuni hizo zimelipa sh. 13,566,400 kuanzia Novemba mwaka 2016 na sh. 7,150,000 katika kipindi cha Februari mwaka jana.

Hali hiyo imebainika kutokana na malalamiko kuhusu uwepo wa pombe zisizokuwa na viwango zinazotishia afya za watumiaji na serikali kukosa mapato, imebainika baadhi ya kampuni zinazozalisha pombe hizo hazilipi kodi.

Aidha kampuni mbili zililipa kodi kwa miezi 12 pekee kati ya Januari mwaka 2016 hadi Desemba mwaka jana huku kampuni nyingine ikiwa imelipa kodi katika kipindi cha miezi tisa pekee ndani ya miaka miwili.

Nyaraka hizo zilionyesha kuwa kampuni nyingine iliyoko Mwanza imelipa kodi kwa kipindi cha miezi minne licha ya kufanya shughuli zake kwa miaka miwili.

Pia kampuni nyingine ya pombe kali iliyoko Moshi mkoani Kilimanjaro, ililipa kodi kwa miezi minne kuanzia Januari mwaka 2016 hadi Desemba mwaka jana, kiasi ambacho sawa na kilicholipwa na kampuni nyingie ya vinjwaji hivyo iliyoko Dar es Salaam.

Pia nyaraka hizo zilionyesha uwepo wa kampuni ambayo imelipa kodi kwa mwezi mmoja pekee katika kipindi cha miaka miwili huku nyingine ikilipa kodi kwa miezi saba katika kipindi hicho cha miaka miwili.

Pia zimeonyesha kuwa kampuni nyingine ililipa kodi kwa miezi mitatu pekee huku kampuni moja pekee ya pombe hizo ikiwa imelipa kodi kwa kwa kipindi chote isipokuwa mwezi Aprili na Mei mwaka jana.

Kuibuliwa kwa nyaraka hizo kumekuja wakati ambapo serikali imekuwa ikitoa msisitizo kwa wawekezaji wazawa kuwekeza kwenye viwanda kwa lengo la kutengeneza ajira na mapato ya kodi serikalini.

Akiongoza mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Jumatatu, Rais John Magufuli, alisisitiza umuhimu wa viwanda huku akiwataka wawekezaji kulipa kodi stahiki serikalini.

Hata hivyo licha ya Rais Magufuli, kuwataka wazawa kutumia bidhaa za ndani, bado kuna uwepo wa pombe kali zisizokuwa na viwango.

Mapema mwaka huu wazalishaji wa pombe hizo wakiwemo na wadau mbalimbali wa biashara waliiomba serikali kuchukua hatua dhidi ya bidhaa hizo zisizokuwa na viwango ili kulinda bidhaa halali sokoni.

Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), kupitia kwa mwenyekiti wao Mkoa wa Dodoma, Deus Nyabiri, alisema serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo.

“Si haki kwa wafanyabiashara haramu kuendelea kutawala sokoni. Hii inasababisha ushindani usiokuwa na usawa dhidi ya wafanyabiashara halali ambao wamekuwa wakiunga mkono serikali kwenye uwekezaji wa viwanda,” alisema.

Aliongeza kuwa wawekezaji wanapaswa kuelewa dhamira ya serikali ya kuifanya nchi kuwa ya viwanda hivyo ni muhimu wakaiunga mkono badala ya kwenda kinyume.

Kwenye Vikao vya Bunge la Februali mwaka huu, baadhi ya wabunge waliitaka serikali kuongeza nguvu kupambana na biashara ya pombe zisizokuwa na viwango kwani zimekuwa zikiuzwa kwa bei nafuu na kuhatarisha afya za watumiaji.

Wakizungumza wakati akichangia hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira, walisisitiza pia baadhi ya viwanda vinavyojihusisha na utengenezaji wa pombe hizo havilipi kodi.

“Kwanini serikali inachukua muda mrefu kukabiliana najambo hili linaloathiri viwanda na kusababisha serikali kukosa mapato,” amesema Mbunge wa Jimbo la Mtera (CCM), Livingstone Lusinde.

Amebainisha kuwa licha ya serikali kuzuia baadhi ya pombe kali lakini pombe hizo zimekuwa zikiingizwa sokoni kwa mtindo mwingine.

Lusinde amesema baadhi ya pombe hizo zimekuwa hazina stika za TBS na TRA na kusababisha kutofahamu ubora wake.

Aliitaka serikali kutoa taarifa kamili ya namna ilivyoweza kukabiliana na sakata hilo.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha hoja hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Suleiman Saddiq, aliitaka serikali kuchukua hatua kali kwa viwanda bandia vinavyotengeneza pombe kali kwa kuwa vimekuwa vikikwepa kodi kwa kuweka stika feki TRA.

Mbunge huyo wa Mvimero (CCM), alishauri kubadilishwa mfumo wa utoaji stika za TRA kwa kuwa zimekuwa zikighushiwa na kusababisha upotevu wa mapato.

IGP, DCI ‘wamkimbia’ Nondo mahakamani Dar

WAKATI Mwenyekiti wa Mtandao wa Wananfunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo akipandishwa kizimbani leo asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam nayo imeanza kusikiliza kesi ya Nondo dhidi ya Serikali, akidai haki ya uwakilishi pamoja na dhamana. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mawakili wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), na wale wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wakiongozwa na Mpoki Mpare na Jebra Kambole wamefika mbele ya Jaji Rehema Semeji na kuwasilisha mashtaka dhidi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mwanasheria Mkuu (AG) na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP).

Katika kesi hiyo namba 49 ya mwaka 2018, mawakili hao wameiomba mahakama kuiamuru serikali kutoa dhamana na kuruhusu haki ya uwakilishi kwa mteja wao Nondo.

Amesema, “Maombi haya yalifunguliwa dhidi ya DCI, IGP, AG tukiomba mahakama kutoa amri ya kuletwa mahakamani kwa mwanafunzi Nondo au kumuachia kwa dhamana kwani ameshikiliwa na polisi kwa muda mrefu bila sababu za msingi kutolewa”

Jaji Sameja ameutaka upande wa Jamhuri kujibu hoja za utetezi Machi 26, 2018.

Jaji Semeji amesikilia maombi hayo na kueleza kuwa shauri hilo litaendelea kusikilizwa Aprili 4 Mwaka huu.

Nondo ambaye ni Mwanafunzi wa Mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitivo Sayansi ya Siasa na Utawala amefikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa.

Na kusomewa mashtaka mawili na wakili wa serikali Abeid Mwandalamo mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, John Mpitanjia.

Mwandalamo Amedai kuwa kosa la kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni Machi 7, 2018 akiwa eneo la Ubungo Dar es Salaam na kuzisambaza kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp kwamba yupo hatarini.

Katika shtaka la pili, ni kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma Mafinga alipokuwa anatoa taarifa kwa askari kwenye Kituo cha Polisi Mafinga kwa kusema kuwa alitekwa na watu wasiojulikana Dar es Salaam na kupelekwa kiwanda cha Pareto Mafinga. Hata hivyo, Nondo alikana mashtaka hayo.

Mwanadalamo amedai ushahidi bado haujakamilika hivyo wanaomba siku chache, kwa kipindi watakachokuwa wanafanya upelelezi mtuhumiwa asipewe dhamana.

Amedai kuwa kwa sababu bado wanafanya upelelezi kwa rafiki wake wa karibu, kama atapewa dhamana anaweza kuingilia na kuharibu upelelezi huo.

Hata hivyo Wakili wa utetezi, Chance Luwoga amesema mashtaka aliyosomewa Nondo yanaruhusu kupewa dhamana hivyo hakuna sababu za msingi za kuzuiliwa kwa dhamana ya mteja wake.

Hakimu Mpitanjia amesema kuwa Mahakama hiyo itatoa uamuzi juu ya dhamanda ya mshukiwa huyo tarehe 26 Machi.

Wafuasi wa Mange Kimambi waanza kuwekwa mbaroni

JESHI la polisi mkoa wa Dodoma linawashikilia watu wawili kwa makosa ya kutumia vibaya mitandao ya kijamii kwa madai ya kuchochea maandamano ya nchi nzima ambayo yanakusudiwa kufanyika Aprili 26 mwaka huu. Anaripoti Dany Tibason … (endelea). 

Maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika Aprili 26 mwaka huu, yanayohamasishwa na Mange Kimambi anayeishi nchini Marekani kwa lengo la kupinga mwenendo wa nchi kwa sasa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema jeshi hilo limewakamata watu wawili ambao wanatumia vibaya mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuchochea maandamano nchi nzima kinyume na taratibu za nchi.

“Kwa muda mrefu sasa kwa makusudi na wakitambua kuwa ni kosa kisheria, baadhi ya watu wasiopenda amani na utulivu wa nchi wanatumia vibaya mitandao ya mawasiliano kuvunja sheria na kuhamasisha chuki dhidi ya serikali kuhamasisha maandamano yasiyo halali yenye viashiria vya kuvuruga amani ya nchi waliyopanga kuyafanya nchi nzima siku ya tarehe 26/4/2018.

“Hapa Dodoma tumekamatwa watu wawili ambao kwa makusudi kwa kutumia mitandao ya simu wanasambaza maneno yenye uchochezi dhidi ya serikali, wanatishia usalama wa nchi wanahamasisha maandamano ya nchi nzima yenye viashiria vya uvunjifu wa amani,” amesema Muroto.

Kamanda Muroto amewataja waliokamatwa kuwa ni Amandus Machali (31) dereva wa NHIF na mkazi wa Kigamboni geti jeusi jijini Dar es Salaam na Yuda Mbata (29), mkulima na mkazi wa kijiji cha Mpanatwa wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Katika tukio lingine Kamanda Muroto amesema kumetokea vifo vya watu watatu wa familia moja katika kijiji cha Gwandi katika wilaya ya Chemba mkoani Dodoma kutokana na watu hao kuangukiwa na ukuta wa nyumba wakiwa wamelala.

Amesema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 18, mwaka huu usiku katika kijiji hicho na kusema chanzo cha vifo hivyo ni kutokana na kuta za nyumba kulowana na maji ya mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali mkoa wa Dodoma.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Misa James (25) Happy James (2) na Mbalu James ambaye hakumtaja umri wake.

Ni sarakasi, Polisi Vs Nondo, Daruso, LHRC

BADO hakijaeleweka. Wakati Mawakili wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) na Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) wakimsaka Abdul Nondo, Jeshi la Polisi bado halijataja alipo. Anaripoti Mwandishi wetu…(endelea).

Daruso na LHRC wamekuwa wakimtafuta Nondo ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchi (TSNP) ili kumwekea dhamana baada ya kuwa mikononi mwa Jeshi la Polisi zaidi ya wiki moja na nusu iliyopita, bado hawajafanikiwa. mpaka sasa Nondo hajapewa dhamana.

Taarifa za awali zinaonesha kuwa Nondo ameshikiliwa na Kituo Kikuu cha Kati cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ambapo LHRC na Daruso walikwenda kufuatilia taratibu za kumwekea dhamana. Hata hivyo, walijibiwa hayupo kwenye kituo hicho.

Leo Mawakili wa LHRC, Jebra Kambole, Jones Sendodo na Reginard Martine ndio walioongoza safari ya kwenda kituoni hapo kwa lengo la kumwekea dhamana Nondo. Hata hivyo polisi walimweleza ‘hayupo hapa.’

Wakati wakiendelea kumsaka Nondo, jana Mawakili hao wa LHRC walifungua kesi ya kulitaka Jeshi la Polisi kumwacha Nondo au kumfikisha mahakamani kulingana na sheria za nchi zinazokataza mwananchi ama raia kuwekwa kituo cha polisi kwa zaidi ya saa 48.

Keshi hiyo itaanza kusikiliza kesho Machi 21 na Jaji Rehema Sameji. Kesi hiyo inalenga kulishikiza Jeshi la Polisi kumpeleka mahakamani au kumwamcha huru Nondo ambaye ni Mwanafunzo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wakili Jones ameuambia mtandao huu kwa njia ya simu kwamba walifika kituoni na kuelezwa kuwa, Nondo hayupo kituoni hapo.

“Tulienda kwenye Ofisi ya Kamanda Mambosasa (Lazaro Mambosasa-Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam), tumeambiwa yupo kwenye kikao.

“Tumepiga simu zake, hapokei. Hata hivyo, Kamanda Mambosasa amekuwa akitukwepa na kuwaambia waandishi kuwa sisi tunaishia mapokezi kitu ambacho sio cha kweli,’’ amesema Sendodo.

Amesema kuwa, mawakili wa LHRC wamekuwa wakipamba ili Nondo apate haki ya kikatiba ya kupata dhamana.

Taarifa zilizoufikia mtandao huu kuwa, uongozi wa (Daruso) chini ya Rais wake Jilili Jeremiah wamefika kituoni hapo na barua za kumdhamini Nondo bila mafanikio.

Vyanzo vyetu vya uhakika vimemuona Jilili na wenzake wakiwa kituoni hapo na barua za udhami ni kwa ajili kumdhamini Mwanafunzi mwenzao.

Yanga sasa kuja kidigitali

KLABU Yanga imezindua kipindi cha televisheni kilichopewa jina la ‘Yanga TV Show’ sambamba na mfumo wa kuwapa habari wanachama wake utakaoitwa ‘Yanga Kidigitali’ vinavyotarajiwa kuanza Aprili Mosi Mwaka huu. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Kipindi cha Yanga TV Show kitakuwa kinarushwa kupitia kituo cha televisheni cha Azam TV wakati mfumo wa kutoa habari kwa wanachama wa Yanga Kidigitali utakuwa unapitia kampuni ya simu za mkononi za Tigo pamoja ya Prime.

Meneja wa michezo wa Azam Tv, Baruhan Muhuza amesema wameingia makubaliano na klabu ya Yanga ya uanzishwaji wa kipindi hicho baada ya majadiliano ya muda mrefu ili kufanya kipindi hicho kuwa cha tofauti.

“Yanga TV Show itakuja na muonekana mpya na wakipekee kwa kuwa itahusisha wachezaji wa zamani wa klabu hii kufanya uchambuzi katika michezo iliopita na itakayokuja katika Ligi Kuu pamoja na kuwajua mwenendo mzima wa timu inapokuwa ndani na nje ya Uwanja,” amesema Muhuza.

Aidha aliongezea ya kuwa Yanga kuwa na kipindi cha televisheni itakuwa fulsa kwa klabu katika kujiongezea mapato kwa kuwa kipindi kinaweza kupata wadhamini kutokana na kuwa cha tofauti na kufanya klabu hiyo iweze kujiendesha yenyewe kwa kuwa na vyanzo vingi vya mapato.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa amesema kuanzisha Yanga TV Show na Yanga Kidigitali ni mikakati ya kuwapa fulsa wanachama wa klabu hiyo kupata habari za timu yao ikiwa pamoja na kujipatia kipacho ambacho kitaifanya waweze kujitegemea kwa kipato.

Abdul Nondo atikisa

JESHI la polisi nchini, bado linaendelea kumshikilia, kinyume na sheria za nchi, Abdul Nondo, mwanafunzi wa mwaka wa tatu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kwa madai ya “kujiteka.” Anaripoti Saed Kubenea…(endelea).

Taarifa zinasema, Nondo anayeshikiliwa na jeshi hilo, tokea tarehe 7 Machi mwaka huu – siku zaidi ya 13 sasa – amenyimwa haki yake ya “kikatiba” ya kukutana na mawakili wake na ndugu zake.

Mwanafunzi huyo ambaye ni mwenyekiti wa mtandao wa wanafunzi wa vyuo vikuu (TSNP), alipotea katika mazingira ya kutatanisha, majira ya saa 5 hadi 6 usiku wa tarehe 6 Machi, huku baada ya kutuma ujumbe unaosema, “I AM AT HIGH RISK” (usalama wangu uko hatarini).

Mara baada ya Nondo kutuma ujumbe huo, taharuki kubwa iliibuka jijini Dar es Salaam kutokana na kutojulikana, nini hasa kilichomsibu kiongozi huyo wa wanafunzi.

Aidha, jeshi hilo halijaweza kumfikisha kumfikisha mahakamani kujibu kile polisi wanachoita, “tuhuma za kusingizia kujiteka.”

Kupatikana kwa taarifa kuwa Nondo amepotea, kulikuja takribani wiki mbili baada ya mauaji ya Akwilina Akwiline, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo cha usafirishaji cha taifa (NIT).

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi “iliyorushwa na askari wa jeshi la polisi,” wakati jeshi hilo likidai kukabiliana na wafuasi Chadema, waliokuwa wanaelekea kwa msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kinondoni, kushinikiza kupewa hati za viapo kwa mawakala wake kusimamia uchaguzi.

Nondo, ni mmoja wa wanafunzi, ambaye amekuwa mstari wa mbele kushinikiza baadhi ya viongozi wa jeshi la polisi na wizara ya mambo ya ndani, akiwamo waziri wa wizara hiyo, Mwigullu Nchemba, kuwajibika kwa mauaji ya mwanafunzi huyo.

Nondo ayeripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha, alipatikana akiwa hai eneo la Mafinga mkoani Iringa. Alidai kuwa alijikuta katika eneo hilo, baada ya kuzinduka kutoka katika lindi la usingizi na kuwauliza wenyeji wa eneo hilo mahali aliko.

Baadaye alijisalimisha kituo cha polisi Mafinga, kabla ya kufikishwa makao makuu ya polisi mkoani humo kwa mahojiano.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kamanda wa polisi kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amekiri jeshi lake kumshikilia Nondo.

Mambosasa amesema, Nondo hakuwa ametekwa, bali alikuwa akiendelea na shughuli zake za kawaida, kwa kumtembelea mpenzi wake.

Alisema, “taarifa kuwa Abdul Nondo aliyedaiwa kupotea katika mazingira ya kutekwa, ulikuwa ni uzushi kwani hakutekwa isipokuwa alikuwa kwa mpenzi wake.”

Hata hivyo, maelezo ya Mambosasa, yanatofautiana na ile ya jeshi la polisi mkoani Iringa, kuwa “Nondo alifika kituoni hapo akiwa hajitambui.”

Tayari mawakili wa Nondo wamewasilisha mahakama kuu maombi rasmi ya kutaka mwanafunzi huyo afikishwe mahakamani. Katika kesi hiyo, washitakiwa ni mkurugenzi wa mashitaka (DPP), mwanasheria mkuu wa serikali (AG) na mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP).

Nayo serikali ya Marekani, imetaka serikali ya Tanzania, kuingilia kati suala hilo na kusikitishwa na vitendo vya utekaji na ukatili nchini.

Kuuza na kununua kemikali mpaka cheti

MKEMIA Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele ameagiza kuwa kila mtu atakayeuziwa au kununua kemikali lazima aoneshe cheti cha usajili kwa kuwa sheria inaagiza kila anayehusika na kemi kali ni lazima asajiliwe. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Mbali na hilo amesema tangu kutungwa kwa Sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani mwaka 2003, taasisi zaidi ya 3,000 zimesajiliwa na Mkemia Mkuu wa serikali.

Prof. Manyele ametoa kauli hiyo alipokuwa akifungua mafunzo ya wauzaji, wasafirishaji, wahifadhi na watumiaji wa kemikali katika kanda ya kati Dodoma.

Amesema anayeleta athari ni mtumiaji wa kemikali ni yule asiyefuata taratibu na kuwa chanzo cha madhara kwa wananchi.

“Wafanyabiashara mnaotumia kemikali mmeingia kwenye ‘level’ ya juu, tuwaombe sana hizo shughuli zenu msije mkathamini biashara zenu mkasahau afya ya watanzania na mazingira yetu ni kosa kisheria,” amesema Prof. Manyele.

Hata hivyo amesema adhabu itatolewa kwa kuzingatia kiwango cha mtaji wa biashara yako.

“Niwaombe sana muwe mnazingatia hii sheria kwa kuwa kemikali nyingi zilikuwa zinaingia nchini kiholela na watumiaji wengi walikuwa wanaingiza kiholela,” amesema Mkemia huyo.

Amesema kuwa serikali inasisitiza kufuata sheria bila shuruti na kufuata taratibu zilizoainishwa kisheria.

“Wapo watu ambao shughuli zao za siku nyingi na hawajapata usajili, lakini wote mtapata usajili uliosawa, niwaombe usimamizi na utekelezaji wa sheria unapaswa uzingatiwe sana,” amesema.

Amebainisha kuwa unaposajili kampuni wale watakaosimamia shughuli wawe waajiriwa na ikiwezekana ofisi ya Mkemia ione barua zao za ajira.

“Udhibiti kwasasa ni wa kiwango cha juu tangu sheria hii ianze kutumika ndani ya miaka 13 ambapo tumeweka mifumo ya udhibiti,” amesema.

Hata hivyo amesema wale wanaoingiza kutoka nje ya nchi udhibiti ni kubwa sana hivyo wajipange vizuri kwenye maeneo yote kwa kuwa atahakikisha anasimamia shughuli za kemikali kikamilifu.

“Serikali ina uwezo wa kutambua aina za kemikali na kiwango cha kemikali zinazoingia na zinaenda wapi, serikali inaendelea kuongeza kasi katika kuzuia matumizi yasiyo sahihi ya kemikali,” amesema.

Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo, Mkemia huyo amesema ni muhimu kwa kuwa mbinu za matumizi ya kemikali zinabadilika hivyo ni vyema kupata mafunzo mara kwa mara.

Dodoma waomba muda vitambulisho vya Taifa

WAKAZI wa kata ya Kizota Manispaa ya Dodoma ambao kwa hivi sasa wapo kwenye zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya taifa, wameomba muda uongezwe ili kuondokana na changamoto ya kukaa muda mrefu kwenye vituo vya kuandikishia. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Wakizungumza wakati wa kuandikisha vitambulisho hivyo katika kata ya Kizota baadhi ya wakazi hao wamesema, kutokana na muitikio wa wananchi kuwa wengi tunaomba muda uliowekwa wa siku tatu uongezwa kwa kuwa ni mdogo.

Fred Kombe mkazi wa Kizota amesema kuwa kutokana na wingi wa wananchi wanaojitokeza kwenye vituo, tunaomba serikali kuangalia kwa umakini ili zoezi hilo liweza kuwafikia watu wote.

“Kutokana na umuhimu wa zoezi hili tunaomba serikali iangalie kwa makini hii ni kutokana na mwitikio mkubwa uliotolewa kwa wanchi wa kuona faida ya kuwa na kitambulisho cha uraia,” amesema.

Naye Nazaeli Julias amesema kuwa muda ambao umepangwa kuna hatari wa wakazi wengi kuikosa fursa ya kujiandikisha kwa wakati, hivyo ni vizuri serikali ikatafakari ili kuwepo kwa muda wa kutosha.

Kwa upande wake, Afisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) mkoa wa Dodoma, Khalid Mrisho amesema kuwa licha ya kukabiliana na watu wengi lakini wamefanikiwa kuweka mashine nyingi ili kuhakikisha kila mmoja kuweza kuandikishwa.

“Pamoja na wingi wa watu wanaofika kujiandikisha bado mashine hizo zina uwezo wa kukabiliana na changamoto kutokana na kuwa na asilimia kubwa ya kuwaandikisha watu wote wanaofika kwenye vituo vya uandikishaji,” amesema.

Naye Mkuu wa Uhamiaji mkoa wa Dodoma, Peter Kundy ambaye ofisi yake inashirikiana bega kwa bega na NIDA, amesema kuwa lengo ni kuhakikisha vitambulisho vinapatikana kwa wananchi wote na kuhakikisha wageni wenye sifa waweze kupata na kutojipenyeza watu wasio na sifa kuweza kupata.

Amesema zoezi hilo la uandikishaji wa vitambulisho vya taifa linaendelea katika kata mbalimbali za mkoa mbali hapa Dodoma ili kuwawezesha wananchi wake kupata vitambulisho hivyo.

Mawaziri hawa hawako salama

WAZIRI wa Kilimo, Charles Tizeba na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina siku zao zinahesabika kutokana kushindwa kuhudhuria bila kutoa taarifa kwenye Mkutano ulioitwa na Rais Jonh Magufuli. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mkutano huo uliwakutanisha wafanyabiashara na watendaji waandamizi wa Serikali, ulifanyika jana Ikulu, Dar es Salaam ni wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ambalo Mwenyekiti wake ni Rais Magufuli.

Rais John Magufuli aliulizia uwepo wa mawaziri hao kwa Waziri Mkuu, Kassim majaliwa ambaye hakuwa na taarifa za kutokuwepo kwao ingawa aliwapa mwaliko wa kuwataka kuhudhuria kwani wao ni wajumbe wa mkutano huo. Hata hivyo mawaziri hao hawakutuma wawikilishi wao kwenye mkutano huo muhimu.

Kutokuhudhuria kuligunduliwa na Rais Magufuli baada ya kumtaka waziri Mpina ajibu masuala mbalimbali yaliyoibuliwa na Fuad Abri, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Asas Dairies ya Iringa kuhusu bidhaa za maziwa.

Mpina hakuwepo yeye wala mwakilishi kutoka katika wizara yake, baadaye Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Kilimo, Tizeba aliyekuwa waziri wa wizara hiyo kabla hajaigawa lakini naye hakuwepo.

Waziri Majaliwa alisema kuwa Mawaziri wote wanaoguswa na sekta za uwekazaji hasa kwenye kilimo na mifugo hivyo walikuwa wanapaswa kuwepo kwenye mkutano huo.

Rais Magufuli alisema inasikitisha kuona baadhi ya watu aliowateua hawajaelewa anataka nini. Alisema inashangaza kuona wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali nchini wamekutana na Serikali kuzungumzia masuala ya kilimo na mifugo, lakini mawaziri wa sekta hizo hawapo.

Alipotafutwa kuzungumzia kutokuwapo kwake katika mkutano huo, Mpina alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo, bali anafuatilia kwa ukaribu kujua nini kimetokea katika mawasiliano hayo.

Ni Wazi Rais Magufuli anayeipigania Tanzania ya Viwanda kwa kuboresha sekta na mazingira rafiki kwa wawekezaji hususani katika eneo la biashara, kilimo na ufugaji hataweza kuvumilia kitendo hiki kinachodhihirisha nia mbaya kwa mazingira ya ukuaji viwanda nchini.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alikuwa safarini mkoani Kigoma kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mifugo, Uvuvi na Maji. Na katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Yohana Budeba alisema yupo kikazi mjini Dodoma

Nondo ‘awaponza’ Sirro, AG na DCI

MAWAKILI wanaomwakilisha Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchini (TSNP), Abdul Nondo wamefungulia kesi Mkuu wa jeshi la Polisi nchini (IGP), Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai (DCI), Mwasheria Mkuu wa Serikali (AG), kwa kumshikilia kwa zaidi ya saa 48 mwanafunzi huyo. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Nondo alitoweka jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Machi 8, mwaka huu kabla ya kupatikana wilayani Mafinga, Iringa ambapo alidai kuzinduka na kujikuta eneo hilo baada ya kutekwa na watu wasiofahamika. Hata hibyo taarifa ya Jeshi la Polisi imedai kuwa kijana huyo hakutekwa bali alienda mkoani humo kumtembelea mpenzi wake.

Tangu tarehe 8 Machi mwaka huu, polisi wanamshikilia mwanafunzi huyo, ikiwa ni zaidi ya siku 11 sasa. Awali alisafirishwa kutoka Iringa mpaka Dar lakini haijajulikana amehifadhiwa katika kituo gani cha polisi huku mawakili na ndugu zake wakidai kuzuiwa kumuona kwa kipindi hicho chote.

Mawakili wa mtandao huo wakiongozwa na Jebra Kambole, Jones Sendodo na Reginald Martine wamefungua shauri la kumtaka IGP, AG na DCI wajieleze kwanini wanaendelea kumshikilia Nondo, na kisha wamuachie kwa dhamana kijana huyo au wamfikishe mahakamani haraka, hilo kwenye mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam kushinikiza kufikishwa mahakamani kwa Nondo.

Wakili Jones Sendodo ameiambia MwanaHALISI Online ameeleza kuwa kesi hiyo imeshafunguliwa na imepangiwa Jaji na kwamba itasikilizwa Tarehe 21 Machi.

Wakili Sendodo amesema kuwa Jeshi la Polisi linatakiwa limmpeleke mahakamani Nondo ili kumshtaki kwa mashtaka wanayoyadai au wamuachie kwa dhamana ya polisi kama bado hawajakamilisha upelelezi.

“Polisi wanaendelea kumshikilia ilihali sisi mawakili wake hawaturuhusu tumuone.”

Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambasasa aliripotiwa hivi karibuni akisema kuwa bado wanaendelea na upelelezi kwenye kesi hiyo na kwamba watamfikisha mahakamani upelelezi ukikamilika.

Makunga ajiuzulu, TEF waridhia

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeridhia kujiuzuru kwa Mwenyekiti wake Theophil Makunga aliyeomba kujiuzulu. Anaripoti Angel Willium … (endelea).

Makunga aliomba kujiuzulu jana Ijumaa kwa kuuandikia uongozi wa jukwaa hilo.
Kutokana na uamuzi huo wa Makunga, TEF walikutana katika mkutano wa dharura na kuridhia barua yake.

Katika ujumbe uliosambazwa na TEF na kusainiwa na Katibu wake, Neville Meena, umeeleza kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wake watakosa busara zake ambazo bado zilikuwa zinahitajika katika ukuaji wa taasisi hiyo.

TEF inamtakia kila la kheri Makunga katika majukumu yake mengine.

Wambura hatunaye tena katika soka

KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imemfungia maisha kutojiusisha na soka Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Michael Wambura baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka matatu yaliyokuwa yakimkabili. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Wambura amekupewa adhabu hiyo baada ya kukutwa na hatia ya kupokea fedha zisizo halali kiasi cha Sh. 84 milioni, pamoja na kukutwa na hatia ya kujipatia fedha, kwa njia ya udanganyifu na kughushi nyaraka sambamba na kula njama ya kulipwa fedha na waliokuwa viongozi wa TFF Jamari Malinzi na Celestine Mwesigwa ambao kwa sasa wanakabiliwa na kesi Mahakamani.

Kamati hiyo imetoa hukumu kwa Wambura kutojihusisha na soka kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013. Baada ya kupatikana na makosa matatu, kamati hiyo ya maadili imefika maamuzi hayo kwenye kikao chao walichokutana jana (Jumatano).

Jana mchana afisa habari wa TFF Clifford Mario Ndimbo aliwaambia waandishi wa habari kwamba Wambura amefanya makosa hayo huku akijua anashusha hadhi ya shirikisho hilo ikiwa ni kinyume na katiba ya TFF.

Marekani yachunguza serikali ya JPM

WAJUMBE wawili kutoka nchini Marekani kutoka katika kitengo cha Mshauri wa Marekani kinachohusu Siasa na Uchumi wametua nchini kwa kile kinachodhaniwa kuchunguza Serikali ya Tanzania Bara inayoongozwa na Rais John Magufuli na ile ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Dk. Ali Mohammed Shein. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Wajumbe hao watajikita katika masuala makuu mawili; hali ya kisiasa pamoja na uchumi. Tayari wajumbe hao wamekutana na Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF).

Taarifa za awali zinaeleza, msukumo huyo unatokana na kuyumba kwa hali ya kisiasa nchini pamoja malalamiko ya kusinyaa kwa uchumi.

Hofu na wasiwasi nchini imeanza kumeya hasa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambapo mpaka sasa, watu wamekuwa wakitoweka/kupotea, kukutwa wameuawa pamoja na wengine kujeruhiwa.

Hali hiyo imetia msukumo wa wasiwasi na hata wengine kuhama nchi wakihofia kuuawa. Tayari watu kadhaa wamepata hifadhi ya ukimbizi nje ya Tanzania kutokana na hofu ya kuuawa akiwemo aliyekuwa mwandishi wa gazeti la MwanaHALISI, Ansbert ngurumo ambaye amehifadhiwa nchini Finland.

Miongoni mwa waliopotea na wanaotafutwa na ndugu zao mpaka sasa ni pamoja na Ben Saanane, aliyekuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda.

Kwenye orodha ya watu waliouawa katika mazingira tatanishi ni pamoja na John Daniel, aliyekuwa Katibu wa Chadema Kata ya Hananasifu, Kinondoni Dar es Salaam.

Mwingine ni Alphonce Mawazo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Godfrey Lwema aliyekuwa Diwani wa Chadema, Kata ya Namawala Kilombero, Morogoro.

Pamoja na hivyo, baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kumekuwepo na matukio ya wananchi kuuawa na kufungwa kwenye viroba na kasha kutupwa mtoni pamoja na baharini ambapo Jeshi la Polisi likiendelee kukalia ripoti ya mauaji hayo.

Matukio mengine yaliyosisimua Tanzania na dunia ni kushambuliwa kwa risasi 38 Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzania Bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) Septemba 7, 2017 Dodoma.

Wajumbe hao kutoka Bunge la Marekani ni John Espinoza na Lauren Ladenson wamekutana na Maalim Seif katika Makao Makuu ya CUF yaliyopo Mtendeni, Zanzibar.

Katika ujumbe waki wa Twitter Maalim Seif amesema, Maalim Seif ameeleza kuwa lengo kuu la wajumbe hao ni kuangalia kwa undani hali ya kisiasa Tanzania Bara, Zanzibar na hali ya uchumi kwa jumla.

Anderson Ndambo ambaye ni Ofisa Habari wa CUF akizungumza na MwanaHALISI Online hakuweka wazi siku ama tarehe ya wageni hao kutua nchini, hata hivyo amesema kuwa, mazungumzo kati ya Maalim Seif na wajumbe hao yataelezwa baadaye.

“Kwa kifupi ugeni huu umekuja kwa ajili ya kujadili hali ya kisiasa na uchumi nchini lakini zaidi tutaelezana baadaye,” amesema Ndambo.

Hata hivyo, MwanaHALISI Online limewasiliana na Msemaji wa Serikali Dk. Hassan Abbas ili kujua uwepo pia ratiba ya wajumbe hao.

“…Nyie MwanaHALISI Online nani amewaruhusu mfanye kazi…, mtaumia. Msishindane na serikali. Kwanza nitumie jina lako kwenye meseji,” amesema Dk. Abas

Kumekuwepo na malalamiko ya vyama vya upinzani nchini kuminywa haki ya kufanya siasa lakini pia baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamikia hali mbaya ya uchumi.

Hata hivyo, serikali imekuwa ikitoa takwimu kuonesha uchumi ukiendelea kuimarika siku hadi siku.

Viongozi TSNP wahojiwa saa saba kuhusu Nondo

JESHI la Polisi nchi limewahoji viongozi wa Mtandao wa wafunzi (TSNP) kama mashahidi kwenye kesi anayotarajiwa kufunguliwa Mwenyekiti wa mtandao huo Abdul Nondo. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Nondo aliripotiwa kutekwa usiku wa Kuamkia Machi 8 Mwaka huu. Jeshi hilo linamtuhumu mwenyekiti huyo kufanya kosa la udanganyifu na kuzua taharuki kwa umma pamoja na wanafunzi wenzake.

Jeshi hilo limewahoji watu wanne ambao ni Alphonce Lusako, ofisa wa ukaguzi wa haki za binaadamu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), na viongozi wa TSNP akiwemo Hellen Sisya, Ofisa Habari, Paul Kisabo Mkurugenzi wa Idara ya sheria na Malekela Brigthon, ambaye ni Katibu wa Mtandao huo.

Viongozi hao waliowasili kwenye Ofisi za Mkuu wa Makosa Jinai (DCI) majira ya saa 3 asubuhi na kumaliza kuhojiwa saa kumi jioni.

Wakili wa viongozi hao Reginald Martine amesema kuwa wamehojiwa kama sehemu ya ushahidi wa jamhuri na amesema kuwa hakujua kilichoendelea kwenye mahojiana hayo kwa kile kilichodaiwa kuwa shauri hilo lipo kwenye uchunguzi na kwamba anaweza kuvuruga ushahidi.

Ofisa habari wa mtandao huo, Hellen Sisya amesema “Ingawa tunaambiwa uchunguzi unaendelea lakini viongozi waandamizi wa serikali akiwemo Waziri wa mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam walishamhukumu mtuhumiwa hata kabla ya uchunguzi wa mashtaka hayo kumalizika.

Ninje wa Chalenji, apewa Ngorongoro Heroes

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemteuwa Ammy Ninje kuwa Kocha Mkuu wa muda wa timu ya Taifa ya Vijana chini ya Umri wa Miaka 20, ‘Ngorongoro Heroes’ ambayo inatarajia kucheza michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya dhidi ya Morocco na Msumbiji. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Ninje ambaye hapo awali alikuwa kocha wa muda wa Timu ta Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ iliyoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika nchini Kenya katika mwaka uliopita na kuondoshwa katika hatua ya makundi.

Ngorongoro Heroes itacheza na timu ya Taifa ya Vijana ya Morocco Jumamosi ya Machi 17, 2018 na dhidi ya timu ya  Msumbiji Jumatano Machi 21, 2018 michezo yote ikichezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Kocha huyo ataiongoza Ngorongoro Heroes katika michezo hiyo miwili ya kirafiki kabla ya kuivaa DR Congo katika mchezo wa kuwania kufuzu kombe la Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 (AFCON U20).

Mchezo huo ambao utachezwa Machi 31 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, na mechi ya marudiano itafanyika baada ya wiki mbili mbili jijini Kinshansha, nchini Congo.

Namba ya simu ya Nondo yazua taharuki

NAMBARI ya simu ya mkononi ya Abdul Nondo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), ambaye bado anashikiliwa na polisi jijini Dar es Salaam, imezua taharuki baada ya kuanza kuita bila kupokelewa huku wakati mwingine ‘aliyenayo’ akiikata. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Namba hiyo ambayo ilitoweka hewani wakati kijana huyo alipodaiwa ‘kupotea’ usiku wa kuamkia Machi 8 mwaka huu.

Kuita kwa namba hiyo bila kupokelewa huku ikikatwa inapopigiwa, kunazua sintofahamu kwani kijana huyo aliyetoweka na kupatikana akiwa Mafinga mkoani Iringa bado anashikiliwa na polisi huku mawakili, ndugu jamaa na marafiki wakizuiliwa kumuona.

Jeshi polisi Kanda Maalumu ya Dar limetoa taarifa mchana wa leo likisema “Nondo hakutekwa (alijiteka), na alitoweka jijini Dar na kuelekea Iringa kwa mpenzi wake huku akitoa taarifa zilizozua taharuki.” Hata hivyo polisi hawakumtaja anayedaiwa kuwa mpenzi wa Nondo aliyetembelewa mkoani Iringa.

Hapo awali namba ya Nondo haikuwa ikipatikana lakini leo tarehe 13 Machi, kuanzia majira ya saa tatu usiku imeripotiwa kuwa hewani na kwamba inaita na kukatwa ingawa kijana huyo yupo mikononi kwa polisi, ikiwa ni zaidi ya siku tano tangu atoweke na baadaye kushikiliwa na polisi Iringa kabla ya kusafirishwa mpaka Dar.

Haijajulikana mara moja ikiwa anayetumia namba hiyo ni Nondo mwenyewe, maofisa wa polisi wanaofanya upelelezi au mtu mwingine.

Serikali yahofiwa kuburutwa ICC

KAULI za viongozi wa serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa wananchi, zinaweza kusababisha kufikishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC). Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Hayo yameelezwa leo na Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mbele ya waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya chama hicho yaliyopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Roderick Lutembeka, Katibu wa baraza hilo mbele ya wanahabari amesema kuwa, viongozi wa serikali wanatoa kauli zinazofifisha matumaini ya wananchi na taifa kwa ujumla na zaidi kutia hofu.

Na kwamba, kumekuwepo na malalamiko ya uvunjwaji wa haki jambo ambalo limesababisha malalamiko kwa jamii lakini serikali inajibu malalamiko hayo kwa kubeza huku uhuru wa mawazo ukiendelea kuminywa.

Lutembeka ameeleza kuwea, jumuiya na taasisi za nje zinashuhudia namna serikali ilivyo vinara katika kubana demokrasia na kuvunja sheria za vyama vya siasa huku kauli za kibabe zikitawala dhidi ya vyama vya upinzani na viongozi wake.

Katibu huyo ametoa mfano wa uchaguzi mdogo katika Majimbo ya Siha na Kinpndoni kwamba, kulitawala vitendo vya ukandamizaji mkubwa wa haki za binaadamu jambo ambalo liliibua hisia za malalamiko na kuonewa huku hisia hazi dhidi ya serikali zikitawala.

Pamoja na hivyo, Lutembeka ameeleza mfano wa kifo cha Akwilina Akwilin, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kilichomkuta wakati wa maandamano ya wafuasi wa Chadema Mkwajuni, Kinondoni.

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi na Jeshi la Polisi wakati wafuasi wa Chadema wakiandamana wakidai hati ya viapo vya mawakala wao kwenye uchaguzi mdogo wa Kinondoni. Akwilina hakuwa miongoni mwa waandamanaji, alikuwa kwenye basi ambapo risasi ilimpata akiwa ndani ya daladala.

Akitaja mifano mingine ametaja tukio la kuuawa kwa Daniel John, aliyekuwa Katibu wa Chadema Kata ya Hananasif, Kinondoni Dar es Salaam. Daniel aliokotwa ameuawa kwenye fukwe za Bahari ya Coco Beach, alikutwa na majeraha na kwamba, matukio hayo na ile mifanyo ya Ben Saanane yanaongeza hofu kwa wananchi.

Mambosasa: Tunamshikilia Nondo kwa kutoa taarifa ya uongo

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linamshikilia Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kwa kosa la kutoa taarifa za uongo na kujiteka. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Kanda ya Dar es Salaam, amewaaambia waandishi wa habari leo, Nondo ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.

Mambosasa amesema Nondo alidaiwa kutoweka jijini Dar es Salaam Machi 6, 2018, lakini alionekana wilayani Mafinga siku inayofuata na kujisalimisha mikononi mwa polisi Machi 7 mwaka huu.

Kamanda huyo amesema baada ya kujisalimisha alifunguliwa jalada la uchunguzi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, wanaendelea kumchunguze kubaini iwapo ni kweli alitekwa au alitoa taarifa za uongo kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kuvuruga amani.

Spika Ndugai apasua vichwa wabunge

SPIKA wa Bunge la Jamhuri, amepanga upya Kamati za Bunge, kufuatia kumalizika kwa muda wa kamati za awali. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Katika mabadiliko hayo, wabunge kadhaa wamehamishwa kwenye kamati walizokuwa awali na kuhamishiwa kwenye kamati nyingine.

Miongoni mwa walioathirika na hamisha hiyo, ni pamoja na mbunge wa Muhenza (CCM), Adadi Rajabu, aliyehamishiwa Kamati ya Bajeti.

Kabla ya mabadiliko hayo, Adadi alikuwa mjumbe kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama na mwenyekiti wa kamati hiyo.

Job Ndugai apangua Kamati za Bunge

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amefanya uteuzi wa wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Machi 12,2018 inasema Spika amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa Ibara ya 96 ya Katibu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taarifa hiyo imesema ibara hiyo imeweka wazi kwamba, Kanuni za Kudumu za Bunge zinafafanua muundo wa shughuli za Kamati za Bunge.

“Kwa msingi huo Kanuni ya 118 ya Kanuni za kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 imeweka Kanuni za Kudumu za Bunge zenye muundo na majukumu mbalimbali kama yanavyofafanuliwa katika nyongeza ya nane. Uteuzi wa wabunge kwenye kamati mbalimbali unaonekana utaratibu katika Kanuni ya 116.”

“Kanuni ya 116(1) inaweka utaratibu kwamba, ujumbe kwenye Kamati za Kudumu za Bunge utadumu mpaka mwisho wa Mkutano wa Kumi wa Bunge ambao ni nusu ya kwanza ya maisha ya Bunge,” anasema Spika Ndugai.

Katika uteuzi huo, wajumbe mbalimbali wamerejea katika kamati zao, wengine wakibadilishwa huku baadhi ya wenyeviti waliokuwa wakiongoza baadhi ya kamati wameondolewa.

“Kwa mamlaka niliyopewa na Kanuni ya 115(3) na kwa kuzingatia vigezo vilivyoanishwa katika Kanuni ya 116(5) nimefanya uteuzi mpya wa ujumbe katika Kamati za Kudumu za Bunge. Wajumbe wa kila kamati wanawajibika kuchagua mwenyekiti na makamu mwenyekiti kwa mujibu wa Kanuni ya 116(10) kuwa viongozi wao,” amesema.

Namaingo wazindua mradi mpya Msolwa

JUHUDI za Taasisi ya Namaingo Business Agents (NBA), imezindua mradi Shamba Mji Msolwa wilayani Mkuranga, Pwani ikiwa ni mwendelezo wa kuinua uchumi wa nchi kupitia kilimo. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mradi wa Shamba Mji utakuwa na hekari 7,000 ambapo utahusisha mashamba na makazi pamoja na huduma za kijamii ikiwa pamoja na soko la kuuza mazao yatakayotokana na mazao ya shamba hilo.

Biubwa Ibrahimu, Mkurugenzi wa Namaingo amesema uzinduzi mashamba hayo yatakuwa kichecheo kikubwa cha kunyanyua uchumi wa wakulima, wakazi wanaozunguka maeneo ya mashamba na nchi kwa ujumla.

Amesema kupitia mradi huo wakulima watapata fulsa ya kupata ushauri wa kupanda mazao kwa ubora ikiwa pamoja na kugeuza kutoka kilimo cha chakula na kulima kilimo cha biashara.

Diwani wa Kata ya Mbezi, Rashid Selungwi, amesema kuwa wananchi wa eneo hilo wamefurahia ujio wa mradi huo utakaowaletea maendeleo makubwa kwani hiyo ni moja ya fulsa kwa wakazi wa Msolwa.

Mwakilishi wa Wazee wa kijiji cha Msolwa, Ali Kitasa ameubariki mradi huo na kuwaombea dua walulima watakaojishughulisha na mradi huo kwani anaamini kuwa mafanikio yao yatawagusa wakazi wa eneo hilo.